February 16, 2017

MAREKANI HAIWEZI KUSHIRIKIANA NA RUSSIA KIJESHI

 
Jim Mattis
Jim Mattis

“Hatuwezi hivi sasa kushirikiana kijeshi. Lakini viongozi wetu wa kisiasa wataendelea kuwasiliana na kutafuta mwafaka,” Mattis amesema hayo katika mkutano na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya majeshi ya kujihami ya nchi za magharibi NATO, Brussels.

Kabla ya ushirikiano wa kijeshi kufanyika, Russia lazima “ithibitishe” iko tayari kuheshimu sheria za kimataifa, Mattis amesema.

Russia Inataka Ushirikiano
Maoni ya Mattis yamekuja baada ya Waziri wa Ulinzi wa Russia Sergei Shoigu kusema Moscow “iko tayari kurejesha ushirikiano na Pentagon.”

Rais Donald Trump alimsifia Kiongozi wa Russia Vladimir Putin wakati wa kampeni na kuendelea kufanya hivyo baada ya kuchukua madaraka na amesema anapenda kuanzisha ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.


Marekani ilisitisha ushirikiano wake wa kijeshi na Russia mwaka 2014 baada ya nchi hiyo kuvamia eneo la Crimea nchini Ukraine.

Udukuzi wa Mitandao Waongezeka
Katika siku ya pili ya mazungumzo ya mawaziri wa NATO Alhamisi Brussels, Katibu Mkuu wa NATO Jenerali Stoltenberg amesema watazungumzia jinsi ya kuzuia kuongezeka kwa udukuzi wa mitandao dhidi ya serikali mbalimbali.

Mattis amesema anaamini NATO inaouwezo wa kupambana na tishio hilo la udukuzi wa mitandao, na amesema marafiki zake wamepokea ujumbe wake vizuri siku iliyopita kuhusu kushirikiana katika gharama za ulinzi.

“Tulizungumza kuhusu kuongezeka kwa uadui unaoukabili umoja wetu, na umechanganyika na vitisho dhidi ya demokrasia yetu na naona ni ushirikiano imara peke yake unaweza kutuondolea hatari hizi zinazoongezeka,” amesema Waziri huyo.


Ombi la Trump na Mattis
Trump na Mattis kwa pamoja wamezihimiza nchi nyingine za NATO kugharamia kifedha taasisi hiyo.

Mnamo July, wakati Trump akiwa mgombea urais alileta mtaharuki Ulaya yote alipopendekeza kuwa Marekani haitoshiriki kulinda wanachama wa Umoja wa NATO ambao hawatoi michango yao.

Marekani Kupunguza majukumu yake

Siku ya Jumatano, Mattis amewatahadharisha mawaziri wa NATO kuwa Washington itapunguza majukumu yake” kwa umoja huo iwapo wanachama hawatatoa kiwango cha asilimia mbili ya pato la taifa kutoka kwenye bajeti zao.

“Marekani itatekeleza wajibu wake, lakini kama mataifa yenu hayataki kuona Marekani ikipunguza majukumu yake katika Umoja huo, kila nchi inatakiwa kuonyesha kwa vitendo inasaidia kwa ajili ya ulinzi wetu wa pamoja,” Mattis amewaeleza mawaziri Jumatano katika mkutano wa faragha.

Mattis hajafafanua ni vipi Washington itabadilisha majukumu yake kwa umoja wenye wanachama 28.

Nchi Zinavyo Changia

Kati ya wanachama wa NATO watano ambao wanatekeleza ahadi zao ni Greece, ambayo inalipa takriban asilimia 2.5, na Poland, Estonia na Uingereza inalipa juu kidogo ya kiwango kinachotarajiwa cha asilimia mbili.


Kwa upande wa wale wasio fikisha kiwango kilichowekwa, Ujerumani inalipa chini ya kiwango kwa asilimia 1.19 na wengi ikiwemo Canada, Itali na Spain inalipa chini ya kiwango. Ufaransa inalipa chini kidogo ya asilimia mbili.
Marekani inalipa zaidi ya asilimia 3.6 ya pato lake la taifa.(Chanzo VOA)

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE