May 10, 2017

WAKULIMA NA WALANGUZI WA MAZAO KWA LUMBESA KUCHUKULIWA HATUA KALI

Mkuu  wa  wilaya ya  Kilolo mkoani Iringa Asia Abdalah  akiwahutubia wananchi  wa  kijiji cha Irindi na Magana kata ya Mahenge
Mazao yakiwa  katika vipimo  vya Lumbesa ,vipimo  ambavyo ni batili

Wananchi kijiji  cha Irindi na magana  Kilolo  wakiwa katika  mkutano  wa  Dc  Kilolo
Mkuu  wa  wilaya ya  Kilolo  akiwahutubia  wananchi  wa  Magana na  Irindi wa pili kulia ni meneja wa vipimo  mkoa wa Iringa  Zainabu I. Kafungo
Wananchi  wakisoma  vipeperushi  vya vipimo  sahihi  vya mazao

Dc Asai akiwasikiliza  wananchi
Na  MatukiodaimaBlog
WALANGUZI wa  mazao    ya  wakulima  na wakulima watakao shindwa kufuata  sheria ya vipimo sahihi na kutumia vipimo batili  maarufu  kwa jina la lumbesa kuuziana mazao   kuchukuliwa hatua kali ya kutozwa faini ama kufikishwa mahakamani  .  
 
Akiwahutubia  wananchi  wa kijiji  cha Irindi  na Magana kata  ya  Mahenge wilayani  Kilolo  mkuu  wa   wilaya  ya  Kilolo  Asia Abdala leo  wakati  wa  ziara  yake  ya  kukagua miundo  mbinu ya elimu  na uhamasishaji  wananchi  kushiriki  shughuli  za uzalishaji mali ,mkuu  huyo  alisema  kuwa  iwapo wananchi  hao  watakubali  kuuza mazao yao kwa  ujazo batili hatua  kali  itachukuliwa kwa  muuzaji na mununuzi .

Hivyo  aliwataka   viongozi  wa  serikali  za  vijiji  na kata  zote kuwasaidia  wakulima  kuuza mazao yao  kwa  faida  na  kuwabana  walanguzi  wa mazao  wanaowapunja  wakulima  hao kwa  kununua mazao kwa  vipimo ambavyo vinawanyonya  wakulima.

 Mkuu   huyo  wa  wilaya  alisema  kuwa wilaya   hiyo  imejaliwa  kwa  kuwa na  ardhi  nzuri  inayokubali mazao ya  kila aina  kama  vitunguu,mahindi ,maharage ,njegere  ,nyanya  na  mazao  mengine  mengi   hivyo jukumu  kubwa  la  mabwana  shamba ni  kuwasimamia  wakulima hao dhidi ya  walanguzi  wa mazao  yao na  kuona  kila  mkulima  ananufaika na kilimo na  sio kuishia  kuwanufaisha  wafanyabiashara .

 Alisema  kuwa chini ya   serikali  ya Rais  Dkt  John Magufuli  serikali inayowajali wananchi  wake   wote  pasipo  kuwabagua asingependa  kuona Kilolo wafanyabiashara   wakiwanyonya   wakulima  na  kuwa kama  walizoea kipindi  kabla ya  Dkt  Magufuli  hajaingia Ikulu basi  ni  vema  watambue  kuwa mwisho  wa  mkulima  Kilolo  kumnufaisha  mfanyabiashara  ama  dalali  wa  mazao mwisho  wake   ulikuwa ni mwaka 2015 ila  serikali  hii  ya awamu ya  tano ipo  kwa  ajili ya  watanzania  wote .

 Hivyo  aliwataka   wakulima wilaya   ya  Kilolo    kuuza mazao  yao  kwa  utaratibu na  kwa   kuzingatia   vipimo sahihi  vinavyotambuliwa na serikali na  sio  vinginevyo .

Meneja  wa  vipimo  mkoa  wa  Iringa  Zainabu Kafungo aliwaeleza  wananchi  hao kuwa  kutokana na elimu  mbali mbali ambayo  imeendelea  kutolewa na  ofisi  yake na  viongozi wa  serikali  mkoani Iringa  kasi ya  wananchi  kuuza mazao yao  kwa  vipimo visivyo   sahihi  imeendelea   kupungua  na  hata   wafanyabiashara  hasa  madalali  wa  mazao  wameendelea  kuogopa  kuwaibia  wakulima .

Alisema  kuwa  ofisi  yake  ni  wakala  wa serikali inayosimamia vipimo vyote  nchini Tanzania  bara lengo ni  kuhakikisha kunakuwepo na  usahihi  wa bidhaa  zinazofungashwa  kwa ajili ya  kumlinda  mlaji asipunjwe  kutokana  na  vipimo apate  huduma  kulingana na pesa  yake .

 Pia  kumlinda  mlaji kwa  kufanya kaguzi  za bidhaa zilizofungashwa  mashambani toka  kwa  wakulima kuwa  zinakuwa  kwenye vipimo  sahihi  na  sio  lumbesa 

Aidha  alisema ufungashaji batili ni ufungashaji kinyume na sheria ya  vipimo  sura  340  mapitio ya mwaka 2002 pamoja na kanuni zake  japo  alisema kumekuwa na changamoto kwa baadhi ya  viongozi maeneo kuhamasisha wananchi kutotii sheria  na  baadhi ya taasisi kuandaa kanuni  zao bila  kurejea sheria  ya  vipimo .

Sheria  inataka kiasi  cha ufungashaji  kwa  uwele ,karanga ,ufuta,wimbi ,mtama ,maharage  na jamii  yake   kilo 90 tu  wakati alizeti  kilo 40,mkaa kilo 30, viazi ,mazao mengine ambayo hayajatajwa ni kilo 100,korosho  kilo 80 na  kuwa faini  mbali  mbali  zipo  wazi kwa  wakiukwaji wa  sheria kwa  Yule  atakayekiuka sheria ya  vipimo hufikishwa mahakamani.

Alisema  kuwa mkulima  wa  wilaya ya  Kilolo ,Mufindi au Iringa wote  wanapaswa  kuzingatia sheria    hiyo  ya vipimo na  kuwa suala la Lumbesa  limepigwa marufuku nchi  nzima  hivyo kwa  mkoa  wa Iringa suala  hilo wanalisimamia kwa  nguvu  zote .


Kwa  upande  wao  wnanchi  hao  wakizungumza katika  mkutano huo mbali ya  kupongeza kwa  mikakati  mizuri ya  serikali  kupitia wakala  wa  vipimo  kuendelea  kuwatetea  wakulima bado  waliomba  serikali  kuwasaidia kupata soko la uhakika la mazao yao pia  kushusha  bei ya  pembejeo  za  kilimo alisema Yohana Sambuli kuwa  kilio  chao kikubwa ni ukosekanaji wa  masoko na pembejeo kuwabagua wakulima hao .
 
  

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE