April 11, 2017

WATETEZI WA HAKI ZA BINADAMU WALAANI MATUKIO YA UTEKAJI NCHINI

MTANDAO WA WATETEZI WA HAKI ZA BINADAMU TANZANIA


TAMKO KWA VYOMBO VYA HABARI JUU YA KUPOTEA KATIKA HALI YA KUTATANISHA, UTEKWAJI NYARA, KUTIWA MBARONI NA VITISHO DHIDI YA WATETEZI WA HAKI ZA BINADAMU TANZANIA
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) wenye wanachama zaidi ya 130, unalaani vikali vitendo haramu vya kukamatwa, kushitakiwa, upotevu na vitisho vinavyotolewa dhidi ya watetezi wa haki za binadamu nchini Tanzania. Watetezi wa haki za binadamu ni pamoja na Wasanii, wanasheria, Waandishi wa Habari, Wanablogu na waandishi wa makala mbalimbali wanaounda sehemu muhimu ya mabadiliko katika jamii. Katika jamii yenye uhuru wa kujieleza, watetezi hawa wa haki za binadamu wana jukumu kubwa zaidi katika ukombozi wa jamii kupitia utoaji wa mawazo na maoni yao. Nchini Afrika Kusini na Marekani, uhuru wa maoni ulitumika kupambana dhidi ya Utawala wa Ubaguzi wa Rangi.
Ikumbukwe pia ya kuwa, uhuru wa maoni ni haki ya binadamu inayolindwa kikatiba na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Ibara ya 18. Hata hivyo, uhuru huo wa maoni nchini Tanzania umeonekana kuminywa na pia baadhi ya watetezi wa haki za binadamu ambao wamejaribu kutoa maoni yao kwa njia ya nyimbo ama uandishi, wamekuwa waathirika wa kukamatwa, kusomewa mashtaka na kupokea vitisho. Sheria kandamizi kama vile Sheria ya Vyombo vya Habari iliyopitishwa hivi karibuni na sheria nyingine za zamani za kibabe, zenye dhumuni la kudhibiti uhuru wa kujieleza zinaleta tafsiri mbaya ya kwamba, haki ya uhuru wa maoni iliyoko kwenye Katiba haina maana.
Tumeshtushwa na vitendo vinavyozidi kushamiri nchini vya kutoweka na kutekwa nyara kwa watetezi wa haki za binadamu na raia, pasipokuonekana jitahada zozote aidha za raia wenyewe ama za viongozi wa wa nchi kuchukua hatua kuvikomesha vitendo hivyo. Kwa mfano, wakati bado mwanaharakati wa kisiasa Ben Saanane hajulikani alipo, mnamo tarehe 5 Aprili, 2017, palitokea tukio jingine la upotevu wa msanii Ibrahim Musa almaarufu kwa jina la usanii; Roma Mkatoliki pamoja na wasanii wenzake Moni, Bello na Emma ambao walitekwa nyara wakati wakiwa katika studio ya muziki ya Tongwe Records na kutojulikana waliko kwa takribani siku mbili. Jeshi la Polisi kupitia RPC wa Kinondoni na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, waliuthibitishia umma ya kuwa hawakuwa na taarifa yoyote kuhusu kituo chochote cha polisi ambacho kilikuwa kikiwashikilia wasanii hao kwa wakati huo.
Katika kipindi chote hicho, wanaharakati mbalimbali, wasanii na umma kwa ujumla walionesha wasiwasi na kutoridhishwa kwao juu ya kupotea kwa wasanii tajwa na hatimaye mnamo tarehe 8 Aprili, 2017, taarifa zilisambaa ya kuwa wanne hao wamepatikana na wako katika kituo cha polisi cha Oysterbay. Hata hivyo, maswali ambayo kila mmoja anajiuliza hivi sasa ni; “Nani alikuwa nyuma ya kupotea kwao?”. Na “Nani aliwapata?” na “Nani aliwarudisha hadi kituo cha polisi Oysterbay?”.
Wasanii hao kwa sasa wako huru na mnamo tarehe 10 mwezi Aprili 2017, Msanii Roma alipata fursa ya kuongea na waandishi wa habari na umma kwa ujumla ambapo ameeleza kuwa walipokamatwa walifungwa vitambaa usoni na kufungwa pingu na walipelekwa sehemu wasiyoijua. Wakati wako huko, kuna mahojiano yalikuwa yakiendela ambapo wakati mahojiano hayo yanaendelea wahanga hao walikuwa wakipata mateso na vipigo bila sababu za Msingi. Msanii huyo ameeleza kuwa maelezo na maswali waliyokuwa wakihojiwa amewaachia polisi wafanye kazi yao na wao ndio watakuja na taarifa kamili juu ya nini kilitokea. 

Wakati hayo yakiendelea, inaonekana sehemu ya umma wa watanzania unaonekana kutoridhishwa na maelezo ya Msanii Roma juu ya sakata hili. Wengi wanahisi maswali ya msingi kuhusu tukio hili hayakuwekwa wazi pengine kwa sababu mbalimbali. 

Maelezo ya Roma yanadhihirisha wazi ya kwamba umma wa Watanzania sasa umeingiwa na hofu ya kuongea ukweli kwa kuhofia kutekwa na /au kukamatwa kinyemela. Hali ya Roma na wenzake inaonekana ni watu waliopata vitisho na mateso huko walikokuwa na pengine huenda ikawa ni sababu mojawapo ya kuogopa kuzungumza zaidi. 

Wamekiri kuwa hali ya usalama nchini ni ndogo sana kwani wasingetegemea kutekwa katika eneo lililozungukwa na viongozi wastaafu wa majeshi ya Tanzania.

Kwa ujumla Mtandao wa Watetezi unatoa pole kwa wote waliotekwa na mateso waliyoyapata toka kwa watesaji. 

Tunawashauri wasisite kueleza wanachokijua kwani kwa kukaa kimya kunaweza fanya wahusika waone ni mchezo wa kila siku. 

Ni muhimu kufahamu kwamba, ni wajibu wa vyombo vya dola kuwalinda raia wake na mali zao. 


Katika Mkutano wa Arobaini na saba; Ajenda 97(b), ya Azimio lililopitishwa na Mkutano Mkuu wa Umoja wa Taifa mnamo tarehe 12 Februari 1993, juu ya Azimio kwa ajili ya Ulinzi wa Watu Wote kupinga Utekelezwaji wa Upotevu wa Watu, Katika Ibara ya 7 inasema kwamba; “Hali yoyote ile, iwe tishio la vita, hali ya vita, migogoro ya kisiasa ndani ya nchi au hali yeyote ile ya dharura ya umma, haiwezi kuhalalisha kupotea kwa mtu”.

Pia sehemu ya 2 Kifungu cha 5, kifungu cha kwanza cha Sheria ya Jeshi la Polisi na Huduma Saidizi kinasema;
"Jeshi la Polisi litaajiriwa katika Jamhuri yote ya Muungano kwa ajili ya kulinda amani, kudumisha sheria na utulivu, kuzuia na kugundua uhalifu, kuwakamata na kuwaongoza watuhumiwa na kulinda mali, na katika utekelezaji wa majukumu yote hayo watakuwa na haki ya kubeba silaha."


 Vitendo hivi vya kutekwa na kupotea kwa watetezi wa haki za binadamu vimekuwa vikitokea na hakuna staiki zinazochukuliwa. Mnamo tarehe 27 Juni, 2012, Dkt.  Stephen Ulimboka  kiongozi wa Chama cha Madaktari alitekwa na kuteswa kikatili kwa kuwa alikuwa mstari wa mbele katika mgomo wa madaktari Tanzania. 

Waliomteka walitumia vyuma kumjeruhi mwili mzima na kumnyofoa kucha za vidole gumba, na pia kutumia vyuma kuponda kucha za vidole vingine. 

Umma ulipata taarifa kwamba, Dkt. Ulimboka alipatikana msituni maeneo ya Mabwepande jijini Dar-es-salaam akiwa amepoteza fahamu na kuvuja damu na kuchukuliwa na msamaria mwema hadi kituo cha Polisi Bunju na ndipo THRDC na LHRC kwa kushirikiana na madaktari, walimchukua hadi Muhimbili kwa huduma za haraka. 


Mnamo tarehe 5 Machi 2013, miezi Tisa mara tu baada ya janga la Dkt. Ulimboka, Mhariri Mtendaji wa New Habari (2006) Ltd, ambaye alikuwa pia Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Bwana Absalom Kibanda, alishambuliwa na kujeruhiwa vibaya nje ya geti la nyumba yake eneo la Mbezi Juu, Dar es Salaam. 

Washambuliaji hao walimkata kipande cha kidole chake cha kulia, wakamtoboa jicho lake la kushoto, wakamng’oa meno na kumnyofoa kucha za vidole.


Mwaka 2015, kijana George Mgoba ambaye ni mtetezi wa haki za vijana, alicheza nafasi muhimu kama mwenyekiti wa wahitimu kutoka National Youth Service. 

Akiwa na mwezake, walitumia njia mbalimbali za amani kama vile mkusanyiko wa amani na haki ya kujumuika. 

Hata hivyo, serikali haikutilia maanani madai yao kutokana na ukweli kwamba nchi wakati huo ilikuwa inakaribia uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

 Katika hali ya kushangaza, mnamo Februari 16, 2015, Mgoba alipotea. Baadae taarifa za kupatikana kwake zilienea, huku ikiripotiwa kuwa alikutwa ametelekezwa maeneo ya Kibaha nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam akiwa amenyolewa nusu-kichwa.

 Alichukuliwa na kulazwa katika hospitali ya Tumbi Wilaya ya Kibaha kwa matibabu, lakini hakupatiwa matibabu yeyote, bali alichukuliwa na kupelekwa kituo cha polisi Oysterbay kwa ajili ya mahojiano na baadaye kuachiwa huru. 

Baadae, kituo cha Polisi Kisutu, Dar es Salaam, kilimshtaki yeye pamoja na watetezi wenzake watano wa haki za binadamu kwa kesi ya jinai namba 38 ya 2015, ya kuendesha mkutano kinyume na sheria.


Mnamo Machi 18 2016, muda mfupi baada ya kuondoka Zanzibar palikuwa na taarifa ya kwamba Bi. Salma Said ambaye ni mwandishi wa Mwananchi Communications Ltd. na mwandishi wa Kampuni ya Kimataifa ya Ujerumani (Deutsche Welle) alikamatwa na polisi. 

Katika kuhakikisha taarifa hizo, ilitubidi kufuatilia kwa ukaribu juu ya suala hilo kwa vyombo vya usalama vya Zanzibar, ndipo tuliposhangazwa kupokea taarifa kuwa jeshi la polisi la Zanzibar wala la Tanzania Bara halikuwa na taarifa yeyote juu ya kukamatwa kwa Bi. Salma.

 Bi Salma alieleza badaye kwamba, alishambuliwa na watu wasiojulikana ambao walimchukua na kumpeleka kusikojulikana mara baada ya kutoka nje ya maeneo ya uwanja wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere.

Aidha, mnamo tarehe 6 Juni, 2016, msanii Vitalist Maembe,ambaye ni mwanamuziki mtetezi wa haki za binadamu alishtakiwa kwa kosa la jinai chini ya sehemu ya 299 ya Kanuni ya adhabu katika Chuo cha TASUBA Bagamoyo na pia kushtakiwa kwa Ugomvi kinyume na kifungu cha 89 (1) cha Kanuni ya Adhabu, alidaiwa kuanzisha ghasia kwa kupiga ngoma za kuita mkusanyiko wa wanafunzi ambao kwa muda huo walikuwa wakifanya mtihani. 

Hata hivyo, kesi dhidi yake ilitetewa vema na THRDC, hivyo upande wa mashtaka ulilazimika kuondoa kesi kwa kukosa vithibitisho vya mashtaka ya kesi hiyo.

Mnamo tarehe 25 Machi, 2017, msanii Emmanuel Elibariki almaarufu kwa jina la usanii; Nay wa Mitego, alitiwa mbaroni akiwa mkoani Morogoro mara baada ya kutoa wimbo wake wa ‘WAPO’, 

unaodhaniwa kulenga kuikosoa serikali na viongozi wa serikali. 

Hata hivyo, baadae msanii huyo aliachiwa huru kufuatia amri ya Mheshimiwa Rais na Waziri wa wizara husika.  

Mwaka huo huo; 2016, Bwana Mexence Mello, Mkurugenzi Mkuu wa Jamii Media ambaye pia ni mtetezi wa haki za binadamu, aliripoti kwa THRDC kwamba familia yake imekuwa ikipokea vitisho mara kwa mara kutoka kwa watu wasiojulikana. 

Vitisho hivyo kwa Bwana Mello vinatokana na kwamba yeye ndiye mmiliki wa Mtandao wa Jamii Forums unaotoa uhuru wa wananchi kujadili mambo ya msingi, ikiwemo mambo yanayohusiana na utetezi wa haki za bianadamu.

Wasiwasi wetu kama watetezi wa haki za binadamu, ni juu ya hali ya hofu ambayo imetanda miongoni mwa wanajamii kuhusu uhuru wa maoni na usalama wa wale wanaosimama kukosoa baadhi ya mambo nchini. 

Kila mtu sasa ana wasiwasi juu ya hatima yake endapo atajihusisha na utetezi wa haki na  uhuru wa maoni, kwa hofu ya kutekwa nyara ama kukamatwa. 

Mambo haya yamekuwa yakijitokeza kwa mwendelezo na wala wahalifu  hawaonekani kukamatwa. 

Hali kama hii ikiachwa kuendelea, itajenga hofu kubwa kwa jamii. 

Mfano Ulimboka, Kibanda, Mgoba na Salma waliopata matatizo haya na wala wahusika wa uhalifu hawakupatikana hadi leo. 

Wito wetu
 Vyombo vya usalama Tanzania vihakikishe kuwa kila raia anaishi kwa uhuru na usalama nchini Tanzania. 

Jeshi la Polisi liwe tayari kuwalinda raia na mali zao na si kutumika vinginevyo.

Serikali na raia kwa ujumla watambue kuwa kuimba ni njia moja wapo kama zingine zinazoweza kutumika kutetea haki fulani au kukosoa uongozi. 

Kwa maana hiyo isionekane jambo jipya kuwaona wasanii wakiimba nyimbo za kukosoa. 

Wasanii wasipewe vitisho, kutekwa wala kukamatwa kinyume na sheria kwa sababu ya nyimbo zao.

AZAKI, vyombo vya habari na umma wa watanzania kwa ujumla wanapaswa kuwa mstari wa mbele kukemea vitendo vyovyote ambavyo vinalengo kuzuia uhuru wa maoni nchini Tanzania. 

Tunapaswa sote kukemea kwa sauti moja hali yoyote inayopinga kufurahia haki zetu.  

 Leo ni Roma na wengine haijulikani siku wala saa ya kutekwa. Watetezi wa haki za binadamu tuungane na kupaza sauti kwa pamoja kupinga vitendo vya utekaji vinavyozidi kushika kasi katika nchi yetu.

Serikali ya Tanzania inapaswa kuzingatia misingi ya kimataifa ya haki za binadamu kama ilivyoelezwa katika Mikataba ya Umoja wa Mataifa ambayo Tanzania ni mwanachama.

 Kwa sababu hii, tunapendekeza kwamba serikali inapaswa kutia sahihi na kuridhia Mkataba wa Kimataifa kwa Ajili ya Ulinzi wa Watu Wote Waliotekwa na Kuwekwa Vizuini.

Tanzania sasa iweke utaratibu wa kuwa na mfumo wa kuendesha mashtaka utakaokuwa mfumo huru (Private Prosecution).

Kwa wale waliotekwa na kuachiwa, wajitahidi kutoa taarifa kamili kwa umma ili kuzuia uendelezaji wa matukio haya.

Serikali ihakikishe wahusika wote wa uhalifu huu wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya haki.

Viongozi wa Dini nao wajitahidi kujiongeza katika matukio kama haya na kukemea kwa nguvu kubwa.

Viongozi wa siasa na Bunge waone namna ya kulijadili suala hili la utekajji na kupotea kwa watanzania wenzetu.

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE