July 10, 2017

KIGWANGALA MGENI RASMI SIKU YA WATU DUNIANI


 Naibu Waziri wa Afya, Dk Hamis Kigwangala anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika sherehe za maadhimisho ya siku ya watu duniani ambayo yatafanyika kesho katika viwanja vya Mwembe Yanga jijini hapa.
Akizungumza leo Jumatatu, Julai 10, katika mkutano na waandishi wa habari Naibu Mwakilishi Mkazi wa Shirikia la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu (UNFPA), Dk Hashina Begum amesema kaulimbiu ya mwaka huu ni 'Uzazi wa mpango, huwezesha watu na kuendeleza Taifa.’
"Afya bora ya uzazi na matumizi ya uzazi wa mpango, huinua uchumi na kufanikisha malengo endelevu kwa kuwawezesha wanawake kumaliza masomo na kupata ajira," amesema Dk Begum.
Amesema uwekezaji katika afya ya uzazi wa mpango ni kumpa haki mwanamke kiuchumi kwani ataweza kuchangia maendeleo.
Daktari wa Afya ya Uzazi wa Wizara ya Afya, Cosmas Swai amesema wananchi watakaofika katika viwanja hivyo watapata burudani, elimu ya afya ya uzazi wa mpango na huduma ya kupima afya bure.
"Kuanzia leo hadi kesho kutwa (Julai 12) Kutakuwa na huduma za uzazi wa mpango bure, kupima Ukimwi, ushauri nasaha, elimu ya afya ya uzazi na saratani ya shingo ya kizazi," amesema Dk Swai.
Mkuu wa idara inayoshughulikia watu iliyopo chini ya Tume ya Taifa ya Mipango, Ibrahim Kalengo amesema kwa upande wa Tanzania, maadhimisho ya siku ya idadi ya watu yatafanyika kitaifa katika viwanja vya Mwembe Yanga na baadhi ya viongozi wa nchi watakuwa London, Uingereza katika mkutano leo usiku.
"Leo usiku mjini London kutakuwa na mkutano wa kujadili afya ya uzazi wa mpango kwa kuangalia maendeleo, malengo yaliyowekwa ni   kuhakikisha ifikapo mwaka 2020 idadi ya wanawake wanaotumia uzazi wa mpango iwe imeongezeka na kufikia 120 milioni," amesema Kalengo.

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE