July 25, 2017

RC MASENZA ATOA WIKI MBILI KWA MJI MAFINGA KUREJESHA MILIONI 110 .....

Mkuu wa mkoa wa Iringa Amina Masenza akisalimiana na walimu shule ya sekondari ya JJ Mungai Leo 

Mkuu wa mkoa na ujumbe wake wakikagua ujenzi wa maabara 
Hili ndilo jengo la maabara lililosimama kwa kukosa pesa 

Na Mtukiodaimablog. 

MKUU wa mkoa wa Iringa Amina Masenza ametoa Wiki mbili kwa Halmashauri ya Mji Mafinga kurejesha fedha kiasi cha shilingi milioni 110 zilizotolewa na wadau wa maendeleo wilaya ya Mufindi kwa ajili ya ujenzi wa maabara katika shule ya Sekondari ya JJ  Mungai. 

Mkuu huyo wa mkoa ametoa agizo hilo leo  wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua maendeleo ya elimu katika wilaya ya Mufindi,alisema ndani ya wiki hizo mbili alizotoa atamtaka mkuu wa wilaya ya Mufindi Jamhuri Wiliam kupeleka taarifa ofisini kwake kuhusu pesa hizo. 

"Nakuagiza mkuu wa wilaya ya Mufindi fuatilia pesa hizi na kama zimetumika katika maeneo mengine zirudishwe zifanye kazi iliyokusudiwa... nasisitiza sana nidhamu ya fedha kila pesa itumike kwa kazi iliyokusudiwa sipendi nidhamu chafu kwenye usimamizi na matumizi mabaya ya Pesa "

Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa serikali imeagiza ujenzi wa maabara ufanyike haraka kwa lengo la kuongeza ufaulu kwa wanafunzi wa masomo ya sayansi na hivyo hatua ya mkuu wa wilaya hiyo kuomba wadau kuchangia pesa hizo za ujenzi wa maabara ilikuwa ni kuunga mkono jitihada za serikali hivyo haipendezi pesa zilizochangwa kwa ajili ya maabara kwenda kutumika kwa kazi nyingine. 

Awali mkuu wa shule ya sekondari ya JJ Mungai Yusuph Mahunda alisema kuwa moja kati ya changamoto katika umaliziaji wa jengo la maabara shuleni hapo ni pesa kukosekana na iwapo wangekuwa na pesa jengo hilo lingekuwa limekamilika mapema. 

Mkuu wa wilaya Wiliam alimweleza mkuu huyo wa mkoa kuwa pesa hizo zilitolewa na Saohili kwa ajili ya ujenzi wa maabara ila zimetumika isivyo jambo ambalo hajalipenda.

Hivyo alitaka wakuu wa idara kuendelea kufanya kazi kama timu na kile wanachokubaliana kifanyike kama walivyopanga badala ya kila mmoja kufanya vyake. 

Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa wilaya hiyo inaendelea na ujenzi wa maabara na tayari maabara 5 kati ya maabara zaidi ya 30 zimekamilika. 

Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji Mafinga Charlesy Makoga alisema kuwa halmashauri yake itachangia milioni 30 kwa ajili ya kuunga mkono ujenzi huo ila alisema hajapendezwa na hajui kwanini pesa za wadau wa maendeleo ya ujenzi wa maabara kutumika katika shughuli nyingine. 

Makoga alisema jumla ya shilingi milioni 220 zilichangwa na Saohili kwa ajili ya maabara kwa ajili ya halmashauri ya Mufindi kiasi cha shilingi milioni 110 na  Mji Mafinga milioni 110 .

Kaimu mkurugenzi wa maendeleo mji Mafinga Voster Mgina alisema pesa hizo zilitumika kuchonga madawati.

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE