February 24, 2017

MAUAJI YA MPELELEZI WA POLISI PWANI YAHUSISHWA NA UGAIDI

Image result for UGAIDIWAKATI watu watatu akiwemo Ofisa Upelelezi wa Wilaya (OC CID) wa Wilaya ya Kibiti mkoani Pwani, Mrakibu wa Polisi, Peter Kubezya, wakiuawa kwa risasi usiku wa kuamkia jana, serikali imesema itawasaka na kuwatia nguvuni wote waliohusika na mauaji hayo yanayohusishwa na matukio yenye mwelekeo wa kigaidi.
Wengine waliouawa ni Ofisa wa Misitu ambaye alikuwa Mkaguzi wa Kituo cha Ukusanyaji mapato ya ushuru katika Kijiji cha Jaribu, Peter Kitundu na Rashid Mgamba ambaye ni mlinzi/mgambo ambao walipigwa risasi kichwani na begani na walikufa papo hapo eneo la tukio.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Bonaventura Mushongi alisema mauaji hayo yalitokea juzi Februari 21, mwaka huu saa 2:00 usiku eneo la Kituo cha kutoza ushuru wa mazao ya kilimo na misitu kilichopo Kijiji cha Jaribu Mpakani, Kata ya Magawa Tarafa na Wilaya ya Kibiti baada ya watu wasiojulikana kuvamia hapo.
Kamanda Mushongi alisema watu hao wanasadikiwa kutumia silaha aina ya SM/SAR na walitumia pikipiki mbili zenye namba za usajili MC 853 AHH aina ya Toyo na MC 799 aina ya Sanlg ambazo walizokuwa wakizitumia na kuzitelekeza eneo la tukio huku wao wakikimbia kwa miguu.
“Wakati tukio la uvamizi huo likiendelea, Kubezya alifika akiwa na polisi wengine ili kuwakabili wahalifu ndipo walipomjeruhi kwa risasi kiunoni wakati wa majibizano ya risasi na kumjeruhi na kufariki dunia wakati akipelekwa Hospitali ya Misheni ya Mchukwi iliyopo Kibiti kwa matibabu zaidi,” alifafanua Kamanda Mushongi.
Alisema watu hao baada ya tukio hilo waliwaita wananchi wachukue mkaa na mazao ya misitu na wahalifu hao waliacha vipeperushi kupinga uwepo wa kizuizi hicho, na kwamba uchunguzi wa awali unalihusisha tukio hilo na matukio yenye mwelekeo wa ugaidi.
Akizungumza wakati alipotembelea eneo hilo la mauaji jana asubuhi, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba alisema serikali haiwezi kuvumilia kuona mauaji kama hayo yakiendelea, huku serikali ikiwa mbioni kuunda Polisi Kanda Maalumu ya Pwani kama njia mojawapo ya kukabiliana na uhalifu.
“Hatutaruhusu hali hii iendelee, tutawasaka na kuwakamata wote waliohusika na mauaji hayo pamoja na wale wanaoshirikiana nao. Serikali haiwezi kuvumilia kuona kwamba mauaji kama haya ya kipuuzi yakiendelea nchini. Tutapambana nao,” alisema Mwigulu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo alikerwa na kitendo cha wananchi wa eneo hilo kwenda kuchukua mkaa na mazao ya misitu wakati maiti zikiwa zimelala chini na huku wauaji wakiwa katika eneo hilo, kitendo kilichoonesha kutokuwana uchungu na hali iliyotokea.
Wakazi wa Mkuranga na Rufiji wameeleza masikitiko yao kutokana na mauaji yanayojitokeza kwa wingi katika siku za karibuni ambayo yameshuhudia pia wenyeviti wa vijiji na watendaji wakiuawa, na kuna madai kuwa Kijiji cha Jaribu Mashariki hakuna mtendaji wala mwenyekiti, wote wamekimbia kuhofia usalama wao.

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE