May 29, 2017

VIJANA WA AFRIKA WAKUMBUKWA NA G7

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres (wa kwanza kushoto) akizungumza kwenye mkutano wa wakuu wa G7 huko Italia. (Picha:Miguel Gra├ža/UN )
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amezitaka kundi la nchi saba G7 zilizo mbele kiuchumi zaidi duniani kuwekeza katika vijana wa Afrika.
Amesema hiyo hii leo huko Taormina, Sicily nchini Italia wakati akihutubia kikao cha G7 kilichokutana mahususi ili kuangala masuala ya ubunifu na maendeleo endelevu kwa lengo la kuimarisha uhusiano na Afrika.
Amesema kasi ya ongezeko la vijana barani Afrika ni kubwa kuliko kokote kule duniani na hivyo..
(Sauti ya Guterres) 
"Faida tunaweza kupata kupitia uwekezaji kwenye elimu hasa ya sayansi na teknolojia. Lakini elimu ya msingi haitoshi pekee, watu wanahitaji stadi ambazo zinaendana na mahitaji ya sasa na ya baadaye kwenye soko la ajira."
Amesema pamoja na kuwekeza katika vijana Afrika, G7 zisaidie kueneza teknolojia za kisasa Afrika, ziwekeze kwenye sekta fanisi, zisaidie nchi za Afrika kufikia umoja wa kikanda, bila kusahau uwezeshaji wanawake na wasichana na kusaidia Afrika kuondokana na  ukwepaji wa kodi.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres (katikati mstari wa nyuma) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Afrika na wale wa G7. (picha:Stephane Dujarric/UN)
Kuhusu kile kinachoitwa mapinduzi ya nne ya viwanda yanayotarajiwa kukumba dunia, Bwana Guterres amesema suala hilo litaleta mabadiliko makubwa kwenye soko la ajira duniani kwa hiyo..
(Sauti ya Guterres)
"Afrika inaweza kuathirika na mabadiliko haya. Tunapaswa kufanya kila tuwezalo kuhakikisha Afrika inaweza kuyahimili. Kufanya hivyo kunahitaji kuimarishwa kwa uwekezaji katika teknolojia na elimu stahiki na kujenga uwezo katika sekta zote."
 Amepongeza G7 kwa kuangazia Afrika katika wakati wa sasa ambao amesema ni  muhimu na pia kwa kuweka kipaumbele katika maendeleo jumuishi na yanayochochea ukuaji kupitia ubunifu.
 Nchi za G7 ni Canada, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Japan, Uingereza na Marekani ambapo pia Muungano wa Ulaya nao unawakilishwa kwenye jumuiko hilo.

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE