February 8, 2017

DAWA ZA KULEVYA WABUNGE FUNGENI MIDOMO MNAJIDHALILISHA


 Mwaka 2015 kipindi cha Kampeni za UCHAGUZI MKUU, wafuasi, wanachama, viongozi na wagombea wa CCM, na vyama vingine isipokuwa CHADEMA na UKAWA, tulitumia muda mwingi sana kuwaasa Watanzania wasiichague Chadema na UKAWA kwa kuwa Mgombea URAIS WAO, EDWARD LOWASSA amekuwa akituhumiwa kwa zaidi ya miaka nane mfululizo kuhusiana na kashfa mbali mbali za ubadhilifu, matumizi mabaya ya madaraka na kadharika.

Tulipambana kweli kweli (mimi nikiwa mmoja wao), kuwataka watanzania wasifanye makosa kuchagua mtu ambaye hatukuamini kama ni sahihi kuwa Rais.

Watanzania baadhi walituelewa, lakini wengine hawakutuelewa hata kidogo, walitukatalia kwa maneo, kwa vitendo na hata walipoenda kupiga kura walitukatalia kwa kupiga kura kumchagua Lowassa katika maeneo yao.

Unajua walichokuwa wanatujibu?. Walikuwa wanasema KWANZA CCM ING’OKE (IONDOKE MADARAKANI), ndio mambo mengine ya tuhuma, Ufisadi na kadharika yatafuata mbeleni huko.

Kipaumbele cha waliotukatalia hakikuwa Ubora wa LOWASSA, kipaumbele chao kilikuwa CCM kwanza Iondoke, maana waliichoka na hawakuamini kwamba kunaweza kutokea ama kupatikana mabadiliko ndani ya CCM, ndio maana walifunga masikio, wakawa wanaimba MABADILIKO LOWASSA na LOWASSA MABADILIKO.
Image result for MAKONDA
 Leo Paul Makonda ameamua kuongeza nguvu kwenye vita tulivyovipigia kelele muda mrefu, miaka nenda miaka rudi, VITA DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA.

MAKONDA ameamua/ amekubali kupuliza Filimbi, ili sisi wakimbiaji, wachezaji tukimbie na tuicheze vita hii iliyotungiwa kila aina ya sentensi.

Ukiondoa Marehemu Amina Chifupa, aliyeahidi kutaja majina ya wauzaji na wahusika wa biashara hii haramu hata kama ingekuwa mume wake, na kuonyesha kudhamiria kufanya hivyo kwa vitendo japo kabla hajafanikisha Umauti ukamfika.

Paul Makonda yeye ametenda, ameita waandishi wa Habari akawaambia kuwa tayari tumewakamata watu watano (akawataja majina), na wengine kadhaa tumewaita wafike polisi siku Fulani. Makonda ameamua kutenda, Lugha ya mtaani tunasema amejivika Mabomu.

Sisi ambao familia zetu, maisha yetu yamekutana na madhara ya moja kwa moja na utumiaji wa dawa hizi, hakika tumemuunga mkono MAKONDA, na tumemuunga mkono bila kujali amemtaja nani na kwanini, bila kujali ni halali kuwataja watu hadharani ama si halali sisi tumemuunga mkono kama wale waliosema CCM KWANZA ITOKE – MENGINE YATAFUATA

Tumeamua BIASHARA HII IKOMESHWE kwanza, Vita hivi vipiganwe kwanza halafu mambo Mengine yatafuata baadae.

 Ndio maana hatukujali wala kusikiliza pale Mbunge MSUKUMA alipoibua tuhuma dhidi ya MAKONDA,

Wala hatukuzijali Kejeli za Mbunge MDEE na BULAYA au MLINGA dhidi ya Vita hivi. Sisi tumeziba Masikio, hatutaki kusikia sauti mbilimbili kwenye vita Hivi, Tunachotaka Tushinde kwanza mambo mengine yafuate baada ya kushinda vita.

Tumeelewa kuwa Vita hivi sio vya makonda peke yake,wala si vya serikali pekee na tumeelewa kuwa WABUNGE WETU walishavishindwa vita hivi, tunajua kuwa wapo wabunge wanufaika wa biashara ya UNGA (kama wenyewe walivyotajana bungeni), wamebaki kubwabwaja tu kudai utawala wa sharia huku wenyewe hawazingatii huo utawala wa sharia.

Mdio maana tumeweka msisitizo kuwa TUSHINDE VITA VYA UNGA KWANZA mengine yafuate
Katika ufahamu wangu wa mapambano ya kihoja na kadharika, moja kati ya njia ya kumvuruga mpinzani wako ama kumshinda ni Kumvamia yeye, ilia ache ama atoke kwenye reli.

Ndio maana MSUKUMA alipomvamia Makonda tukamsikiliza na kumuacha kama alivyo (kwetu sisi Makonda anafaida nyingi kwa sasa kuliko hasara zake ambazo ni Binafsi),

 Leo tena nimesikia Muongozo uliobadilika njiani na kuwa HOJA, muongozo ama hoja iliyotolewa na Mbunge ULEGA wa Mkuranga iliyoungwa mkono na Msigwa wa Iringa mjini.

Ukiusikiliza Muongozo huo ulioombwa, unaweza ukahoji mara mbilimbili aina na kiwango cha uelewa cha wabunge wetu?, wanaonyesha DHAHIRI wabunge wetu wamepaniki,

 Inaonyesha wazi kwamba wabunge wetu ama wana chuki binafsi na MAKONDA au wanaona wivu agenda muhimu hii kwa taifa kushikiwa bango na mkuu wa mkoa tofauti na walivyozoea agenda kama hizi hushikiwa bango na Bunge (hii wameshindwa wenyewe).

Ulega analalamika eti makonda kawadhalilisha wabunge kuwaambia wanalalaga bungeni na kwamba wao ndio wasaidizi wema Rais Magufuli na hivyo Mwenyekiti change kuagiza kamati ya haki na maadili ya Bunge kumuandikia Makonda atoe Ufafanuzi.

 ULEGA na WABUNGE wetu, achene kujidhalilisha, kwani nani hafahamu kwamba wengi wenu hamna kazi Bungeni zaidi ya Kulala na kupiga makofi?, kwanini mnaukataa ukweli huu mchungu, embu ulega ingia mtandaoni andika www.google.com kisha kwenye eneo la kutafuta andika kwa Kiswahili ‘’WABUNGE WALIOLALA BUNGENI’’, zitakuja picha za wabunge mbalimbali wa Bunge letu linaloitwa tukufu wakiwa wanauchapa usingizi mnono, sasa kosa la makonda ni lipi hapo?.

Mbona inafahamika kwa sababu ya Kulala kwenu Bungeni na Kupenda kwenu kupiga piga makofi hata kwa mabo yasiyopaswa ndio maana mkashabikia BUNGE LISIONYESHWE LIVE KIPINDI CHA MIJADALA.

ULEGA na wabunge wenzako, kama kweli hamlali Bungeni na kukoroma, iambieni Serikali basi ionyeshe Bunge LIVE tuwaone mnavyochangia hoja, na muache kujirekodi kupitia simu zenu.

Mnasema makonda amewadhalilisha na kwamba kama alikuwa na mashitaka dhidi yenu angeshitaki kwa spika, mmesahau namna nyinyi mlivyomshambulia mkasahau kuwa kuna tume ya maadili ya viongozi wa umma?, si mngeenda kumshtaki kule na kuuhoji huo utajiri wake?.

Mliongea Bungeni ili iweje, si ili tusikie, sasa ninyi tumewasikia nayeye tumemsikia lakini kwa sasa tumefunga masikio tunataka tuishinde kwanza vita dhidi ya Dawa za kulevya.
Kama kweli wabunge mnaheshimu utawala wa sharia achene kutuhumu watu hovyo hasa ambao si wabunge,
Kama kweli mnaheshimu utawala wa sharia, waandikishieni mikataba ya kazi basi madereva wenu na muanze kuwalipa mishahara, (zaidi ya 70% ya madereva wa wabunge hawana mikataba ya kazi)
ULEGA na wabunge wenzako, sisi huku uswahilini ndio tunaojua kuwa mnatuwakilisha sawa sawa au mnatuzogoa tu, sisi tunajua nani mkweli nani muongo na kwenye hili lan UNGA mwacheni MAKONDA aendelee tu (bila kujali nani katuhumiwa).

Kwa kuwa madhara ya UNGA huikumba jamii hadharani, ni vema aendelee kuwasema hadharani, kama ambavyo tulimpigia makofi marehemu Amina alipotaka kuyataja majina hadharani ndivyo tunampigia makofi makonda anayeyataja hadharani tena ikiwa ni wastani wa miaka 10 baada ya Amina Chifupa Kufariki.

Kutuanzishia Mjadala mpya katikati ya Mjadala muhimu tena dhidi ya mpuliza filimbi wa mjadala huo(Makonda) ni sawa na kutoa tairi moja ya gari katika gari iliyoanza kushika kasi safarini - hakika wewe utaitwa muuaji.

Tumeshaamua, kuwa biashara ya madawa ya kulevya ni hatari na hatuitaki, hivyo hatuchagui namna ya kupambana nayo, tutaipinga kwa namna yoyote ile na yeyote atakayediriki kuturudisha nyuma katika vita hii tutamuhesabu kama ni sehemu ya wanaolea tatizo.

Wabunge wetu mmepoteza uelekeo, isimamieni Serikali kwenye masuala yanayotuhusu sisi wananchi moja kwa moja, kwa hili la UNGA serikali kupitia kwa makonda na polisi imejisimamia na tunaiunga mkono.
HATUTAKI SAUTI MBILIMBILI KATIKA VITA DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA
Ndimi
Habibu Mchange
Mwananchi
076217867

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE