October 17, 2016

WAZIRI MKUU ACHOSHWA NA MADUDU BODI YA KOROSHO


*Aagiza ifanyiwe marekebisho makubwa
*Aishangaa kung’ang’ania minada

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba kuifanyia marekebisho makubwa Bodi ya Korosho na menejimenti yake  baada ya kushindwa kusimamia zao hilo ipasavyo.

Amesema Serikali itafanya mapitio ya bodi zote za mazao ya biashara na imeanza na zao la korosho kisha zao la pamba, tumbaku, kahawa, katani na chai. Katika tathmini na mapitio hayo , bodi itakayobainika kushindwa kutekeleza majukumu yake itavunjwa.

Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana jioni (Jumapili, Oktoba 16, 2016) wakati akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja cha Sokoine wilayani Nachingwea mkoani Lindi. 

Alisema anaishangaa bodi hiyo kuacha kutekeleza majukumu yake na kuingilia minada ya korosho na kuzuia baadhi ya wafanyabiashara wasiweze kununua zao hilo hali inayoashiria kuwepo kwa watu waliopangwa kununua bila ya kufuata utaratibu.

“Bodi leo wamejipa jukumu la kusimamia minada ! sio kazi yao ni kazi ya chama kikuu, zao la korosho linalimwa kutoka mkoani Ruvuma hadi Tanga, mtasimamia minada mingapi viachieni vyama vikuu. Vyama vikuu vikiharibu walalamikaji waje kwenu kama sehemu ya rufaa. Sasa nyinyi mnasimamia minada mnaharibu walalamikaji watakwenda kwa nani  ?  kwa nini mng’ang’anie kwenda kwenye minada,” alihoji Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu alisema Ijumaa (Oktoba 14,2016) bodi hiyo  ilisitisha mnada wa korosho Lindi kwa sababu wanunuzi hawakuweka bondi (dhamana ya mauzo) na alishatoa maagizo ya kuwataka wanunuzi wasiruhusiwe kununua hadi waweke asilimia 25 ya malipo.

Alisema maagizo hayo aliyatoa tangu mwezi Aprili ila  watendaji wa bodi hiyo hawakuyafanyia kazi kwa wakati na badala yake waliwazuia wafanyabiashara waliotaka kununua korosho Lindi kwa madai ya kutokuwa na bondi huku wakiwaruhusu wa Mtwara.

“Kama kule walinunua bila bondi kwa nini wasiwaruhusu na Lindi wakanunua bila  bondi ili nijue kwamba mliamua kugoma kuteleza maelekezo ya Serikali? Au hamkumtaka aliyeshinda  nyie  mlikuwa mnamtaka nani nitashughulika na nyie,” alisisitiza.

Aliongeza kuwa “Nimesema tukitoa maelekezo lazima yatekelezwe na atakayeshindwa hatufai, Mheshimiwa mbunge umelalamika juu ya bodi hawa ndio wabeba maelekezo hatujawahi kuona bodi ya korosho ikienda vijijini kuzungumza na vyama vikuu hata mara moja,”.

Akizungumzia kuhusu suala la wakulima kulazimishwa kufungua akaunti  za kupitishia malipo yao alisema wasiwalazimishe.“Waelimisheni wakulima umuhimu wa kufungua akaunti lakini si kwa kuwalazimisha wote wawe na akaunti hadi yule mwenye kilo tano…na akaunti yenyewe inafunguliwa kwa sh. 100,000,” alisema.

Alisema “’wanashindwa kutekeleza niliyowaagiza, halafu wanasingizia utendaji wao mbovu kuwa ndio maagizo yangu,’ niliwaagiza wapi,” alihoji na kuongeza kuwa  “yapo makundi yanafanya mambo yanavyotaka alafu yakiwazidi mambo wanasingizia viongozi wajuu na ndio wale wanaosema kila kitu nimeagizwa kutoka juu, juu wapi? 

“Lazima tuendelee kudhibiti nidhamu ya vyombo vya tunavyoviunda kwa ajili ya kuwahudumia wananchi. Tutaendelea kusimamia nidhamu kwa taasisi zinazowahudumia wakulima nchi nzima,” alisisitiza.

Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Bw. Godfrey Zambi alimkabidhi Waziri Mkuu msaada wa sh. milioni 16.3 pamoja na nguo kwa ajili ya kusaidia  wananchi walioathirika na tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera Jumamosi, Septemba 10, mwaka huu na kusababisha vifo vya watu 17 na wengine 440 walijeruhiwa.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, OKTOBA 17, 2016

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE