May 31, 2017

TRUMP ATUPIWA SHUTUMA ZA KUGAWA NAMBA YAKE YA SIMU HOVYO

Rais wa Marekani Donald Trump amekuwa akitoa namba yake ya simu ya mkononi kwa viongozi mbalimbali wa dunia akiwaambia kwamba wanaweza kumpigia moja kwa moja.
Lakini hatua hiyo isiyo ya kawaida inayovunja itifaki ya kidiplomasia imezusha wasiwasi kuhusu usalama na usiri wa mawasiliano ya Amiri jeshi mkuu wa Marekani.
Trump amewataka viongozi wa Canada na Mexico kumpigia simu moja kwa moja kupitia simu yake ya mkononi, kwa mujibu wa maafisa wa Marekani wa zamani na wa sasa walio na uelewa na tabia hiyo. Kati ya viongozi hao wawili, ni waziri mkuu wa Canada Justin Trudeau ambaye ametumia mwanya huo kwa mujibu wa maafisa.
Trump pia alibadilishana namba na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron wakati viongozi hao walipozungumza mara moja kufuatia ushindi wa Macron mapema mwezi huu, hayo ni kwa mujibu wa afisa wa Ufaransa ambaye hakutaka kueleza ikiwa Macron alikuwa na dhamira ya kuitumia namba ya simu.
Belgien Donald Trump und Emmanuel Macron auf dem NATO Treffen in Brüssel (Getty Images/AFP/M. Ngan) Donald Trump akiwa na Emmanuel Macron
Dhana ya viongozi wa dunia kuwasiliana kupitia simu inaweza kuonekana kama jambo la kawaida katika ulimwengu wa sasa, wa simu za mkononi. Lakini katika uwanja wa kidiplomasia, ambako mawasiliano ya simu kati ya viongozi ni masuala yanayofuata taratibu, huo ni uvunjaji mwingine wa itifaki kwa rais ambaye ameelezea kukosa imani na njia rasmi za mawasiliano.
Utaratibu na nidhamu ya kufuata itifaki za kidiplomasia limekuwa ni jambo gumu kwa Trump, ambaye hata kabla ya kuingia madarakani alikuwa anapatikana kwa urahisi kwa simu yake na kujiona kuwa mtu aliye huru kutofuata taratibu za kawaida na mtu aliye na ujuzi wa kufikia makubaliano ya biashara.
Kwa kawaida marais huruhusiwa kupiga simu katika laini zilizo salama, hiyo inajumuisha vyumba vichache ndani ya Ikulu ya White House, ofisini kwa rais au katika gari yake ya Limousine. Wataalamu wa usalama wa taifa wanasema, hata kama Trump atatumia simu ya mkononi aliyokabidhiwa na serikali, bado mawasiliano yake yapo hatarini kunaswa na serikali za nje.
Mmoja wa washauri wa zamani wa wizara ya ulinzi ya Marekani na baraza la taifa la usalama Derek Chollet anasema , rais "habebi simu yake ya mkononi" kwa sababu ikiwa mtu yoyote atakuwa anampeleleza ni dhahiri kwamba chochote atakachozungumza kitakuwa kikisikilizwa na watu wengine.
G7 Treffen Sizilien Donald Trump, Shinzo Abe, Justin Trudeau, Jean-Claude Junker, Angela Merkel, Emmanuel Macron (picture-alliance/AP Photo/E. Vucci) Donald Trump akiwa na viongozi wenzake wa G7
Tahadhari hiyo pia inatolewa hata wakati rais anawasiliana na washirika wake. Kama Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alivyojifunza mwaka 2013, wakati siri za Marekani zilipovujishwa na Edward Snowden na kuonyesha kwamba Marekani ilikuwa ikufuatilia mawasiliano yake, kwahiyo mahusiano mazuri hayawezi kuzuia mtu kupelelezwa.
Lakini hatua hiyo ya Trump inamfanya kuonekana mnafiki. Katika kipindi chote cha kampeni za uchaguzi mwaka jana, Trump alimkosoa hasimu wake wa Democratic Hillary Clinton kwa kutumia barua pepe wakati akiwa waziri wa mambo ya nje, na kusisitiza kwamba hafai kupewa taarifa za siri kwasababu ataziweka katika mazingira hatarishi ya kudakwa na maadui wa kigeni.
Mawasiliano ya simu ya rais na viongozi wenzake wa dunia mara nyingi huhusisha mipango ya mapema. Maafisa wa wizara ya mambo ya nje na baraza la usalama wa taifa wanaandaa pointi za kuzungumza na mara nyingi mawasiliano yasiyo rasmi hujulikana kwa wasaidizi wachache wa rais na kisha baadae hurekodiwa na kuhifadhiwa. Ikulu ya Marekani White House hata hivyo haikueleza ikiwa rais anahifadhi mawasiliano yake yasiyo rasmi na viongozi wa dunia.
Hayo yanajiri wakati mkurugenzi wa kitengo cha  mawasiliano ya Ikulu ya White House Michael Dubke akijiuzulu wakati rais Trump akifikiria kuchunguza kwa makini wafanyakazi wake katikati mwa ongezeko la hatua za uchunguzi wa mawasiliano yake na Urusi wakati wa kampeni.

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE