Matukio Daima

Tembelea kila siku kwa habari na matukio mbali mbali..

Matukio Daima

Kwa Habari za Kitaifa.

Matukio Daima

Kwa Habari za Kimataifa.

Matukio Daima

Kwa Habari za Uchumi na Biashara.

Matukio Daima

Kwa Habari za Michezo na Burudani.

July 31, 2012

WALIMU MKOANI RUVUMA WATAKIWA KUREJEA KAZINI

Walimu wakuu wa shule za ,msingi,sekondari na waratibu elimu kata wakiwa katika kikao kilichoitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu aliyesihi kuwahamasisha walimu wote kuacha mgomo na kurejea kazini mara moja.Kikao hiki kimefanyika katika ukumbi wa chuo kikuu huria Manispaa ya Songea(Picha na Revocatus Kassimba
)

Walimu katika mkoa wa Ruvuma wametakiwa kurejea kazini na kuachana na mgomo ambao unawaumiza wanafunzi kwa kuwanyima haki yao ya kupata elimu.

Mwandishi Revocatus Kassimba ambaye ni ofisa habari mkoa wa Ruvuma anaripoti katika mtandao huu kuwa Rai hiyo imetolewa leo na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu wakati alipofanya kikao cha pamoja na walimu wakuu wa sekondari,shule za msingi na waratibu elimu kata wa wilaya ya Songea mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Chuo kikuu huria Manispaa ya Songea.

Mkutano huu aliuitisha ili kurejea kauli ya serikali kuwa mgomo unaoendelea mkoani Ruvuma na nchi kwa ujumla si halali kwani suala hilo lipo katika Mahakama Kuu divisheni ya kazi.

“Nawasihi sana walimu wote rejeeni madarasani wakati huu suala hili likiendelea kushughulikiwa na mamlaka husika” alisema mkuu wa mkoa.

Mkuu wa Mkoa amewapongeza walimu wote ambao toka mgomo huu ulipoitishwa hawajasitisha kutoa Huduma ya kuwafundisha wanafunzi kwani kwa kufanya hivyo wameonyesha uzalendo na heshima kwa serikali ambayo ndiyo mwajili.

Mwambungu alikemea vikali tabia ya baadhi ya viongozi wa chama cha walimu mkoani Ruvuma kupita katika shule na kuhamasisha walimu kugoma na kueleza kitendo hicho ni utovu wa nidhamu kwani shule zote ni mali ya serikali wala si za chama cha walimu (CWT).

“CWT si mwajili wa walimu bali ni chama cha kitaaluma hivyo kinapaswa kuheshimu maagizo ya mahakama na kusitisha mgomo kwa kuwatakia walimu wote warejee madarasani”

Mwambungu amekemea tabia ya baadhi ya viongozi wa CWT kuwahamasisha walimu kugoma kwa kupita mashuleni ambapo ameeleza kuwa serikali inawafuatilia na watakaobainika hatua za kisheria zitachukuliwa kwa makosa ya uchochezi.

Aliongeza kusema kuwa uamuzi wa kugoma ni kuwadhurumu watanzania wengi wakiwemo watoto wa shule wasio na makosa hivyo akawasihi walimu wakuu wa shule za msingi , sekondari na vyuo kuwahamasisha walimu wao kurejea kazini kazi ambayo walimu wakuu wamekubali kuifanya ili kurejesha hali ya ufundishaji katika utaratibu wake.

TAARIFA MBALI MBALI KUTOKA TFF LEO


MECHI YA NGORONGORO HEROES YAINGIZA MIL 12/-

Mechi ya kwanza ya raundi ya pili kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 20 kati ya Tanzania (Ngorongoro Heroes) na Nigeria (Flying Eagles) iliyochezwa juzi (Julai 29 mwaka huu) imeingiza sh. 12,901,000.

Fedha hizo zimepatikana kutokana na watazamaji 3,377 waliokata tiketi kushuhudia pambano hilo lililochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Sehemu iliyoingiza watazamaji wengi ilikuwa viti vya bluu na kijani ambapo 2,697 walikata tiketi kwa kiingilio cha sh. 3,000 kila mmoja. Viingilio vingine katika mechi hiyo vilikuwa sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, sh. 10,000 kwa VIP C na B, na sh. 15,000 kwa VIP A iliyoingiza watazamaji 21.

Mgawanyo wa mapato hayo ni kama ifuatavyo; asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ilikuwa sh. 1,967,949.15, gharama ya kuchapa tiketi sh. 2,250,000, gharama za waamuzi na kamishna wa mechi hiyo sh. 760,000 na ulinzi na usafi kwa Uwanja wa Taifa sh. 2,350,000.

Malipo kwa Wachina (Beijing Construction) sh. 2,000,000, asilimia 20 ya gharama za mchezo ni sh. 714,610.17, asilimia 10 ya uwanja sh. 357,305.08, asilimia 5 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) sh. 178,652.54 na asilimia 65 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) sh. 2,322,483.05.

Mechi ya marudiano ya michuano hiyo ambayo fainali zake zitafanyika mwakani nchini Algeria itachezwa Agosti 12 mwaka mjini Ilorin, Jimbo la Kwara, Nigeria.

PONGEZI KWA UONGOZI MPYA SIREFA

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa pongezi kwa uongozi mpya wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Singida (DOREFA) uliochaguliwa katika uchaguzi uliofanyika Julai 28 mwaka huu.

Ushindi waliopata viongozi waliochaguliwa kuongoza chama hicho unaonesha jinsi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa SIREFA walivyo na imani kubwa kwao katika kusimamia mchezo huo mkoani Singida.

TFF inaahidi kuendeleza ushirikiano wake kwa Kamati ya Utendaji ya SIREFA chini ya uenyekiti wa Baltazar Kimario ambaye amechaguliwa kwa mara ya kwanza.

Uongozi huo mpya una changamoto nyingi, kubwa ikiwa ni kuhakikisha unaendesha shughuli za mpira wa miguu mkoani Singida kwa kuzingatia katiba ya SIREFA pamoja na vyombo vya mpira wa miguu vilivyo juu yake.

Pia tunatoa pongezi kwa Kamati ya Uchaguzi ya SIREFA na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kuhakikisha uchaguzi huo unaendeshwa kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi za wanachama wa TFF.

Viongozi waliochaguliwa katika uchaguzi huo uliofanyika Chuo Cha Maendeleo ya Jamii Singida ni Baltazar Kimario (Mwenyekiti), Hussein Mwamba (Katibu Mkuu), Gabriel Gunda (Katibu Msaidizi), Gabriel Mwanga (Mhazini), Hamisi Kitila (Mjumbe wa Mkutano Mkuu TFF), Omari Salum (Mwakilishi wa Klabu TFF), Yagi Kiaratu na Dafi Dafi (wajumbe wa Kamati ya Utendaji).

Nafasi za Makamu Mwenyekiti, Mhazini Msaidizi na wajumbe wawili wa Kamati ya Utendaji zitajazwa katika uchaguzi mdogo utakaofanyika baadaye.

MICHELSEN AITA 22 KAMBI YA COCA-COLA

Kocha wa timu za Taifa za vijana za Tanzania, Jakob Michelsen ameita wachezaji 22 kwa ajili ya michuano ya kimataifa ya Coca-Cola itakayofanyika baadaye mwaka huu nchini Afrika Kusini.

Baadaye watachujwa na kubaki 16 ambao ndiyo watakaokwenda kwenye michuano ya Afrika Kusini. Wachezaji waliochaguliwa wametokana na michuano ya Copa Coca-Cola iliyofanyika jijini Dar es Salaam na mkoani Pwani kuanzia Juni 24- Julai 2 mwaka huu.

Wachezaji walioitwa ni Abdulrahman Mandawanga (Dodoma), Abraham Mohamed (Mjini Magharibi), Ayoub Alfan (Dodoma), Bakari Masoud (Tanga), Daniel Justin (Dodoma), Denis Dionis (Ilala), Edward Songo (Ruvuma), Fikiri Bakari (Tanga), Hassan Kabunda (Temeke), Joseph Chidyalo (Dodoma), Mutalemwa Katunzi (Morogoro) na Mwarami Maundu (Lindi).

Wengine ni Nankoveka Mohamed (Ilala), Nelson Peter (Morogoro), Omari Saleh (Singida), Rajab Rajab (Mwanza), Said Said (Kagera), Shiza Kichuya (Morogoro), Shukuru Msuvi (Temeke), Tanganyika Suleiman (Kigoma), Tumaini Baraka (Kilimanjaro) na William John (Ruvuma).

Pia Michelsen ameongeza wachezaji saba kwenye kikosi cha Serengeti Boys ambacho Septemba mwaka huu kitacheza na Kenya kuwania tiketi ya fainali za vijana wenye umri chini ya miaka 17 za Afrika zitakazofanyika mwakani nchini Morocco.

Wachezaji walioongezwa kwenye kikosi hicho ambao pia wametoka kwenye Copa Coca-Cola ni Abdallah Baker (Mjini Magharibi), Abdallah Kheri (Mjini Magharibi), Calvin Manyika (Rukwa), Dickson Ambunda (Mwanza), Hassan Mganga (Morogoro), Miza Abdallah (Kinondoni) na Mzamiru Said (Morogoro).

Boniface Wambura

Ofisa Habari

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

WANANCHI WAMEHIMIZWA KUTEMBELEA TOVUTI YA SEKRETARIETI YA AJIRA


Isimila Stone Age Park Iringa
Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Bw. Xavier Daudi amewataka wahitimu na wale wote wenye kutafuta fursa za ajira Serikalini kujijengea utamaduni wa kutembelea tovuti ya Sekretarieti ya Ajira mara kwa mara kwani kila nafasi za ajira zinapojitokeza huwekwa katika tovuti hiyo ili kutoa fursa kwa wadau walioko nje na ndani ya nchi kuweza kuziona kwa urahisi.

Mwandishi Riziki Abraham anaripoti kuwa hayo leo, wakati akiongea na mwandishi wa habari ofisini kwake aliyetaka kujua fursa za ajira zilizoko na taratibu za mchakato wa ajira tangu kutolewa kwa tangazo hadi kupangiwa kituo cha kazi.

Daudi amesema, kwa mfano mwananchi yeyote akitembelea katika tovuti ya Sekretarieti ya Ajira hivi sasa ataona tangazo la kuitwa kazini kwa waombaji kazi waliofaulu katika usaili uliofanyika mwezi Juni, 2012 ambao wanatakiwa kuripoti kwa Waajiri; Wakala wa Vipimo, pamoja na kwa Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii.

Mbali na hilo, pia watakuta tangazo la kuitwa kwenye usaili kwa wale waliokidhi vigezo kulingana na nafasi walizokuwa wameomba kama zilivyokuwa zimetangazwa kwa niaba ya Halmashauri ya Wilaya ya Babati, Chuo cha Mipango Dodoma, Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo, Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo na taasisi nyinginezo.

Aliongeza kuwa katika Tovuti hiyo watakuta pia tangazo la nafasi za kazi 194 zikiwemo nafasi za Wakurugenzi, Wakufunzi Waandamizi wa Vyuo, Wakufunzi Wasaidizi, Wahandisi, Mafundi Sanifu, Wakaguzi wa ndani wa hesabu, Makatibu Mahsusi, Walinzi, Wapishi na kada nyinginezo.

Aidha, amesisitiza ni muhimu kwa waombaji kuzingatia masharti ya tangazo pindi wanapotuma maombi yao kwa njia ya posta ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kupata fursa ya ajira serikalini maana mchakato wa ajira hufuata Sera, Sheria, Kanuni na Taratibu

Katibu wa Sekretarieti ya Ajira alimaliza mahojiano yake kwa kuitaja tovuti ya Sekretarieti ya Ajira kuwa ni www.ajira.go.tz kwa wale wasioifahamu ili waweze kuifahamu.

CCM YAMSHUKIA TUNDU LISU

Mbunge Tundu Lisu

>Yadai orodha yake inalenga kupotosha tuhuma za rushwa zinazowakabili baadhi ya wabunge.
> Anataka kuwaokoa wa Chadema katika sakata hilo.
>Yasema tuhuma za rushwa kwa wabunge lisigeuzwe la kisiasa

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimelaani juhudi zinazofanywa na baadhi ya wanasiasa na vyama vya siasa kujaribu kupotosha na kuuficha ukweli juu ya tuhuma za rushwa zinazowakabili baadhi ya wabunge.

Akizungumza na waandishi a habari leo mjini Dar es Salaam, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, ya CCM, Itikadi na Uenezi Nape Nnauye alisema, zipo juhudi za baadhi ya wanasiasa na vyama vya siasa kujaribu kulifanya suala la tuhuma za rushwa kwa baadhi ya wabunge kuwa la kisiasa kwa malengo yao.

"Mfano mzuri wa juhudi hizi ni kitendo cha Tundu Lissu, ambaye ni mbunge wa Chadema na Mnadhimu Mkuu wa Kkambi ya upinzani Bungeni cha kutoa aliyoiita orodha ya wabunge wanaotuhumiwa kufanya biashara na TANESCO na kwamba ndio watuhumiwa wa rushwa inayozungumziwa", Alisema Nape na kuongeza;

"Cha kushangaza orodha yake ilikuwa na wabunge wa CCM peke yake wakati wote tunajua kuwa yapo majina ya baadhi ya wabunge wa vyama vingine hasa Chadema, yanayotajwa katika orodha ya wabunge wanaotuhumiwa kwa rushwa hii".

Nape alisema juhudi hizo za Lissu na wenzake zinalengo la kuuficha ukweli na kujaribu kuwalinda watuhumiwa wa uhalifu wanaotokana na Chadema.

"Tunamtaka Lissu na wengine wanaofanya juhudi hizo kuacha mara moja, na badala yake tuvipe nafasi vyombo vinavyohusika vichunguze na matokeo ya uchunguzi huo yatangazwe hadharani ili tuwajue wabunge waliotusaliti", alisena Nape.

Alisema CCM inalaani vitendo vya rushwa hasa vinapohusishwa na viongozi ambao wanapaswa kuwa mfano wa kuigwa na kwamba rushwa ya namna hiyo inavuruga sana uchumi wa nchi, hivyo wanaohusika nayo haitoshi kuwaita wala rushwa tu bali ni zaidi ya wahujumu uchumi.

"Wakikithibitika ni muhimu hatua kali zichukuliwe kulikomesha kabisa hili na iwe fundisho kwa wengine", alisema Nape.

Nape alisema CCM inawapongeza watendaji wakuu wa Wizara ya Nishati na Madini wakiongozwa na Waziri wao Prof. Sospeter Muhongo, Manaibu wake, Massele na Simbachawene na Katibu Mkuu, Maswi kwa uzalendo, ujasiri na umahiri wao mkubwa waliouonyesha kwa muda mfupi waliokaa kwenye wizara hiyo.

"Tunaamini uzalendo walioonyesha katika kusimamia wizara hii,utaigwa na watumishi wengine wa umma katika kuhakikisha matumizi mazuri ya rasilimali za nchi zinalindwa ili kuhakikisha maisha bora kwa kila Mtanzania yanatimia. Tunaunga mkono jitihada zao", alisema Nape.

Alisema, pia CCM inalipongeza bunge kwa kuendelea kusimamia serikali na rasilimali za nchi katika kuhakikisha nchi inapiga hatua kubwa ya maendeleo.

"Tunawaomba waheshimiwa wabunge wazidi kutanguliza masilahi ya taifa mbele na uzalendo mkubwa katika shughuli zao za kila siku", alimalizia.

MGOMO WA WALIMU IRINGA WAOTA MBAWA ,CWT WAGEUKWA ,WALIMU WAOMBA ULINZI WA POLISI KESHO

Mwanafunzi wa darasa la Herieth Kitunduru akiwakumbusha masomo wanafunzi wa darasa la tano leo baada ya walimu kugoma
Mkuu wa shule ya Mtwivila Christabela Alfani ambaye ametelekezewa shule ya walimu wenzake leo
Wanafunzi wa darasa la saba shule ya Msingi Kihesa wakiendelea kufundishwa leo baada ya walimu wao kugomea mgomo wa walimu
Mkuu wa shule ya msingi Kihesa ZAbihu Hassan akiwa kazini
Mwalimu wa shule ya Msingi Kihesa akiendelea na kazi leo
hivi ndivyo walivyofanya walimu wa Mtwivila Iringa kwa kujiorodhesha bila kuwepo kazini
Wanafunzi wa darasa la sano s
Mkuu wa shule ya Msingi Wilolesi Gabriel Kameka akiendelea na kazi kama kawaida.

WAKATI mgomo wa walimu nchini ukiendelea kupoteza mwelekeo baada ya baadhi ya viongozi wa walimu kuonyesha kusaliti mgomo huo , walimu mkoani Iringa waomba kupewa ulinzi na jeshi la polisi ili kuwewezesha kuendelea na kazi kama kawaida kwa madai kuwa wanatishwa na wenzao.

Hatua ya walimu hao kuomba ulinzi wa polisi imekuja siku moja baada ya mgomo huo wa walimu kuanza na jeshi la polisi kutoa tamko kuhusu mgomo huo huku likiahidi kuwabana wote watakaotoa vitisho kwa walimu ambao hawaungi mkono mgomo huo.

Mkuu wa shule ya msingi Mtwivila katika Manispaa ya Iringa Christabela Alfani alisema kwa upande wake hadi jana alijikuta akitelekezewa shule hiyo na walimu wenzake ambao walifika na kusaini kitabu cha mahudhuria na kuondoka shuleni hapo.

Hivyo alisema kuwa kutokana na mazingira ya shule hiyo kuzungushiwa uzio hali ya usalama wake na walimu ambao wapo tayari kuendelea na kazi ni mdogo kutokana na kuhofu kuvamiwa na walimu hao ambao wanaunga mkono mgomo huo.

Kwani alisema baadhi ya walimu katika shule hiyo wapo tayari kuendelea na kazi ila wanaogopa kuvamiwa na walimu wenzao hao hivyo iwapo jeshi la polisi litawawekea ulinzi katika mazingira ya shule watakuwa tayari kuendelea na kazi.

"Kama jeshi la polisi limetoa tamko juu ya mgomo huo tunashukuru ila tunaomba sasa tamko hilo litekelezwe kwa vitendo kwa kutuwekea ulinzi katika mazingira ya shule ili tuweze kuendelea na kazi kama kawaida"

Hata hivyo mwandishi wa habari hizi aliyetembelea shule hiyo alishuhudia wanafunzi wa darasa la saba wakikumbushana masoni mbali mbali kwa kumteua mwanafunzi mwezao Herieth Kitunguru ili kusimama kama mwalimu wao kwa kuwaelekeza baadhi ya masomo.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya msingi ya Wilolesi George Kameka alisema kabla ya kumgomea mwajiri wao, wanataka kufahamu tangu kutoka kwa chama chao hicho cha wafanyakazi tangu walimu nchini kote waanze kukatwa asilimia mbili kwa ajili ya kukichangia, mapato na matumizi yake yakoje.

Hata hivyo alisema inashangaza kuona CWT wanahimiza mgomo wakati wao wanaongoza kwa kuwanyanyasa wanachama wake kwa kuwalipa kiasi cha shilingi 20,000 pekee pale wanapofiwa kama rambi rambi huku mwanachama wa CWT anapostafu kazi CWT hakuna fedha yeyote inayomlipa mwanachama huyo zaidi ya kujinufaisha wao viongozi .

"Hawa viongozi wa CWT wanataka kutufanya sisi kama watoto wa kudanganywa na pipi hivi serikali ambayo imetufikisha hapa tulipo na ipo katika mkakati wa kufanya mazungumzo na walimu ili kutuongeza kile tunachodai .....leo CWT inatuambia tumgomee mwajiri anayetulipa wakati wao wanaendelea kutukandamiza ....tunasema hatupo tayari kutumiwa na CWT ambao si waajiri wetu ...leo wanatuhamasisha tugome ila viongozi wetu wanakwenda kazini ....tunasema sisi si watoto tumekua sasa"

Huku mwalimu mkuu wa shule ya Msingi Kihesa Zabihu Hassan akidai kuwa ameongea na walimu wake na wote wamekubali kuendelea na kazi kama kawaida na hawapo tayari kuingizwa katika mgomo huo.

Kwani alisema kwa sasa watoto wa darasa la saba wapo katika maandalizi ya mtihani wa Taifa hivyo kugoma ni kuwakwamisha watoto hao.

Alisema kuna taarifa zisizo rasmi kwamba CWT iko katika mstari wa mbele kudai maslai ya walimu ili mishahara yao ikipandishwa na wao wapandishe michango yao.
Hata hivyo alitaka Chama cha Walimu Tanzania (CWT) iwaeleze kwanza mapato na matumizi ya michango yao ya kila mwezi kwa chama hicho ndipo waitishe mgomo .

“Tunasikia kuna majengo ya walimu yanajengwa nchi nzima, makatibu wa cwt wananuliwa magari, sasa kuna mpango wa kuanzisha benki, lakini hatupewi taarifa ya mapato na matumizi, na hata magari waliyopewa makatibu hayana msaada kwa walimu ambao ndio wenye mali hata kama wakiumwa,”alisema mwalimu huyo.

Alisema mgomo huo unawapa umaarufu viongozi wa chama hicho na hauna maana yoyote kwa walimu wa kawaida kwasababu taratibu za kuongeza mishahara ya walimu hazina tofauti na zile za watumishi wengine wa umma hivyo kuigomea serikali ili kuongeza misharaha si jibu kwa utendaji wao wa kazi kwani hata wakiongeza bado CWT imeendelea kuwachangisha michango walimu hao ambayo mwisho wa siku inaliwa na wajanja wachache.

Alisema mgomo huo una madhara makubwa yatakayoonekana kwenye mitihani ikiwemo ile ya kitaifa.

Alisema kuna haja kwa serikali kusikiliza kero za walimu hao na kuzifanyia kazi kwa kuzingatia uwezo wake badala ya kila mara kulalamika kwamba haina uwezo jambo ambalo linaonyesha wazi walimu kutumika kisiasa zaidi .

Huku baadhi ya wazazi na wananchi wa kada mbali mbali mjini Iringa wameonyesha kupinga mgomo huo huku baadhi ya wazazi wakidai kuwa watawawajibisha walimu hao iwapo watagoma kwani pamoja na serikali kufuta ada ila walimu hao wamekuwa wakichangisha michango kwa ajili ya masomo ya ziada kiasi cha shilingi 50,000 kwa kila mwezi hivyo iwapo watagoma wawe tayari kurudisha chenji zao .

Mary Haule ambaye alipata kuwa afisa elimu Manispaa ya Iringa alisema kuwa mgomo huo kwa walimu hauna tija na kuwataka kusubiri ahadi ya serikali.


Kaimu Katibu wa CWT Mkoa wa Iringa, Peter Mvilli alisema katika baadhi ya vituo, zipo taarifa za mgomo huo kutokwenda vyema kama walivyotarajia.

Tayari mkuu wa mkoa wa Iringa Dkt Christine Ishengoma leo amekutana na viongozi wa CWT ili kuwasihi kusitisha mgomo huo .

Jeshi la polisi mkoa wa Iringa kupitia kwa kamanda wake wa polisi Michael Kamhanda limewahakikishia ulinzi walimu hao ambao wapo tayari kufanya kazi na kuahidi kuwachukulia hatua kali wale wote watakaowafanyia vurugu walimu wasiounga mkono mgomo huo ama kuwatumia watoto kufanya vurugu.

Kamanda huyo wa polisi alisema kuanzia kesho ulinzi utawekwa katika maeneo yote ya shule ili kuwabana wale wote watakaofika kwa lengo la kuvuruga amani shuleni.

IRINGA WAANZA MGOMO WA DALADALA

madereva daladala zinazofanya safari yake kati ya Itamba na M.R mjini Iringa wakiwa katika mgomo kwa siku ya leo wakishinikiza kuruhusiwa kugeuza njiani bila kufika mwisho wa safari
Hapa wakiwa wamelizunguka gari ya afande Stevin kuomba kuruhusiwa kuvunja sheria
Hapa wakimthibiti dereva mwenzao ambao hakubaliani na mgomo huo.

Huku mgomo wa walimu ukiwa bado kumalizika hapa nchini ,madereva wa daladala zinazofanya safari zake kati ya stendi ya M.R Miyomboni mjini Iringa hadi eneo la Itamba nje kidogo ya mji wa Iringa wameanza mgomo wao wa siku moja kupinga utaratibu wa sasa wa kutakiwa kufika mwisho wa safari kwa madai unawatesa kutokana na uhaba wa abiria.

Mtandao huu wa www.francisgodwin.blogspot.com umeshuhudia mgomo huo ulioanza majira ya saa 3 asubuhi huku madereva na makondakta wa daladala zilizokatika mgomo huo wakifanya vurugu kwa kutaka kuwapiga wenzao ambao wanaendelea na kazi.

Madereva hao wamesema kuwa hatua ya kufanya mgomo huo ni kutaka kushinikiza Sumatra kuwabadilishia ratiba ya njia na kuwaruhusu kugeuza daladala zao njiani iwapo katika daladala kutakuwa na abiria mmoja ama chini ya watano.

Pia walidai pamoja na daladala zote kutakiwa kufika mwisho wa safari ila wao wamejiwekea utaratibu wa kuwekeana zamu za kufika mwisho wa safari huku daladala nyingine zikirudia njiani kama hazipo katika zamu hiyo tofauti na ilivyo sasa ambapo daladala ikigeuza njia imekuwa ikiwajibishwa kwa dereva kupokonywa leseni

RAIS KIKWETE AFUTURISHA MKOANI LINDI

Waalikwa wakipakua futari
Kadhi wa Mkoa wa Lindi ambaye pia ni Shekhe Mkuu wa Mkoa Mohamed Saidi Mushangani akitoa neno la shukurani baada ya futari
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwashukuru waalikwa kwa kuhudhuria katika hafla ya futari aliyoandaa
Mkuu wa Mkoa a Lindi Mhe Ludovick Mwananzila akishiriki katika futari hiyo pamoja na waalikwa wengine
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiongea na Mkuu wa Magereza wa Mkoa wa Lindi (kushoto) na Mkuu wa Idara ya Uhamiaji ya mkoa waliokuwa miongoni mwa wageni waalikwa
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akisalimiana na wageni waalikwa baada ya kufuturu
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiagana na wageni wake baada ya futari
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akisalimiana na wachungaji waliokuwa miongoni mwa wageni waalikwaKadhi na Shekhe Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mohamed Saidi Mushangani akitoa neno la shukurani

(picha na Ikulu)

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

RAIS KIKWETE AHUDHURIA MAZISHI YA SHEMEJI YAKE

MJINI LINDI LEO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Jakaya Mrisho Kikwete, amewasili mjini Lindi leo, Jumatatu, Julai 30, 2012 kwa ziara ya siku mbili ambako miongoni mwa mambo mengine atafuturisha wananchi na viongozi wa mkoa wa Lindi.

Aidha, rais Kikwete amehudhuria mazishi ya shemeji yake , Marehemu Amani Kinyozi, aliyefariki siku ya Jumamosi jijini Dar es salaam.

Rais Kikwete, ambaye ameongozana na mke wake Mama Salma Kikwete, alijumuika na mamia ya wakazi wa mji wa Lindi kwenye mazishi hayo, yaliyofanyika katika makaburi ya Mitandi, mjini humo.

Marehemu Amani Kinyozi, aliyefariki akiwa na umri wa miaka 45, ameacha mke na watoto wawili.

Enzi za uhai wake marehemu alikuwa mtaalamu wa kutengeneza mifuko ya karatasi, na pia alikuwa akifundisha kinamama wajasiriamali ufundi huo katika juhudi za kuepukana na matumizi ya mifuko ya plastiki, maarufu kama mifuko ya rambo ya kufungia bidhaa.

Imetolewa na:

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,

Ikulu.

Dar es Salaam.

30 Julai, 2012Habari hii kwa hisani ya FAN CITY LODGE NA NAF BLUE VIEW HOTELI

FAN CITY LODGE IPO MANISPAA YA MTWARA /MIKINDANI NI LODGE BORA YENYE HADHI ZAIDI

Furahia usiku wako ndani ya Fan city lodge ipo Manispaa ya Mtwara/Mikindani Maeneo ya Rahaleo jirani na ofisi za TRA mkoa waMtwara
Ni Lodge ya kisasa mtwara /Mikindani ukifika utaipenda zaidi
Mwonekano mzuri wa Lodge hii ni heshima kubwa kwa thamani ya fedha zako
Kila mmoja hufurahia huduma zetu ukifika hapa hutapenda kufikia Lodge nyingine uwapo Mtwara
Huduma za za mazoezi(GYM) pamoja na INTERNET wakati wote uwapo ndani ya chumba chako
Vitanda ni vya kisasa hakuna mfano
Fan city lodge ipo Manispaa ya Mtwara/Mikindani Maeneo ya Rahaleo
jirani na ofisi za TRA mkoa waMtwara

Wanatoa huduma za malazi,chakula na Usafiri wa ndani na nje ya
mkoa ni pacha na Naf Blue view hotel

huduma za za mazoezi(GYM) pamoja na INTERNET wakati wote uwapo lodge

Waweza kuwasiliana kwa namba
0652 295186 na 0788 030504
MTWARA...
WOTE MNAKARIBISHWA KUPATA HUDUMA BORA NA ZA KISASA ZAIDI SAWA NA MALIPO ULIYOTOA

July 30, 2012

NIMETEGUKA MGUU KATIKA MAZOEZI YA MPIRA LEO

mazoezi noma wadau ni siku ya tano leo toka nimeanza mazoezi ya mpira uwanjani kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wa kirafiki jumapili na madiwani Iringa mjini kwa ajili ya uzinduzi wa timu ya waandishi wa habari za michezo Tanzania (TASWA) mkoa wa Iringa kama mwenyekiti wa TASWA na leo nemeteguka mguu wangu wa kulia katika mazoezi hivyo sipo salama sana kiafya hata sijui kesho nitaamka vipi

KAULI YA RC IRINGA JUU YA SENSA YA WATU NA MAKAZI AGOSTI 26 MWAKA HUU

mkuu wa mkoa wa Iringa Dkt Christine Ishengoma akizungumza na wazee leo

MANENO YA MKUU WA MKOA WA IRINGA, MHE. DR. CHRISTINE G. ISHENGOMA (MB.), WAKATI AKIONGEA NA MAKUNDI MBALIMBALI YA KIJAMII OFISINI KWAKE TAREHE 30 AGOSTI, 2012

· Ndugu Viongozi wa watu wenye ulemavu

· Ndugu wawakilishi wa wazee

· Ndugu Viongizi wa Dini

· Ndugu Viongozi wa Siasa

· Ndugu Waandishi wa Habari

Ndugu Wawakilishi wa Makundi Mbalimbali ya Kijamii:

Sensa ya Watu na Makazi itaanza usiku wa Jumamosi tarehe 25/ 8/2012 kuamkia Jumapili tarehe 26/8/2012. Ili kuhakikisha kuwa Watu wote wanahesabiwa na wanahesabiwa mara moja tu, zoezi hili litaendelea kwa siku saba. Watu wote waliolala katika kaya usiku wa kuamkia siku ya Sensa yaani tarehe 25 kuamkia tarehe 26/8/2012 watahesabiwa.

Ndugu Wawakilishi wa Makundi Mbalimbali ya Kijamii:

Sensa ya Watu na Makazi ni zoezi maalum lenye lengo la kupata idadi ya Watu wote waliopo nchini ambapo taarifa zao za kijamii na kiuchumi hukusanywa. Sensa pia hukusanya hali ya Makazi ya Watu hao. Serikali inafanya Sensa ili kupata taarifa zitakazosaidia katika kupanga, kufanya maamuzi, kusimamia na kutathmini sera na mipango ya maendeleo. Taarifa za Sensa pia hutumiwa na Sekta binafsi na jamii kwa ujumla katika shughuli za kila siku.

Hivyo, ni muhimu kwa wananchi kushiriki Sensa kwa sababu kupitia Sensa Serikali itafahamu mahitaji ya wananchi wa kila rika, mahali walipo na watu wenye mahitaji maalum.

Ndugu Wawakilishi wa Makundi Mbalimbali ya Kijamii:

Siku ya Sensa, karani wa Sensa atafika katika kaya akiwa na dodoso la Sensa na kuuliza maswali ambayo yatajibiwa na mkuu wa kaya au mwanakaya mwingine badala yake. Karani huyo wa Sensa atafika katika eneo la kuhesabia watu akiwa na kitambulisho na atakuwa amevalia sare maalum zitakazomtambulisha. Aidha, atakuwa ameongozana na kiongozi wa eneo unaloishi.

Ndugu Wawakilishi wa Makundi Mbalimbali ya Kijamii:

Kwa mujibu wa Sheria ya Takwimu Na. 1 ya Mwaka 2002 taarifa zote zitakazochukuliwa na karani wa Sensa ni siri na zitatumika kwa shughuli za kitakwimu tu. Karani wa Sensa atakula kiapo cha kutunza siri za taarifa zote atakazokusanya wakati wa Sensa.

Ni wajibu wa kila mwananchi kujibu maswali ya Sensa kwa mujibu wa Sheria ya Takwimu Na. 1 ya Mwaka 2002 ili Serikali iweze kupata Takwimu sahihi.

Ndugu Wawakilishi wa Makundi Mbalimbali ya Kijamii:

Endapo una swali lolote kuhusu Sensa tafadhali usisite kufika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa au Mkuu wa Wilaya na utajibiwa swali lako lolote.

SENSA KWA MAENDELEO JIANDAE KUHESABIWA.