November 4, 2016

Clinton na Trump wapigania majimbo muhimu


Hillary Clinton and Donald TrumpHillary Clinton na Donald Trump wamezidisha kampeni zao, hasa kwenye majimbo yanayoshindaniwa sana, huku kura za maoni zikionesha wamekaribiana sana zikiwa zimesalia siku chache kabla ya uchaguzi mkuu.

Wawili hao kwa mara nyingine wameshambuliana kwenye mikutano ya kampeni, kila mmoja akisema mwenzake hafai kuwa rais.

Bi Clinton, ambaye uongozi wake kwenye kura za maoni kitaifa unaonekana kufutika siku za karibuni, amesema mpinzani wake wa chama cha Republican hawezi kudhibiti hisia zake na ana mtazamo hasi dhidi ya wanawake.

Bw Trump naye amesema Bi Clinton ataandamwa na uchunguzi wa jinai hadi ikulu ya White House.
Mgombea huo anaonekana kuimarika dhidi ya Bi Clinton katika majimbo yanayoshindaniwa, kwa mujibu wa kura za maoni.
  Utathmini wa kura za maoni kitaifa kufikia tarehe 4 Novemba, 2016
Utathmini wa kura za maoni kitaifa kufikia tarehe 4 Novemba, 2016
Alhamisi, mkewe Melania alijitokeza kwenye mkutano wa kampeni kumtetea.
Kwenye hotuba yake ya kwanza tangu Julai wakati wa mkutano wa kitaifa wa chama cha Republican, mwanamitindo huyo wa zamani alizungumzia maisha yake kama mhamiaji na akasema mumewe ataifanya Marekani kuwa nchi ya haki.
Aidha, ameapa kuongoza kampeni dhidi ya watu kudhalilishwa na kudhulumiwa kwenye mitandao iwapo atakuwa mama wa taifa.
Akiongea kwenye viunga vya mji wa Philadelphia amesema atakabiliana na utamaduni ambao "umekuwa kaidi sana na katili".
Hata hivyo, hakuzungumzia tabia ya mumewe ya kuwashambulia na kuwatusi wapinzani wake kwenye mitandao ya kijamii.
Bw Trump ameimarika dhidi ya Bi Clinton katika majimbo kadha ya kushindaniwa, yakiwemo majimbo ya Florida na North Carolina, kwa mujibu wa kura za maoni.
Baadhi ya kura za maoni za kitaifa zinaonesha wawili hao wana kiwango sawa cha uungwaji mkono.
Makadirio ya utafiti wa Reuters/Ipsos yanaonyesha uwezekano wa Bi Clinton kushinda kura za wajumbe 270 zinazohitajika kushinda Jumanne kwa sasa ni 90% chini kutoka 95%.
Bw Trump ndiye anayeonekana kuimarika zaidi, na alifanyia hilo mzaha wikendi ya mwisho inapowadia.
Ametumia habari za FBI kuanzisha uchunguzi mpya kuhusu barua pepe za Bi Clinto kumshambulia zaidi mpinzani wake.
Melania TrumpMelania Trump ameahidi kukabiliana na wanaoshambuliwa watu mitandaoni iwapo mumewe atashinda
"Ndio hao Wanaclinton tena - mwakumbuka vikao vya kumuondoa rais madarakani na matatizo mengine," Bw Trump aliambia waliohudhuria mkutano Jacksonville, Florida.
"Haya siyo mtayotaka, jameni. Twahitaji mtu aliye tayari kfuanya kazi."
Baadaye mkutano wa usiku Carolina Kaskazini, akizungumzia masuala ya ulinzi, alisema hawezi kutafakari Bi Clinton akiwa amiri jeshi mkuu.
Bi Clinton ameendelea kuangazia sifa za Bw Trump, na alisema Carolina Kaskazini: "Ametumia muda wake wote wa kampeni akiwapa filimbi wafuasi wake wenye chuki.
"Hili halijawahi kufanyika kwa mgombea wa chama kikubwa."
  Pharrell Williams na Bernie Sanders wakiwa na Hillary Clinton
Pharrell Williams na Bernie Sanders wakiwa na Hillary Clinton
Aliongeza: "Iwapo Donald Trump atashinda uchaguzi tutakuwa na amiri jeshi mkuu ambaye hajielewi na ambaye mawazo yake ni hatari."

Rais Barack Obama amekuwa akitia bidii kumfanyia kampeni Bi Clinton, akijaribu kuwashawishi wapiga kura vijana na Wamarekani weusi wampigie kura.

Utathmini wa kura za mapema unaonesha huenda wapiga kura weusi hawajitokezi kwa wingi kupiga kura kama walivyofanya kumpigia kura Obama mwaka 2012.
Bi Clinton alipata nguvu zaidi pale mpinzani wake mkuu wa wakati wa mchujo Bernie Sanders alipojitokeza mkutano wake wa kampeni.
Kwenye mkutano huo Carolina Kaskazini Alhamisi jioni Bw Sanders alimsifu Bi Clinton kwa kujitolea kuinua ujira wa chini na kuangazia ukosefu wa usawa.
Nyota wa muziki Pharrell Williams pia alihudhuria na kumsifu Bi Clinton kwa kutetea haki za wanawake.

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE