Zipo namna tofauti za kusherehekea sikukuu hii
kulingana na sehemu watu walipo.
Jumia
Travel ingependa kukushirikisha mambo yafuatayo ambayo yanaweza kuifanya
sikukuu hii kuwa ya tofauti na kipekee tofauti na unavyosherehekea kila
mwaka.
Fanya
maandalizi pamoja na familia. Katika kuhakikisha kwamba kila mtu
anafurahia sikukuu basi ni vema ukawashirikisha kwenye maandalizi yake.
Kama baba au mama wa familia na una watoto au ndugu unaishi nao litakuwa
ni jambo zuri kama mtafanya hata kikao kidogo na kujadili. Kwa mfano,
shughuli zote zitakazofanyika kipindi cha sikukuu, chakula
kitakachopikwa, vinywaji, zawadi, wapi kwa kusherehekea, wageni gani wa
kuwaalika, kupamba nyumba nakadhalika. Hii itasaidia siku hiyo ikifika
kila mtu anafurahia na sio kufanya mambo ambayo yatakufurahisha wewe tu
kuwaacha baadhi ya wengine kunung’unika.
Sherehekea
pamoja na familia na majirani. Mara nyingi sikukuu hupendeza pale
zinaposherehekewa kwa pamoja na ndugu na jamaa. Haijalishi familia
uliyonayo ina ukubwa gani, kujumuika kwa pamoja kunaleta furaha na
muunganiko zaidi miongoni mwa watu. Pia, hata kama una familia ndogo ni
vema ukawashirikisha majirani zako. Unaweza ukapika chakula cha kutosha
na ukaamua kuwaalika au kuwagawia lengo ni kuifanya iwe na shamrashamra
zaidi.
Sherekea
pamoja na watu wenye mahitaji maalum. Sio kila mtu huwa anapata fursa au
kuwa na uwezo wa kusherehekea sikukuu. Na kwa sababu sikukuu ya Eid
al-Fitr husherehekewa kwa siku mbili mpaka tatu (kwa sehemu zingine),
unaweza ukapanga kwamba sikukuu ya moja au mbili ukasherehekea na
familia yako na nyingine ukajumuika pamoja na watu wenye mahitaji
maalumu kama vile watoto wa mitaani, watoto wa mitaani, wagonjwa
mahospitalini, wazee, wafungwa na wengineo.
Wasimulie
watoto kuhusu maisha ya Mtume na namna waislamu wa wakati walivyokuwa
wakisherehekea sikukuu ya Eid-al-Fitr. Sio siku zote watoto
wakishamaliza kupata chakula cha pamoja na familia wakaenda kutembea.
Unaweza kuitumia siku hiyo kwa muda mchache tu ukawakusanya watoto na
kuwasomea hadithi za Mtume Mohammad na namna waislamu wa kipindi hiko
walikuwa wanasherehekea vipi sikukuu hii. Hii itawafanya si tu
kufurahia kwa kuwaongezea maarifa lakini pia kuelewa ni nini maana zaidi
ya siku hii.
Safiri
pamoja na familia. Unaweza ukaamua kusherehekea sikukuu hii kwa kusafiri
mahali tofauti na nyumbani. Mnaweza kutumia gari binafsi kama usafiri,
mkawa mnapumzika kwenye vituo kadhaa kwa ajili ya chakula na kuswali
mpaka mkafika mahali muendapo.
Toa
zawadi kwa ndugu, jamaa na marafiki. Kipindi cha Ramadhan mbali tu na
kuwa ni kipindi cha kufanya toba na kumuomba Mwenyezi Mungu kukupunguzia
dhambi zako lakini pia kutoa zawadi kunaweza kuwa ni njia mojawapo ya
kukuongezea thawabu. Kutoa zawadi ni jambo jema kumfanyia mtu hususani
unapolifanya kwa moyo mkunjufu. Basi kama utakuwa na uwezo unaweza
kununua zawadi kadhaa na kuwapatia ndugu na majirani zako.
Badili
muonekano wa nyumba yako. Itapendeza kama siku ya sikukuu mtaisherehekea
kwenye nyumba yenye muonekano tofauti. Unaweza kufanya hivi kwa
kushirikiana na familia yako ili kupata mwonekano utakaovutia. Mambo
yanayoweza kubadili mwonekano wa zamani ni kama vile kupaka rangi mpya,
kubadili samani za ndani, kununua mapambo, kufanya usafi au hata
mpangilio wa vitu ndani ya nyumba.
Valia
mavazi nadhifu. Tumezoea kwamba linapokuja suala la kuvaa nguo mpya siku
za sikukuu huwa ni watoto pekee wanaopenda kufanya hivyo. Kwenye
familia nyingi imekuwa ni kawaida wazazi kuweka kipaumbele kwa
kuwanunulia watoto nguo mpya. Kutokana na desturi hiyo kuzoeleka
miongoni mwa watu wengi, imewafanya watu wazima kupuuzia kuvaa nguo mpya
kipindi cha sikukuu. Hiyo ni dhana na mawazo ya watu tu na wala
isikufanye ujisikie vibaya kuvaa nguo mpya siku ya sikukuu. Unastahili
kuutendea vema mwili wako kwa kuuvika na mavazi mapya na nadhifu siku
hiyo, kama una uwezo lakini. 

Dhumuni
la kukupatia dondoo hizi ni kuifanya sikukuu hiyo iwe na upekee tofauti
na unavyosherehekea kila mwaka. Jaribu kufanya baadhi ya mambo hayo na
utagundua utofauti mkubwa. Sio lazima ufanye yote yaliyoorodheshwa
kwenye makala haya, machache tu yanatosha. Tofauti na hapo, Jumia Travel
ingependa kukutakia maandalizi na mapumziko mema ya sikukuu ya Eid
al-Fitr!
0 comments:
Post a Comment
AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE