June 22, 2017

MTANDAO UNAOTAJWA KUZALISHA WAUAJI WA KIBITI NA IKWIRIRI


TAA-2
Na Jonas Kamaleki- MAELEZO
Zaidi  ya vijana  2340 wenye  umri wa miaka kati ya 16 na 37 wameamua kujiondoa kwenye mtandao  wa mazoezi ya kigaidi  na kujisalimisha  ili kuishi maisha ya amani na maadili mema baada ya kukutana na ushauri wa  Jopo laViongozi wa Kamati ya  kitaifa   ya Maadili ,Amani na Haki za  Binadamu kwa jamii ya  dini zote nchini.
Hayo yalisemwa leo  na Mwenyekiti wa Kamati ya  kitaifa   ya Maadili ,Amani na Haki za  Binadamu kwa jamii ya  dini zote nchini, Askofu William Mwamalanga katika mahojiano maalum na mwandishi wa habari hii jijini Dar es Salaam.
 Kwa mujibu wa Askofu Mwamalanga, vijana hao kutoka  vijiji  mbalimbali vya vya  huko Ikwiriri na Kibiti wamesema walitumbukia kwenye uhalifu huo  mwaka 2011 ambapo baadhi ya  viongozi wa dini  moja kutoka jijini Dar e Salaam walipita kuhamasisha vijana kujiunga  nao  na kuachana na DINI ya kiislamu na kujiunga na mafundisho yanayotofautina  na uislamu ya kuua  viongozi wote na  wananchi ambao  walikata kuliunga mkono.
 Imeelezwa kuwa asili ya kundi hilo  ni mafundisho yanayopinga uislamu na limejikita kwenye wilaya za Kinondoni, Temeke, Mbagala na Mikoa ya Tanga Kagera, Morogoro, Dodoma, Lindi, Mtwara, Pemba, Tabora na Pwani. Kundi hilo  limekuwa  likifundisha vijana kujiunga na ugaidi kwa muda mrefu katika maeneo ya Songea, Tunduru, Ikwiriri, Kibiti,  Dar es Salaam, Mwanza na Dodoma bila hatua zozote za kuzuia, aliongeza Askofu Mwamalanga.
“Vijana hao wamekiri  kuachana na mtandao wa kundi hilo huku wakiwaomba  viongozi wa dini ya kiislamu nchini kukemea mafundisho ya kareti na ugadi kwenye baadhi ya misikiti”, alisema Askofu Mwamalanga.
Aidha, Kiongozi huyo wa Dini alisema kuwa kundi hilo lilikuwa linawahimiza   wanafunzi wa shule za msingi na sekondari  wakiume na wasichana   kuacha  masomo  na kuolewa na wavulana kujiunga na kundi hilo na wengine kupelekwa  nje ya nchi kujiunga na shule za  ugaidi   hii ndiyo siri ya vijana wengi kwenye mikoa hii kujiunga na mtandao huo na wengi kutoendelea na masomo.   
Askofu Mwamalanga aliongeza kuwa vijana hao  wamempongeza Mkuu mpya wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro kwa uthubutu wake na waledi wa wa kuifanya Rufiji na Ikwiriri kuwa eneo la amani hii itasaidia hata wanafunzi kusoma kwa amani  na hasa wasichana wengi ambao  wamepewa uja uzito na kutelekezwa  na wengine  wapo jijini Dar es Salaam ambako wanaishi maisha duni kwa hofu ya kuuliwa .
 “Ninalaani vikali  mafundisho  ya uhalifu kufundishwa kwenye nyumba za ibada na nawahimiza vijana  hao kuwa askari wa siri wa kufichua  waharifu wote  na kuwataka wale waliojificha misituni kujisalimisha kama wenzao”,alisisitiza Askofu Mwamalanga .
Aidha, Askofu huyo amewataka watendaji wa Serikali ngazi ya Halmashauri  wakiwemo wakuu wa wilaya  kuwapatia vijana ardhi  na kuwakamata  mara moja  watu wanaoeneza elimu ya chuki kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ni Twahuti jina linalomaanisha kuwa  Serikali hii siyo  ya dola la kiislamu.
 Kwa upande wao baadhi ya wazee 140  walioshiriki kwenye maombi na dua maalumu ya kuombea  kukomesha mauaji hayo  wamekiri kuwa   mauaji hayo  hayana uhusiano wowote na dini ya kiislamu wala siasa bali ni uharifu  kama uharifu mwingine .    
Hivi karibuni Serikali imeimarisha ulinzi na usalama katika maeneo ya Ikwiriri na Rufiji pia Kibiti ili kudhibiti mauaji yaliyokuwa yakijitokeza katika maeneo hayo. Kwa sasa hali imetulia na amani inaanza kurejea.

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE