April 19, 2017

MIRADI YA UJENZI WA MASOKO ISIYO RAFIKI NA WANANCHI ILIVYOPOTEZA MAMILIONI YA SHILINGI IRINGA

Na Francis Godwin wa matukiodaima.com,Iringa

MIRADI  ya  ujenzi  wa masoko isiyoshirikisha  maamuzi ya  wananchi  imeendelea kuipotezea mamilioni ya  shilingi Halmashauri  ya Iringa  na Halmashauri  ya  Manispaa ya  Iringa kwa  kujenga  masoko yasiyotumika  kutokana na kutokuwa kipaumbele  halisi cha  wananchi  wa  wilaya  hiyo.

Kwa  kawaida  mradi  wowote  wa  kimaendeleo  unaotokana na fedha  za  wahisani  kama  vile miradi ya  TASAF  ,DADS na DADPS  imekuwa  ikiendeshwa kwa ushirikiano  wa  wananchi  wenyewe  na  miradi  hiyo kwa asilimia  zaidi ya 60  imekuwa  ikiibuliwa na  wananchi  wa maeneo  husika  kulingana na mahitaji  yao na  si vinginevyo.

Miradi  mingi ambayo  imeanzishwa kwa  matakwa ya   wananchi wenyewe kwa   kwa maeneo mbali mbali  ya  mkoa  wa Iringa  imeonekana  ni ukombozi mkubwa   kwa  wananchi  wanaozunguka  miradi  hiyo na hata  baadhi ya  miradi  kufanikisha  kuwakomboa  wananchi hao na hali duni ya maisha .

Japo  baadhi ya miradi iliyojengwa kwa matakwa  ya viongozi bila  kuwepo kwa ushirikishwaji mzuri  wa  wananchi imeonekana kukwama  na  kutokuwa na msaada  wowote kwa  wananchi wanaozunguka miradi hiyo na badala  yake  badala ya  kutumia fedha  hizo  kuwakomboa  wananchi serikali  imejikuta  ikilaumiwa na  wananchi kwa kuanzisha  mradi ambao  si  hitaji lao.

Pia  ukitazama  sera  za  miradi  kama  TASAF na mingine  zinatamka   wazi  kuwa  wananchi  wanapaswa kuchangia nguvu  zao  katika uanzishwaji  wa  miradi hiyo jambo ambalo sehemu kubwa ya  miradi  hiyo ilipofanikiwa  wananchi  walipata kushiriki  vema  ila kwa maeneo ambayo miradi haikufanikiwa hadi  sasa  kuna migogoro  isiyo kwisha kati ya  viongozi wa vijijini na  Halmashauri kutokana na  kulazimisha miradi ambayo kwao  si hitaji la msingi.
Uchunguzi  uliofanywa na mwandishi  wa  makala  haya   katika miradi  ya ujenzi  wa masoko kwenye Halmashauri ya  Manispaa ya  Iringa na Iringa  vijijini  umebaini  kuwepo kwa baadhi ya masoko ambayo  yalijengwa kati ya  mwaka  2007 hadi 2009 yakiendelea  kubaki kuwa makazi ya  ndege na wanyama wa  porini kutokana na kutotumika na   wananchi wanaozunguka masoko  hayo.
Sarah Sanga  ni  mkazi  wa Tagamenda  katika  Halmashauri ya wilaya  ya  Iringa vijijini  anasema kuwa  Halmashauri  hiyo  ilipata  kuwajengea  soko  lililokamilika mwaka 2009 ila ni  kama  wiki  mbili pekee ndizo  wafanyabiashara   waliweza  kuingia  kufanya kazi katika soko hilo kabla ya  kuondoka na  kurudi katika eneo lao la mwanzo.

Anasema  kuwa  tatizo lililopelekea   kutoendelea  na biashara katika  soko hilo ni kuwa  mbali na makazi  ya   watu na hivyo  kukosa wateja  japo  wananchi   walishirikishwa katika  ujenzi  japo  baadhi  walikuwa wakipinga soko  hilo kujengwa  eneo hilo ambalo ndilo ardhi  ilipatikana .

“Hili  soko  sisi tulipendekeza  lijengwe eneo letu la biashara  ambalo ni  mita kama  800 kutoka eneo  hilo ila wao  walilazimisha  kujengwa hapa ….lakini tunajengewa  soko  bila  kupewa mitaji  tutaunza nini hapa  sokoni  wakati  sisi  biashara  zetu ni za  magengeni  na si za kuweka sokoni kama  wao  walivyotujengea  soko”
Hata  hivyo  alisema  ni vema  eneo hilo la soko ili  kuweza  kuwavuta  wateja  zaidi na  wafanyabiashara  wakageuza majengo hayo ya  soko kuwa klabu cha  pombe za  kienyeji  ambayo ndio  ina  soko kubwa katika  kijiji  hicho.
Huku Lusajo kalinga ni  mkazi  wa  kijiji cha Muwimbi anasema  kuwa  wanashindwa kujua hatua ya  serikali  kujenga  soko  eneo la Ulete wakati  wakijua  mahitaji yao  eneo hilo hayakuwa ni  soko bali  bali ilikuwa ni hitaji la maji  safi na  salama ya  bomba  kwa  kipindi  hicho .

Hivyo alisema  sababu  ya  kushindwa  kuendelea  kwa  soko hilo ni kutokana na wananchi wa  eneo hilo  kutokuwa na tabia ya kuuza biashara  zao eneo la pamoja  zaidi ya  kila mmoja kuuza  kivyake mitaani na  baadhi  huuza  bidhaa zao katika klabu  cha  pombe ambako  wateja  huwa wengi zaidi  ukilinganisha na eneo hilo la soko ambalo mfanyabiashara  anaweza  kukaa kwa siku  nzima  bila  kupata  mteja.

Nae Zuwena Mussa  ni mmoja kati ya  wananchi  wanaojishughulisha na biashara  ndogo ndogo  nje  ya soko la  Magari mabovu  kati ya Miyomboni Kitanzini katika Halmashauri ya Manispaa ya  Iringa anasema kuwa  soko  hilo linaendelea  kuchakaa bila  wafanyabiashara  kutumia  kutokana na wafanyabiashara ndogo ndogo  kuogopa  kulipa ushuru wa Tsh 500 pale  wanapoingia kufanya  biashara  katika soko hilo huku  biashara  zao utokaji  wakiwa ndani ya  soko  hilo ni mdogo  zaidi.

Hivyo  anashauri  uongozi  wa Manispaa ya  Iringa kuangalia matumizi  mengine ya  soko  hilo ikiwa ni pamoja na  kufanya tathimini ya  kutosha na kuona eneo  hilo lingeweza  kutumiwa kwa shughuli  ipi  zaidi ya  soko ambalo wafanyabiashara  wameona kama ni mzigo kwao.

Mwenyekiti wa  serikali ya  kijiji cha Tagamenda  Joel Mofuga anasema  kuwa  tatizo la  soko  hilo  la Tagamenda  kuendelea  kuchakaa  bila  kutumika na  wananchi  kugoma  kufanyia biashara  katika  soko  hilo na badala  yake  kuendelea  kulipa ushuru wa Tsh 500 kwa mtu  binafsi ambae anamiliki  nyumba  aliyoijenga  kama  sehemu ya matumizi ya klabu  cha  pombe za kienyeji ambalo ni eneo  lililochangamka  zaidi.

Mofuga  anasema kuwa hivi   sasa mkakati  wa kijiji  hicho katika  soko hilo ni  kupigania  kuingiza umeme katika  majengo hayo  ili  kubadili matumizi ya  soko na kuweka shughuli kama za uungaji wa vyuma ,mashine za kukamua  alizeti  na shughuli nyingine rafiki na  wananchi  badala ya kuendelea  kuliacha  soko hilo  likiendelea kuchakaa.

Hata  hivyo anasema  mradi ambao  ungeweza  kuwakomboa   wananchi wa  eneo hilo ambao  wengi  wao  ni wakulima  ulikuwa ni mradi  wa bwawa la maji ambalo  lingeweza  kutumika kwa  kilimo cha umwagiliaji na  kuwaongezea kipato  zaidi  wananchi wa  eneo hilo.
Mstahiki  meya  wa Halmashauri ya  Manispaa ya  Iringa Aman Mwamwindi anasema kuwa soko  hilo la  magari mabovu limejengwa na  Halmashauri  kwa msaada  wa SIP kupitia  mradi  wa Mazingira  na kuwa mkakati wa  kulifufua unafanyika  ikiwa ni pamoja na kuangalia shughuli ambayo inaweza  kufaa eneo hilo na  moja kati ya shughuli ambayo  wanataka  kuiweka  hapo ni pamoja na kuwatoa  wauza samaki wote mitaani na kuwapeleka  eneo hilo na  likawa maarufu kama  soko la  samaki katika Manispaa ya  Iringa.
Abel Mgimwa ni afisa mipango  wa Halmashauri  ya wilaya ya  Iringa na kaimu mkurugenzi  wa Halmashauri hiyo anasema  kuwa katika Halmashauri  yake  kuna masoko matano  ambayo  yamejengwa kwa  ufadhili  wa DADS na masoko matano mengine yamejengwa  kwa ufadhili wa mradi wa DADPS .
Anataja  masoko ambayo yamejengwa na DADS kuwa ni Muwimbi, Ifunda kibaoni , Ilolompya,Itunundu na Tungamalenga na  kuwa kati ya masoko  hayo   ni masoko mawili ambayo  hayatumiki kabisa  likiwemo soko la Muwimbi na  Ilolompya  wakati mengine yanatumika  vema.
Wakati  kwa mradi  wa DADPS masoko  yaliyojengwa ni  Tagamenda , Ng’enza,Ndiwili  , Luganga na Kitayawa  na  kuwa masoko ambayo hayatumiki baada ya  kujengwa ni Tagamenda na Ndiwili wakati yaliyobaki yanatumika  japo si kwa asilimia  kubwa .
Mgimwa ambae  ndie  alikuwa msimamizi mkuu wa ujenzi  wa masoko  hayo anasema  kuwa ujenzi  huo  umeanza kati ya mwaka 2007  kukamilika mwaka 2009 na  kuwa ukiacha soko la Ifunda  Kibaoni lililojengwa kwa Tsh milioni 38. 9 masoko  mengine yote  yamejengwa kwa zaidi ya  Tsh milioni 64 fedha  kutoka kwa  wahisani.
Pia  anasema  kuwa si  kweli kama  wananchi  hawakushirikishwa katika ujenzi huo kwani  kabla ya  kuanza  ujenzi vikao  vilifanyika na  wao kuonyesha maeneo  ya  ujenzi ila  baada ya  kujengwa  ndipo  walipoanza kususa  kufanya biashara katika masoko hayo .
Anasema  kuwa lengo la  kujenga masoko  hayo ni kuweza  kuwakomboa  wananchi na ambao  wengi  wao  ni wakulima na masoko  hayo  yangewasaidia  kuuza mazao  yao  bila kuibiwa na  wafanyabiashara  ambao wamekuwa  wakinunua mazao majumbani kwa bei  wanayoitaka  wao  kuwa  iwapo mfanyabiashara angefika katika masoko  hayo angeweza  kununua mazao kwa  bei elekezi na sio bei anayoitaka  yeye.
“Kwa hiyo  uwezekano  wa  wakulima  kupunjwa  bei na  wafanyabiashara ingepungua  na kwa  wafanyabiashara  wangeepuka  usumbufu wa  kuzunguka kutafuta  mazao mitaani …..japo  sitaki  kuamini kama  fedha  za ujenzi  wa masoko  hayo zimepotea kwani  tayari Halmashauri  imeanza  kuunda kamati za watumiaji wa masoko hayo  ili  kufufua masoko  yaliyokufa kama  sehemu  ya  kipato cha Halmashauri  pia”anasema  kuwa 
Aidha  anasema  kuwa  iwapo  Halmashauri za vijiji zingeweza  kutumia  kutumia  vema  masoko  hayo pia  wangeweza  kupata mapato  ya  vijiji  kutokana na makusanyo  hayo  kutokana na sehemu kubwa ya asilimia ya kama 20 huenda Halmashauri na vijiji hupata asilimia 80  makusanyo  hayo.
Hata  hivyo alisema kwa  sasa mradi wa DADS  uliisha  toka mwaka 2009 waliondoka na kufunga kazi zao katika mkoa  wa Iringa na  fedha  zilizotakiwa  kulipwa  ziliachwa na tayari  zimelipwa kote wanakodaiwa.
Japo  alisema mradi wa DADPS hadi  sasa bado hawajapata   fedha  yoyote japo kuna taarifa  zisizo rasmi kuwa  mradi  huo awamu ya kwanza  ulionyesha  kushindwa  kufanya kazi vema .
www.matukiodaima.com   0754 026299
 
Nipo ndani  ya  siku 14  nilizopewa na Halmashauri ya  Iringa  kukanusha habari  ya  ubovu wa  jengo la biashara lililopo  eneo la stendi kuu Manispaa ya  Iringa  usikose Kesho nakuja na taarifa  nyingine ndani ya  siku 14  nitafanya kazi Halmashauri  ya  Iringa  kuibua habari  wasizozipenda ila  wananchi  wanazipenda

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE