April 2, 2017

TFF YATUPA RUFAA YA DRFA


Kamati ya Rufani za Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), imetupa rufaa Saleh Saleh maarufu kama Ndonga aliyelalamikia kuhusu uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) kadhalika kumlalamikia Mwenyekiti wa sasa wa chama hicho, Almas Kasongo akitaka ang’olewe kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi wa sasa.

Pia katika uamuzi wake huo Kamati ya Rufaa za Uchaguzi ya TFF, imesema kila upande ubebe gharama zake kwani rufaa hyo haina sababu za msingi za kusitisha mchakato wa usaili au kuweza kumuengua Kasongo katika kinyang’anyiro cha kugombea uongozi DRFA.

Saleh Ndonga alikata rufaa dhidi ya Kamati ya Uchaguzi ya Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) - Mrufaniwa wa Kwanza - na Mwenyekiti wa sasa wa DRFA, Almas Kasongo –Mrufaniwa wa Pili akitaka jina lake liondolewe katika orodha ya wagombea wa nafasi ya uenyekiti wa DRFA.

Pingamizi lake liliegemea kwenye sababu kuu mbili ambazo ni mosi, ni kwamba Kasongo hakuwa na sifa za kuwania tena nafasi hiyo ya mwenyekiti wa DRFA kwa kile alichodai kukosa sifa za uadilifu, uaminifu kadhalika ni mvunjaji wa katiba kwa mujibu wa katiba ya DRFA. 

Pia alidai kuwa alishindwa kuitisha mkutano mkuu kwa muda unaotakiwa.

Pingamizi hilo awali liliondolewa na Kamati ya Uchaguzi ya DRFA na hivyo akakosa imani za kamati hiyo na kwenda kwenye Kamati ya Rufaa za Uchaguzi. 

Alidai kwamba Kamati ya Uchaguzi ya DRFA ilikosea kikatiba kuondoa pingamizi bila kujali hoja za msingi kikatiba zilizokuwamo kwenye pingamizi lake.

Hivyo Ndonga mbele ya kamati ya rufani za uchaguzi inayoongozwa na Dk. M. Lugaziya alitaka chombo hicho cha TFF kufuta uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya DRFA, iondoe jina la Kasongo na asiweze kugombea nafasi ya uongozi wa mpira popote Tanzania; arudishe gharama za pingamizi na aamuriwe kurejesha gharama nyingine zozote ambazo kamati inaona inafaa azilipe.

Mrufaniwa Kasongo alipinga rufaa hizo kwa maelezo ya jumla kuwa uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya DRFA ulikuwa sahihi na rufaa iliyoletwa rufani iliyoletwa na Ndonga haina mashiko hivyo akaomba itupiliwe mbali.

Kasongo alieleza kuwa kinachoelezwa kuwa ni hesabu zingeweza kuletwa kwenye mkutano wa Uchaguzi ambao ufanyike Februari, lakini umesogezwa mbele hadi Aprili 9, mwaka huu na kamati iliona kuwa kuchelewa kwa taarifa ya hesabu zilizokaguliwa katika mazingira haya hakuwezi kuchukuliwa kama ni kilelelezo cha kukosa uadilifu au uaminifu.

 Hiyo  inaweza kuwa ni hukumu ya mapema mno.

Kuhusu kushindwa kuitisha mkutano, mrufaniwa Kasongo alitetea kuwa aliitisha kwa mujibu wa katiba isipokuwa kulikuwa na kipindi ambacho Ndonga na baadhi ya viongozi wa Chama Cha mpira wa Miguu cha Temeke (TEFA) walifungiwa kabla ya busara zake na Rais wa TFF, Jamal Malinzi kuwarejesha madarakani kutokana na mzozo iliyodhirisha kulikuwa na uasi uliosababisha kufungiwa.

Kamati imejiridhisha kwamba kwa mujibu wa Katiba Ndonga na wenzake walikuwa na nafasi ya kuomba mkutano wa dharura, jambo ambalo hakuna ushahidi kama wamewahi kufanya hivyo baada ya kurejea madarakani bada ya kutiwa hatiani kwa makosa ya uasi.

Kamati imezitaka kamati zote za uchaguzi wanachama wa TFF kama vile mikoa na klabu, kufanya kazi zao kwa weledi.

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE