Matukio Daima

Tembelea kila siku kwa habari na matukio mbali mbali..

Matukio Daima

Kwa Habari za Kitaifa.

Matukio Daima

Kwa Habari za Kimataifa.

Matukio Daima

Kwa Habari za Uchumi na Biashara.

Matukio Daima

Kwa Habari za Michezo na Burudani.

May 31, 2015

WAZIRI NYALANDU KUCHUKUA FOMU ZA URAIS JUNI 7 MJINI DODOMA


 
Waziri wa mali asili  na utalii Lazaro Nyarandu na waumini mbalimbali baada ya Ibada ya jumapili Jijini Arusha katika Kanisa la KKKT  Diyoyosis ya Mjini Kati ambapo Waziri Nyarandu alitumia nafasi hiyo kutangaza rasmi siku atakayochukua fomu ya kuwania nafasi ya kuteuliwa kupeperusha bendera ya kuwania Urais kupitia chama cha Mpindunzi .
Waziri wa mali asili na utalii Lazaro Nyarandu akibadilishana mawazo na Kada wa chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA  James Olemilia baada ya ibada ya jumapili iliyofanyika katika Kanisa la KKKT Diyosisi ya mjini kati Arusha ambapo Nyarandu alitumia nafasi hiyo kutaja rasmi kuwa tarehe 6 mwezi ujao atachukua fomu ya kuwania nafasi ya kuteuliwa kupeperusha bendera ya CCM kuwania urais .

Mpiga picha  wa Chanell ten Arusha Aristrides Dotto na Elia Mbonea mwandishi wa gazeti la Mtanzania wakifanya mahojiano na  Waziri wa mali asili na utalii Lazaro Nyarandu mara baada ya ibada ya jumapili  katika Kanisa la KKKT  Diyoyosis ya Mjini kati ambapo Waziri Nyarandu alitumia nafasi hiyo kutangaza rasmi siku atakayochukua fomu ya kuwania nafasi ya kuteuliwa kupeperusha bendera ya kuwania Urais kupitia chama cha Mpindunzi.
 **************
WAZIRI wa Mali Asili na Utalii, Lazoro Nyalandu ambaye alishatangaza nia ya kukiomba chama Chake cha Mapinduzi (CCM) kumteua kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, anataraji kuchukua fomu ya kutimiza adhma yake hiyo Juni 7 mwaka huu mjini Dodoma.

 
ametangaza rasmi kuchukua fomu ya kuwania nafasi hiyo baada ya kutangaza nia yake miezi saba iliyopita mkoani Singida.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha jana, Nyalandu ambaye ni Mbunge wa Singida Magharibi, baada ya kushiriki ibada ya jumapili  katika kanisa la KKKT Usharika wa mjini Kati Arusha.

Nyalandu anaungana na makada wengine wa CCM kuingia katika kinyang’anyiro hicho ambapo anasema mpango na dhamira yake ya kuwania kuteuliwa na chama chake uko palepale huku akijinasibu kuwa dunia itaandika historia pale atakapo ibuka kidedea kwa kupeperusha bendera ya ccm katika kinyang’anyiro hicho.

 “Mpango na dhamira yangu ya kuomba ridhaa ya Chama change kuniteua kugombea urais mwaka huu upo palepale na dunia itaandika historia pale nitakapo ibuka kidedea na kuipeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi wa mwaka huu,” alisema Nyalandu.

Waziri Nyalandu atakungana na makada na Mawaziri wakongwe katika siasa za Tanzania katika kuwania nafasi hiyo ndani ya CCM kama akina Edward Lowassa, Steven Wasira, Bernard Membe, Samuel Sitta, na wengineo wengi ambao tayari wameshatangaza nia na dhamira yao ya kuutaka urais.

ANDIKENI WOSIA KUEPUSHA MIGOGORO - WAZIRI MKUU

 

WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amewataka Watanzania wote nchini wajenge tabia ya kuandika wosia ili kuondoa matatizo ya mirathi pindi mume anapoaga dunia. 

Ametoa wito huo leo mchana (Ijumaa, Mei 29, 2015) wakati akizindua kampeni ya kuandika wosia kwenye maadhimisho ya miaka 25 ya Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA) yaliyofanyika katika viwanja vya Karimjee, jijini Dar es Salaam. 

Akizungumza mara baada ya kushuhudia uandishi wa wosia mbele ya wakili, Waziri Mkuu alisema uandishi wa wosia ni suluhisho la migogoro mingi inayosababishwa na wanandigu ambao wakati mwingine wala hawakushiriki kuchuma mali wanayogombea. 

“Kuandika wosia siyo uchuro kama ambavyo watu wengi wanadhani… ninatoa kwa Watanzania kuandoak wosia mapema kwani inasaidia kuondoa matatizo ya mirathi baada ya mmoja wao kuondoka duniani,” alisema.

“Mtua anapaswa kutamka mali nilizonazo ni kadhaa na endapo nitakufa mali hii apewe fulani, na hii fulani na nyingine fulani. Hati hii inapaswa kutunzwa kwa mwanasheria, benki au kwa Kabidhi Wasii. Tusipolifanya hili, matatizo yataendelea kuwakumba wajane na watoto walioachwa na marehemu,” alisema. 

Aliipongeza TAWLA kwa kuchukua jukumu la kuhamasisha umma kuhusu suala la uandishi wa wosia lakini pia akawataka wanachama wa TAWLA wajikite zaidi kwenye kutetea haki za makundi maalum kama walemavu wa ngozi, vikongwe na watu kutoka makabila madogodogo. “Haya makundi yana shida zao ambazo hazifanani na watu wengine. Nendeni vijijini, mkatoe elimu, jueni changamoto wanazokabiliana nazo, wasikilizeni shida zao na muone ni njia gani mnaweza kuwasaidia,” alisema. 

Akitoa mfano, Waziri Mkuu alisema katika kipindi cha miaka nane kuanzia mwaka 2006 hadi 2014, jumla ya vikongwe 2,219 waliuawa katika mikoa ya Geita, Simiyu, Mara, Kagera na Mwanza ambayo alisema yote iko Kanda ya Ziwa. “Mauaji haya yanasababishwa na imani potofu za kishirikina; jamii kuwa na uelewa mdogo wa sheria; ukosefu wa imani za kiroho; ukosefu wa elimu; na waganga wa kienyeji kupiga ramli,” alisema. 

Alisema makabila madogo yanakabiliwa na matatizo ya ardhi ambayo ndiyo tegemeo lao kuu, vikongwe na watu wenye ulemavu wa ngozi wanatishiwa usalama wa maisha yao bila sababu yoyote. “Nendeni mkatoe elimu zaidi kwa watu hawa ili tuwalinde wazee wetu, makabila madogo kama Wahadzabe na Wasandawe pamoja na ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi,” alisisitiza. 

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki maadhimisho hayo, Mwenyekiti wa TAWLA, Bi. Aisha Bade alisema chama hicho kimetumia wanasheria wanawake zaidi ya 200 na wasaidizi wa kisheria 400 (paralegals) kutoa msaada wa kisheria kwa watu mbalimbali ambao hawana uwezo kumudu gharama za kesi.

“Katika mwaka 2014, tumetoa msaada wa kisheria kwa watu zaidi ya 10,000 ambao hawana uwezo kumudu gharama za kesi kwenye mikoa mbalimbali hapa nchini,” aliongeza.

Naye Balozi wa Sweden nchini, Bw. Lennarth Hjelmaker, akizungumza kwa niaba ya wadau wa maendeleo nchini alisema Serikali ya nchi hiyo ilitenga kiasi cha sh. bilioni 4 kusaidia mpango wa miaka minne wa chama hicho wa kuimarisha utawala bora, uwajibikaji na usawa wa kijinsia.

“Hadi sasa tumekwishatoa sh. bilioni 3.5 ambazo kati ya hizo, sh. bilioni 1.1 zimetumika kusaidia wanawake wapatiwe haki zao; sh. milioni 500 zimetumika kutoa mafunzo kwa watumishi wa afya ili watoe huduma rafiki za afya ya uzazi kwa vijana na sh. milioni 700 zimetumika kutoa mafunzo kwa viongozi wa ngazi ya chini wanaohusika kutoa maamuzi. Kiasi cha sh. bilioni 1.2 kimetumika kuendeleza shughuli za chama,” alifafanua.

Pamoja na kutoa elimu kwa jamii na kutetea haki za akinamama na wasichana, Balozi huyo wa Sweden alisema kuna haja ya kuweka mkazo ili kuwafikia wanaume na wavulana wengi zaidi ili waweze kujirekebisha na kubadili tabia na mitazamo yao dhidi ya wanawake na wasichana.

 


May 30, 2015

DC MBONI AFUNGUA KONGAMANO LA UWT MUFINDI ATOA RAI KWA WANAWAKE KUGOMBEA NAFASI ZA UONGOZI IKIWEMO YA URAIS KATIKA UCHAGUZI MKUU MWEZI OCTOBA

Mkuu wa  wilaya ya  Mufindi Bi Mboni Mhita akifungua  kongamano la  Umoja wa  wanawake Tanzania (UWT) wilaya ya Mufindi leo
Mkuu  wa  wilaya ya  Mufindi Bi Mboni Mhita wa  pili  kulia akiwa na viongozi mbali mbali wa UWT mkoa na wilaya ya Mufndi na Iringa vijijini kutoka kushoto ni mwenyekiti  wa UWT mkoa Bi Zainabu Mwamwindi ,mwenyekiti wa UWT wilaya ya Mufindi Bi Marcelina Mkini katibu  wa wazazi  mkoa wa Iringa Bw  Geofrey Kavenga  na mwenyekiti  wa UWT wilaya ya Iringa vijijini Bi Shakra  Kiwanga
Washiriki  wa kongamano la UWT wilaya ya Mufindi wakimshangilia mkuu wa wilaya ya  Mufindi hayupo pichani
Mkuu  wa  wilaya ya  Mufindi mkoani Iringa Bi Mboni Mhita katikati  akiwa na mwenyekiti wa umoja  wa wanawake Tanzania (UWT)  mkoa wa Iringa Bi Zainabu Mwamwindi (kulia) na mwenyekiti wa UWT wilaya ya  Mufindi Bi Marcelina Mkini ambae ni mjumbe wa NEC Taifa  akiwakilisha wilaya ya  Mufindi  leo   wakati wa ufunguzi wa kongamano la  wanawake wa  wilaya ya Mufindi lililofanyika mjini Mafinga (picha na Francis Godwin)

Mwenyekiti  wa UWT  wilaya ya Mufindi Bi Marcelina Mosha  akimkaribisha mgeni  rasmi
Washiriki wa kongamano hilo  wakifuatilia mafunzo ya afya  na uzazi na yale ya ujasiliamali
Katibu  wa UWT Mufindi
Viongozi  wa UWT mkoa na wilaya pamoja na DC mufindi  wakifuatilia mafunzo
Mtaaluam wa afya  akitoa  semina ya afya kwa  washiriki
Mtaalam wa afya  akitoa  elimu ya matumizi  sahihi ya kondom
Mwenyekiti wa UWT wilaya ya  Iringa vijijini Bi Shakra  kiwanga akitoa  salam  zake
Na Francis Godwin, Mufindi

MKUU  wa  wilaya ya  Mufindi mkoani  Iringa Bi Mboni Mhita amewataka   wanawake  kujitokeza kwa  wingi kugombea nafasi mbali mbali za uongozi ikiwemo nafasi ya Urais katika  uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi Octoba mwaka  huu

Alisema ushindi  wa  wanawake  katika nafasi mbali mbali ikiwemo  ya udiwani ,ubunge na urais ni kubwa zaidi  iwapo wanawake wenyewe watajiamini na  kuepuka na maneno ya   watu ambayo kimsingi wengi  wao wanatamani  kuona wanawake  wakiwa nyuma .

 Bi  Mboni ambae ni mjumbe wa NEC Taifa alitoa rai hiyo leo katika  ukumbi wa CCM wilaya ya Mufindi  wakati akifungua  kongamano  la  umoja wa wanawake Tanzania (UWT)   alisema  kuwa muda  ukifika  wanawake  hawana  sababu ya  kuogopa  kuingia katika nafasi mbali mbali  za uongozi na  kuwa  wale  wenye  uwezo wa kugombea udiwani ,ubunge na Urais  wajitokeze bila  katika mapambano kuogopa .

Alisema  kikubwa si wanawake  kuwatazama  wenzao  wanapoingia katika mapambano  ila ni kuona  wanawake  wanatengezeza  jeshi  moja  la mapambano ya  kumsaidia kwa nguvu  zote mwanamke mwenzao anayesimama katika  kuwania nafasi  za uongozi.

Bi Mboni  alisema vijana  pia hawana  sababu ya  kuchangamkia nafasi za  uongozi mbali mbali katika uchaguzi ujao badala ya  kuwa  nyuma na  kuwa kwa upande  wake anajivunia kuwa  mkuu wa  wilaya ya  Mufindi nafasi  ambae  pia ni mkuu wa wilaya mwenye umuri mdogo zaidi   kuliko wote nafasi aliyeteuliwa na Rais Dr Jakaya  Kikwete jambo  ambalo anampongeza Rais  kwa uteuzi huo japo  kabla ya uteuzi  huo  alikuwa ni makamu mwenyekiti  wa UVCCM Taifa .

Pia  alisema  kuwa yeye pia ni miongoni mwa  wajumbe wa NEC Taifa  wadogo  zaidi ila  pia alipata  kuchaguliwa  kuwa kiongozi  wa  vijana barani Afrika na  kuwa nafasi zote   hizo amekuwa akizipata kutokana na kuthubutu na  kutojinyanyapaa kama mwanamke.

Hivyo  alisema wakati  umefika  wa vijana na  wanawake  nchini  kutumia nafasi  ya  uchaguzi mkuu wa  mwaka  huu  kujitokeza  kuwania nafasi mbali mbali bila kuogopa .

Awali akimkaribisha mkuu  huyo  wa  wilaya kufungua kongamano hilo mwenyekiti UWT  wilaya ya  Mufindi Bi Marcelina Mkini mbali ya  kumpongeza mkuu  huyo wa wilaya ya  Mufindi kwa utendaji wake mzuri bado  alisema  kuwa  wanawake  katika  wilaya ya  Mufindi  kwa  mwaka  huu  wamejipanga kugombea nafasi zote tatu ya udiwani ,ubunge na Urais

Kuwa ushindi  wa  wanawake katika nafasi mbali mbali za uongozi utatokana na  ushirikiano mzuri  wa  wanawake wenyewe katika  kuwaunga mkono  wale  wote  wanaogombea nafasi   mbali mbali na  kuwa falisafa ya UWT Mufindi ni wanawake Kwanza .

Bi Mkini ambae ni mjumbe wa NEC Taifa  akiwakilisha  wilaya hiyo ya  Mufindi   alisema  kuwa  wanawake  wa  wilaya   hiyo ya  Mufindi wamehamasishwa  vya  kutosha   kuweza kujitokeza kugombea nafasi mbali mbali  za  uongozi na  kuwa mwitikio  wa wanawake kuanza  kuamka   kugombea nafasi  za  uongozi  ulianza  kuonekana katika uchaguzi  wa  serikali za mitaa uliofanyika mapema  hivi karibuni kwa wanawake kuonyesha ushiriki  mzuri katika mchakato huo.

Bila  kutaja  kutaja  idadi ya  wanawake  walioshinda katika uchaguzi  huo bado  alisema matokeo mazuri ya uchaguzi  wa  serikali za  mitaa ambayo yaliiwezesha  wilaya ya  Mufindi  kuongoza   kwa mkoa wa Iringa kwa CCM kushinda kwa zaidi ya aslimia 90 katika uchaguzi huo wa  serikali za mitaa ni moja kazi nzuri ya  wanawake katika ushiriki  wao katika  uchaguzi  huo.

Kwani  alisema nguvu kubwa  iliyoonyeshwa na  wanawake wa  wilaya   hiyo ni chachu ya kubadili mtazamo uliokuwepo  wa  wanawake  kuendelea  kuwa madaraja ya  kuvusha wanaume  wanaogombea hivyo mtazamo huo kwa  sasa umeanza  kupotea baada ya  wanawake  kuonyesha ushiriki  wao katika  kugombea nafasi mbali mbali za  uongozi .

Bi Mkini  alisema ushahidi  wa  nguvu ya  wanawake  katika kampeni upo wazi katika  wilaya  hiyo ya Mufindi ambayo mkuu  wa wilaya ni mwanamke ,mkurugenzi ni Mwanamke na mjumbe wa NEC Taifa ambae ni  yeye mwenyewe na kuwa nafasi hiyo  aliipata baada ya  kupambana na wanaume .


MWISHO

MCHUMI WA WIZARA YA VIWANDA NA BIASHARA KUGOMBEA UBUNGE JIMBONI KWA WAZIRI MGIMWA ASEMA WANA MUFINDI WAJIANDAE KWA NEEMA MPYA ......

Bw Exaud Kigahe mgombea  ubunge  jimbo la Mufindi kaskazini
Exaud Kigahe
Wanahabari  wakimsikiliza Bw Kigahe  wakati  akitangaza  nia ya  kugombea ubunge
MDAU  mkubwa  wa maendeleo ya elimu katika wilaya ya Mufindi mkoani Iringa na mzaliwa wa kijiji cha Nungwe, wilayani Mufindi Mkoani Iringa Bw Exaud Kigahe ambae ni mchumi mkuu wa  wizara ya viwanda na biashara amepania kuwakomboa kimaendeleo wakazi wa  jimbo la Mufindi Kaskazini linaloongozwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mahamudu Mgimwa iwapo  watamchagua kuwa mbunge wa  jimbo hilo.
Akizungumza na wanahabari juzi wakati akitangaza nia hiyo, Kigahe ambaye ni Mtaalamu wa Takwimu anayefanya kazi katika Wizara ya Viwanda na Biashara jijini Dar es Salaam alisema; “ni haki yangu kikatiba katika mchakato mzima wa demokrasia ya kweli, nilifanya hivyo mwaka 2010 lakini kura hazikutosha nataka kuingia tena mwaka huu.”
Katika kura za maoni za CCM za mwaka 201, Mgimwa alipata kura 6,386 huku Mungai akipata kura 3,430 na yeye (Kigahe) akiwa mshindi wa tatu kwa kupata kura 1,208.
Alisema anataka kugombea ubunge katika jimbo hilo huku akifahamu kwamba wananchi wake wengi ni masikini pamoja na  wana rasilimali za kutosha.
“Tuna ardhi nzuri inayofaa kwa kilimo cha mazao mbalimabli ya chakula na biashara kama chai, pareto na miti,” alisema.
Alisema wakati wilaya hiyo ikiwa na shamba kubwa kuliko mengine yote ya miti nchini, bado baadhi ya shule zake hazina madawati, milango na madirisha.
Alisema anataka kuingia katika kinyang’anyiro hicho huku kipaumbele chake kikiwa ni elimu kwani hazina hiyo ndio pekee inayoweza kusaidia kubadili maisha, uchumi na maendeleo ya ujumla ya wilaya ya Mufindi.
“Watoto wetu wakiwezeshwa, wakapata elimu bora wanaweza kushiriki kupambana na umasikini kwa kutumia rasilimali zilizopo,” alisema.
Alisema kwa muda mrefu jimbo la Mufindi Kaskazini limeendelea kupata viongozi wasio na mbinu za kuibadili hali hiyo.
Aliyataja maeneo mengine atakayoyapa kipaumbele endapo atashinda kura za maoni na kuchaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo kuwa ni pamoja na kuwashirikisha wananchi na serikali kuboresha sekta ya afya, kilimo, maji, biashara, mawasiliano na miundombinu ya barabara. Katika Uchaguzi Mkuu wa 2010, Mgimwa aliwania ubunge wa jimbo hilo baada ya kumuangusha katika kura za maoni, Joseph Mungai; kigogo aliyebahatika kushika uwaziri wa wizara mbalimbali katika awamu za serikali zote ikiwemo ya serikali ya Mwalimu Julius Nyerere na Jakaya Kikwete.

Katika awamu ya kwanza ya Rais Jakaya Kikwete, Mungai alipata kuwa Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika kabla hajahamishiwa katika wizara ya Mambo ya Ndani.

HIKI NDICHO ALICHOKISA LOWASA LEO ARUSHA

HOTUBA YA MHESHIMIWA EDWARD LOWASSA KWENYE MKUTANO NA WAANDISHI WA HABARI KWA AJILI YA KUTANGAZA NIA YA KUOMBA KUTEULIWA KUWA MGOMBEA WA CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM) KWA NAFASI YA URAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA


UTANGULIZI:

Ndugu zangu wana-CCM na Watanzania wenzangu,

Hii ni siku muhimu kwangu na kwa nchi yetu. Leo nimeamua kuwaita ili kuwatangazia rasmi Watanzania wenzangu azma yangu ya kutaka kuomba ridhaa ya chama chetu, Chama Cha Mapinduzi (CCM), niweze kuteuliwa kuwa Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Nasema hii ni siku muhimu kwangu kwa sababu naamini historia yangu itainakili kama ni siku ambayo kwa mara ya pili katika maisha yangu nimejitokeza kuwania kuiongoza nchi yetu kupitia chama chetu. Mara ya kwanza ilikuwa ni mwaka 1995 wakati wa uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi hapa nchini nilipojitokeza nikiwa pamoja na Rais Jakaya Kikwete; wakati ule sote tulikuwa wanasiasa vijana. Tulikwenda pamoja kuchukua fomu ndani ya Chama na baadaye tukafanya mazungumzo ya pamoja na waandishi wa habari. Tulileta hamasa kubwa pale tulipofanya jambo ambalo halikuzoeleka kwa Watanzania kwa kutangaza kwamba yeyote atakayepita kati ya wawili sisi basi mwenzake ambaye hatafanikiwa angemuunga mkono.

Ningeweza kujitokeza tena mwaka 2005 lakini nikaamua kwa dhati kabisa kumuunga mkono moja kwa moja Rais Jakaya Kikwete. Nikiwa Mwenyekiti wa Kampeni niliwaongoza wenzangu kufanikisha ushindi mkubwa wa mgombea tuliyemuunga mkono na baadaye ushindi mkubwa wa asilimia 80 wa Chama Cha Mapinduzi kwenye uchaguzi mkuu wa 2005.

Nitaeleza kwa nini nimeamua kujitokeza tena mwaka huu na kwa nini naamini mimi ndiye mtu sahihi wa kuiongoza nchi yetu wakati huu. Mpaka hapa itoshe tu kuwaeleza ni kwa kwa nini naamini leo ni siku muhimu kwangu.

Lakini nasema ni siku muhimu kwa nchi yetu pia. Nasema hivyokwa sababu naamini inajibu wito wa mahitaji ya sasa ya uongozi wa Taifa letu wa kumpata kiongozi imara atakayewaongoza Watanzania kujenga taifa imara. Na hili pia nitalieleza kwa kina.


HALI YA NCHI NA MATARAJIO YA WATU:

Miaka 48 iliyopita katika jiji hili la Arusha, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage alianzisha mchakato wa kujenga taifa huru kiuchumi na kupiga vita maadui umaskini, ujinga na maradhi kwakutumia silaha ya kujitegemea. Leo hii, wakati taifa likijiandaa kwa Uchaguzi Mkuu ujao, hatuna budi kutafakari tulikotoka, tulipo na tunapotaka kwenda ili tuweze kubuni upya mikakati ya kuhitimisha azma aliyo kuwa nayo Mwalimu, ili tujenge taifa huru, lenye utulivu, mshikamano, amani na maendeleo.


Nchi yetu hivi sasa inapita katika kipindi kigumu cha mpito katika maeneo yote makuu ya maisha yetu – katika siasa, katika uchumi na katika maisha ya kijamii.

Kisiasa, tumeshuhudia kuongezeka kwa vuguvugu la mfumo wa vyama vingi ambapo ushindani kati ya vyama vya siasa unazidi kuwa mkali na kwa bahati mbaya kufikia sura ya kuonekana kama vile ni mapambano ya watu binafsi badala ya mapambano ya sera na dira ya kuongoza nchi. Tunashuhudia kuongezeka uhasama binafsi kati ya wanasiasa ndani ya chama kimoja kimoja na pia kati ya wanasiasa wa chama kimoja dhidi ya kingine. Kadiri siku zinavyokwenda, hali inazidi kuzorota na ikiachiwa kuendelea nchi yetu inaweza kujikuta mahali pabaya. Kukua kwa ushindani ni jambo jema linalokomaza na kurutubisha demokrasia yetu na tukiwa na ushindani wenye afya unaweza kuwa chachu ya kuleta mabadiliko mema kwa wananchi na kupelekea kuongezeka kwa kasi ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika nchi yetu. Kinyume chake ushindani unaochukua sura ya chuki binafsi au kukomoana na hata kulipizana visasi si ushindani wenye tija na tunapaswa kuutafutia tiba. Tunahitaji uongozi imara kusimamia kipindi cha mpito kutoka siasa muflisi za aina hii na kuelekea kwenye siasa mpya zinazoimarisha ushindani wenye tija unaojikita katika kushindana katika kuwapatia huduma bora Watanzania.

Kiuchumi, tumeshuhudia ukuaji mzuri na kuongezeka kwa mapato ya ndani ya Serikali na uimarishaji wa mfumo wa uwajibikaji na ulipaji kodi. Kwa upande mwengine, Serikali ya Rais BenjaminiMkapa na Rais Jakaya Kikwete imefanya kazi kubwa katika uendelezaji wa sekta ya mafuta na gesi asilia ambapo kiwango kikubwa cha gesi asilia kimegunduliwa. Tanzania sasa imekuwa ni miongoni mwa nchi zinazovutia uwekezaji mkubwa katika sekta hiyo ambayo inatajwa kwamba inaweza kuja kubadilisha kabisa maisha ya Watanzania. Hata hivyo, kipindi hiki cha mpito kuelekea ujenzi wa uchumi wa kisasa kimeshuhudia kuongezeka kwa hofu na wasiwasi miongoni mwa wananchi kwamba hawatonufaika naukuaji huu wa uchumi na ugunduzi wa utajiri mkubwa wa gesi asilia. Kwa upande mwingine, vijana wanataka kuona ukuaji wa uchumi na ugunduzi wa utajiri huo unakwenda sambamba na uzalishaji wa ajira zenye maana ili waweze kukabiliana na changamoto za maisha yao. Niliwahi kusema kwamba tatizo la ukosefu wa ajira likiachiwa bila ya kutafutiwa ufumbuzi imara ni bomu linalosubiri kulipuka. Vijana wasio na ajira hupoteza matumaini na ni rahisi kughilibiwa kuingiza nchi katika machafuko.Tunahitaji uongozi imara kuweza kuikabili hali hiyo na kuitafutia suluhisho maridhawa.

Kijamii, kipindi cha karibuni tumeshuhudia mabadiliko makubwa ya tabia miongoni mwa raia katika hali ambayo haijawahi kuwa sehemu ya utamaduni wa Watanzania. Kumekuwa na ongezeko la kutisha la matukio ya uhalifu linalokwenda sambamba na wananchi kuonyesha wanapoteza imani na taasisi zinazosimamia sheria na usalama na kuamua kujichukulia sheria mikononi mwao. Kumeripotiwa matukio mengi yakiwemo ya kuvamiwa vituo vya polisi, askari kupigwa na kuporwa silaha, matumizi makubwa ya nguvu katika utatuzi wa migogoro mbalimbali hasa ile ya kijamii, mathalani migogoro ya wakulima na wafugaji, mivutano ya kidini na pia mivutano baina ya viongozi wa dini wenyewe kwa wenyewe na baina ya viongozi wa dini na wale wa Serikali. Matokeo yakemshikamano wa taifa nao unaingia majaribuni. Mara nyingine wananchi wanatuuliza viongozi iwapo hii ndiyo nchi tuliyoachiwa na waasisi wetu. Tunahitaji uongozi imara wa kukabiliana na changamoto hizi na kurudisha mshikamano wa taifa letu na watu wake.


WATANZANIA WANATAKA MABADILIKO:

Ndugu zangu, mnaweza kujiuliza kwa nini nimeyaeleza yote hayo na yana mahusiano gani na dhamira yangu ya kutangaza nia ya kutaka kuiongoza nchi yetu kupitia CCM?

Nimeyaeleza haya kwa sababu haya na matukio mengine yanayoendelea nchini yamepelekea Watanzania kutaka mabadiliko. Watanzania wanataka mabadiliko yatakayowawezesha kuzishinda changamoto hizi na kuwaongoza kujenga Taifa imara ambalo kila mwananchi wake anaishi akiwa na uhakika wa mahitaji yake muhimu na papo hapo akijiridhisha kwamba leo yake ni bora kuliko jana yake, na kesho yake itakuwa bora zaidi kuliko leo yake. Kwa maneno mengine, Watanzania wanahitaji mabadiliko yatakayowapa uongozi imara unaoweza kuwaongoza kujenga taifaimara. Hii ndio Safari ya Matumaini.

Chama chetu, Chama Cha Mapinduzi (CCM), na watangulizi wake, TANU na ASP, kimepata bahati ya kuungwa mkono na Watanzania tokea enzi za kupigania uhuru, wakati wa Uhuru wa Tanganyika na Mapinduzi ya Zanzibar, na pia miaka yote tokea Uhuru, Mapinduzi na hatimaye Muungano wetu. Watanzania hawajawahi kushuhudia chama kingine kikiongoza Serikali zetu zaidi ya CCM. Wamekiamini na wanaendelea kukiamini. Hata katika yale majimbo machache ya nchi yetu ambayo hatukufanya vizuri katika uchaguzi, ukiangalia kwa undani utaona si kwamba watu wa maeneo hayo wana matatizo na CCM kama Chama bali wana matatizo na baadhi ya viongozi ambao walishindwa kukiwakilisha vyema Chama na kutambua matakwa ya wananchi hao.

Mimi naamini kwamba hata katika kipindi hiki ambapo Watanzania wanaonekana kutaka mabadiliko bado wanaendelea kuamini kwamba watayapata mabadiliko hayo ndani ya CCM. Lakini kama alivyotupa wasia Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, mwaka 1995 wakati wa uchaguzi mkuu wa kwanza chini ya mfumo wa vyama vingi hapa nchini, Watanzania wasipoyapata mabadiliko hayo ndani ya CCM watayatafuta nje ya CCM. Mimi naamini kwamba CCM tunao uwezo wa kuwapa Watanzania mabadiliko wanayoyataka. Tuwape imani na imani hiyo iwe ni ya dhati na ya ukweli kwamba CCM inao uwezo wa kuwapa uongozi imara wanaouhitaji kwa ajili ya kujenga taifa imara.

Vyama vya siasa vinajumuisha watu na vinaongozwa na watu. Moja ya hulka ya binadamu ni kubadilika kulingana na mahitaji ya mazingira anayoishi. Kwa maneno mengine, binadamu ni ‘dynamic’. Kwa sababu hiyo basi, hata vyama vya siasa vinapaswa kuwa ‘dynamic’. CCM haijapata kuwa na upungufu wa sifa ya ‘dynamism’. Kwa zaidi ya miongo mitano sasa, CCM (na kabla yake TANU na ASP) iliweza kubadili dira na mwelekeo wake ili kwenda sambamba na mahitaji ya Watanzania ya wakati husika. Ndiyo maana tumepita katika vipindi tofauti vya mpito kwa mafanikio makubwa licha ya changamoto nyingi zilizotukabili. Tanzania imeendelea kuwa nchi ya amani licha ya kubadili mfumo wetu wa siasa kutoka ule wa chama kimoja kuja vyama vingi; licha ya kubadili mwelekeo wa uchumi wetu kutoka ule wa dola kumiliki njia zote kuu za uchumi kuja katika uchumi wa soko unaozingatia ushiriki mpana wa Watanzania wa matabaka yote; na hata karibuni kabisa katika mchakato wa kuipatia nchi yetu Katiba mpya.Tanzania tumeweza kufanya mabadiliko ya uongozi mara nne katika hali ya amani na maelewano, jambo ambalo nchi nyingi za Afrika zimeshindwa. Ni imani yangu kwamba tukijikubalisha tunaweza tena kuwapa Watanzania wanachokitaka katika zama hizi za sasa. Lakini ni lazima tuoneshe dhamira hiyo kwa dhati ili, kama alivyotuasa Mwalimu Nyerere, Watanzania wasiyatafute mabadiliko hayo nje ya CCM. Nasisitiza tena kwamba CCM inao uwezo wa kuwapa Watanzania mabadiliko wanayoyataka, lakini pia wananchi wana hiali kuchagua mabadiliko wanayoyataka.


UONGOZI UNAOHITAJIKA KULETA MABADILIKO YANAYOTAKIWA:

Rais Jakaya Kikwete amefanya kazi kubwa katika kipindi chake na kama ambavyo amekuwa akisisitiza mara kwa mara katika hotuba zake za karibuni ni kwamba yeye ametekeleza wajibu wake kwa kuweka misingi imara ya ujenzi wa Taifa la kisasa lenye uchumi madhubuti na unaoweza kukua kwa kasi. Amesema anamwachia atakayemkabidhi uongozi wa nchi yetu baada ya yeye kumaliza muda wake kuendeleza pale atakapoachia.

Kwa maoni yangu ili kuifanya kazi hiyo na kuzikabili changamoto nilizozieleza, nchi yetu inahitaji uongozi wenye sifa zifuatazo:

-    Uongozi wenye uthubutu, usioogopa kufanya kufanya maamuzi magumu;

-    Uongozi thabiti na usioyumba;

-    Uongozi makini na mahiri;

-    Uongozi wenye ubunifu na wenye upeo mkubwa;

-    Uongozi utakaozikabili changamoto kifua mbele na siyo kuzikimbia;

-    Uongozi unaoamini katika mfumo shirikishi katika ujenzi wa Taifa;

-    Uongozi unaozingatia muda katika kutekeleza majukumu yake.

Naamini pia kwamba wananchi wanataka Rais ajaye wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania awe na sifa kuu zifuatazo:

-    Aweze kuwaunganisha Watanzania (kukabiliana na viashiria vya migawanyiko ya aina mbali mbali inayoinyemelea Tanzania);


-    Aweze kuja na sera na mikakati ya kuinua uchumi wa Tanzania na kukuza pato la Mtanzania;ikiwemo kupunguza tofauti ya kipato kati ya aliyekuwanacho na wasiokuwanacho;


-     Aweze kuja na sera na mikakati ya kuzalisha ajira kwa vijana wetu;


-     Aweze kutokomeza mianya ya rushwa kwa vitendo;

-    Aweze kuwa mfano wa kuchapa kazi na kuwajibika;


-     Asimamie nidhamu ya matumizi ndani ya Serikali;


-     Aweze kusimamia ukusanyaji wa mapato ya Serikali;


-     Aweze kutumia fursa yetu ya kijiografia kibiashara


UONGOZI IMARA, TAIFA IMARA:

Naamini kwamba uongozi wa juu wa nchi katika nafasi ya Urais si kazi ya lelemama na unahitaji utashi. Kabla hata ya kutakiwa na wenzako ni lazima kwanza wewe mwenyewe uamini na uwaaminishe wenzio kwamba unao uwezo wa kuwaongoza wananchi wenzako. Na katika hilo, rekodi yako ni lazima izungumze na kulithibitisha hilo.

Binafsi nina hazina ya uzoefu na rekodi njema ya matokeo ya kazi nilizozifanya katika uongozi na utumishi wa umma ndani ya CCM na ndani ya Serikali. Nilianza kazi nikiwa Katibu Msaidizi wa CCM katika mikoa ya Shinyanga, Arusha na Moshi. Nimekuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa na Kamati Kuu ya CCM. Niliingia Bungeni mwaka 1985 na baadae mzee wangu, Rais Ali Hassan Mwinyi, akaniamini kwa kuniteua kuwa Waziri. Nimekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Waziri wa Ardhi, Makaazi na Maendeleo ya Miji, Waziri wa Mazingira, Waziri wa Maji na hatimaye Waziri Mkuu.

Miongoni mwa mafanikio ninayojivunia katika uongozi na utumishi wangu, na ambayo Watanzania wanayatambua na naamini wanayathamini, ni pamoja na:

-    Nikiwa Waziri wa Maji chini ya uongozi mahiri wa Rais Mkapa,tulithubutu kushawishi na kuongoza hatua za kukataa kufungika na makubaliano yaliyowekwa na wakoloni ambayo yalikuwa yanazizuia nchi zilizopakana na Ziwa Victoria zisiweze kufaidika ipasavyo na maji ya Ziwa hilo. Leo hii ndugu zangu wa Kanda ya Ziwa wanafaidika na ujasiri wetu katika kukabiliana na suala hilo zito.

-    Nikiwa Waziri wa Mazingira, tulipanda miti mingi zaidi kuliko wakati mwingine wowote tokea Uhuru na pia kuwakabili kikamilifu na kuwachukulia hatua waliochafua na kuharibu mazingira.

-    Nikiwa Waziri Mkuu, tulisimamia agizo la Rais Kikwete na kufanikisha utekelezaji wake ndani ya miaka miwili kwa kujenga shule nyingi za sekondari kuliko wakati mwingine wowote tokea Uhuru.

-    Kipindi hicho hicho, tulisimamia agizo la Rais Kikwete la kuanzisha Chuo Kikuu cha Dodoma na kuhakikisha kinakamilishwa kwa wakati. Leo hii Chuo Kikuu hicho ni fahari ya Tanzania.

Tunapomtafuta Rais wa Jamhuri ya Muungano ni lazima tukumbuke kwamba tunamtafuta mtu ambaye atakuwa pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama katika nchi yetu. Na kwa Chama Cha Mapinduzi tunamtafuta mtu ambaye atakuwa pia Mwenyekiti wa Chama chetu.

Naamini kwa vigezo vyote, nina kila sifa ya kubeba dhamana hizo nzito. Katika mambo ambayo najivunia na sitoyasahau katika historia yangu ni kushiriki kwangu kuilinda nchi yangu pale ilipohitajika. Nilishiriki kikamilifu katika Vita vya Kagera nikiwa miongoni askari wa mstari wa mbele wa mapambano. Nikiwa Mbunge nilipata heshima ya kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama. Naamini Watanzania hawatakuwa na wasiwasi wa usalama wao nikiwa Amiri Jeshi Mkuu.

Nimeeleza uzoefu wangu kwenye Chama na huo hauhitaji maelezo zaidi. Ninakijua vyema Chama Cha Mapinduzi kiasi cha kutosha kabisa kukiongoza kama Mwenyekiti wake pale wakati utakapofika. Wana-CCM wanajua nikikabidhiwa uongozi, Chama chetu kitakuwa chini ya nahodha madhubuti, mzoefu na asiyeyumba.

Kutokana na rekodi yangu hii, naamini ninazo sifa za kuwaongoza Watanzania wenzangu katika zama mpya za ujenzi wa Taifa la kisasa lenye watu wazalendo walioshikamana na lenye uchumi imara unaomnufaisha kila Mtanzania. Naamini ninao uwezo wa kuwapa Watanzania Uongozi imara kwa ajili ya ujenzi wa Taifa Imara.


DIRA YANGU NA MATARAJIO YA WATANZANIA:

Mfumo tuliojiwekea hapa nchini unaelekeza kila chama cha siasa kinachosimamisha mgombea Urais na kinachowania kuongoza nchi yetu kuja na Ilani ya Uchaguzi ambayo ndiyo inayoweka misingi ya sera zitakazofuatwa na Serikali itakayoongozwa na chama hicho pale kinapopewa ridhaa ya kuongoza nchi. Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimekuwa ni cha kupigiwa mfano katika kutayarisha Ilani bora na ndiyo maana mara zote kimepewa ridhaa ya kuongoza nchi yetu. Tumefanya hivyo tokea enzi za mfumo wa chama kimoja na tumeendelea kufanya vizuri katika mfumo wa kushindanisha sera kupitia vyama vingi. Najua kwamba Ilani ya CCM ya mwaka 2015 imo katika hatua za mwisho za kukamilishwa na itakapopata baraka za vikao vya Chama itakuwa ndiyo msingi wa utendaji wa Serikali ya Awamu ya Tano itakayochaguliwa Oktoba mwaka huu. Hata hivyo, naamini pia kwamba mgombea mwenyewe anayetaka ridhaa ya Chama na ya Watanzania kuongoza nchi naye anapaswa kueleza dira yake.

Mimi, baada ya kutafakari kwa kina changamoto tulizo nazo na matarajio na matumaini waliyo nayo Watanzania, naamini kwamba Uongozi imara unaolenga kujenga Taifa imara unapaswa kuwa na dira yenye malengo yafuatayo:


-    Kuimarisha Muungano wetu kwa kuyashughulikia yanayotutenganisha na kuyafanyia kazi ili yasivuruge yale yanayotuunganisha ambayo ni mengi zaidi na makubwa zaidi.


-    Kushughulikia matumizi mabaya ya siasa za udini na ukabila kwa kuimarisha siasa zilizoshiba uzalendo na zenye kutuelekeza kwenye Utanzania wetu.


-    Kujenga uchumi imara na wa kisasa, na ambao ni shirikishi unaomnufaisha kila Mtanzania aliyeko mjini au kijijini. Tunapaswa kubadili hali tuliyo nayo sasa ambapo Kilimo kinaonekana kama kimesahauliwa na wakulima wetu wanaonekana wanakata tamaa.Wafugaji na wavuvi nao wanahisi sekta zao hazijapewa umuhimu unaostahiki. Tunahitaji kuondokana na hali iliyopo sasa ya kuwa Taifa linalouza malighafi na badala yake kuwa Taifa linalosindika na kusarifu mazao na kutengeneza wenyewe bidhaa zitokanazo na malighafi yake. Ndani ya miaka mitano ijayo tutahakikishatunaiondolea Tanzania sifa ya kusafirisha malighafi na badala yake kusindika mazao yanayozalishwa hapa nchini kama pamba, kahawa, chai na korosho na kuyaongezea thamani (value addition).Mkakati huu utazalisha ajira nyingi na kuongeza mapato ya fedha za kigeni nchini. Tunahitaji kujielekeza kwenye kujenga viwanda na kuleta ajira. Tuna vivutio vingi sana vya utalii lakini bado Tanzania inapitwa na nchi kama Afrika Kusini katika kuingiza idadi kubwa ya watalii. Kwa nini nchi kama Dubai iweze kuvutia watalii kwa mamilioni na Tanzania tushindwe? Tunapaswa kukabiliana kikamilifu na hisia zilizopo miongoni mwa wananchi kwamba Tanzania hainufaiki ipasavyo na utajiri wa rasilimali zake nyingi ilizo nazo. Tutajipanga zaidi kuhakikisha tunanufaika kama nchi na rasilimali zetu kama madini na gesi asilia. Hii ndio Safari ya Matumaini


-    Kukuza kipato cha wananchi na kunyanyua hali za maisha ya watu wetu. Tunapaswa kuhakikisha kuwa ukuaji wa uchumi tunaouzungumzia unamnufaisha Mtanzania aliyeko mjini au kijijini na kwamba hali za Watanzania wa matabaka yote zinanyanyuka na kwamba wanaridhika na kuuona uhalisi wa ukuaji wa maendeleo tunayoyazungumzia.


-    Kuondokana na sifa mbaya ya kuwa Taifa ombaomba. Kwa wingi wa rasilimali tulizo nazo na neema ya ardhi, maziwa, mito na bahari Tanzania tuna kila sababu ya kuacha kuwa ‘bakuli la ombaomba’ na badala yake kuwa ‘mkoba wa neema’ katika Afrika.We can transform our nation from being the begging bowl to become the bread basket of Africa.


-    Kujenga mfumo mpya wa elimu unaojielekeza kuwatayarisha vijana wetu waweze kuajirika, kujiajiri na kushindana katika soko la ajira. Tumepiga hatua kadhaa katika elimu lakini kiwango cha elimu bado ni hafifu. Pamoja na kuwa na shahada (degrees), bado wahitimu wetu hawawezi kushindana kwenye soko la ajira. Wakati tunazungumzia kuunganisha soko la ajira katika Afrika Mashariki,hatuna budi kujikita kubadili mfumo wetu wa elimu na kuuelekeza kwenye mafunzo ya ufundi na stadi yanayowajenga wahitimu wetu kuwa wabunifu na wenye kujiamini katika kukabiliana na changamoto za maendeleo duniani.


-    Kuhakikisha tunakabiliana ipasavyo na kulipunguza kwa kiasi kikubwa kama si kulimaliza kabisa tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama. Ni jambo la kusikitisha kwamba tumezungukwa na mito na maziwa lakini bado watu wetu hawana maji ya kunywa hata ndani ya Dar es Salaam.

-    Kujenga na kusimamia mfumo imara wa kutekeleza sera na sheria tunazozitunga na kuzipitisha kwa lengo la kumtumikia Mtanzania na kumjengea uwezo wa kubadili maisha yake ili tuweze kwenda sambamba na viwango vya kimataifa. Tanzania imepata sera na sheria nzuri sana lakini utekelezaji wake umekuwa hafifu. Tumekuwa wepesi wa kutunga sera na sheria lakini wazito mno wa kuzitekeleza na kuzisimamia. Uongozi imara wenye kulenga ujenzi wa Taifa imara utahakikisha tunakuwa mfano wa utekelezaji wa sera na sheria tulizo nazo na mpya zitakazotungwa kukabiliana na malengo tuliyojiwekea.


Mambo haya niliyoyaeleza hapa ndiyo yatakayokuwa msingi mkuu wa utendaji wa Serikali nitakayoiongoza pale nitakapopewa ridhaa ya kubeba bendera ya CCM katika nafasi ya Urais na pia nitakapopewa ridhaa ya kuliongoza Taifa letu kupitia uchaguzi mkuu wa mwaka huu.RAMANI YA UONGOZI IMARA NINAOUAMINI (LEADERSHIP ROADMAP):

Kama nilivyotangulia kusema, kazi ya kuongoza nchi si lelemama na hasa unapoongozwa na dhamira ya dhati na msukumo wa ndani ya nafsi unaojielekeza kubadilisha maisha ya wananchi wenzako waliokuamini uwaongoze. Kwa vyovyote vile, hiyo haiwezi kuwa kazi ya mtu mmoja. Ni kazi ya pamoja. Lakini ili muweze kufanya kazi kama timu moja iliyojipanga kisawasawa kuleta mabadiliko yanayohitajika na ili muweze kweli kutoa Uongozi imara unaojikita kujenga Taifa imara hapana budi kiongozi mkuu anayeongoza timu hiyo aweke ramani anayokusudia kuifuata katika kutoa uongoziimara anaoukusudia yaani ‘Leadership Roadmap’.

Pamoja na kuwa sehemu ya uongozi huko nyuma, kutakuwa na maamuzi na matumaini mapya. Ramani ya uongozi imaraninayokusudia kuutoa kwa wenzangu na ambayo nitaitumia kuiongoza timu yangu katika kuwatumikia Watanzania wenzangu itajikita katika maeneo yafuatayo:


1. Kurejea kwenye Katiba katika kuainisha nia, dhamira na malengo yetu ya kujenga jamii inayozingatia misingi ya demokrasia, udugu na amani. Muhimu katika hili ni kukemea tabia mbaya zinazochochea mfarakano katika jamii kama vile matumizi mabaya ya siasa za udini na ukabila. Aidha moja ya misingi muhimu ya Katiba ni Muungano wetu. Itakuwa dhamira yangu kuimarisha misingi ya Muungano pamoja na udugu wa damu nahistoria ya ushirikiano iliyojengwa na waasisi wetu, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Sheikh Amri Abeid Karume na kuyaenzi Mapinduzi matukufu ya Zanzibar.


2. Kujenga fikra mpya za kurejesha kujiamini na kufufua azma ya kujitegemea kama Taifa. Ni dhahiri kuwa pamoja na rasilimali zetu, bado Tanzania ni taifa tegemezi. Bado tunajidanganya kuwa wafadhili watatujengea nchi. Tukumbuke, nchi zinajengwa nawananchi wake. Nasi pia lazima tujikomboe kifkra na tuondokane na utamaduni wa kuwa tegemezi. Tuanze kwa kujipiga kifua kwa kujiamini kuwa tunaweza kujitegemea na kuijenga Tanzania sisi wenyewe.Kujiamini na kujitegemea ndio uhuru wa kweli.


3. Kujenga uzalendo, uadilifu ikiwa ni pamoja na kuimarisha uwazi katika shughuli zote za serikali na kupambana na rushwa.Watanzania tumepoteza uzalendo kwa kiasi kikubwa. Kuna vitendo vinavyoashiria kuwa hatuipendi tena nchi yetu. Tunashabikia wizi na rushwa. Inabidi turejee kwenye misingi ya taifa letu misingi ya uadilifu na uzalendo. Tukumbuke kuwa hatuwezi kujenga uchumi wa kisasa kama tutaruhusu rushwa ishamiri. Wawekezaji hawataleta mitaji yao kwa wingi kama rushwa itaendelea kutawala katika huduma serikali na wananchi hawawezi kupata huduma bora kama rushwa itaendelea kutawala. Ni lazima tuipinge rushwa kwa vitendo sio maneno.4. Kujenga Serikali madhubuti, makini na yenye nidhamu inayoendeshwa kwa misingi ya sheria, uwazi na uwajibikaji.Maendeleo ya watu hayawezekani bila serikali kusimamiautekelezaji sera na miradi na kuleta ufanisi katika kutoa huduma na kusimamia maendeleo. Tumekuwa wepesi wa kutunga sera lakini wazito wa kuzitekeleza na kuzisimamia.


5. Kuleta msukumo mpya wa ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi katika ujenzi wa uchumi wa kisasa na unaojitegemea. Sekta binafsi ndiyo nyenzo ya uchumi imara. Inazalisha mali, ajira na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika pato la taifa kwa kulipa kodi. Ilisekta hii itoe mchango unaotakiwa katika maendeleo ni lazima ifanye kazi na serikali kwa karibu. Tukumbuke, bila uchumi imarahakuna huduma bora!


6. Uwekezaji katika huduma za jamii. Elimu na afya bora, mazingira, makazi safi na maji salama ndiyo mihimili ya maendeleo ya watu. Hii inawezekana tu iwapo serikali itakuwa na sera na utashi wa kuutambua uboreshaji wa huduma za jamii kama ndiyo lengo kuu la maendeleo ya nchi. Serikali nitayoiongoza itahakikisha kuwa kila Mtanzania anapata elimu bora na inayogharamiwa na serikali kama mimi na wenzangu tulivyopata. Wakatitunazungumzia kuunganisha soko la ajira katika Afrika Mashariki, hatuna budi kurekebisha mfumo wetu wa elimu na kuuelekeza kwenye mafunzo ya ufundi na ustadi yanayowajenga wahitimu wetu kuwa wabunifu, wenye kujiamini, wenye uwezo kushindana katika soko la ajira na wa kujiajiri. Napenda kusisitiza kuwa elimu ndiyo muhimili wa maendeleo, ndiyo mkombozi wa kweli wa binadamu. Mimi ni mfano hai wa ukombozi wa elimu. Elimu ndiyoimenivusha kutoka kijijini kwetu Ngarash na kunipa upeo wa kitaifa. Mama akiwa na elimu atajua umuhimu wa kumpeleka mwanae shule, anapata lishe bora na chanjo stahili na kuwa anaishi katika mazingira safi. Elimu ndilo jibu la umaskini, maradhi na ujinga.Taifa lililo elimika ni taifa lenye maendeleo.
7. Kujenga uchumi shirikishi unaolenga kuondoa umaskini.Mkakati wa kuondoa umaskini Tanzania lazima ujikite kwenye nguzo za ushiriki wa kila Mtanzania katika uchumi wa taifa. Kwa misingi hii, tukiweza kupunguza umaskini, tutaweza pia kupunguzatofauti za kipato ambazo tukiziacha ziendelee kukua kwa kiasi cha sasa, zinaweza kuhatarisha utulivu na amani katika jamii yetu.Uchumi shirikishi ndio silaha dhidi ya umaskini.


8. Kuimarisha ulinzi wa nchi na usalama wa raia na ujirani mwema.Itakuwa nia yangu kuimarisha misingi iliyojengwa kulinda na kudumisha umoja na amani nchini. Kadhalika, nitahakikisha kuwa usalama wa mipaka ya Tanzania unaimarishwa kwa misingi ya ujirani mwema na kutanzua migogoro na matatatizo yoyote na nchi jirani, kwa njia ya diplomasia na mazungumzo.

HITIMISHO:

Hii ndiyo misingi na dira ya uongozi wangu. Nachelea kusema kuwa haitakuwa kazi rahisi. Lakini kwa ushirikiano wa kila mmoja na maamuzi magumu, yote yanawezekana. Tumeona nchi nyingi zilizosimamiwa na utawala thabiti wa serikali za kimaendeleo zikikabili na kupunguza umaskini katika kizazi kimoja. Kama mataifa mengine yamefanikiwa, tena bila raslimali kama zetu, kwa nini sisi tushindwe? Tuna kila sababu ya kufanya maamuzi magumu sasa ili kuwajengea Watanzania matumaini mapya ya maendeleo. Naomba nisisitize kuwa katika uongozi wangu hakutakuwa na nafasi ya majungu, na visasi. Hatutaangalia nyuma bali tutasonga mbele kwani ndicho Watanzania wanakitarajiakutoka kwa uongozi uliojengwa kwenye misingi bora.


Ndugu Watanzania:-


Ni maono yangu kuwa siku si nyingi nchi yetu itaanza safari yenye uelekeo wa matumaini na neema tele kwa wananchi.


Ni maono yangu kuwa siku si nyingi sisi kama Watanzania kwa umoja wetu tutajivunia kuishi katika nchi tunayoipenda na inayoendeshwa kwa misingi ya utawala bora, chini ya serikali ya kimaendeleo iliyojengwa kwenye fikra mpya za uzalendo, uadilifu, utendaji na uwajibikaji.


Ni maono yangu kuwa Peke yangu sitaweza, lakini kwa maamuzi magumu na ushirikiano wa kila mmoja wetu ikiwa ni pamoja na wagombea wenzangu ndani ya CCM, inawezekana kuanza safari hii ya Matumaini Mapya.

Kabla ya kumaliza hotuba yangu hii fupi, kuna mambo matatu ningependa kuyaweka wazi hapa.


La kwanza, linahusu msingi wa uongozi ninaouamini na ambao nimeusema mara kadhaa hapa. Msingi huo ni UWAJIBIKAJI.Watanzania wananifahamu mimi si mtu wa maneno, ni mtu wa vitendo. Naamini kwa dhati kabisa kwamba huwezi kuwa na Uongozi imara utakaoweza kusimamia ujenzi wa Taifa imara iwapo huna ujasiri wa kuwajibika. Mimi nimeongoza kwa mfano, na pale ilipobidi, nilikubali kuwajibika na kubeba dhamana ya uongozinilipojiuzulu nafasi ya Waziri Mkuu.


La pili, mimi si mtu wa visasi. Siamini katika kuangalia ya nyuma. Yaliyopita si ndwele, tugange yajayo. Na kwa nini tuangalie nyuma wakati kama taifa tuna kazi kubwa sana mbele yetu inayohitaji kufanywa? Mimi ni Mkristo; najifunza kutoka kwa Bwana Yesu ambaye alipoulizwa: “Nisamehe mara ngapi?” Alijibu, “Samehe mara sabini mara saba”. Nitaenzi na kudumisha utamaduni huu wenye sura ya utu na heshima.


La Tatu, natambua kwamba dhamana ya Urais ni shughuli nzito hasa kwa taifa ambalo lina changamoto nyingi. Nataka niwahakikishie Watanzania wenzangu kwamba afya yangu ni njema kuweza kuwatumikia katika jukumu hili zito. Pamoja na vijineno vinavyosemwa pembeni, mimi mwenyewe ndiye ninayejijua zaidi. Nawahakikishia kuwa nisingekuja hapa leo na kueleza nia yangu hii ingekuwa sina uhakika na afya yangu.

Natoa RAI kwa Chama changu cha CCM, nadhani umefika wakati kwamba tutende tofauti na mazoea, watu wote walionyesha nia ya kutaka kuongoza, liundwe jopo la madaktari wa ndani na nje ya nchi tupimwe afya zetu, kwa hili najitolea kuwa wa KWANZA KUPIMWA afya yangu


Safari tuianze leo, hatuna kesho nyingine.Ahsanteni sana kwa kunisikiliza

NEC YAKAMILISHA MAANDALIZI UBORESHWAJI WA DAFTARI LA WAPIGA KURA KWA MIKOA 4

Maandalizi ugawaji wa mashine kwa ajili ya kuandikisha wanchi katika daftari la wapiga kura kwa Kanda ya 5 Tano kati ya Sita yamekamilika leo Mei 29, 2015 zaidi ya Biometric Voter Registration (BVR) zipatazo 1492 zinaanza kusambazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Kuanzia mapema Alfajiri Kanda ya Tano ni Mikoa ya Mara, Arusha, Manyara na Kilimanjaro.  Picha na Cathbert Angelo Kajuna

MRATIBU MKAZI WA UN NCHINI NA WAZIRI MAMBO YA NDANI YA NCHI WATEMBELEA ENEO LA MAPOKEZI YA MUDA KWA WAKIMBIZI MJINI KIGOMA

IMG_0495
Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP), Alvaro Rodriguez (wa pili kushoto) akiongozana na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mh. Mathias Chikawe (wa tatu kushot0) pamoja na Mkurugenzi wa Idara ya huduma za Wakimbizi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Harrison Mseke (katikati), Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mtaifa la kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), Joyce Mends-Cole (wa pili kulia), Mkuu wa ofisi ya Shirika la Umoja wa Mtaifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) Kasulu, Kigoma, Amah Assiama-Hillgartner (kulia) mara tu baada ya kuwasili kwenye viwanja vya Lake Tanganyika mjini Kigoma, eneo ambalo Wakimbizi wanapokelewa na kupewa huduma ya kwanza kabla ya kuelekea katika eneo maalum ya Nyarugusu, wilayani Kasulu mkoani Kigoma.(Picha zote na Zainul Mzige wa modewjiblog)
Na Modewjiblog team
Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mh. Mathias Chikawe katikati ya wiki wametembelea eneo la mapokezi ya Wakimbizi kutoka Burundi lililopo katika viwanja vya Lake Tanganyika mjini Kigoma.
Walipofika katika eneo hilo la mapokezi waliojionea huduma mbalimbali zilizokuwa zikitolewa na Mashirika ya Umoja wa Mataifa likiwemo Shirika la kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), Shirika la Kimataifa Ia Uhamiaji (I.O.M), Shirika la kuhudumia Watoto (UNICEF), Shirika la Chakula duniani (WFP), Shirika la afya duniani (WHO) pamoja na Shirika la UNFPA linaloshughulikia mahitaji ya wanawake hasa wale waliokuwa wajawazito.
Wakimbizi wengi waliofika eneo hilo walikuwa na afya dhoofu kutokana na kusafiri kwa umbali mrefu.
Kutokana na hali hiyo baadhi yao ilibidi wapatiwe huduma ya kwanza kabla ya kupelekwa eneo maalum lililotengwa kwa ajili ya makazi yaliyotengwa kwa Wakimbizi ikiwemo kambi ya Nyarugusu iliyopo katika wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma.
Hata hivyo kambi hiyo ya Nyarugusu ina uwezo wa kuchukua sio zaidi ya Wakimbizi 50,000 lakini sasa ina Wakimbizi zaidi ya 48,000 kutoka Burundi na 60,000 kutoka Jamuhuri ya watu wa Congo.
Aidha Waziri Chikawe alisema kuwa Serikali imetenga eneo maalum ambalo litajengwa kambi mpya itakayojulikana kama Nyarugusu B ambayo itakuwa ni mahususi kwa Wakimbizi kutoka Burundi.
Mh. Chikawe alisema kuwa kambi hiyo itakamilika ndani ya miezi mitatu kutoka hivi sasa, ili kuwatenganisha Wakimbizi kutoka Congo na Burundi.
IMG_0457
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mh. Mathias Chikawe akizungumza na wafanyakazi wa wa mashirika ya Umoja wa Mataifa wanaoandikisha Wakimbizi wanaowasili kwenye uwanja wa Lake Tanganyika kabla ya kuelekea katika kambi ya Nyarugusu, iliyopo wilayani Kasulu mkoani Kigoma.
IMG_0468
Mkuu wa ofisi ya Shirika la Umoja wa Mtaifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) Kasulu, Kigoma, Amah Assiama-Hillgartner (kushoto) akifafanua jambo kwa Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP), Alvaro Rodriguez (wa tatu kushoto) pamoja na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mtaifa la kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), Joyce Mends-Cole (wa pili kushoto) walipotembelea uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma.
IMG_0504
Mmoja wa watoa huduma kwenye kituo cha muda cha Wakimbizi katika viwanja vya Lake Tanganyika akipuliza dawa ya kuua wadudu kwenye mifereji inayozunguka uwanja huo kwa ajili ya kujikinga na magonjwa mbalimbali ya milipuko ikiwemo Kipindupindu.
IMG_0512
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mh. Mathias Chikawe (wa pili kulia) akizungumza na baadhi ya Wakimbizi kutoka Burundi waliokuwa kwenye foleni ya kupanda mabasi kuelekea kambi ya Nyarugusu kwenye makazi maalum yaliyotengwa na Serikali ya Tanzania yanayohudumiwa na Shirika linalohudumia Wakimbizi (UNHCR) na mashirika mengi ya Umoja wa mataifa. Wanne kulia ni Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP), Alvaro Rodriguez na wa kwanza kulia ni Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mtaifa la kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), Joyce Mends-Cole.
IMG_0440
Foleni ya Wakimbizi kutoka Burundi kuelekea kwenye mabasi maalum yaliyoandaliwa na Shirika la IOM kuwapeleka kwenye eneo maalum la kambi ya Nyarugusu iliyopo wilayani Kasulu mkoani Kigoma.
IMG_0524
Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP), Alvaro Rodriguez (kulia), Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mh. Mathias Chikawe (wa pili kulia) pamoja na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mtaifa la kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), Joyce Mends-Cole wakishuhudia baadhi ya Wakimbizi wakipakia kwenye mabasi maalum yaliyoandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la IOM tayari kuelekea katika kambi ya Nyarugusu iliyopo wilayani Kasulu, mkoani Kigoma.
IMG_0525
IMG_0544
IMG_0550
Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP), Alvaro Rodriguez (aliyeipa mgongo kamera kushoto), Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mh. Mathias Chikawe (wa pili kushoto) pamoja na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mtaifa la kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), Joyce Mends-Cole wakiagana na baadhi ya Wakimbizi wanaoelekea kwenye kambi ya Nyarugusu wilayani Kasulu mkoani Kigoma kutokea katika kituo cha muda cha mapokezi na huduma za afya kilichopo katika viwanja vya Lake Tanganyika mjini Kigoma.
IMG_0475
Baadhi ya wakina mama na watoto zao wakiwa wamejipumzisha ndani ya viwanja vya Lake Tanganyika huku wakisubiri safari ya kuelekea katika kambi ya Nyarugusu, iliyopo wilayani Kasulu mkoani Kigoma.
IMG_0523
Wahudumu wa mashirika mbalimbali ya Umoja wa Mataifa wakiwapulizia dawa maalum kwenye mikono na miguu kwa ajili ya kuua bakteria kabla ya kuingia ndani ya mabasi na kuelekea katika kambi ya Nyarugusu iliyopo wilayani Kasulu mkoani Kigoma.
IMG_0531
IMG_0536
IMG_0563
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mh. Mathias Chikawe akiwa ameambatana na Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP), Alvaro Rodriguez (kushoto) wakielekea kutembelea mabanda mbalimbali ya huduma za afya yaliyopo kwenye viwanja vya Lake Tanganyika yanayotoa huduma kwa Wakimbizi wanaowasili kabla ya kupekwa kambini.
IMG_0559
Pichani juu ni baadhi ya watoto wakipatiwa matibabu ndani ya kituo cha muda kabla ya kuelekea kambi ya Nyarugusu iliyopo wilayani Kasulu mkoani Kigoma.
IMG_0568
Wazazi na watoto wakiwa kwenye hema maalum, huku nwengine wakiwa kwenye dripu za kuongezewa maji mwilini.
IMG_0558
IMG_0569
Wafanyakazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na waandishi wa habari wakisafisha mikono yao na kupuliziwa dawa maalum katika viatu mara baada ya kutembelea mahema yenye wagonjwa mbalimbali Wakimbizi kutoka Burundi wanaopatiwa matibabu kwenye kituo cha muda kilichopo kwenye viwanja vya Lake Tanganyika mjini Kigoma.
IMG_0578
Baadhi ya watoto wakijiliwa na kujifaraji kwa kucheza mpira katika kituo maalum cha kupokelea Wakimbi wanaotafuta hifadhi nchini Tanzania wakitokea nchini Burundi katika uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma.
IMG_0581
Pichani juu na chini ni familia za Wakimbi wakiwa wamejipumzisha kwenye kituo cha muda katika viwanja vya Lake Tanganyika huku wakisubiri safari ya kuelekea katika kambi ya Nyarugusi iliyopo wilayani Kasulu mkoani Kigoma.
IMG_0583
IMG_0500
Sehemu ya eneo la uwanja wa Lake Tanganyika.

MTANZANIA DKT WINNIE AULA WHO.................................

                                           Na Mwandishi Wetu
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani, Dk. Margaret F. Chan amemteua Dk. Winnie Mpanju-Shumbusho kutoka Tanzania kuwa Mkurugenzi Mkuu Msaidizi wa Shirika la Afya Duniani, upande wa masuala ya Ukimwi, Kifua Kikuu, Malaria na Magonjwa yaliyosahaulika. 

Uteuzi huu umetangazwa rasmi na Dk. Chan wakati wa kikao cha 68 cha Baraza Kuu la Shirika la Afya Duniani kilichoanza tarehe 14 hadi 26 Mei, mwaka huu, Geneva nchini Uswisi.

Dk. Mpanju-Shumbusho ni mtaalamu na kiongozi mwenye uzoefu wa miaka zaidi ya 30 katika ngazi za juu za uongozi katika sekta ya Afya na Ushirikiano wa Kimataifa.

Kabla ya uteuzi huu, Dk. Mpanju-Shumbusho alikuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu Msaidizi ndani ya Shirika la Afya Duniani upande wa Ukimwi, Kifua Kikuu, Malaria na Magonjwa yaliyosahaulika na akiwa na cheo cha Ukurugenzi wa Idara inayoshughulikia Ushirikiano wa Shirika la Afya Duniani na Mfuko wa Dunia wa kupambana na Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria (Global Fund to Fight AIDS, Tuberculosis na Malaria). 

Dk. Mpanju-Shumbusho pia ni mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani kwenye Bodi ya Mfuko wa Dunia wa kupambana na Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria na Bodi mbalimbali za kimataifa.

Hapo awali, Dk. Winnie Mpanju-Shumbusho alikuwa Mkurugenzi wa Idara ya kudhibiti Ukimwi na magonjwa mengine katika WHO, Makao Makuu Geneva, Uswisi.

Kabla ya kujiunga WHO, aliwahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa East, Central and Southern Africa Health Community Secretariat yenye makao makuu yake, Arusha, Tanzania. 

Vilevile, aliwahi kuwa Mkuu wa Idara na Mhadhiri Mwandamizi, Idara ya Afya ya Jamii na Mgonjwa ya Watoto, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, (Muhimbili University of Health Science). 

Katika wadhifa huu, Dk. Winnie pia alikuwa mwanzilishi wa mipango mbalimbali ya afya na taaluma na Mshauri Mkuu wa Wizara ya Afya, Tanzania upande wa Afya ya Jamii. Pia amewahi kuwa mjumbe wa Bodi mbalimbali za kimataifa.

Dk. Mpanju-Shumbusho ana Shahada ya Udaktari kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam; vilevile ana Shahada ya Uzamili katika Afya ya Jamii kutoka Chuo Kikuu cha Tulane, Marekani na Shahada ya Uzamili katika Medicine (Paediatric and Child Health) kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Vilevile ana Shahada ya Uzamifu na Shahada nyingine mbalimbali.

Akiwa Mkurugenzi na Mtaalamu katika Shirika la Afya Duniani, amekuwa mstari wa mbele kuandaa, kuongoza na kutekeleza mipango mkakati ya Dunia ya kujenga na kuimarisha sekta ya afya, hususani katika nchi maskini na zinazoendelea. 

Mipango hii imezaa mafanikio makubwa ikiwamo kujenga uwezo wa nchi maskini kukabiliana na maradhi na afya za kina mama na watoto. 

Sambamba na hilo, mipango hiyo pia ilifanikisha upatikanaji wa dawa za gharama nafuu katika nchi maskini ili kuweza kumudu gharama za matibabu kwa watu maskini. 

Nchini Tanzania, Dk. Mpanju-Shumbusho ameweza kufanikisha upatikanaji wa matibabu na huduma nasaha za kusaidia kudhibiti ugonjwa wa Ukimwi, Kifua Kikuu, Malaria na magonjwa yaliyosahaulika.

Dk. Shumbusho ameolewa na ana watoto wawili, wa kiume na kike.