April 7, 2017

WAZIRI MWANAMAMA APANDISHWA KIZIMBANI KWA UFISADI

Mahakama Kuu ya Shirikisho ya Nigeria imesikiliza kesi ya waziri wa zamani wa mafuta wa nchi hiyo anayekabiliwa na kashfa ya rushwa wakati wa uchaguzi katika juhudi za kuhakikisha rais wa zamani wa nchi hiyo Goodluck Jonathan anashinda katika uchaguzi wa 2015.
Shirika la habari la Ufaransa AFP limeripoti kuwa, Diesani Allison-Madueke ni waziri wa kwanza wa serikali ya Jonathan kupandishwa kizimbani.
Waendesha mashtaka wamedai kuwa waziri huyo wa zamani wa Nigeria alitoa hongo ya karibu dola milioni moja na laki nne katika juhudi za kuhakikisha Jonathan anashinda kwenye uchaguzi huo.
Mshauri wa zamani wa usalama wa taifa wa Nigeria ameiambia mahakama hiyo kwamba dola bilioni 2.1 ziliondolewa kwenye vita dhidi ya Boko Haram na kuingizwa katika kampeni za kuhakikisha Jonathan anashinda. Bi Allison-Madueke, 56, hakuwepo mahakamani wakati kesi hiyo ilipotajwa jana Jumatano.
Goodluck Jonathan, rais wa zamani wa Nigeria

Amekuwa akiishi mjini London Uingereza tangu Jonathan aliposhindwa katika uchaguzi wa 2015. Maafisa wa Shirika la Uhalifu wa Kitaifa la Uingereza walimshikilia kwa muda mfupi mwaka 2015 kwa tuhuma za kuhusika katika utakatishaji fedha.
Hata hivyo waziri huyo wa zamani wa Nigeria hakuweza kupatikana ili kutoa maoni yake kuhusu suala hilo. Mawakili wake nao hawakupatikana kuzungumzia jambo hilo.
Jaji Mohammed Idris wa mahakama hiyo ametoa dhamana ya Naira milioni 50 kwa maafisa wawili wa uchaguzi Yisa Olarenwaju na Tijani Bashir, wanaohusishwa na kesi hiyo na kuwataka wakabidhi pasi zao za kusafiria.
Bi Allison-Madueke alikuwa waziri mwenye nguvu katika serikali ya Goodluck Jonathan tangu mwaka 2010 hadi 2015. Katika kipindi hicho, gavana wa Benki Kuu ya Nigeria alitangaza kupotea risiti za mafuta zenye thamani ya dola bilioni 20.

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE