November 9, 2016

MEYA KIMBE ASEMA HAKUNA TOFAUTI TENA KATI YAKE RC NA DC IRINGA


Image result for meya  Kimbe na DC kasesela Rc
MSTAHIKI   meya  wa Manispaa ya  Iringa Alex  Kimbe  (Chadema)  amesema  kuwa tofauti  zilizokuwepo  kati yake  na  viongozi wa  serikali  ngazi ya  wilaya na mkoa  wa Iringa  imemalizika na  sasa  wapo pamoja  kwa  ajili ya  kuwatumikia  wananchi wa Iringa.

Huku akilia na  waganga  wa tiba  ya asili ambao  baadhi yao wamekuwa  wakijiingiza katika vitendo vya ubakaji  watoto  wadogo na  kutaka  viongozi wote kwa  pamoja  kuungana  kupambana na  waganga  hao  wanaosababisha ongezeko la matukio ya ubakaji mjini Iringa .

Akizungumza katika  mahojiano maalum kwenye  kituo cha Radio Country Fm ya mjini hapa  leo Kimbe  alisema  kuwa  awali  kulikuwepo na hali ya  kutokuelewana kati yake na  ofisi ya  mkuu wa  wilaya ya  Iringa Richard  Kasesela na ile ya  mkoa chini ya  mkuu wa mkoa Amina Masenza kwa  kuvutana  katika baadhi ya maamuzi ila kwa  sasa hali kama  hiyo haipo tena .

' kwa  sasa  tumemaliza  tofauti  zetu ambazo yawezekana kwa  ajili ya itikadi za  kisiasa ama  vinginevyo nawashukuru  sana  viongozi hawa  yaani mkuu wa wilaya  Kasesela na  mkuu wa mkoa wa Iringa mama Masenza  tupo nao  vizuri na tunafanya kazi pamoja .......sitegemei kama  kutakuja  kutofautiana tena lengo letu kusonga mbele '

Hivi  karibuni  kumekuwepo na mvutano mkubwa  kati ya  viongozi hao hasa  katika  masuala  yanayohusu maendeleo ya  Manispaa ya  Iringa kwa  kila mmoja kutoa  maagizo yake jambo  ambalo  lilionyesha  kuwachanganya  zaidi  wananchi wa Manispaa ya  Iringa.

Meya  Kimbe  alisema  kuwa tofauti zilizokuwepo kati yao wamekwisha  imaliza kwa  kukaa pamoja yeye na mkuu wa wilaya pamoja na  mkuu wa mkoa na  kukubaliana kuachana na  tofauti  hizo na  badala  yake  kuungana pamoja  ili  kufanya kazi ya  kuwatumikia  wananchi wa Halmashauri ya Manispaa ya  Iringa ambayo  kimsingi  inaongozwa na Chadema  ila kwa  sasa vyama  vimewekwa kando na  kuwa chama kimoja cha  kuwaletea wananchi maendeleo.

Akizungumzia  kuhusu ongezeko la matukio ya  ubakaji katika mji wa Iringa  alisema  kuwa katika suala   hilo  viongozi  wote  wanapaswa  kushikamana  ili  kupambana na  waganga  wa  tiba asilia ambao  wameongezeka zaidi katika  mji wa Iringa na  baadhi yao  wamekuwa  wakidanganya  watu kwenda  kubaka  watoto ili  kupata utajiri .

' Sitakubali  kuona  waganga   hawa  wa kienyeji  wakiendelea  kuchochea watu kwenda kubaka  watoto ...maana  kwa sasa kila kona ya mji wa Iringa unakutana na mabango ya  waganga  wa kienyeji na  wengi  wao ni wale  ambao  hawajulikani hawajasajiliwa hivyo tutawakamata  wote  wanaofanya kazi  hiyo bila  kuwa na kibali  tumechoka kuendelea kuona matukio  haya ya  ubakaji'

kwa nyakati  tofauti  wakizungumza na  wanahabari mkuu wa  mkoa  wa  Iringa  Amina Masenza na mkuu wa  wilaya ya  Iringa Richard Kasesela   walisisitiza umuhimu wa  viongozi wa  vyama  vya siasa  wakiwemo madiwani na Mstahiki  meya  kufanya kazi kwa maslahi ya  wananchi  badala ya  kuendeleza siasa .

Viongozi hao   walifikia hatua  hiyo kufuatia kuwepo kwa  mvutano wa stendi  ya mashine tatu ,stendi ya daladala ya Maktaba jambo ambalo  lilionyesha  kuwepo kwa  mvutano mkubwa kwa  kila mmoja  kutoa maagizo yake  japo baada ya  viongozi hao  kukaa pamoja hivi  sasa hali ya mvutano  huo imetoweka na sehemu  kubwa viongozi wote hao  wamekuwa  wakiendelea  kufanya kazi pamoja .

MWISHO

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE