May 10, 2017

MARUFUKU WANAFUNZI KUPIKA CHAKULA SHULENI - DC KILOLO

Mwanafunzi  wa  darasa  la  sita  shule ya msingi Mlowa  kata ya  Mahenge  wilaya  ya  Kilolo mkoa  wa Iringa  aliyefahamika kwa  jina moja la Jane  akiandaa  chakula shuleni hapo
Wanafunzi  wakiwa katika  foleni ya  uji
Mwanafunzi  akifurahia  uji
Mwanafunzi wa  shule ya Msingi Mlowa Kilolo  akiwa darasani  akijisomea  huku akinywa  uji

Na  MatukiodaimaBlog 
KUFUATIA  utaratibu uliowekwa na shule ya Msingi Mlowa  kata ya  Mahenge  wilaya  ya  Kilolo mkoani Iringa kuwatumia  wanafunzi  kujipikia  chakula shuleni hapo ,serikali  wilaya ya Kilolo imepiga marufuku wanafunzi wa shule za msingi wilayani humo kujipikia chakula wakati wa muda wa masomo .

Agizo  hilo  limetolewa na mkuu  wa  wilaya ya  Kilolo  Asia Abdalah jana  wakati akizungumza  na walimu pamoja na kamati ya shule ya msingi Mlowa kata ya Mahenge wakati wa ziara yake ya kukagua miundo mbinu ya shule,alisema kuwa hajapendezwa na utaratibu wa shule hiyo wa kuwaacha wanafunzi kuingia jikoni kujiandalia chakula cha mchana badala ya kujisomea.

Hivyo aliagiza kamati ya shule hiyo na shule nyingine zote wilaya ya Kilolo kutafuta wapishi watakaofanya kazi ya kuwaandalia chakula wanafunzi hao na hatapenda kuona wanafunzi wakiacha masomo na kuingia jikoni kupika chakula .

 " Sijapendezwa hata kidogo kuona wanafunzi wapika chakula badala ya kusoma naagiza kuanzia leo shule zote kutafuta wapishi wa kuwahudumia wanafunzi hao na sitegemei kuona tena wanafunzi wanajipikia chakula....natoa muda hadi jumatatu wiki ijayo iwe mwisho "

 Pamoja na kupiga marufuku wanafunzi kutumika kuandaa chakula iwe muda wa mapumziko ama muda wa masomo bado mkuu huyo wa wilaya alipongeza jitihada mbali mbali zinazofanywa na kamati ya shule hiyo kwa kukamilisha vyumba viwili vya madarasa na kuwaepusha wanafunzi waliokuwa wakisomea chini ya mti kuanza kusomea darasani .

 Alisema kuwa kazi kubwa inayofanywa kamati ya shule hiyo chini ya usimamizi wa afisa mtendaji wa kijiji Murady Nchimbi ni kazi nzuri inayopaswa kupongezwa na kuigwa na watendaji wa vijiji vingine huku akipongeza walimu wa shule hiyo kwa kuifanya shule hiyo kuwa katika orodha ya shule kumi bora kwa matokeo ya darasa la nne .

 Pia mkuu huyo wa wilaya aliahidi kuwachukulia hatua kali wale wote wanaokwamisha maendeleo ndani ya wilaya hiyo na kuwa iwapo kijiji husika kimeweka sheria ndogo ama taratibu ya michango ya maendeleo ni lazima kila mmoja kuwajibika kuchangia na kutaka vyombo vya kisheria pindi vinapotimiza wajibu wake kuzingatia pia sheria ndogo ndogo na taratibu za vijiji .

 Mwenyekiti wa kijiji cha Mahenge Said Mhina alisema kuwa hivi sasa wananchi wanajipanga kwa ajili ya ujenzi wa jiko katika shule hiyo ili kuondokana na shule hiyo kuendelea kupikia chini ya mti kama jiko la shule .

 Aidha mwenyekiti huyo alisema changamoto kubwa inayowakabili katika kuendelea na ujenzi wa shule hiyo ni kutokana na baadhi ya wananchi kugoma kuchangia michango halali iliyowekwa na kijiji na pindi wanapofikishwa mahakama ya mwanzo huachiwa na hakimu wa mahakama hiyo .

“ Tunaomba sana mkuu wa wilaya utusaidie kulifanyia kazi hili maana tunashindwa kuendelea na ujenzi mbali mbali shuleni hapa kutokana na kukwamishwa na mahakama kwa kuwaachia wanaokwepa maendeleo na wakiachiwa huzuia wengine kutoa michango”

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE