March 19, 2017

MADAWATI YALIYOTENGENEZWA KWA AGIZO LA MAGUFULI KILOLO YANYESHEWA NA MVUA ,WANAFUNZI WASOMEA CHINI YA MITI .....

Wanafunzi wa darasa la tatu shule ya Msingi Igunda kata ya Nyanzwa  wilaya ya  Kilolo  wakisomea chini ya  mti kutokana na uhaba wa  vyumba vya madarasa mawili katika shule hiyo Picha na MatukiodaimaBlog
Darasa la awali  shule ya msingi Igunda kata ya Nyanzwa  wilaya ya  Kilolo mkoani Iringa Picha na MatukiodaimaBlog

Mmilikiwa na mtandao huu  FrancisGodwin akitembelea shule ya msingi Igunda kata ya Nyanzwa wilaya ya  Kilolo mkoani Iringa 
...........................................................................................................................................
Na MatukiodaimaBlog

MADAWATI zaidi ya 50 yaliyotengenezwa kwa agizo la Rais Dkt John Magufuli kupitia pesa za mfuko wa jimbo la kilolo na fedha za wadau wa maendeleo yameendelea kuharibika nje na mvua kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa katika shule ya msingi Igunda kata ya Nyanzwa wilaya ya Kilolo mkoani Iringa.

Uchunguzi uliofanywa na mtandaowamatukiodaimaBlog katika shule ya Msingi Igunda umebaini uharibifu mkubwa wa madawati hayo.

Baadhi ya wazazi wanaosomesha watoto wao katika shule hiyo wamelalamikia hatua ya madawati hayo kuendelea kunyeshewa na mvua nje huku watoto wao wakisomea chini ya miti.

Amina Sanga alisema kuwa jitihada kubwa zilifanywa na mbunge wao Venance Mwamoto na viongozi wa wilaya ya kilolo wakiongozwa na mkuu wao wa wilaya Asia Abdalah kusimamia utengenezaji wa madawati ila jitihada hizo ni bure.

Hivyo aliomba uongozi wa kijiji na kata kuanzisha mpango wa ujenzi wa vyumba vya madarasa ili kuondoa kero ya watoto kusomea nje chini ya miti.

Kwani alisema hatari kubwa ya wanafunzi hao kusomea chini ya miti ni kupigwa na radi hasa kipindi hiki cha mvua kubwa.

Pia kuhusu madawati hayo alisema bila kuchukua hatua za haraka pesa iliyotumika kutengeneza madawati hayo itapotea kwa kipindi kifupi.

Huku mkuu wa shule hiyo akigoma kuzungumzia changamoto hiyo ya wanafunzi wa darasa la tatu na awali kukaa nje pamoja na uharibifu wa madawati hayo kwa madai hana mamlaka ya kulizungumzia hilo pasipo ruhusa ya mwajili wake.

Akizungumza kwa njia ya simu juu ya madawati hayo kuendelea kuharibika na watoto hao kusomea chini ya miti mkuu wa wilaya ya Kilolo Ásia Abdalah na mbunge wa Kilolo Venance Mwamoto walisema Kuwa jitihada mbali mbali zinafanyika kutatua tatizo hilo.

Mbunge Mwamoto alisema awali tatizo lilikuwa ni madawati tayari kupitia pesa za mfuko wa jimbo amefanikiwa kutatua tatizo hilo.

Kuwa uongozi wa wilaya chini ya mkuu wa wilaya uliweza kusimamia vema zoezi hilo na sasa Kilolo hakuna tena mwanafunzi anayekaa chini ila baadhi ya shule madawati yamezidi hivyo zaidi ya wanafunzi.

"Mimi mbunge kazi yangu ni kuunga mkono shughuli za maendeleo zinazofanywa na wapiga kura wangu wao waanzishe ujenzi wa vyumba vya madarasa mimi nitafika kuwaunga mkono kwa vifaa vya viwandani kama bati na saruji "alisema Mwamoto

Kuwa tayari amekwisha changia shughuli za maendeleo kata mbali mbali za jimbo hilo ikiwemo kata hiyo ya Nyanzwa na ataendelea kuchangia kwani hapendi kuona wanafunzi wanateseka.

Kuwa hofu yake ni kuchakaa mapema kwa madawati hayo na iwapo viongozi wa kijiji wangebaini mapema kuwa mahitaji makubwa katika shulê hiyo ni vyumba vya madarasa basi toka mwanzo wangeelekeza nguvu katika ujenzi wa vyumba vya madarasa kuliko kuacha madawati yakinyeshewa na mvua na kupigwa na kwa.

Mkuu wa wilaya ya Kilolo Asia alisema kuwa toka ateuliwe na Rais Dkt Magufuli kazi yake kubwa yeye na mkurugenzi wa halmashauri hiyo kwa kushirikiana na viongozi wa kisiasa imekuwa ni kutatua changamoto ya vyumba vya madarasa ambayo ni kubwa katika wilaya hiyo.

Kuwa tayari amefanikisha kuwaingiza darasani wanafunzi wa Shule kama mbili ambao walikuwa wakisomea chini ya miti na zoezi la kutafuta  wadau  wa ndani ya  wilaya   hiyo na nje kwa ajili ya  kusaidia  ujenzi wa  vyumba  vya madarasa Kilolo unaendelea na amekwisha wafuata  wadau mbali mbali  jijini Dar es Salaam  kuomba msaada .


Shule  ya msingi ya msingi  Igunda ni shule ambayo ni mkondo B wa  shule ya Msingi Nyanzwa  iliyopo  umbali wa takribani Kilomita moja pekee  kutoka shule  hiyo na shule ya Nyanzwa  inavyumba vitatu vya madarasa ambavyo havitumiki  kwa mujibu wa mkuu wa shule ya msingi Nyanzwa Venance Mbogo.

Usikose Mwendelezo  wa habari  hii  endelea kutembelea matukiodaimaBlog kila  wakati iwapo una taarifa zozote ama tangazo kwa  ajili ya kutangaza picha simu 0754026299 
Email;fgodwin94@gmail.com

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE