March 27, 2017

WATUMISHI WA WIZARA YA FEDHA WATAKIWA KUSIMAMIA UKUSANYAJI MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA ZA SERIKALI

*Na Benny Mwaipaja, WFM-Morogoro*

Watumishi wa Wizara ya Fedha na Mipango nchini wametakiwa kuendelea kuunga
mkono juhudi za Serikali za kuiletea nchi Maendeleo ya haraka kupitia
falsafa ya uchumi wa viwanda utakao iwezesha nchi kuwa ya uchumi wa kati
ifikapo mwaka 2025 kwa kusimamia ukusanyaji wa mapato ya Serikali na
kusimamia matumizi yake ipasavyo.

Rai hiyo imetolewa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango,
katika Hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo
Bi. Dorothy Mwanyika, wakati akifungua mkutano wa 13 wa Baraza la
Wafanyakazi wa Wizara hiyo unaofanyika mjini Morogoro kwa siku mbili.

Bi. Mwanyika amesema kuwa Mabaraza ya wafanyakazi sehemu za kazi, yana
malengo ya kuongeza tija, ufanisi na ushirikishwaji wa wafanyakazi katika
uongozi wa pamoja mahali pa kazi kama agizo la Rais Na. 1 la mwaka 1970
likisomwa pamoja na miongozo mingine linavyo elekeza.

Aidha amewataka wajumbe wa Baraza hilo kukumbuka maelekezo ya viongozi
wakuu wa nchi wakiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.
Dkt. John Pombe Magufuli, kuhusu kusimamia ukusanyaji wa mapato na nidhamu
ya matumizi ya Fedha za Umma, ili kujenga uchumi wa Viwanda na kufikia
maendeleo stahiki.

“Tuunge mkono juhudi za Serikali kwa kutafsri maelekezo ya viongozi kwa
vitendo ili kuthibitisha msemo usemao Wizara ya Fedha na Mipango ndiyo moyo
wa Serikali” alisisitiza Bi. Mwanyika.


Pia Bi. Mwanyika amewashukuru viongozi wa Wizara hiyo kwa kufanikisha
mpango wa Serikali wa kuhamia Dodoma ambapo katika awamu ya kwanza
wafanyakazi 184 wameripoti mkoani humo licha ya kuwepo kwa changamoto
mbalimbali ikiwemo ukosefu wa makazi.

Hata hivyo amewataka watumishi hao
kushirikiana katika kutatua changamoto hizo kwa pamoja.

Kwa upande wake Katibu wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo Bw. Cyprian
Kuyava, amebainisha mafanikio yaliyopatikana kutokana na maazimio
mbalimbali ya Mkutano uliopita wa mwaka 2015/2016 kuwa ni pamoja na
kuboresha huduma kwa watumishi, kuboresha mazingira ya kazi na kuongezeka
kwa mshikamano miongoni mwa wafanyakazi licha ya ufinyu wa Bajeti.

Naye Mkurugenzi wa huduma za Sheria wa Wizara ya Fedha na Mipango Bi Susana
Mkapa amesema Watumishi wa Wizara hiyo wako tayari kuunga mkono juhudi za
Serikali za ukusanyaji wa mapato, kubana matumizi na hatua ya Serikali
kuhamia Dodoma.

Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Fedha unafanyika kwa siku
mbili kuanzia Machi 27 hadi 28, 2017, huku ajenda kuu ikiwa kufanya mapitio
ya utekelezaji wa Bajeti ya Mwaka 2016/2017 na kujadili makadirio ya bajeti
ya mwaka 2017/2018.

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE