May 17, 2017

HUYU NDO KIM JONG UN ANAYEMSUMBUA RAIS TRUMPKiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-Un
(CNN) TANGU alipokabidhiwa madaraka baada ya kifo cha baba yake mwaka 2011, kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un ameshangaza na kuchanganya wengi kutoka pale alipokuwa mtu asiyejua lolote katika siasa hadi kuwa mjuzi hasa wa fani hiyo.
Mwezi uliopita, wakubwa kisiasa kutoka kila kona nchini humo walikusanyika katika mji mkuu wa nchi hiyo wa Pyongyang kwa ajili ya Mkutano Mkuu, ambao kwa kiasi kikubwa ni kama wa kukamilisha ratiba (symbolic) tu na ulihudhuriwa na Kim akiwa kama mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi cha Korea, ambacho ndicho kinachotawala.
Hotuba katika tukio hilo zililenga katika kusifu “mwongozi wa Kiongozi Mkuu Kim Jong Un,” kulingana na shirika la habari nchini humo la KCNA.
Wakati anasifiwa na wanasiasa hao nguli nchini mwake, ni mambo gani ameweza kutekeleza katika kipindi cha miaka mitano ya utawala wake?

Uchumi

Tangu achukue uongozi wa nchi yake miaka mitano iliyopita, mrithi huyu wa familia ya Kim amefanya kazi nzuri ya kuimarisha utawala wake na kuijenga nchi katika sura yake mwenyewe, anasema Choi Jong-kun, profesa msaidizi katika Chuo Kikuu cha Yonsei Kitengo cha Sayansi ya Siasa huko nchini Korea Kusini.
“Tunatazama miaka mitano ya uongozi wake,” Choi analiambia shirika la utangazaji la CNN. “Anajaribu kufanya vitu vingi kwa wakati mmoja. Amebadili uchumi wa nchi kuliko ambavyo baba yake aliweza kufanya, na kwa kiasi kikubwa ameendeleza uwezo wa nchi yake katika nyanja za nyuklia na makombora.”
Nick Bisley, mkurugenzi mtendaji katika Chuo Kikuu cha La Trobe huko Melbourne nchini Australia, anasema usalama ambao utahakikishwa iwapo silaha za kinyuklia zitapatikana ni muhimu zaidi wakati huu kabla ya kupeleka nguvu zake katika jaribio la kufanya mageuzi ya kiuchumi kwa nchi hiyo.
“Ni pale tu watakapokuwa wanajiamini kwamba wanazo silaha za kinyuklia na kwamba wapo salama ndipo tutaona mageuzi ya kiuchumi,” anasema Bisley.
“Matokeo mazuri ni kwamba atafuata mfumo wa China – akiona kuwa nchi yake ipo salama atafuata mfumo wa kiuchumi wa China lakini hata hilo likishatokea, hatutarajii kuona mabadiliko ya aina yoyote kisiasa.”

Kujiimarisha madarakani
Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un wakati wa sherehe za kuadhimisha siku ya Jua, ambayo ni muhimu sana nchini mwake mwisho wa wiki iliyopita.

Kujiimarisha madarakani imekuwa ndiyo siri ya mafanikio yake, na sehemu kubwa ya mafanikio hayo yanatokana na ukatili na umwagaji mkubwa wa damu.
Taarifa moja kutoka kundi moja la wachambuzi wa mambo (think tank) nchini Korea Kusini inayofahamika kama Taasisi ya Mkakati wa Usalama wa Taifa, inadai kwamba kiongozi huyo wa Korea Kaskazini alitoa amri ya kuuawa kwa kiasi cha watu 340 tangu alipoingia madarakani mwaka 2011 – miongoni mwa watu hao, 140 walikuwa ni maafisa wa ngazi za juu serikalini, katika jeshini na katika chama kinachotawala nchini humo cha Workers Party.
Katika mauaji yote hayo, hakuna yaliyofanyika kikatili kama yale ya mjomba wake, Jang Song Thaek mwaka 2013.
Kim hakuwa anafahamika hadi alipoingia madarakani mwaka 2011 na wengi wanamwona Jang kama aliyefanya kazi kubwa kuhakikisha kwamba anashika hatamu ya uongozi wa nchi. Kuondolewa ghafla kwa Jang ilikuwa ni dalili kwamba Kim alikuwa anaondoa mabaki ya uongozi wa zamani katika serikali yake, Bisley anasema.
“Kuonyesha ubabe kunakofanywa na viongozi – kusema kwamba ‘ondoka’ na ‘haupo’ – ni muhimu katika tawala za kidikteta,” anasema Micheal Madden, kutoka Korea Kusini.
Kwa kuchukua hatua hiyo hadharani, huku vyombo vya habari vya serikali vikimtangaza Jang kuwa “msaliti wa vizazi vyote,” Kim alihakikisha kuwa hakutakuwa na malalamiko juu ya uamuzi huo.
“Jinsi ilivyotokea, kwamba walifanya haya kupitia vyombo vya serikali, hii ni tabia ya Kim Jong Un,” anasema Madden.
“Watu wengi waliingiwa na hofu juu ya uimara wa uongozi wakati Jang alipokamatwa,” Choi anasema. “Lakini nilisema kwamba nguvu zake zimeimarishwa kiasi kwamba angeweza kumwondoa hata msaidizi wake.”
Kila kitu kinamtazama Kim sasa, Bisley anasema. “Watu wanaotazama hali ya mambo nchini humo wanaona kama hatua za kuondoa watu zimekwisha.”
Hata hivyo, taarifa za kuuawa kwa mawaziri wasaidizi watano mwezi Februari mwaka huu, ambao walikuwa wanafanya kazi chini ya mkuu wa usalama ambaye ametengwa nchini humo Kim Won Hong, inaonyesha kwamba mambo bado yanaendelea.

Mpango wa nyuklia

Ili aweze kujiimarisha zaidi ni lazima atimize ndoto ya muda mrefu ya taifa hilo kumiliki silaha za kinyuklia. Utawala huo upo katika hatua za mwisho kupata silaha hizo, na ile sifa ya kuwa miongoni mwa mataifa machache yanayozimiliki.
“Ipo imani kwamba mabomu ya nyuklia ni jambo la lazima na sehemu muhimu ya utambulisho wa Korea Kaskazini, usalama na heshima ulimwenguni,” anasema Bisley.
Katiba ya nchi hiyo ilibadilishwa mwaka 2013 ili kuonyesha nchi hiyo kuwa ina nguvu za kinyuklia, na wakati mipango yote ya kinyuklia na makombora bado inakabiliwa na vikwazo vya hapa na pale, ipo imani ulimwenguni, kwamba ni muda tu kabla nchi hiyo haijaweza kuwa na silaha chache lakini zinazoweza kufanya kazi za kinyuklia.
Tangu Kim alipoingia madarakani, mpango aliorithi toka kwa baba yake umepiga hatua kubwa mbele, anasema Choi.
Mpango wa makombora umefanikisha kuweka satelaiti angani – japo kwa kiasi fulani tu cha mafanikio – na “ameendeleza makombora ya masafa marefu na kupiga hatua kubwa kuelekea kwenye kuunda bomu la nyuklia ambalo litaweza kufungwa kwenye kombora (miniaturization),” anaongeza Choi.
Na wakati bado uongozi unaendeshwa na uaminifu kwa Kim, lakini jambo ambalo limesaidia sana katika kupiga hatua mbele ni kujali uwezo wa mtu kikazi badala ya upendeleo kutokana na ukaribu au urafiki,” Madden anasema.
“Kim Jong Un amewapandisha vyeo watu wengi ambao hapo awali hawakuwa wanafahamika… kutokana na uwezo wao kazini na si uaminifu wao kwake au kwa watu wake,” jambo ambalo limetoa nafasi kwa watu wenye uwezo kupanda vyeo, anasema.

Mtawala kijana wa kisasa?

Wakati Kim anachukua madaraka akiwa na umri mdogo, viongozi wengi wa karibu wameendelea kuwa ni wazee, anasema Madden.
Kim, ambaye anaaminika atakuwa katika miaka ya mwanzo ya thelathini – taarifa juu ya mwaka wake wa kuzaliwa haifahamiki hadharani – bado ni kijana mdogo zaidi katika serikali, anakubali Bisley.
Kuna uwezekano mdogo kwamba vijana nchini humo wataweza kuchukua nafasi za juu za uongozi ili kuwa pamoja na Kim.
“Kusipokuwa na mabadiliko ya kweli kisiasa, hali itaendelea kuwa inatokana na uaminifu kwa Kim,” Bisley anasema. Ni “kitu cha kwanza, muhimu zaidi cha kununulia madaraka.”
Hata hivyo, anabadili siasa za Stalin ambazo ndizo zilikuwa msingi wa uongozi wa baba na babu yake.
“Kim Jong Un hajafanya mengi katika kuhakikisha kuwa yeye ndiyo alama ya uongozi. Hakuna vifungo vya shati vyenye picha yake, hakuna jitihada kubwa za kumwonyesha kama ilivyokuwa kwa baba na babu yake,” anasema Choi.
Choi anafananisha miaka hii mitano ya zama za Kim Jong Un na kipindi ambacho kinasukuma mambo kwenda mbele. Wakati wa miaka hii ya awali amefanya kazi sana – na mara nyingi bila huruma – ili kuiweka nchi katika mtazamo wake.
Na wakati wanasiasa nchini humo walipokutana tena kusheherekea mafanikio ya chama chao, nafasi ya Kim madarakani katika taifa ambalo halieleweki zaidi duniani inaonekana kuimarika zaidi.

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE