June 3, 2017

TAMKO KWA VYOMBO VYA HABARI JUU YA KUKAMATWA KWA MRATIBU WA MTANDAO WA WATETEZI WA HAKI ZA BINADAMU NDUGU ONESMO OLENGURUMWA

MTANDAO WA WATETEZI WA HAKI ZA BINADAMU TANZANIA

TAMKO KWA VYOMBO VYA HABARI JUU YA KUKAMATWA KWA MRATIBU WA MTANDAO WA WATETEZI WA HAKI ZA BINADAMU NDUGU ONESMO OLENGURUMWA NA NDUGU BARAKA JOHN MRATIBU WA MTANDAO WA WANAFUNZI TANZANIA (TSNP) WAKIWA KATIKA SHUGHULI HALALI ZA UTETEZI.

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) wenye wanachama zaidi ya 130, unalaani vikali kitendo cha kukamatwa, kwa Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao Ndugu Onesmo Ole Ngurumwa akiwa katika majukumu halali ya utetezi.

Ndugu Onesmo amekamatwa na Polisi leo tarehe 03/06/ 2017 akienda kuhudhuria Kongamano la uzinduzi wa kitabu cha SAUTI YA WATETEZI WA HAKI VYUONI kilichoandikwa na Ndugu Alphonce Lusako ambaye ni Katibu mkuu Taifa wa Asasi ya Mtandao wa Wanafunzi Tanzania(TSNP). Pamoja na Mratibu bwana Ole Ngurumwa, Mwratibu  wa Mtandao wa wanafunzi Tanzania (TSNP) ambao ndio waandaaji wa kongamano hilo pia alikamatwa na polisi.  Mara baada ya kufikishwa moja katika kituo cha polisi Magomeni,  Wakili wa Mtandao bwana Jones Sendodo aliomba maelezo kuhusu kukamatwa kwa mratibu na baadhi ya waandaaji ila alijibiwa kuwa maelekezo toka kwa wakubwa yanasubiriwa.

Awali, uzinduzi wa kitabu cha SAUTI YA WATETEZI VYUONI ulipaswa kufanyika katika ukumbi wa Tume ya Sayansi na Teknolojia na taratibu zote za kimkataba zilikwisha kufanyika. Ni jana tu ambapo waandaaji wa kongamano hilo walitaarifiwa kuwa hawawezi tena kupewa ukumbi. Hakuna sababu zilizotajwa kuhusiana na uamuzi huo.

 Waandaaji kwa kushirikiana na Mtandao waliweza kuandaa ukumbi mwingine kwa ajili ya kongamano hilo, na ndipo leo asubuhi askari Polisi walifika katika ukumbi wa Ubungo plaza na kuzuia kongamano lisifanyike huku wakiwakamata waandaaji pamoja na Mratibu bwana Onesmo.

Hivi karibuni kumekuwepo na kukamatwa, kushitakiwa, upotevu na vitisho vinavyotolewa dhidi ya watetezi wa haki za binadamu nchini Tanzania. Watetezi wa haki za binadamu wamesajiliwa  na wanafanya kazi kihalali nchini  kama sehemu muhimu ya mabadiliko katika jamii.

 Katika jamii yenye uhuru wa kujieleza na kukusanyika, watetezi hawa wa haki za binadamu wana jukumu kubwa zaidi katika ukombozi wa jamii kupitia utoaji wa mawazo na maoni yao kupitia maandishi.

 Kwa mfano Nchini Tanzania Katika harakati za kupambana na ubepari nchini na kuhimiza ujamaa Mwalimu Nyerere aliweza kuandika vitabu mbalimbali juu ya umuhimu wa ujamaa na kujitegemea.

Ikumbukwe pia ya kuwa, uhuru wa kukutana na kushirikiana na watu wengine imetambuliwa kikatiba katika ibara ya 20(1)  kwamba Kila mtu anastahili kuwa huru, bila ya kuathiri sheria za nchi, kukutana na watu wengine kwa hiari yake na kwa amani, kuchanganyika na kushirikiana na watu wengine. Pia ibara ya 18 ya katiba hiyo imeeleza haki ya  kujieleza na kutoa maoni  ni haki ya binadamu inayolindwa kikatiba.

Wito wetu
Ndugu Onesmo na Bwana Baraka waachiwe huru mara moja na kuruhusiwa kuendelea na shughuli iliyokuwa imeandaliwa kihalali bila kuvunja sheria yeyote ya nchi.

Vyombo vya usalama Tanzania hasa Polisi wahakikishe wanatenda haki na kuwa vihakikishe vinasimamia uhuru wa raia na usalama wake kwa kuwa jukumu lao kubwa ni  kuwalinda raia na mali zao na si kutumika vinginevyo.

AZAKI, vyombo vya habari na umma wa watanzania kwa ujumla wanapaswa kuwa mstari wa mbele kukemea vitendo vyovyote ambavyo vinalenga kuzuia uhuru wa kikatiba wa kukusanyika kihalali na kutoa maoni nchini Tanzania.

Watetezi wa haki za binadamu tuungane na kupaza sauti kwa pamoja juu hali ya kukandamiza uhuru na shughuli halali za watetezi unavyozidi kushika kasi katika nchi yetu.

Imetolewa leo tarehe 03/6/2017 na;
Wanachama wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania.

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE