Matukio Daima

Tembelea kila siku kwa habari na matukio mbali mbali..

Matukio Daima

Kwa Habari za Kitaifa.

Matukio Daima

Kwa Habari za Kimataifa.

Matukio Daima

Kwa Habari za Uchumi na Biashara.

Matukio Daima

Kwa Habari za Michezo na Burudani.

May 29, 2017

VYUO VIKUU DSM VYAMSIFU MAGUFULI


1
Rais wa Serikali ya Wanafunzi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DARUSO) akisisitiza jambo wakati wa mkutano na waandishi wa Habari uliofanyika leo Jijini Dar es Salaam ukilenga kutoa tamko la DARUSO kuhusu kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali hasa matokeo ya Tume ya kuchunguza kiwango cha madini kwenye makontena 277.Kulia ni Waziri wa Ulinzi wa Serikali hiyo Bw. Richard Augustine na kushoto ni Waziri Mkuu wa Serikali hiyo Bw. Sintau Fredrick
unnamed
 Rais wa Serikali ya Wanafunzi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DARUSO) akisisitiza jambo wakati wa mkutano na waandishi wa Habari uliofanyika leo Jijini Dar es Salaam .
(Picha  na Frank Mvungi-Maelezo)
…………………
Frank Mvungi-MAELEZO
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amepongezwa na Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (DARUSO) kwa kusimamia vyema rasilimali za Taifa ili ziweze kuwanufaisha watanzania wote.
Kauli hiyo  imetolewa leo Jijini Dar es Salaam na  Rais wa (DARUSO) Bw.John Jilili wakati wa mkutano wao na vyombo vya habari uliolenga kutoa tamko la kuunga mkono juhudi za Mhe. Rais kwa kuunda Tume iliyochunguza na kutoa matokeo kuhusu mchanga (makinikia) unaosafirishwa nje ya nchi.
“Kuanzia  sasa uchakataji (processing) ufanyike hapa nchini na mikataba yote iwe na kipengele kinachoyalazimisha makampuni yanayopewa leseni ya kuchimba madini kuwa na mitambo ya kuchenjua makinikia ya madini yanayozalishwa na migodi hiyo.” alisema  Jilili
Akifafanua zaidi Jilili amesema kuwa mikataba yote ya Madini ni vyema ikatazamwa upya na kuzingatia maslahi mapana ya Taifa na si ya watu wachache, kwani kwa kufanya hivyo kuonyesha dhamira ya dhati ya Serikali katika kuleta mageuzi katika sekta ya madini nchini.
Katika mapendekezo yao DARUSO imebainisha kuwa Watanzania wangependa kuona Mikataba na Sheria zilizopo zinaruhusu ukaguzi wa mara kwa mara migodini ili Serikali ijiridhishe kuhusu kiwango cha madini kinachozalishwa katika migodi hiyo pamoja na Serikali kuwa na ubia wa asilimia 50 au 49 na wawekezaji katika sekta ya madini.
Aidha Jilili alisema vyema pia kwa vyema kwa Viongozi wote waliopewa dhamana ya kuwaletea wananchi maendeleo wakatekeleza wajibu huo kwa uzalendo na kuepuka kuingia mikataba inayowezesha kuiletea hasara Serikali.
“Tunapenda kuwaomba watanzania wote wasomi na wasio wasomi kumsaidia Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli kufikia lengo lake la kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi na hayo yanawezekana tu kwa kuweka uzalendo mbele na maslahi ya Taifa kwanza.” Alisisitiza Jilili
Aliongeza kuwa nidhamu na uwajibikaji katika sehemu za kazi ni jambo la muhimu kwa Watendaji waliokabidhiwa majukumu ya kusimamia sekta mbalimbali kwani kwa kufanya hivyo  kutawezesha kuzaliwa kwa Tanzania mpya chini ya Uongozi wa Serikali ya awamu ya Tano.
“DARUSO inamthibitishia Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli na Watanzania wote kuwa iko sambamba nae katika harakati zake za kuikomboa nchi yetu katika Nyanja zote ikemo kiuchumi” Alisisitiza Jilili

KAULI YA KWANZA YA SIRRO KAMA IGP


1
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro amewasisitiza wananchi kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo kwa kutoa taarifa za wahalifu waliopo katika maeneo yao jambo ambalo litapunguza au kuondoa kabisa uhalifu nchini.
IGP Sirro ameyasema hayo leo Ikulu Jijini Dar es Salaam alipokuwa  akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuapishwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli kuwa Mkuu mpya wa Jeshi la Polisi la Tanzania.
Amesema kazi kubwa ya Jeshi la Polisi ni kulinda na kuhakikisha usalama wa raia na mali zao hivyo ni wajibu wa jeshi hilo kuhakikisha nchi nzima ina ulinzi wa kutosha utakaopelekea wananchi kuishi kwa amani na utulivu na kuwawezesha kufanya kazi zao bila kubugudhiwa.
“Uhalifu hauwezi kupungua kwa kutegemea Jeshi la Polisi pekee bali tunahitaji nguvu ya pamoja ili kushinda vita hiyo, ushirikiano wa wananchi unahitajika kwa kiasi kikubwa”,Alisema IGP Sirro.
Ameongeza kuwa kipaumbele cha kwanza katika utendaji wake kwenye  nafasi hiyo ni kupambana na uhalifu pamoja nidhamu ya watendaji kazi kwani bila nidhamu, kazi ya kupambana na wahalifu haiwezi kufanikiwa.
Aidha, amewahakikishia wananchi wa Mkoa wa Pwani ambao umekuwa na mauaji na uhalifu wa mara kwa mara kuwa atafanyia kazi changamoto zinazowakabili na  kuhakikisha wananchi wake wanaishi kwa amani na utulivu.
Kwa upande mwingine, IGP Sirro amemshukuru Rais Dkt. Magufuli kwa kumuamini na kumteua katika cheo hicho pia amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Paul Makonda kwa ushirikiano wake wakati alipokuwa akitumikia cheo cha Kamishna wa Polisi wa Kanda maalum ya Dar es Salaam.
Kabla ya uteuzi huo, IGP Sirro alishika nyadhifa mbali mbali zikiwemo za Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Kamanda wa kikosi cha operesheni maalum na Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es salaam.    

SERIKALI YAFUNGA MASHINE ZA KUDHIBITI EBOLA NCHINI

unnamed
Waziri wa Afya ,Maendeleo yajamii,Jinsia ,Wazee na Watoto Ummy Mwalimu akiongea mbele ya waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam kuhusu hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kujikinga na Ugonjwa wa Ebola  uliopo nchini Congo ili usiingie Tanzania.
…………………………
Na Ally Daud-WAMJW DAR ES SALAAM
SERIKALI imeongeza mashine nne za kupimia virusi vya ugonjwa wa Ebola katika mipaka ya Holoholo,Mutukula,Rusumo na Silali ili kudhibiti na kutambua hali ya maambukizi ya ugonjwa huo kwa wasafiri wa ndani na nje ya Tanzania.
Akizungumza hayo wakati wa mkutano na waandishi wa Habari leo jijini Dar es salaam Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amesema kuwa hatua mbalimbali zinachukuliwa kuhusu kujikinga na ugonjwa huo usiingie nchini.
“Moja ya hatua tuliyochukua kama Wizara ya Afya ni kuweka mfumo wa kufuatilia magonjwa (Intergreted Disease available system) na kujua  taarifa za wasafiri katika mipaka yote kwa  wanaotoka nchini Congo kuingia Tanzania ili kujua wanapotoka mpaka wanapofikia hakuna maambukizi ya ebola “ alisema Waziri Ummy.
Aidha Waziri Ummy amesema kuwa mbali na hatua hizo Serikali imegawa vifaa vya kujikinga na maambukizi ya Ebola ikiwemo gauni la kujikinga,mawani,mabuti pamoja na vidonge vya Chroline katika mipaka yote ili kuzuia maambukizi ya ugonjwa huo kwa watumishi wanaofanya kazi mipakani.
Kwa mujibu wa Waziri Ummy amesema kuwa wanaendelea kutoa elimu kwa kuweka mabango yanayohusu ebola katika mipaka yote na vituo vya kusafiria ikiwemo viwanja vya Ndege,Bandari na vituo vya mipakani na kupitia njia ya simu kwa kupiga namba 117 kwa mitandao yote.
“Hakuna mtu aliyethibitishwa kuwa na ugonjwa wa ebola nchini Tanzania hivyo watanzania msiwe na hofu ila tuchukue tahadhari na kupata elimu zaidi ili kujikinga na ugonjwa huu” alisisitiza Waziri Ummy.
Mbali na hayo Waziri Ummy ameamua kuunda timu huru ya watu sita itakayoongozwa na Daktari Bingwa wa magonjwa ya kinamama Prof. Charles Majige ili kuchunguza upya tukio la Bi. Asma Elias ya kuibiwa kichanga  katika hospitali ya Temeke baada ya kukataliwa ripoti ya awali iliyotolewa na Mganga Mkuu wa Dar es salaam.

ALIYEKUWA ANAGOMBEA URAIS ASHIKILIWA KWA KUTAKA KUJIUA


Baadhi ya wanaume wakisajiliwa kama wapiga kura nchini Kenya kufuatia kuanzishwa kwa shughuli hiyo siku ya Jumatatu
Mmoja wa waliojitokeza kugombea urais katika uchaguzi mkuu mwezi Agosti nchini Kenya alijaribu kujirusha kutoka jumba la ghorofa, taarifa katika vyombo vya habari nchini humo zinasema.
Bw Peter Solomon Gichira anadaiwa kujaribu kujirusha kutoka ghorofa ya sita katika afisi za Tume Huru ya Uchaguzi (IEBC) jijini Nairobi baada ya ombi lake la kutaka kuwania urais kukataliwa Jumamosi jioni.
Mkuu wa polisi wa Nairobi Japheth Koome amesema Bw Gichira atafunguliwa mashtaka ya kuzua fujo eneo la umma, kuharibu mali na kujaribu kujitoa uhai.
Kwa mujibu wa gazeti la Daily Nation, mkuu wa polisi wa kituo cha Central Robinson Thuku alisema Bw Gichira alikuwa ameenda afisi za IEBC kufuatilia ombi lake alipofahamishwa kwamba ombi lake lilikataliwa.
Ni hapo ambapo alianza kulalamika na akavunja dirisha na kujaribu kuruka nje lakini akazuiwa na maafisa wawili ambao pia walimkamata.
Bw Thuku alisema mwanasiasa huyo atafikishwa mahakamani Jumatatu.
Polisi walikataa kumwachilia dhamana na kusema wanamzuilia kwa ajili ya usalama wake.
Mgombea mwenza wa Bw Gichira, Kelly Watima, hata hivyo alisema mwenzake amekuwa akihangaishwa tangu alipotangaza nia ya kutaka kuwania urais.
"Bw Gichira amekuwa akihangaishwa na maafisa wa IEBC na sasa polisi wanamzuilia ndipo akose fursa ya kuwasilisha karatasi zake za uteusi …mbona wanamuogopa…je, ni kwa sababu ni tishio kwao?" alisema, kwa mujibu wa Daily Nation.
Bw Gichira ni miongoni mwa wanasiasa kumi waliokuwa wameeleza nia ya kutaka kuwania urais lakini wakakosa kuidhinishwa na tume hiyo kwa kukosa kutimiza amsharti mbalimbali.
Kuna wagombea kumi walioidhinishwa, ambao wamekuwa wakiwasilisha karatasi zao Jumapili na leo Jumatatu.
Miongoni mwa waliofanikiwa kuwasilisha karatasi zao Jumapili ni aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga, mgombea huru Ekuru Aukot na Abdouba Dida ambaye pia aliwania urais mwaka 2013.
Waliopangiwa kuwasilisha karatasi zao za uteuzi leo ni pamoja na Rais Uhuru Kenyatta ambaye anawania kwa mara ya pili.
MAAJABU YA WATOTO WALIOUNGANA IRINGA

        Miaka 21 iliyopita, familia ya Alfred Mwakikuti na Naomi Mshumbusi ilijaaliwa kupata watoto pacha, Maria na Consolata. Lakini hawakuwa pacha wa kawaida; walikuwa wameungana na hakukuwapo na uwezekano wa kuwatenganisha.
Hawakuweza kujulikana mapema hadi walipofikia umri wa kwenda shule. Hapo ndipo vyombo vya habari vilipotangaza kwa nguvu habari ya watoto wao, baada ya Mwananchi kuiibua.
Mwaka 2010 walimaliza elimu ya msingi na 2014 elimu ya sekondari na mwaka huu wamemaliza elimu ya juu ya sekondari.
Wakati wote huo gazeti hili limekuwa nao pamoja katika kila hatua na sasa linakuletea habari mfululizo za maisha yao kuanzia leo. Mwandishi wetu, Tumaini Msowoya anaongea nao kwa kirefu kuhusu maisha yao, changamoto, mafanikio na matamanio yao. Sasa endelea…
Tumaini Msowoya, Mwananchi tmsowoya@mwananchi.co.tz
Kilolo. Acheni Mungu aitwe Mungu kwa kuwa maajabu yake ni makubwa na hayaelezeki.
Maajabu hayo ya Mungu yanadhihirika katika muujiza wa watoto pacha, Maria na Consolata Mwakikuti waliozaliwa wakiwa wameungana.
Pacha wengi walioungana huwa wanadumu kwa kipindi kifupi na wengine hupoteza maisha yao wakati madaktari wanapojaribu kuonyesha ubingwa kwa kuwafanyia upasuaji ili watenganishwe.
Maria na Consolata ni miongoni mwa pacha ambao Mungu ameruhusu waishi pamoja mpaka leo.
Si tu kwamba, Mungu ameruhusu pacha hao kuishi, bali amekuwa akionyesha maajabu yake kwa kuwawezesha kufanikiwa katika kila hatua.
Maria na Consolata ni pacha wa kipekee waliogeuka kivutio, si tu kwa sababu wameungana, bali ni kutokana na namna walivyochukulia maisha hayo ya kuishi katika mwili mmoja na kuzishinda changamoto za kimaisha, wakifanya vizuri katika elimu ambayo ndiyo changamoto yao kubwa kwa sasa.
Hivi karibuni walihitimu kidato cha sita katika Shule ya Sekondari Udzungwa iliyopo kijiji cha Kifabaga, Kilolo mkoani Iringa.
Pacha hao walizaliwa mwaka 1996, katika hospitali ya Misheni ya Ikonda, iliyopo kijiji cha Ikonda, Wilaya ya Makete mkoani Njombe .
Mwaka 2010, walitikisa taifa baada ya kufaulu mitihani yao ya darasa la saba na hivyo kuwa na sifa ya kuendelea na masomo ya sekondari.
Miaka minne baadaye mapacha hao walitikisa tena baada ya kufaulu mitihani mingine ya kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Maria Consolata ya Kilolo.
Hivi sasa kila mmoja ndani na nje ya nchi, anasubiri matokeo ya kidato cha sita ya kinadada hao yatakapotangazwa.
“Japo sisi ni yatima na wenye ulemavu kutokana na kuungana kwetu, haya yote si sababu ya kufeli darasani na kushindwa katika maisha. Tunajiamini na tuna uhakika kwamba tunaweza. Ni bidii tu,” anasema Consolata.
Siku niliyopata nafasi ya kushinda nao, si tu nilipata habari bali nilijifunza mengi kutoka kwao.
Ni wakarimu, wacheshi, wapole, wenye upendo na si watu wa kukurupuka kujibu, bali hutafakari kwanza.
Haichukui muda mrefu kuwazoea mapacha hawa, kwa kuwa ni wachangamfu.
Japokuwa safari yangu ya kuelekea Kidabaga, Kilolo wanakoishi mapacha hao ilikuwa ya kusuasua kutokana na uhaba wa usafiri, uchovu uliisha mara nilipobisha hodi nyumbani kwao na kupokelewa kwa nyuso zilizojaa tabasamu na bashasha.
“Karibu nyumbani kwetu, jisikie huru,” alisema mmoja wao wakati wakinikaribisha kwa furaha. Mara nyingi wanapozungumza, huwa wanatamka maneno kwa pamoja.
Pacha hawa ni watoto yatima.  Baba yao Alfred Mwakikuti na mama yao Naomi Mshumbusi walifariki dunia nyakati tofauti.
Baba alifariki wakati wakiwa na umri wa miaka mitatu na mama yao alifariki wakati wakiwa vichanga.
“Bora baba tuna kumbukumbu kidogo alikuwaje, mama yetu hatukuwahi kumuona kabisa,” anasema Consolata.
Tangu wakati huo, wamekuwa wakilelewa na wamisheni na kwa sasa wapo chini ya Shirika la Masista Wamisionari wa Shirika la Maria Consolata,  Nyota ya Asubuhi linalofanya shughuli zake Kijiji cha Kidabaga wilayani Kilolo.
Mkuu wa shirika hilo, Sister Idda Luizer anasema wanafurahi kuwalea watoto hao ambao alisema ni wacha Mungu.
Kwa kweli wamebadilika tofauti kabisa na miaka sita ya nyuma wakati nilipozungumza nao, wakiwa Ikonda wilayani Makete mara baada ya kuhitimu darasa la saba.
“Zamani tulikuwa na hisia tofauti, tulipenda tofauti lakini kwa sasa tumejikuta tukipenda na kuhisi pamoja,” anasema Consolata.
Consolata anaongea zaidi kuliko Maria na wanapotembea, hutumia mikono na miguu.
Wanao uwezo mkubwa wa kutunza kumbukumbu, kwa sababu licha ya kuwa mara ya kwanza kukutana nao ilikuwa 2010, bado waliweza kunitambua na hata kuniita kwa jina.
Mwaka huo nilipozungumza nao walitamani kusomea teknolojia ya mawasiliano, ndoto iliyozima kutokana na namna wanavyoendelea na elimu ya juu.
Ndoto yao sasa ni kuwa walimu.
Pia, wanataka kufika chuo kikuu na wakihitimu wafunge ndoa ya mume mmoja.
Namna walivyoungana  
Miujiza ya Mungu inaonekana katika umbile lao. Maria na Consolata wameungana kuanzia kifuani. Wanachangia tumbo, wana kitovu kimoja, kiuno kimoja, mikono minne yote ikiwa na nguvu za kufanya kazi na miguu mitatu.
Mguu mmoja una miguu miwili ndani yake; ni kama wameunganishwa kwa kufunikwa na ngozi.
Hii inamaanisha kwamba ukiugusa mguu huo upande mmoja wa ngozi ataitika Maria na upande mwingine, ataitika Consolata.
“Mguu huu mmoja ni wa kwetu wote, ukiugusa upande mmoja Maria anasikia na upande mwingine, mimi nasikia,” anasema Consolata.
Maumbile haya ndio sababu kubwa ya pacha hao kutembea kwa mikono na miguu.
Watembeapo mara zote Maria huwa chini kidogo na mara zote huwa anapumua kwa shida, hali inayoonyesha kwamba Consolata huwa anamuelemea mwenzake.
Matembezi yao huwa ni katika eneo la nyumbani kwao na wanapotaka kutoka, huwa wanatumia kiti cha magurudumu.
Pamoja na kwamba wameungana, kila mmoja ana sehemu zake za siri na kila mmoja anajisaidia kwa wakati wake.
Consolata anasema kila mmoja huwa anasikia maumivu kwa wakati wake.
Kitu pekee ambacho huwa wanapata maumivu kwa pamoja ni makalio ambayo huchoka zaidi wanapokaa kutokana na aina ya ulemavu. Ikiwa mmoja atahitaji kulala basi mwingine hulazimika kumvumilia mwenzake hadi anapoamka au naye aamue kulala.
“Mchana mwenzangu akisinzia, huwa tunalala tu kwenye kochi kwa sababu ni kubwa na haina haja ya kuingia chumbani. Mmoja akilala, mwingine hubaki akimsubiri mwenzake au basi wote tulale,” anasema.
#MwananchiMAAJABU

NENO LA MWISHO LA ERNEST MANGU KWA IGP SIMON SIRRO


Aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu amewataka wananchi kumpa ushirikiano IGP mpya, Simon Sirro katika kukabiliana na matukio ya uhalifu nchini hasa katika Mkoa wa Pwani.
Mangu ameyasema hayo leo Ikulu jijini Dar es salaam baada ya Rais John Magufuli kumwapisha Sirro kuongoza jeshi la polisi nchini.
Mangu ambaye anasubiri kupangiwa kazi nyingine amesema anamfahamu Sirro kama mchapakazi mzuri na ataweza kutekeleza majukumu yake ya kuhakikisha kwamba Tanzania inakuwa na amani.
Alipoulizwa wito wake kwa Sirro kuhusiana na hali tete katika wilaya za Rufiji na Kibiti mkoani Pwani, Mangu amesema "Sirro anafahamu anachotakiwa kufanya katika hilo, nimefanya naye kazi kwa karibu, ninachoomba ni askari na wananchi wote wampe ushirikiano."
Sirro ameapishwa leo kuwa IGP, kabla ya uteuzi huo alikuwa kamanda wa polisi (RPC) katika mikoa ya Tanga, Mwanza na Shinyanga. Baadaye alikwenda kitengo cha operesheni na mafunzo polisi makao makuu, kisha akahamishiwa kitengo hicho kanda maalumu ya Dar es Salaam kabla ya kuwa kamishna wa kanda hiyo.

VIJANA WA AFRIKA WAKUMBUKWA NA G7

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres (wa kwanza kushoto) akizungumza kwenye mkutano wa wakuu wa G7 huko Italia. (Picha:Miguel Graça/UN )
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amezitaka kundi la nchi saba G7 zilizo mbele kiuchumi zaidi duniani kuwekeza katika vijana wa Afrika.
Amesema hiyo hii leo huko Taormina, Sicily nchini Italia wakati akihutubia kikao cha G7 kilichokutana mahususi ili kuangala masuala ya ubunifu na maendeleo endelevu kwa lengo la kuimarisha uhusiano na Afrika.
Amesema kasi ya ongezeko la vijana barani Afrika ni kubwa kuliko kokote kule duniani na hivyo..
(Sauti ya Guterres) 
"Faida tunaweza kupata kupitia uwekezaji kwenye elimu hasa ya sayansi na teknolojia. Lakini elimu ya msingi haitoshi pekee, watu wanahitaji stadi ambazo zinaendana na mahitaji ya sasa na ya baadaye kwenye soko la ajira."
Amesema pamoja na kuwekeza katika vijana Afrika, G7 zisaidie kueneza teknolojia za kisasa Afrika, ziwekeze kwenye sekta fanisi, zisaidie nchi za Afrika kufikia umoja wa kikanda, bila kusahau uwezeshaji wanawake na wasichana na kusaidia Afrika kuondokana na  ukwepaji wa kodi.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres (katikati mstari wa nyuma) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Afrika na wale wa G7. (picha:Stephane Dujarric/UN)
Kuhusu kile kinachoitwa mapinduzi ya nne ya viwanda yanayotarajiwa kukumba dunia, Bwana Guterres amesema suala hilo litaleta mabadiliko makubwa kwenye soko la ajira duniani kwa hiyo..
(Sauti ya Guterres)
"Afrika inaweza kuathirika na mabadiliko haya. Tunapaswa kufanya kila tuwezalo kuhakikisha Afrika inaweza kuyahimili. Kufanya hivyo kunahitaji kuimarishwa kwa uwekezaji katika teknolojia na elimu stahiki na kujenga uwezo katika sekta zote."
 Amepongeza G7 kwa kuangazia Afrika katika wakati wa sasa ambao amesema ni  muhimu na pia kwa kuweka kipaumbele katika maendeleo jumuishi na yanayochochea ukuaji kupitia ubunifu.
 Nchi za G7 ni Canada, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Japan, Uingereza na Marekani ambapo pia Muungano wa Ulaya nao unawakilishwa kwenye jumuiko hilo.

RAIS TRUMP ATAKA KUJITOA KWENYE MKATABA WA MAZINGIRA

Mtandao wa habari wenye makao yake mjini Washington, Marekani umeripoti kwamba Rais Donald Trump amewaambia "watu anaowamini" ataachana na makubaliano ya kihistoria ya tabia nchi yaliofikiwa Paris Ufaransa.
Mtandao wa habari wenye makao yake mjini Washington nchini Marekani umeripoti kwamba Rais Donald Trump wa Marekani amewaambia "watu anaowamini" ataachana na makubaliano ya kihistoria ya tabia nchi yaliofikiwa Paris Ufaransa ambayo mtangulizi wake Barack Obama ameyasaini hapo mwaka 2016 kupunguza kiwango cha utowaji wa hewa ukaa gesi yenye kuchafuwa mazingira duniani.
Kutokuwepo kwa hali ya uhakika kuhusiana na msimamo wa Marekani juu ya suala la tabia nchi kumewatibuwa viongozi wenzake katika mkutano wa kilele wa nchi za G7 zenye maendeleo makubwa ya viwanda duniani ambao umemalizika Jumamosi huko Taormina, Sicily nchini Italia bila ya kuwepo kwa maafikiano ya sauti moja kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Rais Donald Trump amesema atotowa uamuzi wa mwisho wiki hii iwapo Marekani iendelee kubakia katika makubaliano ya tabia nchi yaliyofikiwa Paris au ijitowe. Trump ametowa tangazo hilo la ghafla katika mtandao wa Twitter baada ya kuhimili shinikizo kutoka kwa viongozi wa Ulaya waliokuwa wakimtaka abakie katika mkubaliano hayo.
Vyanzo vya kuaminika
G7 Gipfeltreffen Donald Trump spricht mit Angela Merkel und Beji Caid Essebsi (Reuters/J. Ernst) Viongozi wa nchi za G7 katika mazungumzo.
Ikitaja vyanzo vitatu vyenye uwelewa wa moja kwa moja wa mipango ya Trump ukurasa wa kutowa habari wenye kuheshimika Axios umeripoti Jumamosi kwamba kiongozi huyo wa Marekani amewaambia washauri wake wakuu ataitowa Marekani kwenye makubaliano ya tabia nchi yaliofikiwa Paris mwaka 2015.
Ukurasa huo umeanzishwa mwaka jana na mmojawapo wa wasisi wenza wa kisiasa na mkuu wa zamani wa waandihishi  wa Ukulu ya White House.Ukurasa huo wa Axios umesema iwapo ni kweli utabiruwa sera za tabia nchi za mtangulizi wake Barack Obama na kutuma ishara ya mapambano kwa dunia nzima kwamba suala la kuongezeka kiwango cha joto duniani si miongoni mwa vipau mbele vya Trump.
Ukurasa huo wa mtandao umekiri kwamba rais huyo tajiri mkubwa kabisa amebadili mawazo yake juu ya ahadi kadhaa madhubuti alizotowa wakati wa kampeni tokea aingie madarakani hapo mwezi wa Januari.
Uamuzi wiki hii
G7 Gipfeltreffen in Taormina Italien US-Präsident Donald Trump (Reuters/D. Martinez) Rais Donald Trump wa Marekani.
Trump amewaambia viongozi katika mkutano wa G7 kundi la mataifa lenye maendeleo makubwa ya viwanda duniani huko Italia hapo Jumamosi(27.05.2017) kwamba atatowa uamuzi wake kuhusu iwapo Marekani iendelee kuunga mkono makubaliano ya kihistoria ya tabia nchi katika kipindi kisichozidi wiki moja.Nchi za kundi la G7 zinajumuisha miongoni mwa nchi nyengine Ujerumani,Uingereza,Canada,Ufaransa na Japani.
"Nitatowa uamuzi wa mwisho juu ya mkataba wa Paris wiki ijayo!" ameandika Trump kwenye mtandao wa Twitter bada ya huko nyuma kuita ongezeko la joto duniani kuwa ni "dhihaka".
Ukosefu wa kujitolea wa Trump kwa makubaliano hayo ya tabia nhi ambayo yanazitaka nchi kujifunga kupunguza kiwango kikubwa sana cha utowaji wa hewa ukaa kupunguza madhara ya kuongezeka kiwango cha ujoto duniani kumewatibuwa washirika wa jadi wa Marekani ikiwemo Ujerumani.
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amesema mazungumzo ya G7 kuhusu tabia nchi yamekuwa na matatizo magumu sana.Amewaambia waandishi wa habari majadiliano kuhusu tabia nchi yalikuwa magumu sana na kama sio kusema hayaridhishi kabisa" na kwamba "hakuna dalili iwapo Marekani itabakia katika makubaliano ya Paris au hapana."
Mkubaliano hayo ya kihistoria ya tabia nchi yalisainiwa na nchi 195 mjini Paris hapo mwezi wa Disemba mwaka 2016 na kuanza kufanya kazi miezi 11 baadae.Mkataba huo umezifunga nchi kuzuwiya kuongezeka kwa ujoto kupindukia nyuzi joto mbili kiwango kilichokuweo kabla ya enzi za viwanda.

MAGAZETINI JUMATATU MAY 29,2017 HABARI KUBWA IGP MANGU ATUMBULIWAMay 28, 2017

IGP MANGU ATUMBULIWA ,SIRO AVAA VIATU VYAKE

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro.Kamanda SIRO awa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP, ERNEST MANGU atenguliwa na Rais John Magufuli leo