June 12, 2017

CHENGE NA MAWAZIRI KADHAA KUPANDISHWA KIZIMBANI

Rais John Magufuli ameyakubali mapendekezo yote yaliyotolewa na Kamati ya Pili ya Uchunguzi wa Makinikia, na kuanza kutoa agizo kwa vyombo vya dola kuwachukulia hatua ikiwemo kuwahoji wahusika waliotajwa kwenye ripoti hiyo wanaodaiwa kusaini mikataba ya madini isiyo na masilahi kwa Taifa .
Magufuli ametoa agizo hilo leo Juni 12, 2017 baada ya kupokea ripoti ya matokeo ya uchunguzi wa kamati hiyo iliyowasilishwa na Mwenyekiti wake, Nehemiah Osoro, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
“Kigoda ametangulia, waliobaki muwahoji je hizo hela zilizowafanya hivi zimewapeleka kwenye uwekezaji ili tujuwe na tuzichukue tusaidie masikini. Lazima tuchukue maamuzi magumu haijalishi yanamgusa nani kama rafiki yao au nani,” amesema Magufuli
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, inawataja mawaziri wa nishati na madini waliopita, makamishna wa madini na washauri wa masuala ya sheria wa serikali za awamu zilizopita ambao wanadaiwa kusaini mikataba tata pamoja na kuongeza muda wa leseni na maeneo ya uchimbaji madini kinyume cha sheria bila kuzingatia masilahi ya taifa.
Jina la waziri wa kwanza lililotajwa kwenye ripoti hiyo, ni pamoja na Marehemu Abdallah Kigoda ambaye anadaiwa kuufanyia marekebisho mkataba wa madini wa mgodi wa Bulyanhulu, yaliyoipelekea serikali kupoteza hisa zake asilimia 15, pamoja na mkataba wa Geita Gold Mime LTD ambao unadaiwa kuotoa nafuu mbalimbali za kodi jambo linalokosesha serikali.
Hata hivyo, baada ya serikali kulipwa dola milioni 5 za mauzo ya hisa zake kwa mgodi wa Bulyanhulu, ilitakiwa kulipwa dola  laki moja kila mwaka kufuatia makubaliano iliyoingia na mgodi huo, lakini kwa mujibu wa ripoti hiyo, inaeleza kuwa hakuna sehemu inayoonyesha serikali ililipwa fedha hizo jambo linaloashiria serikali kupoteza haki ya kumiliki hisa na kutopata gawiwo.
Majina mengine yaliyotajwa kwenye ripoti hiyo ni, Nazir Karamagi na Daniel Yona ambapo wakati walipokuwa mawaziri wa nishati na madini kwa nyakati tofauti walisaini mikataba miwili ya kampuni ya uchimbaji madini ya Tangier, ambapo wa kwanza ulisainiwa na Yona mwaka 2003 na kufanyiwa marekebisho na Karamagi mwaka 2007, katika mikataba hiyo serikali haikuwa na hisa pia ilitoa naafu kubwa ya kodi  na nafuu ya 15% ya mtaji kwa kampuni hiyo na kuikosesha serikali mapato.
Aidha, ripoti hiyo iliwataja mawaziri waliopita, William Ngeleja na Profesa Sospeter Muhongo kuwa waliongeza muda wa leseni na maeneo ya uchimbaji madini kinyume cha sheria bila kuzingatia masilahi ya taifa, kampuni za uchimbaji madini ikiwemo ya NorthMara.
Katika hatua nyingine, ripoti hiyo haikumuacha aliyekuwa mshauri wa serikali katika masuala ya sheria, Andrew Chenge, pamoja na makamishna wa madini waliotoa leseni zenye utata ikiwemo Dalalai Kafumu, Paul Masanja na Kaimu Kamishna Madini Mhandisi Ally Samaje.
Kufuatia mikataba ya madini kuwa na utata, Dkt. Magufuli amemuomba Spika wa Bunge Job Ndugai haraka iwezekanavyo kuruhusu Bunge kuirejesha bungeni ili ipitiwe upya na kufanyiwa marekebisho.
“Kutokana na haya, sababu sheria zetu ni za ovyo nitaomba wataalamu wa sheria kupitia Wizara ya Sheria ya Profesa kabudi, mkawe na timu ya wanasheria waaminifu pitieni sheria zote. Na nitamuomba spika tuzipekeke bungeni hata tukiongeza kipindi wakajadili sheria zote wakazipitie hata kwa kukaa wiki nzima, pitieni kifungu kwa kifungu. Haiwezekani dhahabu ni yako anakuchimbia unapata 4 asilimia 96 inaenda kwao hata unachostahili hupati,” amesema.
Na Regina Mkonde

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE