April 4, 2017

RC IRINGA AFUNGUA WARSHA YA MADIWANI HALMASHAURI YA MUFINDI, NA MANISPAA YA IRINGA LEO


Mkuu  wa  mkoa wa Iringa  Amina Masenza  akifungua warsha ya mafunzo kwa  madiwani mkoa  wa Iringa leo  kulia ni mkuu wa  wilaya ya  Mufindi Wiliam Jamhuri na kushoto ni mratiobu wa mafunzo hayo Dkt  Peter  Chulima
Madiwani  kutoka  Halmashauri  za Mufindi  ,Mafinga mji na Iringa  mjini  wakiwa katika mafunzo
Madiwani  wa Halmashauri ya  Manispaa ya  Iringa
HOTUBA YA MAFUNZO KWA WAHESHIMIWA MADIWANI KUPITIA MRADI WA UIMARISHAJI WA MIFUMO YA SEKTA ZA UMMA (PS3) TAREHE 4 APRILI, 2017
 
Kiongozi wa Timu ya Mradi wa PS3
Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya
Wenyeviti wa Halmashauri
Waheshimiwa Madiwani
Wakurugenzi wa Halmashauri
Makatibu Tawala wa Wilaya
Maafisa Utumishi
Wakufunzi
Waalikwa
Mabibi na mabwana
 
Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetukutanisha leo mahali hapa, kwa ajili ya mafunzo elekezi yanayotarajiwa kufanyika kwa siku hizi mbili. Kwenu wageni wote mliotoka maeneo mbalimbali na kuja Mkoani kwetu, karibuni sana.
 
Nimefurahi kupata nafasi hii muhimu ya kufungua mafunzo haya kwa waheshimiwa Madiwani.  Furaha yangu inatokana na kwanza, umuhimu wa tukio lenyewe; lakini pili, kwakuweza kukutana na wadau wetu wakubwa sana, ambao ni watekelezaji wa Mradi wa Uimarishaji Mifumo ya Sekta za Umma. 
 
 Wadau wetu hawa walifika Mkoani kwetu kwa mara ya kwanza Februari, 2016 kwa ajili ya uzinduzi wa Mradi. Wakati wa uzinduzi wa Mradi kuna changamoto mbali mbali ambazo ziliibuliwa, moja wapo ikawa kuwajengea uwezo Waheshimiwa Madiwani.  
 
Mradi ulianza kuwapa mafunzo Madiwani wa Halmashauri mbili za Kilolo na Iringa ambazo zimo katika awamu ya kwanza ya mradi.  Wakati huo naambiwa waliahidi kuja kufundisha Halmashauri zilizobaki.
 
 Leo ninapowaona hapa PS3 ni utekelezaji wa ahadi yao waliyotoa. Hii ina maana PS3 wako makini katika kuendesha shughuli zao kwa kufuata taratibu ambazo tunakubaliana nao. Atimizaye ahadi ni muungwana.
 
Pia, napenda kuwashukuru Watu wa Marekani ambao wanafadhili Mradi huu pamoja na mafunzo haya kupitia Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID).
 
  Msaada wao kwa Mkoa wetu wa Iringa ni mkubwa, kwani PS3 ni mradi wa kipekee kwa maana ya kugusa eneo la mifumo ambalo ni eneo mtambuka kwa sekta zote, kinyume na mazoea ya kuwa na miradi ambayo inalenga sekta moja moja.
Ndugu Washiriki,
Mafunzo haya kwa Madiwani wa Manispaa ya Iringa, Halmashauri ya Mji wa Mafinga na Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi yana umuhimu wa kipekee sana. 
 
Ni mafunzo yanayolenga kumwongezea ujuzi Mh. Diwani. Madiwani ndio wawakilishi wa wananchi, ni watu ambao wanaoyajua matatizo na changamoto mbalimbali zilizoko kwa wananchi wa kawaida, na hata katika maeneo ya pembezoni ambako pengine ni nadra kutembelewa na wawakilishi wa juu kutoka Serikalini.  
 
Ni muhimu basi kwa wawakilishi hawa kupatiwa Mafunzo elekezi, ambayo yatawapa nyenzo nzuri kinadharia na kivitendo juu ya wajibu wao. 
 
Naomba nisisitize kwamba maendeleo ya nchi hayaji kutokana na utendaji wa Serikali Kuu peke yake, bali mzizi wa maendeleo lazima uanzie kwenye shina, yaani kwa wananchi.  Wananchi hawa wa kawaida mwakilishi wao ni Diwani.  Hii inaonyesha namna mafunzo haya yalivyo na umuhimu kama tuna nia ya kweli ya kuleta maendeleo katika nchi yetu na kama tuna nia ya kweli ya kutaka mwananchi wa kawaida afaidike.
 
Nimefurahi kuona kwamba mafunzo haya yanaendeshwa na Chuo cha Serikali za Mitaa – Hombolo.  Hombolo wana uzoefu mkubwa katika hili, na nina uhakika kwamba Waheshimiwa Madiwani watafaidika kutokana na mafunzo haya.  Rai yangu ni kwamba kinachofundishwa hapa hakitakiwi kuishia hapa, bali utekelezaji wake unatakiwa kwenda katika maeneo ya wananchi mnaowawakilisha. Hao wananchi ndio wenye nchi, na hivyo wanastahili kufaidi matunda ya nchi yao.
 
Tuna bahati kwamba wadau kama USAID wanaona umuhimu wa mafunzo haya kufanyika, hivyo basi na sisi tusiangushane, bali tuwe mabalozi wema katika harakati za kutetea Utawala Bora unaoshirikisha wananchi kikamilifu, ili hata Madiwani wa Halmashauri zingine nchini wakiwatazama waone tofauti, tena tofauti chanya.
 
Ndugu Washiriki,
Lengo la kuwajengea uwezo Waheshimiwa Madiwani linatokana na sababu zifuatazo:- 
 
1.               Madiwani waliochaguliwa ama kuteuliwa, wanatokana na taaluma na fani tofauti-tofauti, hivyo upo umuhimu wa kuwajengea uwezo, kuwapa maarifa na mtazamo wa pamoja juu ya usimamizi na uendeshaji wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa, Muundo wa Serikali za Mitaa, Sheria za Serikali za Mitaa, na masuala mtambuka katika jamii, ikiwemo masuala ya Ukimwi, Jinsia, na Makundi Maalum.
 
2.               Madiwani ni wawakilishi wa wananchi, na wana madaraka ya kisheria ya kuzisimamia mamlaka ya Serikali za Mitaa kupitia vikao mbalimbali vya Kisheria.
 
3.               Katika kutekeleza majukumu yao, Madiwani wanahusika pia katika maeneo ya Utawala Bora na Ushirikishwaji wa Wananchi, Usimamizi wa Rasilimali Watu na Rasilimali Fedha.
 
4.               Mafunzo haya yanalenga kuwajengea Waheshimiwa Madiwani misingi thabiti katika usimamizi wa rasilimali za Halmashauri na Serikali za Mitaa kwa ujumla.
 
5.               Mafunzo yanalenga kuwajengea uwezo wa kuhoji na kusimamia mambo mbalimbali katika Halmashauri kupitia vikao, na kuzingatia taratibu za uendeshaji wa vikao katika Halmashauri.
 
6.               Mafunzo yatasaidia kuwawezesha Waheshimiwa Madiwani kujifunza mbinu za ushirikishaji na uhamasishaji wa jamii kushiriki katika uibuaji na usimamizi wa miradi ya maendeleo.
 
7.               Mafunzo yatawajengea uwezo Wah. Madiwani katika masuala ya Usimamizi wa Fedha, Uibuaji wa Vyanzo vya Mapato, na Usimamizi wa Manunuzi ya Umma katika MSM.
 
Ndugu Washiriki,
Binafsi kama Kiongozi wa Serikali katika Mkoa wa Iringa, natarajia kuona mafunzo haya yanatumika kama ilivyokusudiwa, Madiwani wanapata uelewa na maarifa kuhusu uendeshaji wa MSM.
 
Katika kumalizia, nawashukuru sana wafadhili wa Mradi huu ambao ni Watu wa Marekani kupitia Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID), na timu nzima ya Mradi wa PS3.
 
Iringa ipo tayari kufanya kazi na mradi huu na tunasema asante kwa kuja kujiunga nasi katika harakati zetu za kuhahakikisha kwamba Mkoa wetu unakuwa mbele katika kusukuma maendeleo ya nchi yetu kuelekea katika kuwa nchi ya uchumi wa pili ifikapo mwaka 2025.
 
Baada ya kusema haya, naomba nitamke rasmi kwamba mafunzo haya yamefunguliwa rasmi.
 
Asanteni kwa kunisikiliza.

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE