October 25, 2016

MASHINDANO YA PIGA MPIRA OKOA TEMBO YAANZA KUTIMUA VUMBI IRINGA

Mkuu  wa  mkoa  wa Iringa Amina Masenza   akisoma  kauli mbiu ya mashindano ya kombe la Spanest
MASHINDANO  ya soka yenye lengo la  kupambana na vitendo  vya  ujangili  katika  Hifadhi ya  Ruaha  mkoani Iringa wa  mradi Kuboresha Maeneo Yaliyohifadhiwa Kusini mwa Tanzania (SPANEST)  Spanest Cup 2016 yameanza  kwa  kishindo kwa  kuzishirikisha   timo za  vijijni vyote 24   vinavyozunguka  hifadhi ya Taifa  ya  Ruaha.

Mashindano  hayo yenye  kauli mbiu   piga mpira okoa Tembo   yamezinduliwa na  mkuu wa  mkoa  wa Iringa Amina Masenza juzi na  kuwataka  washiriki  wa mashindano hayo  kuwa mabalozi  wema kwa  kuwafichua   wale  wote  wanaojihusisha na  vitendo vya ujangili .

Alisema  kuanzishwa  kwa mashindano hayo  ni  hatua  nzuri  yenye  lengo la  kuwafanya vijana   kujihusisha  zaidi na  michezo badala ya  kutumika  kufanya  ujangili  jambo  ambalo halikubaliki  na asingependa  kusikia ama  kuona kijana  kutoka  moja kati ya  vijiji   hivyo  vinavyoshiriki mashindano hayo anakamatwa  kwa  tuhuma za ujangili.

Kuwa  pamoja na  kuwa eneo la  hifadhi ya  Ruaha  ni moja kati ya maeneo yanayoongoza  kwa kuwa na idadi kubwa ya  Tembo  ukilinganisha na  hifadhi nyingine  hapa  nchini  ila  bado  eneo  hilo linachangamoto  kubwa  ya ujangili  na baadhi ya  wanaohusika na tuhuma  hizo  za ujangili zinaonyesha   kuwa vijana ni wengi  zaidi  kujiingiza katika ujangili .

Hivyo  alisema  jitihada  zinazofanywa na Spanest kwa  kuanzisha mashindano hayo ya  michezo  kwa  vijana   zitaongeza  hamasa kwa  vijana  kushiriki  kikamilifu katika ulinzi  wa  Tembo na  kuwafichua wale  wote  wanaojihusisha na   vitendo  vya ujangili katika maeneo  yao .

“ Kwa  kuwa  mchezo  wa mpira  wa  miguu  unapendwa  zaidi na  vijana basi  hii iwe  ni fursa kwa  vijana  kupewa elimu  ya  kulinda  Tembo na   hifadhi  hiyo  ili  kuongeza uchumi wa Taifa …… wanyama pori  wanachangia  sana kuongeza  uchumi wa Taifa   letu  hiyo iwapo   Tembo anahifadhiwa ana  uwezo  wa  kuishi  zaidi ya miaka 70 na kwa  muda  wote  huo  atakuwa  analiongezea Taifa  uchumi “

Mratibu wa SPANEST, Godwell Ole Meing’ataki alisema mradi umeongeza mara zaidi zawadi ya fedha taslimu kwa mshindi wa kwanza hadi wa tatu wa ligi hiyo inayoshirikisha timu hizo zinazoundwa na vijiji vinavyozunguka hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

Meing’ataki alisema zawadi kwa mshindi wa kwanza atakayepata kombe, medali, seti moja ya jezi, cheti na kutembelea hifadhi ya Ruaha imeongezeka kutoka Sh 300,000 hadi Sh Milioni moja.

Kwa upande wa mshindi wa pili atakayepata medali, cheti na mipira miwili imeongezeka kutoka Sh 200,000 hadi Sh 700,000 na ya mshindi wa tatu anayepata cheti na medali imeongezeka kutoka Sh 100,000 hadi Sh 500,000.

Huku Kaimu Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Moronda Moronda alisema wazo la kuunganisha vijana katika vita ya ujangili linaonekana kuwa njia muafaka ya kutokomeza ujangili kutokana na ukweli kwamba vijana ndiyo walengwa wakubwa katika kushawishika kuingia kwenye maeneo yaliyohifadhiwa na kufanya ujangili.


Katika  mchezo  huo wa  Uzinduzi wa mashindano hayo  ulioshuhudiwa na mkuu wa  mkoa wa Iringa  timu ya  Itunundu  ambao ni mabingwa  watetezi wa  kombe  hilo  lililoanzishwa mwaka  juzi   kwa mara ya kwanza  waliweza  kuibuka  na  ushindi wa  goli 2  dhidi ya watani  wao  Kimande Fc  ambao walitoka patupu.

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE