July 28, 2017

MAKINDA HATARI LIGI KUU TANZANIA BARA MSIMU UJAO

Na Salym Juma, Arusha
Ligi kuu ya Uingereza ni miongoni mwa ligi 5 maarufu Duniani. Mara nyingi kabla ya kuanza kwa EPL, wachezaji kadhaa wamekuwa wakipewa nafasi ya kufanya vyema ila kumekuwa na ‘surprise’ ya wachezaji vijana kila msimu wa EPL. Kutokana na hilo, leo hii nimekuja na listi ya wachezaji vijana ambao wanapaswa kuchungwa msimu ujao wa 2017/2018. Wachezaji hawa ni vijana wadogo ila hawamulikwi na kamera kama ilivyo kwa kaka zao.
Alfie Mawson ni kijana mdogo mwenye miaka 23. Japokuwa jina lake ni dogo ila kiwango chake hakielezeki. Tangu ajiunge na Swansea 30 August 2016 amefanya makubwa katika michezo 27 aliyocheza kama mlinzi wa kati. Mawson ameisaidia Swansea kusalia kwenye ligi kuu kutokana na kufanya vyema kwenye idara ya ulinzi, idara ambayo ilikuwa dhaifu kabla ya kupata nguvu kutoka kwa Mawson. Huenda akafanya vyema na kugombaniwa baada ya msimu kuisha.
Mawson ni Beki anayeweza kufunga, anapanda na amejaaliwa nidhamu uwanjani. Jezi namba 6 aliyorithi kutoka kwa Ashley William anaitendea haki pale Liberty Stadium na magoli 4 aliyofunga msimu uliopita yametosha kuisaidia timu yake. Mechi yake ya kwanza dhidi ya Watford iliyomalizika kwa sare ya 0–0 ilimfanya atajwe kama mchezaji bora wa mchezo kutokana na kiwango chake bora kabisa. Kutokana na haya, ‘Dogo’ huyu ni wa kuchunga sana msimu ujao.
Jérémie Boga ni kinda wa Chelsea ambaye amekuwa mtamu siku za karibuni. Japokuwa Chelsea hawana desturi ya kuwapa nafasi makinda ila huenda Jérémie Boga akapata nafasi ya kucheza hasa katika michuano ya FA na EFL. Boga amehudumu kwenye timu mbalimbali kama mchezaji wa mkopo kwenye timu za Stade Rennais na Granada ambayo alifanya makubwa msimu uliomalizika. Boga alihudumu kwenye timu ya vijana ya Chelsea kuanzia 2009-2015 na kupandishwa timu ya wakubwa.
Watu wengi walianza kumfatilia Boga mnamo April 2, 2017 pale Barcelona ilipoinyuka Granada 4–1 na hii ilikuwa baada ya Boga kusawazisha goli. Kiwango chake murua cha kukaba, kasi na kufunga kilimfanya aitwe kwenye kikosi cha Chelsea kinachojiandaa na msimu. Kwa sasa ana miaka 20 na tayari ameshaiwakilisha Ivory Coast kwenye michezo miwili licha Ufaransa kumshawishi kubadili uraia. Endapo Chelsea watamtoa kwa mkopo pale EPL basi tegemea makubwa kutoka kwake.
Dominic Solanke, huyu ni zao la academy ya Chelsea na mara kadhaa mashabiki wa Chelsea walikuwa wakitaka apewe nafasi ya kucheza pale Darajani. Magoli 4 aliyofunga kwenye michuano ya Dunia ya U-20 iliyomalizika kwa Uingereza kuwa mabingwa yalitosha kuwashawishi Liverpool kumsajili mapema May 30, 2017. Penye ukweli, uongo hujitenga Dominic Solanke anaujua mpira na Liverpool hawatajuta kumsajili mshambuliaji huyu ambaye alikuwa mchezaji bora wa michuano ya Dunia ya U-20.
Akiwa Chelsea, Solanke amefanya makubwa katika ngazi ya vijana hasa kwenye michuano ya FA na UEFA. Goli zuri alilofunga akiwa na Liver dhidi ya Crystal Palace ni ishara tosha kuwa anapaswa kuchungwa na Mabeki pindi msimu utakapoanza. Jurgen Klop ni muumini wa vijana, uumini huu huenda ukamnufaisha Solanke ambaye amekosa nafasi Chelsea licha ya kiwango chake cha kuridhisha. Miaka yake 19 inatosha kumpa nafasi ya kudumu pale Anfield.
Tammy Abraham ni zao la Chelsea kama alivyo Dominic Solanke na Jérémie Boga ambao wapo kwenye listi hii. Uwezo wake wa kufunga ni mkubwa na hii ndio sababu iliyowafanya Swansea City kumsajili kutoka Bristol City sehemu ambayo alifanya makubwa kwa kupasia kamba mara 23 katika michezo 41. Swansea inatarajia kuimarisha idara yake ya ushambuliaji ambayo imekuwa chini ya Fernando Llorente. Huenda Tammy akapenyeza katika Kikosi cha kwanza cha Swansea.
Licha ya Chris Wood kuwa mfungaji bora wa ligi daraja la kwanza msimu uliopita, Tammy alikuwa wa Pili nyuma ya Wood ambaye tulimuona kwenye michuano ya Mabara. Chelsea inaongozwa na Mitch Batshuay na Alvaro Morata kwenye idara ya ushambuliaji hivyo Tammy ni ngumu kupata nafasi Darajani hali ambayo iliwafanya Chelsea kunusuru kiwango chake kwa kumpeleka Swansea kwa mkopo. Hifadhi maneno yangu, Tammy atafanya makubwa msimu ujao akiwa Swansea.
Ademola Lookman ni Mshambuliaji wa Everton ambaye ana asili ya Nigeria. Ukweli haufichiki kwenye mpira, Lookman ana kiwango mujarab kwenye soka. Kiumri na kimaumbile ni mdogo ila kiuchezaji ni hatari sana. Goli la 4 alilolifunga dhidi ya Man City pale alipochukua nafasi ya Ross Barkley lilimfanya amwage chozi kwa furaha na hapa ndipo watu walipoanza kumfuatilia. Namtabiria makubwa pale Goodison Park msimu ujao kwani naamini atapata nafasi kubwa ya kucheza.
Lookman alikuwa sehemu ya wachezaji wa Uingereza waliowasha moto kwenye michuano ya Kombe la Dunia la vijana U-20 iliyomalizika kwa Uingereza kushinda taji hilo. Alifunga magoli 3 na kuwa nyuma ya Solanke. Lookman amecheza mara 8 msimu uliomalizika ila katika michezo hiyo ameonesha kiwango cha kuridhisha hali inayomfanya kutabiriwa makubwa msimu ujao. Ronald Koeman amekuwa Muumini wa Vijana kitu ambacho kitamnufaisha Lookman.

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE