May 17, 2017

TRL KUAGIZA TRENI ZA DAR ES SALAAM


Kutokana na ongezeko la idadi ya abiria wanaotumia treni za jiji hasa inayoenda Pugu, Kampuni ya Reli Nchini (TRL) imesema ina mpango wa kuagiza treni za ndani ili kuboresha huduma za usafirishaji.
Hayo yameelezwa leo Mei 17, 2017 na Meneja wa Usafirishaji TRL, Iddy Mzugu wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, ambapo ameeleza kuwa, ongezeko hilo limesababisha baadhi ya abiria kuvunja taratibu za usalama za usafiri wa treni ikiwemo kudandia mabehewa baada ya milango kufungwa huku treni ikiwa inatembea.
“Tumefanya utafiti wa soko na kubaini kuna ongezeko kubwa la idadi ya abiria, sasa hivi treni iliyopo ina mabehewa 19 ya muda, hata hivyo ni kinyume cha sheria ya SUMATRA kwa hiyo hatuwezi kuongeza mabehewa mengine. Shirika mpango wake ni kuanza kutumia treni za ndani,kwa hiyo tuko katika hatua za kuziagiza,” amesema
Hata hivyo, amesema TRL kuanzia sasa haitasita kuwachukulia hatua abiria wanaovunja taratibu za usalama za usafiri wa treni za jiji, na kwamba atakayekamatwa kwa kosa hilo, atafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria ikiwemo kupigwa faini au kufungwa jela miezi sita.
“Kilichotokea tunasikitika sana, sababu kuna baadhi ya abiria hudandia kwa nguvu treni na mtu huwezi kumzuia na haturuhusu hilo kufanyika. Sasa tutakachokifanya ili kudhibiti hilo, ni kumpeleka polisi atakayebainika kufanya hivyo na kisha mahakamani ambapo atafungwa jela miezi sita au faini ya shilingi elfu hamsini,” amesema.
Kwa upande wake Inspekta Frank Gadau akizungumza kwa niaba ya  Kamanda wa Kikosi cha Polisi Reli, Simon Chillery, amesema Kamanda Chillery amemuomba Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Ernest Mangu kumuongeza idadi ya polisi kwa kuwa walioko sasa hawatoshi kudhibiti abiria kutokana na wingi wao.
“Askari waliopo hawakidhi idadi ya abiria, Kamanda wa Reli amemuomba IGP kumuongezea idadi ya polisi ili kila kituo kiwe na polisi wa kutosha kwa ajili ya kuwadhibiti abiria ambao hawataki kufuata sheria, kanuni na taratibu za matumizi ya usafiri salama wa treni hasa kwa kuning’inia nje ya mabehewa wakati treni ikitembea,” amesema.

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE