November 16, 2016

Wakazi wa Nzega zaidi ya 100 waanza kufaidi mkopo wa “WanaNzengo Airtel Fursa”

Mbunge wa Jimbo la Nzega Mjini Mhe, Hussein Bashe (kushoto) akibadilishana mkataba wa thamani ya shilingi milioni 20  na Meneja wa huduma kwa jamii wa Airtel Bi Hawa Bayumi (kulia) mara baada ya kusaini mkataba huo Nzega na  kushudiwa na   mkuu wa wilaya wa Nzega Mh, Godfrey Ngupula. 

kampuni ya Airtel Tanzania kwa kushirikiana  na Nzega Urban Trust Fund  imeanza kutoa mikopo kwa wajasiriamali wadogo wadogo katika mji wa Nzega  mara baada ya kuzindua mfuko maalumu utakaowawezesha wajasiriamali kupata mikopo iliyo na riba ndogo na nafuu sana kwa lengo la  kuendeleza miradi yao ya kibiashara!
 Mradi huo  ujulikanao kama “WanaNzengo Airtel Fursa” ulibuniwa kwa jitihada za  Mbunge wa Nzega mjini Mheshimiwa na Hussein Mohammed Bashe na kuzinduliwa mwanzoni mwa mwezi Novemba chini ya udhamini wa Airtel na kuwekwa chini ya uratibu wa taasisi ya Nzega Urban Trust Fund.  Programu hii ya mikopo kwa wajasiriamali wadogo wadogo imeonyesha mafanikio katika hatua za awali kwa kuwezesha  makundi 20  yenye wafanyabiashara zaidi ya 100  kupata mikopo.

 Akiongea kuhusu mikopo hiyo  Meneja Programu wa Nzega Urban Trust Fund, Bw. Felician Andrew alisema “Tangu kuzinduliwa kwa mpango huu tumepokea maombi mengi sana toka kwa wajasiriamali ndani ya mji huu wa Nzega na leo tunayofuraha kuwapatia mikopo watu wapatao 100 ndani ya vikundi 20 vya awali baada ya kutimiza taratibu zote na kukidhi vigezo vya kupewa mikopo hii. 

 Tunaamini hii sasa itakuwa fursa pekee kwa wafanyabiashara na wakazi wa Nzega kukuza biashara zao”

 Aliongeza kwa kusema “Mikopo hii tunayotoa imelenga kukuza mitaji ya wafanyabiashara wadogo wadogo na ndio maana riba yake ni ndogo sana kwani tunatoza asilimia 1 kama riba. 

Tumeweza kufanya hivi kwa vile Kampuni ya simu za mkononi ya Airtel ilituwezesha kwa kutupatia fungu la fedha kiasi cha shilingi million 20 ili kutekeleza program hii ambayo ni endelevu na Airtel wamefungua mlango wa fursa!”.

 Ili kupata mkopo ikiwa wewe ni mjasiliamali na mkazi wa Nzega unatakiwa kujaza fomu ya maombi ya mkopo, ukiwa katika kikundi kisichozidi wala kupungua idadi ya watu 5 ambao wote mnapaswa kuwa watumiaji wa Mtandao wa Airtel, kwa kuwa fedha hizi hutolewa kwa mfumo wa Airtel Money.

 Ni matumaini yetu wajasiriamali watatumia fursa hii vyema katika kuinua mitaji yao lakini vilevile sisi tumejipanga ili kuhakikisha tunawafikia wafanyabiashara wengi zaidi. Mpango wetu ni kuhakikisha ifikapo mwishoni mwa mwaka huu tuweze kuwawezesha takribani wafanyabiashara 200 kupitia programu hii. 

 Kwa upande wake meneja huduma kwa jamii wa Airtel , Hawa Bayumi alisema”Airtel tunaendelea kutimiza dhamira yetu  kwa vitendo kupitia mradi wetu wa Airtel FURSA na kuwawezesha wajasiriamali wadogo wadogo hususani vijana  kuinua uchumi wao. “WanaNzengo Airtel Fursa” ni sehemu ya mikakati yetu katika kuhakikisha tunafikia malengo yetu na kuinua shughuli za jamii inayotuzunguka. 

 Vikundi vilivyonufaika ni pamoja na C. C.M Vijana,  Vumilia,  Purity,  Huruma,  Upendo Group,  Upendo Na Amani B.B.C,  Unyanyembe, Luquman, Isamilo Soko Kuu, Maua, Mama Lishe Parking, Tofali Choma, Umoja Wa Wakata Tairi, Amka Na Badilika, Seba Akujiwe, Umoja Lingini, Nzega Tanzania Deaf Society, Upendo Magharibi, Sister Group Na Hamarzon.

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE