June 10, 2017

WAZIRI MHAGAMA AZINDUA MRADI WA DONBOSCO NET TANZANIA

HOTUBA YA MHE. JENISTA J. MHAGAMA (MB.), WAZIRI WA  NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU – SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WATU WENYE ULEMAVU KATIKA UZINDUZI WA MAFUNZO  YA STADI ZA KAZI KATIKA FANI ZA UJENZI, UFUNDI MAGARI, TEHAMA NA NGUO KWA VIJANA 3,440 KUPITIA TAASISI YA DONBOSCO NET TANZANIA TAREHE 09 JUNI, 2017; IRINGA


  • Mhe. Anthony Mavunde, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira);

  • Mhe. Amina Masenza, Mkuu wa Mkoa wa Iringa;
  • Ndugu Peter Kalonga, Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu);

  • Bi. Wamoja Ayubu, Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa;
  • Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi Don Bosco Net Tanzania;
  • Vijana wa Mafunzo;
  • Wanahabari;
  • Wageni waalikwa;
  • Mabibi na Mabwana.

Awali ya yote, naomba nichukue fursa hii kuushukuru Uongozi wa Mkoa wa Iringa kwa kutupokea vizuri na kutuhakikishia usalama wetu tukiwa hapa Iringa, Vilevile shukrani za dhani nizitoe kwa Taasisi ya Don Bosco Net Tanzania kwa kukubali kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu katika kutekeleza Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi wa Vijana Wetu kwa kutoa mafunzo ya stadi za kazi mbalimbali; mafunzo ambayo yatawasaidia vijana hawa kujiajiri au kuajiriwa na hatimaye kushiriki katika kujenga uchumi wa Taifa. 

Viongozi wa DonBosco,
Moyo wa ushirikiano mliouonesha wa kufundisha vijana wetu unajenga imani kwa Serikali ya kushirikiana nanyi zaidi katika kukuza stadi za kazi kwa vijana wa taifa letu. Nikushuru wewe Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi, Padri Celestine kwa jitihada zako ulizoonesha tangu tulipoingia makubaliano hadi sasa. Wataalamu wako na Wetu wamekuwa bega kwa bega kuhakikisha zoezi hili linaendeshwa kwa ufanisi. Aidha, nirudie tena kuushukuru uongozi wa Mkoa wa Iringa kwa kuamua kujumuika nasi leo hii wakati tunapozindua Kitaifa mafunzo haya ya vijana 3,440 watakaojifunza stadi mbalimbali katika FANI ZA UJENZI, UFUNDI MAGARI, TEHAMA NA NGUO kupitia Taasisi hii.

Ndugu vijana  na wageni waalikwa,
Serikali imeweka mipango na mikakati mbalimbali ya kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa nchi ya uchumi wa kipato cha kati ifikapo mwaka 2025. Mwelekeo wa miaka mitano ya sasa kuanzia 2016 hadi 2021 ni kujenga Taifa lenye Viwanda vya kuzalisha bidhaa za kutosheleza mahitaji ya soko la ndani na kuuza nje ya nchi.  Ili kufikia azma hii, nguvu kazi yenye ujuzi wa kutosha kumudu mahitaji ya soko la ajira inahitajika. Kwa umuhimu huo, Serikali imeandaa Programu ya Kitaifa ya kukuza ujuzi wa nguvukazi ya Taifa hususan vijana; programu hii ni ya miaka mitano ambapo utekelezaji wake umeanza kwa kutoa fursa kwa vijana kupata ujuzi katika Sekta mbalimbali kama vile sekta ya Nguo, Ngozi, Ujenzi, Utalii, Ufundi wa Magari, n.k. Hivyo, Vijana mliopo hapa leo ni sehemu ya utekelezaji wa  programu hii.

Ndugu vijana  na wageni waalikwa,
Kabla ya kutengeneza programu ya kukuza ujuzi nchini, tulifanya Utafiti wa nguvukazi wa mwaka 2014 na kubaini kuwa idadi kubwa ya nguvu kazi iliyokua kwenye ajira  takriban asilimia 79.9 inakiwango cha chini cha ujuzi, na asilimia 16.6 ina kiwango cha kati cha ujuzi na asilimia 3.6 ina kiwango cha juu cha ujuzi. Hivyo tuliona kwa uwiano huu ni vigumu kuweza kufikia uchumi wa viwanda na hatimaye nchi ya kipato cha kati ambapo kiwango kinachotakiwa kutufikisha huko ni cha uwiano wa angalau asilimia 12 kwa ujuzi wa kiwango cha juu; asilimia 34 kwa ujuzi wa kiwango cha kati na kutozidi asilimia 54 kwa ujuzi wa kiwango cha chini. Hivyo, Serikali ikaamua kutengeneza programu ya kitaifa ya miaka mitano ambayo imejikita katika kukuza ujuzi wa nguvukazi yake kufikia viwango vinavyokubalika kutufikisha katika uchumi wa kipato cha kati kupitia uchumi wa viwanda.
Ndugu vijana na wageni waalikwa;
Katika kuhakikisha kuwa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/17 - 2020/21) unatekelezeka ipasavyo, Serikali kupitia Programu ya Kukuza Ujuzi Nchini inalenga ifikapo Mwaka 2021 vijana 100,000 wapate mafunzo kupitia Programu za Uanagenzi; Pili, kutoa mafunzo kwa vitendo kwa wahitimu 1,200,000; Tatu, kutoa mafunzo ya kuongeza ujuzi kwa wafanyakazi 1,700,000; na Nne, kutambua na kurasimisha ujuzi uliopatikana wa vijana 1,000,000 waajiriwa na waliojiajiri ili kuziba nakisi hiyo ya ujuzi.
Ndugu vijana  na wageni waalikwa,
Katika Jumuiya ya Afrika Mashariki tumekubaliana kuwa ifikapo mwaka 2018, katika soko la Afrika Mashariki tuachane na nguo na viatu vya mitumba kutoka nje ya Jumuiya. Hivyo, mafunzo haya ni maandalizi ya kuhakikisha kuwa tunakuwa na vijana wengi wenye sifa na stadi za kutengeneza bidhaa mbalimbali ikiwemo viatu na nguo ili kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa mstari wa mbele katika kutimiza makubaliano ya Jumuiya. Pia, lengo lingine la Mafunzo haya ni kuhakikisha tunakuwa na vijana wengi wenye stadi mbalimbali za kuwawezesha kufanya kazi katika viwanda vilivyopo na vitakavyojengwa.
Hivyo, vijana mliochaguliwa kujiunga na mafunzo haya mtambue kuwa mna jukumu kubwa la kutimiza ahadi ya nchi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na pia kutimiza azma ya kuwa na nchi ya viwanda. Tunaposema nchi ya viwanda tunategemea nguvukazi ya taifa ambayo ni vijana kutumika ipasanyo kwa kujipatia ajira za kuajiriwa au kujiajiri kupitia viwanda.
Katika sekta ya nguo na Viatu tayari tumeanza kutoa mafunzo ambapo jumla ya vijana 3,000 wanapata mafunzo ya kubuni na kushona nguo kwa kutumia teknolojia za kisasa kupitia Viwanda vya TOOKU Dar es Salaam na MAZAVA Morogoro. Aidha, Vijana 1,000 watapata mafunzo ya kutengeneza bidhaa za ngozi ikiwemo viatu, Pochi, n.k.
Ndugu vijana na wageni waalikwa;
Leo tutafanya uzinduzi wa mafunzo ya stadi mbalimbali za kazi kwa vijana 3,440 watakaopata mafunzo kupitia vyuo 8 vilivyo chini ya Taasisi ya Don Bosco Net Tanzania katika fani za
·         Useremala (vijana 250),
·         Uashi (vijana 195),
·         Ufundi magari (vijana 302),
·         Uchongaji wa vipuri (vijana 158),
·         Ufundi bomba (vijana 195),
·         Ufundi vyuma (vijana 250),
·         Umeme (vijana 160),
·         TEHAMA (vijana 1,010),
·         Kuweka Terazo na Vigae (vijana 120); na
·         Ushonaji nguo (vijana 800).

Ni imani yangu kuwa vituo vyote vimejiandaa vema kutoa mafunzo bora kwa vijana wetu. Sisi kama waratibu na wasimamizi tutafuatilia kwa karibu utekelezaji wake. Hivyo, ubora wa mafunzo mtakaoutoa utatoa mwelekeo wa kuendelea kushirikiana na Serikali katika awamu zijazo na pia kuwezesha Tanzania ya Uchumi wa Viwanda.

Ndugu vijana;
Mmebahatika kuwa wa kwanza, kupata mafunzo katika Taasisi hii ya DonBosco kupitia programu ya Taifa ya kukuza ujuzi. Niwasihi muwe na bidii katika kujifunza ili mpate weledi katika fani mnazo somea. Fursa hii mliyoipata ni ya kipekee, hivyo, mfahamu kuwa  huu ujuzi mnaoupata  ni kwa faida yenu na msingi mmojawapo wa maisha yenu.

Ndugu, Wageni Waalikwa
Nichukue fursa hii kutoa wito kwa Viwanda na Taasisi  mbalimbali zijitokeze kwa wingi kushirikiana na Serikali  kwa kutoa nafasi za mafunzo kwa vitendo kwa vijana wetu ili kuwajengea umahiri wa stadi za kazi na kuwezesha kuwa na vijana wenye ujuzi bora wa kujiajiri na kuweza kuwaajiri wakati watakapowahitaji.  Niwaombe waajiri walio tayari kushirikiana nasi, wawasilishe maombi yao Ofisi ya Waziri Mkuu; au kupitia Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) au kupitia Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF).

Ndugu, Wageni waalikwa
Nichukue fursa hii pia kuomba vyombo vya habari vikiwemo Radio, Televisheni, Magazeti na mitandao ya kijamii kuhamasisha waajiri na umma wa watanzania kuelewa dhana na umuhimu wa mafunzo kwa vitendo mahala pa kazi. Wahamasishe waajiri kutoa nafasi za mafunzo kwa vitendo kwa vijana walioko mafunzoni na wanaohitimu mafunzo. Serikali kwa kushirikiana na chama cha waajiri Tanzania (ATE) pamoja na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) wameshaandaa miongozo ya mafunzo kwa vitendo kazini inayotumika kuongoza mafunzo  kwa vitendo mahala pa kazi. Hivyo, nashauri waajiri wote na wananchi kwa ujumla waisome na waielewe ipasavyo miongozo hiyo.

Ndugu, vijana;
Napenda kuwasihi muitumie nafasi hii kama fursa itakayowapa mtaji wa kujifunza stadi mbalimbali na baadaye kuweza kuunda vikundi na kuanza kufungua viwanda na kampuni ndogo ndogo za kutengeneza bidhaa mbalimbali na pia muweze kushindana na kupata zabuni za Serikali na za Sekta Binafsi. Serikali tunafahamu changamoto ya upatikanaji wa Mitaji kwa vijana; hivyo tunaendelea na majadiliano ya ndani kuona ni namna gani tutaboresha mifuko yetu ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ili kuweza kutoa mikopo kwa vijana hususan waliopata mafunzo kupitia programu hii ili waweze kuanzisha shughuli za kiuchumi kupitia viwanda vidogo vidogo.

Ndugu Vijana na wageni waalikwa,
Mwisho, kwa mara nyingine tena niwapongeze kwa kuitikia wito wa kushiriki mafunzo haya, na ninaomba niwasihi tena kuweka bidii katika kujifunza kwa ustadi wa hali ya juu. Niwashukuru pia viongozi wenzangu wa Mkoa mliofika kushiriki nami katika uzinduzi huu. Vijana hawa ni wetu, tuwasaidie kwa kadri tunavyoweza, punde watakapo maliza mafunzo haya waweze kujiajiri kupitia viwanda. Ni Vema pia tukaweka utaratibu katika maeneo yetu ya kiutawala kuhakikisha tuna tenga maeneo ya kuanzisha viwanda vidogovidogo kuwezesha vijana hawa kujiajiri.  Rais wetu ameshaelekeza kutenga maeneo ya kuwezesha vijana kujiajiri. Aidha, Waziri Mkuu ameendelea kusisitiza na ameshaelekeza Mikoa yote kutenga maeneo ili vijana waweze kuyatumia kujiajiri. Hivyo ni vema tukazingatia maelekezo ya viongozi wetu.
Baada ya kusema hayo napenda kutamka rasmi kuwa mafunzo haya ya stadi za kazi katika FANI ZA UJENZI, UFUNDI MAGARI, TEHAMA NA NGUO KWA VIJANA 3,440 KUPITIA TAASISI YA DONBOSCO NET TANZANIA yamezinduliwa rasmi. 

AHSANTENI KWA KUNISIKILIZA

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE