February 16, 2017

MAKAMU WA RAIS AZUNGUMZIA DAWA ZA KULEVYA NCHINI

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan ameunga mkono jitihada za kupambana na dawa za kulevya nchini kama hatua ya kuliokoa na taifa janga hilo ambalo limesababisha madhara makubwa katika jamii.
Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na watendaji wa halmashauri ya wilaya ya Ilemela, Mkoani Mwanza.
Makamu wa Rais amesisitiza kuwa mapambano dhidi ya dawa za kulevya yatakuwa ni endelevu lengo likiwa kukomesha kabisa uuzaji,usambazaji na utumiaji wa dawa hizo kama hatua ya kuokoa kizazi cha sasa na kijacho nchini.
Amesema kamwe serikali ya wamu ya Tano hatarudi nyuma katika vita dhidi ya dawa za kulenya na ameomba wananchi waendelee kutoa taarifa za siri kwa vyombo vya dola zitakazosaidia kuwabaini watu wanajihusisha na biashara hiyo ili waweze kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Kuhusu tatizo la uvuvi haramu, Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amewaagiza viongozi wa mikoa ya kanda ya Ziwa wakiwemo viongozi wa Mwanza na mikoa mingine nchini kuanzisha mara moja oparesheni kali ya kupambana na wavuvi haramu katika Ziwa Victoria ambao wamechangia kwa kiasi kikubwa kupungua kwa samaki katika Ziwa hilo.
“Viwanda vya samaki kwa sasa havipati samaki wa kutosha hali ambayo imezorotesha shughuli za kuchakata samaki hivyo nawaagiza viongozi wote kupambana ipasavyo na wavuvi haramu na kamwe wasionewe huruma” amesisitiza Makamu wa Rais.
Makamu Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amesisitiza kuwa mapambano dhidi ya dawa za kulevya nchini ni muhimu yakaenda pamoja na oparesheni ya kukomesha uvuvi haramu katika Ziwa Victoria na maeneo mengine nchini.
Amesema wavuvi haramu wamechangia kwa kiasi kikubwa kupungua kwa samaki katika maziwa mbalimbali nchini kwa sababu wanatumia nyavu haramu ambazo zinaharibu mazalia ya samaki hivyo ni lazima hatua stahiki zichukuliwe dhidi yao ili kukomesha kabisa tatizo hilo.
Wakati huo huo halmashauri ya wilaya ya Ilemela, imetekeleza maagizo  14 yaliyotolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa mwaka jana alipofanya ziara ya kikazi wilayani humo likiwemo suala la watumishi wa halmashauri kukaa karibu na maeneo ya ofisi ambapo mpaka sasa wakuu wa idara 23 wanaishi ndani ya wilaya ya Ilemela ikilinganishwa na hapo awali ambapo watumishi hao walikuwa wanakaa nje ya wilaya hiyo hali ambayo inatajwa ilichangia kuzorotesha utendaji kazi kwenye halmashauri hiyo.
Kufutia hali hiyo, Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni mlezi wa halmashauri hiyo amepongeza viongozi wa wilaya hiyo pamoja na watendaji wa halmashauri kwa kutekeleza maagiza yake kwa haraka na kwa wakati.
Amesema yeye kama mlezi wa halmashauri hiyo atahakikisha halmashauri inafanya kazi kwa ubora wa hali ya juu katika utoaji wa huduma za uhakika kwa wananchi na kuondoa haraka changamoto mbalimbali zizowakabili wananchi hao ikiwemo uimarishaji wa miundombinu ya barabara.

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE