February 15, 2017

RC MASENZA AAGIZA SHULE YA SEKONDARI ISMANI KUWA YA 10 BORA KITAIFA,AZUIA MAANDAMANO YA WALIMU MKOANI IRINGA

RC  Iringa Amina Masenza

  Walimu  wa  shule ya sekondari  Ismani na  watumishi  wa  mkoa wa Iringa katika kikao  cha mkuu wa mkoa

Na MatukiodaimaBlog

MKUU wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza amewataka Walimu wa Shule ya sekondari Ismani wilaya ya Iringa kukutana kuweka mikakati itakayo iwezesha Shule hiyo kuingia katika Shule 10 bora Kitaifa.

Huku akipiga marufuku maandamano ya Walimu ndani ya Mkoa wa Iringa kwa kisingizio cha kudai haki  pasipo wajibu.

Akizungumza Leo na Walimu wa Shule ya sekondari Ismani Mkuu huyo wa Mkoa alisema amepata kusikia katika Vyombo vya Habari kuwa kuna Walimu wanahamasishwa kufanya maandamano ya kudai Haki zao.

Alisema kuwa kimsingi hakuna Kiongozi anayewazuia na asiyependa Walimu waliotimiza wajibu wao  na kufuata taratibu za kudai madai yao kunyimwa haki  yao.

Hivyo haoni sababu ya wao kuandamana barabarani badala ya kutumia njia sahihi ya kuikumbusha serikali kuwalipa madai yao bila wao  kuandamana.

Mkuu huyo wa Mkoa alisema baadhi ya Walimu madai yao wanayodai hayapo kwenye mafaili yao na hayatambuliki hivyo kwa wakati mwingine mwalimu anapokwenda kutibiwa nje ya kituo  chake  cha kazi ni lazima aende kwa utaratibu na kumbukumbu za madai yake  kuweka kwenye faili  lake.

Pia alisema lazima kuweka mkakati wa Walimu kujiwekea mikakati ya kuifanya Shule hiyo kuwa nafasi ya 10 bora na njia pekee ambayo amewaagiza wakurugenzi ni kuingia mikataba na Walimu hao na yeye kuingia mkataba na wakuu wa wilaya.

Kwa Walimu alitaka kuendelea kuongeza jitihada za kufundisha ili hata wale wenye  Sifa ya kupandishwa daraja wapandishwe kutokana na uwezo wao  kikazi na si vinginevyo.

Alisema kuwa suala la Walimu kupandishwa madaraja limesitishwa kwa ajili ya kupisha uhakiki wa watumishi hewa na baada ya kukamilisha zoezi hilo  watafahamishwa wote wenye  Sifa ya kupandishwa daraja.

Aidha alionya Walimu kuendelea kupoteza muda wao kwa kushinikizwa kufanya maandamano.

"Najua kuna mtu  yupo nyuma yenu anawachochea kufanya mgomo huu ila  yeye si mwalimu na hana madai yoyote anayoidai serikali"

Kuhusu upungufu wa Walimu wa somo  la Sanyansi na Hesabu kwa Shule hiyo yenye Walimu wanne pekee alishauri uongozi wa Shule hiyo kuendelea kuwatumia Walimu wa Chuo cha Mkwawa ambao wapo masomoni kwa ajili ya kupunguza upungufu wa Walimu shuleni hapo.

Awali akizungumza na wanafunzi wa Shule hiyo mkuu  huyo wa Mkoa  aliwataka wanafunzi hao kusoma  kwa juhudi na kuachana na mafataki wakiwa Shule.

Kwa upande wake mwalimu Erick Mlelwa alimwomba mkuu  huyo wa mkoa  kumsaidia kufuatilia sababu za kusitishiwa mshahara wake kwa zaidi ya miezi nane  sasa.

Akimjibu mwalimu huyo baada ya taarifa toka kwa Afisa elimu sekondari wilaya kuwa alisitishiwa mshahara kutokana na utoro alisema kuwa alichokitafuta mwalimu huyo amekipata kutokana na utoro wake ambao hata yeye hakubali kuona mtumishi mtoro katika Mkoa wake.

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE