April 7, 2017

UMMY ALLY MWALIMU (ATOA TAMKO KUHUSU SIKU YA AFYA DUNIANI TAREHE 7 Aprili 2017

ummymwalimu
Siku ya Afya  Duniani, huadhimishwa duniani kote kila mwaka tarehe 7 ya Mwezi wa Aprili. Maadhimisho haya yameridhiwa na nchi zote  wanachama wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Tanzania ikiwa mojawapo. 
Katika kuadhimisha siku hii, Shirika la Afya Duniani linatoa  kaulimbiu yenye  ujumbe maalum  ambao unalenga  kuhamasisha  na kuelimisha jamii juu ya suala mojawapo muhimu na lenye manufaa kiafya kwa nchi zote wanachama.
Kaulimbiu  ya  Maadhimisho ya  Siku ya  Afya  Duniani mwaka  huu  wa  2017 ni : ‘SONONA TUZUNGUMZE’. Kwa Kiingereza ni ‘’DEPRESSION : LETS TALK’’
Kaulimbiu hii inalenga kuhamasisha wadau wote na jamii kwa ujumla  kutambua ukubwa wa tatizo hili kitaifa na kimataifa, visababishi vyake, umuhimu wa kubadili tabia na mienendo hatarishi ili kudhibiti na kujikinga na ugonjwa huu na namna ya kupata huduma ya matibabu ya sonona.
Nchi yetu kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na wadau itaadhimisha siku hii kwa kutoa elimu kuhusu namna ya kukabiliana na ugonjwa wa sonona katika jamii zetu.
Tunapozungumzia afya tunamaanisha hali ya ustawi wa mwanadamu  kimwili, kiakili na kijamii. Mtu mwenye afya njema ya akili anaaminika kutengemaa katika namna anavyofikiri, anavyohisi, na anavyotambua mambo, ambayo kwa pamoja hujionyesha katika matendo yake ya kila siku ikiwa ni pamoja na jinsi anavyohusiana na kushirikiana na wenzake katika familia na jamii kwa ujumla.
Sonona ni ugonjwa ambao unaathiri uwezo wa mtu kufikiri, kuhisi, kutambua na kutenda, na hivyo kuwa na tabia au mwenendo ulio tofauti au usioendana na jamii husika kiimani, kimila, kidesturi, na ki-nyanja nyingine za kijamii. Tabia hizo zinatokana na ugonjwa huu kuathiri ufanisi na shughuli za mtu husika (mgonjwa) pamoja na kuathiri uhusiano wake katika jamii na hivyo hatimaye huathiri jamii nzima inayomzunguka.
Kulingana na takwimu za hivi karibuni za Shirika la Afya Duniani, zaidi ya watu milioni 300 kwa sasa wanaishi na ugonjwa wa sonona duniani, ikiwa ni ongezeko la zaidi ya asilimia 18 kati ya mwaka 2005 hadi 2015.
Kuna dalili mbalimbali ambazo mtu mwenye Sonona anaweza kuonesha ikiwemo ; Mtu kuwa na Msongo mkubwa wa mawazo, Kukosa raha, Kukosa usingizi na hamu ya kula, Kujitenga na watu au jamii inayomzunguka na Mara nyingne kutaka kujiua au kuwaua wenzake.
Iwapo unahisi una dalili au mwenzio ameonesha dalili kama zilizotajwa unashauriwa kuzungumza na mtu wako wa karibu unayemwamini kuhusu matatizo yako yanayokukabili ili upate ushauri na faraja itakayokupunguzia msongo wa mawazo. Vilevile, pata muda wa kutosha kula, kupumzika au kulala, endelea kufanya shughuli ulizokuwa unafanya kabla ya kupata Sonona. Lakini, ukiona dalili zinaendelea, basi pata ushauri wa kitaalam kutoka kwa mtoa huduma za afya katika kituo cha afya kilicho karibu yako.
Vilevile, Takwimu za Shirika la Afya Ulimwenguni zinaonesha kuwa kati ya kila watu 5 mmoja kati yao ana matatizo au alishapata matatizo ya Sonona, Aidha miongoni mwa watu wanaopata matatizo ya Sonona ni wachache tu ambao wanaweza kufikia na kupata huduma ya afya, na hata hao wanaohudhuria katika vituo vya Afya ni wachache wamekuwa wakigundilika kuwa na tatizo la Sonona.
Hivyo, kuna haja ya huduma za afya ya akili na saikolojia kutolewa katika maeneo yetu ya kutolea huduma tukianzia katika huduma za afya ngazi ya jamii, hii ikiwa ni pamoja na kuwa na kitengo maalumu kinachotoa huduma hizo katika hospitali zote nchini pamoja na kuboresha upatikanaji wa dawa za kutibu magonjwa ya Sonona.
Vilevile, kuna umuhimu wa kuwajengea uwezo watoa huduma za afya ili waweze kutambua na kubaini mapema dalili za ugonjwa huu na kutoa matibabu stahiki au rufaa kwa wakati muafaka. Suala la kuimarisha matibabu ya magonjwa ya akili na saikolojia katika hospitali za mikoa na rufaa nalo ni la muhimu sana. Hivyo Serikali inapeleka wataalamu wa afya ya akili katika vituo hivyo, wakiwemo Madaktari Bingwa ili kuweza kutoa huduma kwa wagonjwa wa nje na wale wa ndani/ waliolazwa
Watu wengi wamekuwa hawajui matatizo na magonjwa ya Sonona, na kufikia hatua ya kuamini kwamba magonjwa hayo ni laana, kurogwa, kuwa na mapepo au kutupiwa majini. Ugonjwa huu unaweza kumtokea mtu yeyote, wa rika lolote, na muda wowote. Hivyo basi wananchi, wanafamilia na jamii kwa ujumla tunapaswa kujua na kutambua dalili za magonjwa ya akili na kuweza kupunguza unyanyasaji, unyanyapaa na kuwatenga wagonjwa hawa.
Katika maadhimisho haya wataalamu watajikita kuelimisha jamii juu ya ugonjwa wa Sonona na kupunguza vitendo vya unyanyasaji, unyanyapaa na kuwatenga wagonjwa, hivyo kuwawezesha kufikishwa maeneo ya utolewaji wa huduma na tiba mapema ili wasaidiwe kama walivyo wagonjwa wengine.
Kutokana na Taarifa ya Hali ya Afya ya magonjwa ya Akili ya mwaka 2015/16 nchini Tanzania inaonesha kuwa takribani Wagonjwa 41,789 waligundulika kuwa na tatizo la Sonona. Hata hivyo hii ni idadi ndogo ikilinganishwa na ukubwa wa tatizo linavyokisiwa. Sababu ikiwa ni wagonjwa wachache wanao hudhuria katika vituo vya kutolea huduma kwa matatizo mbalimbali ya afya ya akili na matatizo ya kisaikolojia hapa nchini.
Ziko sababu mbalimbali ambazo hupelekea jamii kupata ugonjwa wa sonona. Sababu hizi zimegawanywa katika makundi makubwa matatu ; Kwanza ni sababu za kibailojia ; pili ni sababu za Kisaikolojia ; na tatu, ni sababu za Kijamii. Sababu za kibailojia ni pamoja na kurithi vinasaba ambavyo husababisha aina mbalimbali za magonjwa ya akili, kuugua magonjwa mbali mbalimbali yanayoshambulia ubongo na mfumo wa fahamu kama vile malaria kali, homa ya uti wa mgongo, saratani au uvimbe katika ubongo, VVU au magonjwa nyemelezi yanayosababishwa na upungufu wa kinga mwilini. Lakini pia kuna magonjwa mengi ya kimwili ambayo huleta madhara ya afya ya akili na kusababisha mtu kuugua ugonjwa wa Sonona ; mfano ni Figo kushindwa kufanya kazi, magonjwa ya Ini, magonjwa ya Moyo, upungufu wa damu, upungufu wa lishe bora, magonjwa ya mfumo wa hewa yanayosababisha ubongo usipate hewa ya kutosha, upungufu wa maji mwilini pamoja na Kisukari.
Sababu za Kisaikolojia ni kushindwa kukabiliana na matatizo ya kijamii au changamoto mbalimbali zinapotokea,  kuwa na mtazamo hasi katika maisha ya kila siku ambayo pia hupelekea kufanya maamuzi yasiyo sahihi, kunyanyaswa kihisia (emotional abuse), pamoja na upweke.
Sababu za kijamii zinazoweza kusababisha mtu kupata ugonjwa wa sonona ni umaskini uliokithiri, kutengwa pamoja na kubaguliwa na jamii, kunyanyaswa kimwili na kingono, kuwa tegemezi, kupotelewa au kuharibikiwa na mali (kupoteza mali, kupoteza kazi au kuwa mlemavu), kukosa huduma muhimu, unyanyapaa na unyanyaswaji. Pia kutokewa na majanga mbalimbali  au matukio mbalimbali ya kuumiza sana au kuhuzunika (traumatic events) kama vile kufiwa na mtu wa karibu,  kubakwa, kuunguliwa nyumba, mafuriko nk. Kukosa huduma muhimu, magomvi katika mahusiano na katika jamii, kukosa msaada wa kijamii pale mtu anapoelemewa na
Ugonjwa wa Sonona (Depression)  ambao upo kwa kiwango kikubwa sana katika jamii yetu haupatiwi matibabu kwa haraka kwa sababu mara nyingi mgonjwa anakuwa hana vurugu zozote bali hujitenga zaidi na kuwa mnyonge na mkimya. Ila ni ugonjwa ambao usipopatiwa matibabu kwa haraka unaweza kupelekea mtu kushindwa kufanya kazi kwa ufanisi, kukosa raha, kupunguza umakini katika kazi, kujiua au hata kuua wengine.
Serikali imeendelea na utekelezaji wa Sera ya Afya ya mwaka (2007) ambayo inalenga kutoa huduma bila malipo kwa wagonjwa wa akili na magonjwa mengine yasiyo ambukiza. Aidha Sera ya mwongozo wa huduma za Afya ya Akili pia inasisitiza utoaji wa huduma za Afya ya Akili, ukiwemo uginjwa wa sonona bila malipo.
Ili kuboresha hali ya Afya ya Akili na matatizo ya kisaikolojia, Sonona ikiwa miongoni,  Serikali kwa kushirikiana na wadau imehakikisha ya kwamba:-
  1. Watumishi wa Afya wanapewa mafunzo maalum ya namna ya kuwahudumia  wagonjwa wa Sonona na matatizo ya kisaikolojia kwa jamii.
  2. Inaweka utaratibu wa kufuatilia wagonjwa wa Sonona kwenye Jamii (Community Mental Health Services).
  3. Aidha, serikali inaaendelea kuimarisha vituo vyake vya Afya ya msingi na utengamao wa akili nchini. (Primary Health Care and Rehabilitation Centers).
  4. Kufanya tafiti mbalimbali zinazosaidia kuboresha huduma za kuzuia na kudhibiti magonjwa ya Sonona katika jamii.
  5. Kutoa matibabu ya kisaikolojia kama huduma ya kwanza (Psychologicol Criss Intervention) pale inapotokea maafa au majanga mbalimbali katika jamii.
  6. Watoa huduma za Afya nchini kupatiwa mafunzo maalumu juu ya utoaji wa huduma za awali za kisaikolojia mahali popote walipo ili waweze kuwahudumia wananchi hasa katika kipindi cha maafa mablimbali kama vile mafuriko, milipuko, tetemeko la ardhi, ajali,  kufiwa, kupoteza mali au kiungo, matukio ya kubakwa, ili kuwawezesha kukabilina nayo bila ya kuathiri Afya zao za akili.
Kwa kuhitimisha napenda kutoa wito na kuwakumbusha kuwa Sonona inaweza kuzuilika iwapo tutajenga familia zetu juu ya mahusiano mazuri, kupendana na kupeana faraja na kusaidiana miongoni mwetu.
Tuchague marafiki ambao tunaweza kuzungumza nao pindi tunapohitaji ushauri na faraja juu ya matatizo yanayotukali katika maisha yetu ya kila siku. Pia, ni vizuri kuwasaidia watu wenye Sonona kupata ushauri wa kitaalam toka kwa watoa huduma za afya katika vituo vya huduma za Afya.
LIMETOLEWA NA MHE : UMMY MWALIMU (MB)
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE