May 3, 2017

UBAKAJI,KUMINYWA UHURU WA KUONGEA NA KUJICHUKULIA SHERIA MKONONI VILIITESA TANZANIA 2016

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) imezindua ripoti ya Haki za Binadamu ya mwaka 2016 ambapo utafiti wake ulihusisha wilaya za mikoa kumi ikiwemo Iringa, Mbeya, Rukwa Tabora, Kilimajaro, Kagera na Kigoma.
Akizungumza baada ya uzinduzi , leo Mei 3,2017 jijini Dar es Salaam, mwakilishi wa watafiti na mwandishi wa ripoti hiyo kutoka LHRC, Paul Mikongoti amesema bado kuna ukiukwaji mkubwa wa haki za kiraia, kisiasa, makundi maalumu pamoja na changamoto ya upatikanaji wa huduma bora za kijamii hasa maeneo ya vijijini.
Akiifafanua ripoti hiyo, Mikongoti ameeleza kuwa tangu mwezi Januari hadi Disemba 2016 kumekuwa na ukiukwaji wa haki za kisiasa kufuatia ukatazwaji wa mikutano ya hadhara ya kisiasa pamoja na watu kukusanyika, kitendo kinacho ingilia na kuathiri utendaji wa shughuli za vyama vya siasa.
Pamoja na Msajili wa Vyama vya Siasa kuingilia majukumu ya vyama vya siasa, na migogoro ya kisiasa iliyopelekea kucheleweshwa kwa chaguzi za mameya katika halmashauri za majiji ambayo vyama vya upinzani vilikuwa na nguvu ikiwemo Kilombero, Dar es Salaam na Tanga.
“Tangu serikali hii ilipoingia madarakani 2015 kumekuwa na makatazo ya utendaji wa shughuli za kisiasa, pia msajili wa vyama vya siasa aliungana na serikali kuzuia shughuli za vyama vya siasa kinyume na sheria na katiba,” amesema.
Kufutia ukiukwaji huo wa haki za kisiasa, Mgeni rasmi katika uzinduzi wa ripoti hiyo, Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufaa, Eusebia Munuo ameshauri serikali  kutozuia utendaji wa shughuli za vyama vya siasa ikiwemo kutozuia mikutano ya hadhara.
“Hili eneo linahitaji kuangaliwa sababu awali watu walikuwa wanakutana na kufanya mikutano ya hadhara, hatutegemei tena kuona mabomu ya machozi yakitawanya waliokusanyika, bali tunahitaji kuona watu wa usalama wanalinda watu. Wasisahau kwamba dhana kubwa ni utawala bora ambao hauletwi kwa mabomu bali ni kwa kuzingatia sheria na raia watafuata sheria pindi waonapo viongozi wakifuata sheria,” amesema Jaji Munuo.
Kwa upande wa haki za kiraia, Mikongoti amesema bado kuna ongezeko la matukio ya watu wanaojichukulia sheria mkononi kuua raia ambapo matukio 705 yaliripotiwa, ukiukwaji wa uhuru wa kujieleza ukilinganisha na ilivyokuwa mwaka 2015 baada ya kuanza kutumika kwa sheria ya makosa ya mtandao ya mwaka 2015 na ya huduma ya vyombo vya habari 2016.
Hata hivyo, ripoti hiyo inaonyesha kupungua kwa vifo vitokanavyo na ajali, mauaji ya albino, na yanayotokana na imani za kishirikina hasa kwa wakongwe ambapo kwa mwaka 2016 watu 394 waliuawa ukilinganisha na 2015 ambapo watu 425 waliuawa, huku mkoa wa Tabora ukiendelea kuongoza kwa mauaji hayo ukifuatiwa na Mbeya na Shinyanga.
Kuhusu haki za makundi maalumu, ameeleza bado kuna changamoto ya ongezeko la watoto kubakwa na kulawitiwa ambapo kesi 2571 ziliripotiwa huku Dar es Salaam ikiongoza kwa kuwa na matukio 345 ikifuatiwa na Mbeya 177 na Morogoro 160. Pia katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Dar es Salaam kumeripptiwa matukio ya watoto kulawitiwa wakiwa shuleni.
Hali kadhalika, ongezeko la ndoa na mimba za utotoni ambapo Tanzania imekuwa nchi ya kwanza kwa ukanda wa Afrika Mashariki na ya tatu barani Afrika kwa kuwa na ongezeko la mimba za utotoni ambapo watoto 300 kutoka shule za msingi na sekondari hasa kwenye mikoa ya Dodoma, Kilimanjari na Mara walipata mimba za utotoni.
“Kwa upande wa haki za makundi maalumu, wanawake wamekuwa waathirika wakubwa wa ukatili wa kijinsia ikiwemo ubakwaji ambapo kesi zaidi ya 2800 ziliripotiwa mwezi Juni 2016, huku mkoa ya Dar es Salaam ukiongoza kwa kuwa na matukio 1030 kutoka 972 mwaka 2015 ukifuatiwa na Kilimanjaro ambayo matukio yaliongezeka kutoka 92 mwaka 2015 hadi 151 kipindi kama hicho 2016,” amesema.
Kwa upande wa upatikanaji wa huduma bora za Kijamii, Mikongoti amesema bado kuna changamoto ya upatikanaji wa dawa, upungufu wa wataalamu wa afya na ongezeko la wanafunzi kufuatia sera ya elimu bila malipo ambalo limepelekea upungufu wa madarasa na waalimu.

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE