May 23, 2017

MFUMO WA BIMA KUBORESHA KILIMO AFRIKA


Wajumbe kutoka mataifa kadhaa ya Kiafrika wanakutana mjini Kampala katika kongamano la Shirikisho la Bima Afrika kujadili miongoni mwa mambo mengine mfumo wa bima kwa kilimo.
Kampala Konferenz Agrarkultur (DW/L.Emmanuel) Wadau wa sekta za bima na kilimo wamekutana Kampala, Uganda kujadili ufadhili kwa sekta ya kilimo hasa katika nyakati hizi ambapo hali ya hewa imekuwa inazidi kutotabirika.
Zaidi ya wajumbe 1,000 kutoka Afrika pamoja na wadau wengine katika sekta ya bima kutoka mataifa mengine wanajadili masuala mbalimbali kuhusu biashara ya kilimo na bima ili kujitokeza na ufumbuzi wa kushirikisha idadi zaidi ya watu kufahamu manufaa ya bima.
Miongoni mwa sekta wanazolenga kuvutia kuchukua bima ni ile ya kilimo. Ijapokuwa kilimo ndicho uti wa mgongo wa uchumi wa Afrika, wakulima wengi hawawezi kupata mikopo kutoka benki nyingi kwani kilimo ni biashara inayochukuliwa kuwa yenye matatizo makubwa.
Biashara ya mashaka
"Ukizingatia hali ya hewa isiyobashirika kutokana na mabadiliko ya tabianchi, kilimo ni biashara yenye mashaka mengi hivyi si rahisi kushawishi benki kutoa mikopo kwa wakulima ila tu kwa zisizo na mashaka na hatari ya kupata hasara," alisema waziri wa kilimo wa Uganda Vincent Bamulangaki Sempijja.
Kwa mtazamo wa baadhi ya wadau, kutokuwepo kwa fursa za bima katika kilimo ndicho chanzo cha wakulima wengi kupoteza mtaji wao na kuvunjika moyo hasa katika enzi hii ya kasi ya mabadiliko ya tabianchi.
Asha Omar Faki, mratibu  wa mipango katika wizara ya kilimo maliasili, mifugo na uvuvi  Zanzibar chini ya mpango wa kuendeleza sekta ya kilimo na kuimarisha sekta ya mifugo. Anasema mfumo wa bima utawasaidia wakulima kuwa na uhakika kwa kuwa endapo mazao yao yataharibiwa wanaweza kulipwafidia.
Kampala Konferenz Agrarkultur (DW/L.Emmanuel) Baadhi ya washiriki wa kongamano la shirikisho la bima Afrika lililoangazia ufadhili wa sekta ya kilimo, ambalo lilifanyika mjini Kampala Mei 23, 2017.
Kulingana na wataalamu wa masuala ya bima, mataifa kama Uganda yamekosa kunufaika kutokana na mazao yao kama vile ndizi kwenye masoko ya kimataifa kwa sababu wakulima hawafanyi juhudi kuzingatia ubora kukidhi kiwango cha kimataifa.
Licha ya nchi hiyo kuwa yenye eneo kubwa la migomba duniani, inaingiza pato la dola milioni 20 tu kila mwaka kutokana na zao la ndizi ilhali Brazil iliyo na eneo dogo la mashamba ya ndizi inaingiza hadi dola bilioni 3.
Teknolojia kutabiri hali ya hewa na misimu
Wadau katika sekta ya bima wana imani kwamba wanaweza kutumia teknolojia za kisasa kutabiri hali ya hewa na misimu na hivyo kuwa na muundo tayari wa kuwafidia wakulima pale wanapoathirika kutokana na kiangazi au mafuriko.
"Teknolojia za satellite hutusaidia kupima viwango vya mvua na kasi ya upepo kwenye kila eneo la ulimwengu. Hivyo ni fursa kwa bima ya kilimo kushughulikiwa hata mashinani vijijini ambako hakuna kampuni za bima," anasema Bernd Kohn, mkuu wa shirika la Munich Re la nchini Ujerumani.
Uganda ni mojawapo ya mataifa ambayo yamechukua hatua za kuanzisha mfumo wa bima ya kilimo. Hatua hii inalenga kuwahakikishia wakulima kwamba pale wanapochukua bima ya kilimo na kupata hasara basi watafidiwa.

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE