July 25, 2017

SPIKA APOKEA MAJINA YA WABUNGE CUF WALIOTIMULIWA......

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
________________________
Mhe. Spika amepokea barua kutoka kwa Mhe. Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Wananchi (CUF) na Mhe. Magdalena Sakaya, (MB) - Kaimu Katibu Mkuu (CUF) ambapo wamemuarifu kuhusu uamuzi wa Baraza Kuu la Chama hicho kuwafukuza Wabunge wanane (8) na Madiwani wawili kwa makosa kadhaa ya kinidhamu.
Katika barua hiyo, viongozi hao wamewataja wanachama hao ambao ni Wabunge kuwa ni: -
1. Mhe. Severina Silvanus Mwijage, (MB);
2. Mhe. Saumu Heri Sakala, (MB);
3. Mhe. Salma Mohamed Mwassa, (MB);
4. Mhe. Riziki Shahari Ngwali, (MB);
5. Mhe. Raisa Abdallah Mussa, (MB);
6. Mhe. Miza Bakari Haji, (MB);
7. Mhe. Hadija Salum Ally Al-Qassmy, (MB); na
8. Mhe. Halima Ali Mohamed, (MB).
Aidha, barua hiyo imeainisha makosa yao kuwa ni kukiuka Kifungu cha 83(4) na (5) cha Katiba ya Chama hicho kwa kutenda makosa yafuatayo: -
1. Kukihujumu Chama katika uchaguzi wa marudio wa Madiwani wa tarehe 22 Januari, 2017;
2. Kumkashifu na kumdhalilisha Mwenyekiti wa Taifa wa Chama hicho, Prof. Ibrahim Haruna Lipumba, Naibu Katibu Mkuu na Mbunge wa Kaliua, Mhe. Magdalena Hamisi Sakaya, (MB) na Wakurugenzi wa Chama;
3. Kushirikiana na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kupanga oparesheni waliyoiita “ONDOA MSALITI BUGURUNI” wakiwa na lengo la kumuondoa Mwenyekiti halali wa Chama hicho kinyume na taratibu za Katiba ya CUF na Sheria ya Vyama vya Siasa ya Mwaka 1992;
4. Kuruhusu na kuipa fursa CHADEMA kuwa msemaji wa masuala ya CUF kinyume na matakwa ya Katiba ya CUF;
5. Kulipia pango na kufungua ofisi ya CUF Magomeni bila kufuata taratibu za kikatiba; na
6. Kuchangia fedha zilizotumika kukodisha ma-bouncer kwa lengo la kuwadhuru Viongozi watiifu wa Chama akiwemo Mwenyekiti wa Taifa, Prof. Ibrahim Haruna Lipumba; Naibu Katibu Mkuu, Mhe. Magdalena Hamisi Sakaya, (MB) na Mhe. Maftaha Nachuma, (MB), Mkurugenzi wa CUF wa Mambo ya Nje na Mbunge wa Mtwara Mjini.

Mhe. Spika angependa kuuarifu umma kuwa, suala la kuwaondoa uanachama ni la utashi wa Vyama vyenyewe; na kila Chama kina utaratibu wake, hivyo bado anaendelea kuitafakari barua hiyo; na taarifa rasmi kuhusu maamuzi ya Spika kwa Wabunge waliofukuzwa ataitoa hapo baadaye.
Imetolewa na:
Ofisi ya Spika,
S. L. P. 941,
DODOMA.
25 Julai, 2017

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE