Matukio Daima

Tembelea kila siku kwa habari na matukio mbali mbali..

Matukio Daima

Kwa Habari za Kitaifa.

Matukio Daima

Kwa Habari za Kimataifa.

Matukio Daima

Kwa Habari za Uchumi na Biashara.

Matukio Daima

Kwa Habari za Michezo na Burudani.

January 31, 2014

DC KILOLO AWALILIA WAJAWAZITO WAWILI WALIOPOTEZA MAISHA WAKIENDA KUJIFUNGUA MJINI IRINGA

Mkuu wa wilaya ya Kilolo Gerald Guninita  ameuomba mfuko  wa bima ya afya (NHIF) kuwaidia  kuboresha  Hospital ya wilaya ya Kilolo kutokana na  kuongezeka kwa vifo vya wanawake  wajawazito baada ya   ndani ya  mwezi mmoja huu  wanawake  wajawazito  wawili  kupoteza maisha   wakati  wakikimbizwa katika Hospital ya   Rufaa ya  mkoa  wa Iringa.

Mkuu  huyo wa wilaya  aliyasema hayo leo  wakati  wa kikao  cha kamati ya ushauri  cha mkoa wa Iringa kilichofanyika katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo.

Kwani  amesema jitihada zinazofanywa na NHIF katika  mkoa wa Iringa ni kubwa na kuiwezesha wilaya ya Kilolo kuendelea  kufanya vizuri katika   mfuko huo na  hivyo kuomba mfuko kuboresha  Hospital   hiyo ya  wilaya  ili kuepusha  wajawazito  kuendelea  kupoteza maisha kwa  kukosa huduma  bora za afya.  

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) mkoa wa Iringa, Emmanuel Mwikwabe akiwasilisha taarifa ya utendaji wa mfuko  huo mkoa  wa Iringa alisema kuwa kuna haja ya kuunda tume maalum ya kuchunguza dawa katika Hospital na vituo  vya afya kwani ukifanya  uchunguzi utabaini  kuwepo kwa matumizi  yasiyo mazuri ya  dawa  hizo.

Alisema kuwa changamoto za mfuko  huo na ule  wa CHF au  TIKA katika mkoa  wa Iringa ni  pamoja na  Halmashauri  kushindwa kuwasilisha maombi ya Tsh milioni 96.6 kwa  ajili ya malipo ya tele kwa tele  na  hivyo kukwamisha  wanachama wake  kunufaika na mifuko  hiyo.

Pia  suala la usimamizi mbaya  wa fedha  za  uchangiaji wa  huduma  za matibabu  (NHIF na CHF ) badala ya fedha zitokanazo na NHIF na CHF   kutumika kuboresha huduma za matibabu zinazotumika katika shughuli  ambazo ziko nje ya  miongozo  ya matumizi ya fedha  za uchangiaji.
 Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) mkoa wa Iringa, Emmanuel Mwikwabe akitoa  taarifa  za mfuko  huo leo katika kikao cha RCC
.....................................................................................
 Hata  hivyo  mkuu  wa mkoa  wa Iringa Dr Christine Ishengoma alitoa muda wa miezi  mitatu kwa Halmashauri ambazo hazijapeleka  fedha  hizo kuhakikisha zinafanya  hizo ndani ya miezi mitatu ijayo.
HOT NEWSssssss RC IRINGA ATAKA MAKAHABA NA MASHOGA WAKUSANYWE HARAKA

RC Iringa Dr Christine Ishengoma
Hawa ni  wanaume  waliofunga  ndoa

 Hawa ni wanawake  wanaofanya biashara ya kuuza miili (ukahaba)
 ...........................................................................................
SERIKALI ya  mkoa  wa  Iringa  imeagiza  kuwepo kwa mkakati  wa kuwasaka  watu  wanaume  wanaojihusisha na biashara ya  ushoga  na wale  wanawake  wanaofanya  shughuli za kuuza miili  yao maarufu kama ukahaba.

Agizo hilo  limetolea   usiku  huu katika kikao cha kamati ya ushauri ya  mkoa  wa Iringa  kinachoendelea  hadi sasa majira  haya ya saa 1.59 usiku  huu katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo.

Hatua  ya mkuu  huyo wa mkoa  kutoa agizo  hilo  imekuja baada ya mstahiki meya  wa Halmashauri ya Manispaa ya  Iringa Amani Mwamwindi kuwaeleza wajumbe wa kikao  hicho kuwa  mbali ya kusikia kutoka majiji kama Dar es salaam na mengine hapa nchini kuwepo kwa biashara  za ukahaba na ushoga ila uchunguzi  unaonyesha mji wa Iringa ni miongoni mwa miji ambayo biashara  hiyo ya ushoga na ukahaba  inaendelea  kukua kwa  kasi na hivyo  kutaka kuwepo kwa  mkakati  wa kupambana na biashara  hiyo haramu.

" Ndugu  wajumbe Manispaa ya  Iringa ina watu  wanaofanya  biashara ya ushoga na ukahaba na  mimi kama meya  nina ushahidi  wa kutosha ambapo idara  inayohusika na viti  dhidi ya UKIMWI Halmashauri ya Manispaa ya  Iringa wanaujua mtandao mzima  wa biashara  hiyo  haramu"

Kutokana na ushahidi  huo usio na shaka kutoka kwa meya  Mwamwindi mkuu  wa mkoa  alilazimika  kusimama na kuutaka mkoa  kuweka mkakati wa  kuwakusanya watu hao  wote  ili kuweza kuwasaidia kwa kuwapa miradi  rafiki  badala ya kuendelea na biashara  hiyo haramu  .

" Tusiwaache  wapotee hawa ni watanzania  wenzetu na yawezekana  kuwakusanya na kuwapa  elimu  ili kuachana na shughuli  hizo pia  kuwapa miradi ya  kufanya kwa ajili ya kuwaingizia kipato na sio  kwa shughuli  hiyo"

Mkuu  huyo wa mkoa alisema  wakati  umefika kwa mkoa  wa Iringa  kuweka mkakati kabambe wa  kupambana na madawa ya kulevya , ukahaba na ushoga katika mkoa  huo.

NI LINI MWANAMKE NA MTOTO WA PEMBEZONI ATATENGEWA BEJETI YA KUMKOMBOA?

Wanawake  wakazi  wa  kijiji  cha Masege katika wilaya ya Kilolo mkoa  wa Iringa  wakitoka  shamba huku  wakiwa  wamebeba  kuni ,majembe na watoto mgongoni kama  walivyokutwa na kamera  ya matukiodaima hivi karibuni  hivi sasa tujiulize ni lini bajeti zetu zitawatazama  wanawake na watoto hawa  wa pembezoni mwa nchi  yetu ama tutaendelea  kuwa na bajeti rafiki na wananchi wa mijini

SIMBA YAIKARIBISHA OLJORO JKT DAR


Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania inaingia raundi ya 16 wikiendi hii kwa mechi nne ambapo kesho (Februari 1 mwaka huu) Simba itakuwa mwenyeji wa Oljoro JKT katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Viingilio katika mechi hiyo itakayochezwa kuanzia saa 10 kamili jioni ni sh. 5,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 kwa VIP A. Refa atakuwa Nathan Lazaro kutoka mkoani Kilimanjaro wakati Kamishna ni Hakim Byemba wa Dodoma.

Uwanja wa Azam uliopo Mbagala siku hiyo kutakuwa na mechi kati ya wenyeji Ashanti United na Mgambo Shooting kutoka Handeni mkoani Tanga kwa viingilio vya sh. 3,000 kwa sh. 10,000.

Jumapili (Februari 2 mwaka huu) ni Yanga vs Mbeya City (Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, saa 10 kamili jioni), na Azam vs Kagera Sugar (Uwanja wa Azam Complex, Chamazi saa 10 kamili jioni).

Ligi hiyo itaendelea Jumatano (Februari 5 mwaka huu) kwa mechi kati ya Tanzania Prisons vs Coastal Union (Uwanja wa Sokoine, Mbeya), Mgambo Shooting vs Ruvu Shooting (Uwanja wa Mkwakwani, Tanga), Rhino Rangers vs Oljoro JKT (Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora), na JKT Ruvu vs Ashanti United (Uwanja wa Azam Complex, Chamazi).

SERENGETI BOYS YAPANGIWA AFRIKA KUSINI
Timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) itacheza na Afrika Kusini katika mechi za mchujo kutafuta tiketi ya kucheza Fainali za Afrika kwa umri huo zitakazofanyika mwakani nchini Niger.

Serengeti Boys ambayo pamoja na nchi nyingine 17 zimeingia moja kwa moja katika raundi ya pili itaanzia mechi hiyo nyumbani kati ya Julai 18-20 mwaka huu wakati ile ya marudiano itafanyika nchini Afrika Kusini kati ya Agosti 1-3 mwaka huu.
Ikifanikiwa kuitoa Afrika Kusini, Serengeti Boys itacheza mechi ya raundi ya tatu na ya mwisho na mshindi wa mechi kati ya Misri/Sudan vs Congo Brazzaville.

Nchi nyingine ambazo zimeingia moja kwa moja raundi ya pili ni Afrika Kusini, Angola, Benin, Botswana, Burkina Faso, Congo Brazzaville, Ethiopia, Gabon, Ghana, Ivory Coast, Mali, Morocco, Nigeria, Rwanda, Senegal, Tunisia na Zambia.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) inatarajia kutangaza benchi la ufundi litakaloiongoza Serengeti Boys hivi karibuni.

TFF MPYA YATIMIZA SIKU 100
Kamati mpya ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) chini ya Rais Jamal Malinzi, Februari 4 mwaka huu inatimiza siku 100 tangu iingie madarakani katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 28 mwaka jana.

Hivyo, Rais Malinzi atazungumza na waandishi wa habari Februari 7 mwaka huu kuelezea utekelezaji wa Ilani yake ya uchaguzi. Muda na mahali utakapofanyika mkutano huo mtaarifiwa baadaye.

BODI YA LIGI YAZIPIGA JEKI KLABU ZA FDL
Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imetoa sh. milioni 1.5 kwa kila klabu ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL).

Uamuzi wa kuzisaidia timu hizo ulifanywa katika kikao cha TPLB kilichofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam ambapo fedha hizo zitalipwa kupitia kwenye akaunti za klabu husika. Hivyo klabu ambazo hazijawasilisha akaunti zao TPLB zinatakiwa kuwasilisha haraka.

Klabu za FDL ni African Lyon, Burkina Moro, Friends Rangers, Green Warriors, Kanembwa JKT, Kimondo, Kurugenzi Mafinga, Lipuli, Majimaji, Mkamba Rangers, Mlale JKT na Mwadui.

Nyingine ni Ndanda, Pamba, Polisi Dar es Salaam, Polisi Dodoma, Polisi Mara, Polisi Morogoro, Polisi Tabora, Stand United, Tessema, Toto Africans, Trans Camp na Villa Squad.

Boniface Wambura Mgoyo
Ofisa Habari na Mawasiliano
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

MSOMI WA CHUO KIKUU CHA IRINGA AJA NA MKAKATI WA KUUTANGAZA MKOA KIUTALII ZAIDI

Mhadhili  wa  chuo  kikuu cha Iringa Jimson Sanga  akiwasilisha mada  juu ya mkakati  wa  kuutangaza  utalii wa mkoa  wa  Iringa kwa  kupitia makumbusho ya  Chif Mkwawa ,jiwe  Gangilonga mnala  wa  vita  kuu ya dunia ,makaburi ya jumuiya  ya madolla na vivutio  vingine  vingi ambavyo  vipo ila havipewi  uzito  katika kutangaza .

Iwapo wahitaji  kujua historia ya  Mtanzania  kupitia wakazi wa  mkoa  wa Iringa kabila  la  wahehe  ambalo wajerumani  wamekuwa  wakifika Tanzania  kujifunza hasa  mkoa wa Iringa utaendelea  kupata  hapa

WAZIRI MKUCHIKA AGOMA KUMUONGELEA LOWASSA NA MBIO ZA URAIS 2015

Mwenyekiti  wa  CCM Taifa Rais Dr  Jakaya  Kikwete kushoto akimnadi Lowassa jimboni kwake katika uchaguzi mkuu wa mwaka  2010
 Waziri Mkuchika (kushoto) akihojiwa na mzee  wa matukiodaima leo mjini Iringa 
..................................................................................................................................................
HUKU  baadhi  ya  makundi  yakiendelea  kuibuka na kutoa kauli mbali mbali  dhidi ya waziri mkuu aliyejiuzulu Edward Lowassa kuwa ameanza kampeni za Urais mapema , waziri  wa Nchi, Ofisi ya Rais, (Utawala Bora) Ndugu George Mkuchika amesema  kuwa hajafanya  utafiti wowote juu ya Lowassa  hivyo hawezi  kuzungumzia chochote  kama ni rushwa ama lah.

Waziri mkuchika  alitoa kauli  hiyo mjini Iringa leo  wakati  akihojiwa wa wanahabari mara  baada ya  kumaliza kutoka hotuba yake ya maadili na Rushwa kwa watumishi  wa umma katika kikao cha kamati ya ushauri  (RCC) cha  mkoa wa Iringa  katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo .

Kwani  alisema Taasisi ya  kuzuiana na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) nchini  imekuwa  ikiwakamata   watu na kuwafikisha mahakakani  bila  kuogopa kiongozi ama mtu wa chini na kuwa  utendaji wa taasisi hiyo  umekuwa ukiziongatia haki kwa kila mhusika.

Mkuchika  mbali ya  kugoma  kulizungumzia suala la Lowassa bado alisema  kuwa suala la Rushwa ni suala ambalo halikubaliki na kuziagiza Halmashauri  ya   wilaya  nchini  kuchunguza mienendo  ya  watumishi ambao waongoza  kwa kumiliki  mali mara  baada ya  kuingia serikalini  ili  kujua utajiri  huo wa haraka wanaotoa  wapi.

Hata  hivyo   akihojiwa  juu ya  sakata  ya aliyekuwa mshindi wa kura  za maoni ndani ya  CCM katika mchakato wa ndani ya chama hicho mwaka 2010 Frederick Mwakalebela suala lake kuchukua muda mwingi zaidi na kurudishwa mahakamani mara kwa mara  alisema ili kuwa si kwa lengo la kumuonea ila ilikuwa ni kutafuta sheria inasemaje katika  hilo na mahakani ndicho  chombo  pekee  cha kutafsiri sheria  hivyo maamuzi ya mahakamani siku  zote ni sahihi katika kutafuta  haki.


Awali Waziri Mkuchika  akihutubia katika ufunguzi wa kikao  hicho cha RCC alisema  kuwa  mikakati ya  ofisi yake  katika  kupambana na  watumishi  wasio na maadili ambao  wanashindwa  kufanya kazi  ya umma na  kutumia ofisi  za umma kujinufaisha  wenyewe.

Alisema kuwa  iwapo  watumkishi  wa umma hawatakuwa na maadili katika  uwajibikaji  wao  wa kila  siku ni  wazi suala la rushwa katika idara  wanazoongoza  zitaendelea   kuongezeka  hivyo  kuifanya  jamii  kuendelea  kuchukia serikali  yao.

Hata  hivyo  alisema ni  vema Halmashauri  kuhakikia  kamati za maadili ya  watumishi  zinafanya kazi vema  ili  kuwabaini  watumishi  wasio na maadili  katika Halmashauri  zao.

Pia  alisema serikali  kila mwaka  imekuwa ikipelekea fedha  zaidi ya asilimia 70 kwa Halmashauri kwa ajili ya manunuzi  ila matokeo  yake  badala ya  fedha  hizo  kutumika katika manunuzi wajanja  wamekuwa  wakizitumia kujinunulia mali  zao jambo ambalo alidai  halitavumilika katika wataki  huu.

" Haiingii akilini  kuna  mtumishi ameingia katika ajira  akiwa hana hata  gari  wala nyumba ila baada ya miezi  miwili ya  utumishi  wa umma unakuta  ana nyumba za kisasa, magari  na mali  nyingi ambazo mazingira ya upatikanaji  wake yanatia  shaka .....lazima  kuwa makini  sana na maofisa ardhi na  wakuu wengine  wa  idara "

Aidha  alisema katika  kukomesha  vitendo vya  rushwa katika Halmashauri ya idara  mbali  mbali za serikali  amewaagiza makamanda wa taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU ) kuhakikisha  wanatoa  elimu kwa  mabaraza ya madiwani wa Halmashauri  zote nchini  ili  kuhakikisha vitendo vya rushwa  katika Halmashauri  vinakomeshwa.

Waziri Mkuchika  alisema  kuwa   hadi sasa kwa nchi zinazoongoza  kwa utawala bora katika  jumuiya ya  Afrika Mashariki   takwimu  zinaonyesha kuwa  kati ya nchi  tano  Tanzania ni nchi ya pili  kwa utawala  bora   .

Pia  alisema  chanzo  cha  mmomonyoko  wa maadili kwa mtumishi  wa umma  ni pamoja na tamaa ya mali  kwa  watumishi hao hali  inayosababishwa na kutoridhika na  kipato  halisi  wanachokipata pamoja na ubinafsi  wa kujitazama  wao badala ya  Taifa .

"Takwimu  kuhusiana na vita  dhidi ya  Rushwa  na  uwajibikaji kwa viongozi  unakabiliwa na changamoto  nyingi..... takwimu kuhusiana na vitendo  vya Rushwa  katika kipindi  cha kuanzia mwezi Julai 2012 hadi  Juni 2013 zinaonyesha  kuwa na jumla ya taarifa 81 zilipokelewa kati  ya hizo  65 zilifanyiwa kazi  uchunguzi  na kufunguliwa majalada .....aidha katika kipindi  hicho jumla ya kesi mpya 12 zilifunguliwa katika mahakama mbali mbali za mkoa wa Iringa na kesi 5 kati ya  hizo zilitolewa  hukumu na  wahusika kupewa adhabu mbali mbali" alisema waziri Mkuchika

Kuwa Halmashauri  ya  wilaya  pamoja na idara ya afya ndizo zinaongoza kwa kuwa na taarifa nyingi kwa upande wa idara za serikali  ambapo  kila moja ilipatikana na taarifa  16 huku idara ya mahakama  inafuatia kwa taarifa  6 wakati  polisi na idara ya  elimu zikiwa na taarifa 5 kila moja  idara ya maliasili taarifa  tatu  na idara ya mwisho kwa kuwa na taarifa  ndogo za rushwa ni idara ya ardhi  na  TANROADS ambayo ilikuwa na taarifa  moja ,Tanesco taarifa  moja,SIDO mbili,ofisi   ya mkuu wa wilaya  tatu ,na sekta  binafsi taarifa  tatu.

Mkuchika alisema kuanzia  sasa  maofisa wa Takukuru wilaya ya mkoa hakuna kushinda  ofisini na badala yake kwenda kwa  wananchi  kutoa elimu  ya Rushwa na  kuzitaka  taasisi mbali mbali zikiwemo za dini kutosita  kutoa taarifa kwa Takukuru  kuomba  maofisa  wake kufika na kutoa elimu katika mikusanyiko.

Mwenyekiti  wa Halmashauri ya  wilaya ya  Iringa Stephano Mhapa  mbali ya  kumpongeza  waziri Mkuchika kwa utaratibu  wake wa kuzunguka katika mikoa na kuzungumza katika vikao  vya RCC bado alimshauri  kufanya mikutano ya hadhara  kwa wananchi  zaidi ambao  ndio  wanaathiriwa  zaidi na rushwa ndogo  zinazoendelea  kutolewa na kuvuruga ubora wa  miradi.

Huku  mkuu  wa wilaya ya  Mufindi  Evarista  Kalalu  alisema  kuwa  mbali ya wilaya  yake ya Mufindi  kuongozana na maofisa wa TAKUKURU katika mikutano  yake wilayani ila bado  inapaswa TAKUKURU  kujipanga kwa  kutenga bajeti  ya  kufikisha  elimu zaidi kwa wananchi.

Kwani  alisema  iwapo  TAKUKURU haitakuwana nguvu zaidi  ya  kuwafikia  wananchi  wa pembezoni  zaidi  bado vita  dhidi ya  Rushwa  itaendelea  kuzungumzwa  pasipo  kueleweka  vema.

Mkuu  huyo wa wilaya  alisema Rushwa inayotesa wananchi ni ile inayotokana na uwajibikaji mbaya  wa  viongozi wa serikali  za vijiji na kata  ambao  ndio  wamekuwa  wakiongoza kwa  rushwa ndogo ndogo ambazo  zinaendelea  kutesa  wananchi .

Mkuu  wa  mkoa  wa Iringa Dr Christine  Ishengoma  aliwataka  watumishi  wote wa umma na  wananchi wa mkoa  wa Iringa  kushirikiana katika mapambano  dhidi ya  Rushwa kama  njia ya kuongeza kasi  ya maendeleo katika mkoa.

Dr Ishengoma alisema  kuwa iwapo  kila mmoja atajikita katika vita  dhidi ya  Rushwa mkoa  wa Iringa  unaweza kuwa mkoa wa mfano kwa maendeleo makubwa bila  Rushwa

Katika hatua  nyingine  mkuu  wa mkoa  wa Iringa Dr Ishengoma  aliagiza Halmashauri zote za mkoa  wa Iringa ndani ya miezi mitatu  kuitisha  semina ya utawala  bora  katika  suala la Rushwa na maadili  kwa madiwani  wake.

"Mheshimiwa  waziri napenda kukuhakikishia  kuwa tunaye  kamanda wa TAKUKURU Mzuri  katika mkoa  wa Iringa japo kamanda nakuomba usije kutia  kiburi kwa waziri  wako  kutokana na sifa  hizi  ambazo  nimepata  kukupa hapa  leo"

Kamanda  wa Takukuru  mkoa  wa Iringa Bi Emma Kuhanga  alisema kuwa  mkoa  wa Iringa  umeendelea  kupambana na vitendo  vya  Rushwa na kuwa suala la  watumishi  wanaofika na kumiliki mali nyingi  habari zao wa kwanza  kuzibaini ni wakurugenzi na maofisa  utumishi ambao ndio  wamekuwa  wakijua mienendo  yao japo alisema bado  wataendelea  kufuatilia watumishi  wanaofanya vitendo  vya ufisadi kwa ajili ya kujilimbikizia mali katika mkoa

MKUTANO WA NAIBUK KATIBU MKUU WA CCM BARA BW NCHEMBA KUMNADI MGOMBEA UDIWANI KATA YA UKUMBI

Katibu wa CCM Iringa mjini nakaimu katibu wa mkoa Hassan Mtenga  kushoto akicheza na naibu katibu mkuu wa CCM bara Mwingulu Nchemba wenye jezi ya  Taifa  wakati kwaya  ikitumbuiza  katika kampeni  za udiwani kata ya Ukumbi wilaya ya  Kilolo
Naibu katibu mkuu  CCM Bara  Mwigulu Nchemba akiwahutubia  wananchi wa Ukumbi katika mkutano wa kampeni za udiwani kata ya Ukumbi wilaya ya  Kilolo mkoani Iringa

MBOLEA YA MINJINGU MAZAO YAWAGONGANISHA WENYEVITI WA HALMASHAURI YA MUFINDI NA IRINGA KIKAONI

 Mfuko  wa  mbolea ya  Minjingu mazao
WAKATI  mkuu wa mkoa wa Iringa  Dr Christine Ishengoma akiunga mkono matumizi ya mbolea ya Minjingu mazao  kwa  kutaka  viongozi   wote kuendelea  kuhamasisha  wananchi kutumia na wale  wasiotaka  kutumia  kurejesha vocha  hizo za mbolea ,umezuka mvutano mkubwa katika kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa kati ya mwenyekiti wa Halmashauri ya Iringa Stivin Mhapa na mwenyekiti wa Halmashauri ya  wilaya ya Mufindi Peter Tweve.

Wenyeviti  hao  wameonyesha  kutofautiana  wakati  wa  kikao  cha kamatin ya ushauri ya mkoa kilichofanyika katika  ukumbi wa Siasa ni  Kilimo ambapo  diwani Mhapa  alionyesha kupinga kwa nguvu  zote matumizi ya mbolea  hiyo na kutaka wananchi  kurejeshewa  pesa  zao asilimia 41  walkiochangia kwa ajili ya pembejeo huku mwenyekiti  mwenzake Tweve  akipinga.

Awali  mkuu  wa mkoa  alisifu matumizi ya  mbolea  hiyo kuwa ni mbolea  nzuri  inayoongeza kasi  ya uzalishaji wa mazao  na hata  kumtaka Mhapa  kusimama  kutoa ushuhuda katika kikao  hicho jinsi ambavyo anavyoweza kuvuna  gunia  30  kwa  hekari  moja jambo ambalo alidai ni mafanikio ya minjingu mazao na hivyo  kumsimamisha  kuelezea  wajumbe  mafanikio hayo .

" Kwanza  utanisamehe  mheshimiwa mwenyekiti wa Halmashauri ya  Iringa sikukusimamisha mapema kuelezea jinsi  unavyopata  magunia  30 kwa hekari moja hebu  sasa  simama  uwaelezee wajumbe ili kuwapa  matumaini  wananchi " alisema mkuu  huo wa mkoa.

Hata  hivyo  mhenyekiti  huyo Mhapa  hakuweza kueleza mafaniko hayo na badala  yake  alianza kwa kusema anasikitika sana kuona  serikali ikilazimisha  kutumia  mbolea  hiyo huku wananchi  wakiendelea  kuikataa .

"Kwa masikitiko makubwa  ndugu  mwenyekiti ninaomba  serikali  kuwarudishia  wananchi fedha  zao  walizochangia asilimia 41 kwani mbolea  hii  ni bomu na  wananchi  wanahisi kuwa  serikali imewafanyia utapeli  wa  fedha zao....mimi naomba  serikali irudishe  fedha za wananchi kwani tabu kubwa  tunaipata  sisi  viongozi wa chini ambapo  wananchi  hawatuelewi na kutuona  sisi  pamoja na chama changu CCM ni matapeli...ninaomba kama  hakuna faida  ya cha juu asilimia  10 ambayo  viongozi wanaopigia  debe  wanapata basi  wananchi  wapewe  fedha  yao"

Mhapa  alitaka wakulima  kujichagulia  mbolea  wanayoitaka na  serikali kuweka  ruzuku katika mbolea  zote  badala ya kulazimisha  kutumia mbolea  hiyo ya Minjingu mazao ambao hakifai  hata  kidogo.
 
Huku  mwenyekiti wa Halmashauri ya  Mufindi Bw  Tweve  akiipongeza  serikali kwa mbolea hiyo  kuwa ni  nzuri na katika Halmashauri  yake ya Mufindi  wanakitumia na imesaidia  sana  kuongeza uzalishaji wa mazao.

" Kweli  naipongeza  serikali kwa mbolea  hii  kwetu Mufindi mbolea  hii  inasaidia  sana kuongeza uzalishaji wa mazao"

Wakati  huo  huo Mhapa  alisema kuwa  hadi  sasa katika Halmashauri  hiyo aliyekuwa mbunge  wa jimbo la Kalenga  Dr Wiliam Mgimwa alijitolea  kujenga mabweni 8  katika  jimbo la Kalenga  ila hadi  sasa ni bweni moja pekee ambalo limejengwa  na  wahusika  kwa sasa wamesimama na mbaya  zaidi  wahusika wa ujenzi huo hawajui  lugha ya kiswahili  wala Kiingereza sasa  imekuwa ni shida  sana kujua kama wataendelea kujenga ama  vipi.

Hata  hivyo  alisema anampongeza  sana  mbunge wa jimbo la Isimani Wiliam Lukuvi ambae ni  waziri wa nchi ofisi ya waziri mkuu  sera na uratibu wa bunge ambae amejaribu  kuwasaidia kwa kukutana na mkalimani  wao na boss  wao ambapo  jitihada bado  zinaendelea chini ya Lukuvi.HII NDIO TAARIFA KAMILI YA MTANGAZAJI KENNETH WA EATV ALIYETOWEA TOKA JUZI NA KUKUTWA LEO AKIWA AMEKUFA


Mwandishi Kenneth Kidago Lyanga afariki dunia

Mtangazaji wa Habari za Michezo wa East Africa Radio Kenneth Kidago Lyanga amefariki dunia nyumbani kwake Mwenge Mlalakua, Jijini Dar es Salaam.

Mipango ya mazishi ya Kenneth Lyanga inafanywa na familia yake.

Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Marehemu Kenneth Kidago Lyanga Mahala Pema Peponi.
Mtangazaji wa Habari za Michezo wa East Africa Radio Kenneth Kidago Lyanga amefariki dunia nyumbani kwake Mwenge Mlalakua, Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza namtandao  huu  wa www.matukiodaima.com mfanyakazi  mwenzake Amos Arois alisema kuwa  Lyanga ambae  pia alikuwa ni mwandaji wa vipindi wa East Africa Radio iliyopo chini ya IPP media toka juzi hakuweza  kupatikana kazini na hivyo kupelekea  wafanyakazi  wenzake kuwa na hofu kubwa .

Kwani  alisema kuwa mbali ya  kutofika kazini  bila taarifa bado  simu  yake ya mkononi ilionekana kuita  bila kupokelewa na kabla ya  kutoweka alipata kufanya kazi  yake  vema ya kuandaa vipindi na kuaga vema kurejea  nyumbani kwake Mwenge .

Hata  hivyo  alisema kuwa kutokana na kuendelea kumtafuta bila mafanikio ndipo  walipolazimika  kufika nyumbani kwake alikokuwa akiishi na baada ya  kugonga mlango wake ambao  ulifungwa kwa ndani hakukuwa na majibu  yoyote kabla ya kupiga  simu na kusikia ikiita ndani ya chumba  chake.

Alisema kutokana na hali  hiyo walilazimika kuvunja Mlango na kukuta mwandishi  huyo akiwa amefariki  dunia zoezi  hilo limefanyika leo asubuhi kwa  kubaini mwili  wa mtangazaji huyo.

Aidha  alisema dalili zinaonyesha mtangazaji  huyo amefariki dunia zaidi  ya siku  moja kabla ya leo ijumaa kuukuta mwili  wake  huo na kuwa kwa kabla ya kukutwa amekufa hajapata  kulalamika wala kutoa taarifa ya ugonjwa .

 Mipango ya mazishi ya Kenneth Lyanga inafanywa na familia yake.

Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Marehemu Kenneth Kidago Lyanga Mahala Pema Peponi.

PINDA AZINDUA RASMI MAPITIO YA MFUMO WA UWEKEZAJI TANZANIA

Waziri Mizengo Pinda
.....................................................................
 Na mwandishi maalum ,Dar
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi zitakazonufaika katika masuala ya uwekezaji nchini endapo itatekeleza kikamilifu Mapitio ya Mfumo wa Uwekezaji yaliyowasilishwa na Taasisi ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (OECD).
 
Ametoa kauli hiyo leo mchana, wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuzindua kitabu cha  Mapitio ya Mfumo wa Uwekezaji kwenye ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.
 
Akizungumza katika uzinduzi huo, Waziri Mkuu Pinda  alisema kuwa malengo ya mapitio ya  mfumo huo ni kuboresha hali ya uwekezaji na biashara nchini ambayo matokeo yake yatasaidia kuongeza wawekezaji katika maeneo mengi.
 
“Kuna maeneo ya uwekezaji yanayopata uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje ya nchi (Foreign Direct Investment -FDI) ambayo ni umeme, mafuta, gesi, madini, viwanda, ujenzi na huduma za jamii.”
 
Amesema kuwa matokeo ya jitihada hizi ni makubwa na yameonekana ndani ya miaka miwili tu. Akitoa mfano, alisema: “Kilimo kimeweza kukua kutoka dola za marekani  milioni 304.5 mwaka 2010 hadi dola za marekani milioni 355.4 katika mwaka 2011. Vilevile kwenye sekta ya Umeme na Gesi imekua kutoka dola za kimarekani  milioni 328.6 hadi dola za kimarekani  539.8 mwaka 2011.”
 
Kutokana na matokeo hayo, Waziri Mkuu ameeleza kuwa Tanzania ina fursa nyingi zikiwemo rasilimali, nafasi yake kijiografia na historia ya siasa safi ambazo zinaifanya iwe kivutio kikubwa cha uwekezaji. Hali hiyo Waziri Mkuu alisema, imesaidia Pato la Taifa kuendelea kukua kwa asilimia sita kwa miaka 10 mfululizo na mwaka jana ilikua kwa asilimia saba na sasa inatarajiwa kufika asilimia 7.2 kwa mwaka huu.
 
Miongoni mwa maeneo yanayohusishwa na mfumo huu wa mapitio ya Uwekezaji ni yale yaliyoainishwa katika Matokeo makubwa sasa ambayo ni Kilimo, Maji, Uchukuzi, Elimu na Nishati.
 
“Ili kufanikisha maeneo hayo ni muhimu tukajenga mazingira bora ya uwekezaji, hivyo Serikali inawataka wadau wote kwa kushirikiana na Sekta binafsi kuchambua kwa makini mapendekezo ya mapitio ya mfumo huo ambayo yanatumika pia kuharakisha mafanikio ya Matokeo makubwa sasa”, alisisitiza Waziri Mkuu.
 
Waziri Mkuu alisema Serikali ya Tanzania inashukuru sana Taasisi ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (OECD) kwa kuweka sura maalum kwenye kitabu hicho  inayozungumzia changamoto za uwekezaji kwenye sekta ya kilimo na jinsi ya kukabiliana na changamoto hizo.
 
“Ninatumaini kuwa utekelezaji wa mapendekezo haya utaongeza ufanisi wa mchakato huu na kuhakikisha kuwa tunazitumia fursa zilizopo na nyingine zaidi katika kuboresha uwekezaji katika kilimo nchini. Na kwenye kilimo ninamaanisha kilimo mazao, mifugo, uvuvi na nyuki,” aliongeza.
 
Mapema, Naibu Katibu Mkuu wa Taasisi ya OECD, Bw.  Rintaro Tamaki, alisema mazingira ya uwekezaji nchini yanabadilika kila mara kutokana na kuvumbuliwa kwa rasilimali mpya kama vile gesi, makaa ya mawe ambazo zinasababisha watu wavutive kuwekeza nchini.
 
Kutokana na kugunduliwa na sekta hizo, Serikali isizipuuzie sekta za zamani hususan Sekta ya kilimo, cha msingi ni kuboresha sekta hii kwa kuanzisha viwanda ili kuongeza thamani ya mazao yenu”.
 
(mwisho)

RC IRINGA AAGIZA WANAFUNZI WALIOSHINDWA KURIPOTI SEKONDARI NA WAZAZI WAO WAKAMATWE

Mkuu wa mkoa  wa Iringa Dr Christine Ishengoma katikati akitoa maagizo ya  kukamatwa kwa  wazazi na wanafunzi  walioshindwa  kupeleka  watoto  wao  Sekondari.

MKUU  wa  mkoa  wa  Iringa Dr Christine Ishengoma  ameagiza  viongozi  wa vijiji ,kata  ,tarafa na wilaya  kuwachukulia  hatua  kali  wazazi  na  wanafunzi  walioshindwa  kujiunga na kidato cha kwanza  pamoja na kuchaguliwa .

Mkuu  huyo  wa mkoa  alitoa agizo hilo leo  wakati  akifungua  kikao cha kamati ya  ushauri ya mkoa  wa Iringa kilichofanyika katika ukumbi  wa Siasa  ni  Kilimo mjini  Iringa na kuhudhuriwa  na  waziri wa  nchi  ofisi ya  Rais ( Utawala  bora )George  Mkuchika.

Alisema kuwa  wazazi  wa  wanafunzi  waliofaulu kujiunga na elimu ya  sekondari mwaka  huu ni  vema  kuhakikisha  wanawapeleka  watoto wao  shule  vinginevyo utaendeshwa msako  mkali wa  kuwabaini  wanafunzi  ambao  wameshindwa  kuanza elimu ya  sekondari  ili  kuwachukulia hatua kwa kuwafikisha mahakamani.

Kwani  alisema kuwa  mkoa  hautapenda  kuona  wanafunzi hao  waliofaulu  kujiunga na elimu ya  sekondari  wakiendelea  kubaki  nyumbani huku  wenzao  wakiendelea na masomo ya  sekondari.

Hivyo  alisema kwa  kuwa ni wajibu wa kila mzazi  kumpatia  elimu  mtoto  wake  serikali  haitasita  kuchukua hatua kwa  mzazi atakayeshindwa  kusomesha mtoto  elimu  ya msingi na sekondari  .

Dr Ishengoma  aliwataka  wazazi  wote  wenye  watoto  wanaotakiwa  kujiunga na elimu ya msingi na wale  waliochaguliwa  kwenda  sekondari  kuhakikisha  wanatimiza  wajibu  wao kabla ya  serikali  kuchukua hatua ya  kuwafikisha  mahakamani kwa kushindwa  kusomesha   watoto . 

Hata  hivyo mkuu  huyo wa mkoa  alipongeza  jitihada  mbali mbali  zinazofanywa na Halmashauri  ya Manispaa ya  Iringa katika kuendelea  kuboresha  elimu kwa kuifanikishia  Halmashauri  hiyo kushika nafasi ya tano kitaifa .

Dr Ishengoma  alitaka  kuandaliwa kwa  zawadi  kwa ajili ya Halmashauri  hiyo pamoja na  zawadi  nyingine kwa Halmashauri ya Kilolo kwa  kushika nafasi ya mwisho  kimkoa .
 
katika  hatu  nyingine  mkuu  huyo wa  mkoa aliwataka  wananchi  wa Halmashauri ya Manispaa ya  Iringa  ambao wanamiliki magari  kuhakikisha  wanalipa  ushuru wa maegesho katika mji  huo na iwapo watashindwa  kulipa ushuru  huo ni vema  wakaacha magari yao nyumbani na kuja mjini kwa usafiri wa daladala ama kwa miguu.

Mkuu  huyo alisema  kuwa kumekuwepo na usumbufu mkubwa kwa  watu  waoakusanya ushuru  kusumbuliwa na baadhi ya  wamiliki wa magari  ambao  wamekuwa  wakikwepa  kulipa ushuru  huo .

Kwani  alisema kitendo cha  kushindwa kulipa ushuru  wa maegesho  ni sawa na kuhujumu uchumi wa Taifa  na hivyo suala  hilo halitavumilika hata  kidogo.

Wakati  mstahiki  meya  wa Halmashauri ya Manispaa ya  Iringa Aman Mwamwindi  mbali ya kuwashukuru  wajumbe wa kikao   hicho kwa kuipongeza Manispaa ya  Iringa kwa kufanya  vema bado alisema kuna  changamoto kubwa  ya madeni ya  walimu kiasi cha Tsh  bilioni 1.3  fedha ambazo  walimu hao  wanapaswa  kulipwa.

Huku  kuhusu  suala la ushuru  Mwamwindi alisema kuwa kuna tetesi   kuwa serikali inampango wa kufuta  ushuru  wa mazao  jambo ambalo ni hatari  zaidi katika uhai wa Halmashauri  za  wilaya katika kujiendesha .


 

WATANZANIA WAOBWA KUWASAIDIA WAATHIRIKA WA MAFURIKO MOROGORO. Wahanaga  wa mafuriko  mkoani Morogoro  wakijiokoa katika mafuriko
.............................................................................................................
Mwandishi Kenneth  John wa www.matukiodaima.com ,Dar


Wito  umetolewa  kwa  watanzania  kusaidia  waathirika  waliokubwa  na  janga  la  mafuriko  huko  Dakawa,Dumila  na  Kilosa  mkoani  Morogoro.

Wito  huo  umetolewa  na  chama  cha  msalaba  mwekundu  Tanzania  kupitia  Rais  wake  Dr,  George  Nangale  ambapo   alisema  kuwa  serikali  pamoja  na  wadau  mbalimbali  wameendelea  kutoa  misaada  ya  dharura,lakini  mahitaji  hadi  sasa  bado  ni  makubwa.

Nangale  aliendelea  kusema  kuwa  takwimu  zilizopo  zinaonyesha  zaidi  ya  watu  12,000  ambao  ni  sawa  na  kaya  3,000  ziliathirika  vibaya  na  mafuriko   hayo.

Nangale  alisema  kuwa  baada  ya  kutokea  kwa  mafuriko  hayo  chama   cha  msalaba  mwekundu  Tanzania, kilichukua  hatua  za  haraka  za  kutoa  msaada  wa  mahitaji  mbalimbali  ikiwemo  mablanketi (300),Vyandarua  (300),ndoo  za  maji  (300)  pamoja  na  dawa  za  kusafisha  maji  ya  matumizi  ya  nyumbani  katoni  5, Ambapo  mahitaji  yote  hayo  alisema  yana  thamani  ya  takribani  shilingi  milioni  kumi  na  mbili.

Pamoja  na  hayo  Nangale  alibainisha  mahitaji  muhimu  ambayo  bado  hayajapatiwa  ufumbuzi  wa  kutosha  hadi  hivi  sasa  ambapo  ni  pamoja  na  makazi  ya  dharura,magodoro,  vyombo  vya  kupikia,nguo,mablanketi,vyandarua,madawa  ya  binadamu,chakula,sabuni  za  kufulia,mashuka  pamoja  na  vyoo.

Na  hivyo  chama  kinatoa  rai  na  kuwaomba  wananchi  wote  walioguswa  na  maafa  hayo  kuchangia  kwa  hali  na  mali  kwa  kutoa  misaada  mbalimbali  kwa  kuiwasilisha  makao  makuu  ya  chama  cha  msalaba  mwekundu  Tanzania  yaliyopo  Mikocheni, plot  namba  53 block  C  karibia  na  kituo  cha  Clouds  Fm.

Vile  vile  Nangale  alisema  kuwa  kwa  wale  watakaopenda  kuchangia  kwa  fedha  taslim  wanashauriwa  kutuma  michango  yao  kupitia  namba  za  simu  0715-796073  hiyo  ni  kwa  wale  wa  Tigo  pesa    na  M-pesa  ni  0756-014426,na  Airtel money ni  0689-589337  au  kuwasilisha  moja  kwa  moja  katika  idara  ya  fedha/uhasibu  ya  chama  cha  msalaba  mwekundu  Tanzania  makao  makuu.

Sambamba  na  hayo  Nangale  amewahakikishia  wananchi  wote  kufikisha  misaada  yote  itakayotolewa  kwa  walengwa  kwa  ukamilifu  na  haraka  iwezekanavyo

Itakumbukwa  kwamba  mafuriko  haya  yalitokea  asubuhi  ya  januari  22,2014  na  kusababisha  madhara  mengi  ikiwemo  familia  kupoteza  kabisa  makazi  yao, ambapo  zaidi  ya  nyumba  1,200  zilibomoka  kabisa , mali  na  vifaa  mbalimbali  vya  majumbani  vilisobwa  na  maji  na  vingine  kuharibiwa  ikiwemo  akiba  ya  chakula, miundombinu  ya  barabara  kuharibika ,  kupotea  kwa  mifugo,  pamoja  na  vyoo  kufurika  au  kubomoka  kabisa  na  vifo.