Matukio Daima

Tembelea kila siku kwa habari na matukio mbali mbali..

Matukio Daima

Kwa Habari za Kitaifa.

Matukio Daima

Kwa Habari za Kimataifa.

Matukio Daima

Kwa Habari za Uchumi na Biashara.

Matukio Daima

Kwa Habari za Michezo na Burudani.

August 31, 2011

AJALI YAIAMSHA USINGIZINI SERIKALI RUVUMAMheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Dkt. Christine G. Ishengoma (Pichani)ameliagiza Jeshi la Polisi Mkoani Ruvuma kufanya ukaguzi wa kina katika magari yote yanayotumika kusafirisha abiria katika wilaya zote.

Katika agizo hilo, Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, amesisitiza juu ya umuhimu wa kuyachunguza, kuyakagua na kuyazuia magari yote yenye hitilafu za kiufundi yasifanye kazi ya kusafirisha abiria na mizigo.

Lengo la agizo hilo ni kudhibiti matukio ya ajali ambazo zinaweza kugharimu maisha ya wananchi pindi ajali zinapotokea. Hii inafuatia tukio la hivi karibuni ambapo gari la abiria linalofanya shughuli zake kati ya Mbinga na Mbamba-bay kupata ajali na kusababisha vifo vya watu sita na wengine kujeruhiwa. Ajali hiyo ilitokea katika kijiji cha Chunya ikiihusisha gari lenye namba T.270 BDG.

Katika ajali hiyo, gari hilo lilikuwa limepakia abiria na mizigo miongoni mwake yalikuwa mafuta ya Diesel na Petrol, hivyo baada ya ajali kutokea, mafuta yalishika moto na kusababisha vifo hivyo.

Ili kutekeleza agizo hilo, Jeshi la Polisi Mkoa litatakiwa kukagua na kuwazuia wenye magari ya abiria kubeba mizigo ya mafuta ya diesel/petrol katika magari yao, kudhibiti na kuzuia gari kubeba abiria wengi zaidi ya uwezo wake na mwisho kuyazuia magari yote yasiyo na sifa na vigezo vya kubeba abiria kufanya hivyo kwa mujibu wa sheria ya usalama barabani.

Mwisho, Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa anatoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wote waliopoteza ndugu zao kufuatia vifo hivyo na aidha, anawatakia pole na kuwafariji abiria wote waliojeruhiwa katika ajali hiyo na amesisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wote waliosababisha ajali hiyo kutokea.

Imetolewa na:

Revocatus A. Kassimba,

Afisa Habari,

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa,

RUVUMA.

RAIS DKT KIKWETE AWA MGENI RASMI SWALA YA EID EL FITR DODOMA,DKT BILAL DAR

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, (wa pili kulia) Rais Mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi (kulia), Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Salum, wajumuika pamoja na waumini wa dini ya kiislamu kuswali swala ya Eid El-Fitr, iliyofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam leo, . Picha na Muhidin Sufiani-OMR
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akiwasalimu waumini walishiriki swala ya Iddi katika msikiti wa Kichangani leo asubuhi(picha na freddy Maro)

Baadhi ya waumini wa dini ya kiislamu wakiswali swala ya Iddi katika msikiti wa Kichangani uliopo Magomeni mapipa jijini Dar es Salaam leo asubuhi

MBUNGE FILIKUNJOMBE AWAZIDI UJANJA WACHAKACHUAJI WA ZAWADI ZA WANAMICHEZO JIMBONI

Mbunge wa jimbo la Ludewa Mhe.Deo Filikunjombe (kushoto) akikabidhi kombe kwa mabingwa timu ya Manga Fc baada ya kuifunga timu ya Ilininda FC katika mashindano ya Filikunjombe Cup yanayoendelea katika kata zote za wilaya ya Ludewa
mbunge wa jimbo la Ludewa mkoani Iringa Deo Filikunjombe (kulia) na diwani wa viti maalum kata ya Madilu wakikabidhi kombe kwa mabingwa wa mashindano ya Filikunjombe Cup timu ya Manga FC

MBUNGE jimbo la Ludewa Deo Filikunjombe (CCM) akataa kutoa zawadi ya Ng’ombe iliyochakachuliwa kwa mabingwa wa mashindano ya Filikunjombe Cup katika kata ya Madilu baada ya viongozi wa kijiji kutaka kufanya ufisadi wa ng’ombe huyo kwa kununua kitoto cha ng’ombe badala ya ng’ombe mkubwa kama alivyoagiza .

Mbunge huyo alifikia uamuzi huo wa kuikataa ng’ombe hiyo baada ya kuonyeshwa ng’ombe huyo wa zawadi na kulazimika kusimamisha mchezo ili wachezaji kukubaliana kwanza kama wapewe ng’ombe huyo ama fedha taslimu .

Akikabidhi kombe kwa mabingwa wa fainali hiyo mbunge Filikunjombe alisema kuwa mashindano hayo yalishilikisha timu nne za vijijini vyote vitatu vinavyounda kata ya Madilu ikiwemo timu ya Madilu Fc , Ilininda FC na Manga Fc ambao walitwaa ubingwa huo.

Hata hivyo mbali ya kata zote kukabidhiwa kombe ,jezi ,mipira na Ng’ombe ila kwa kata hiyo alishindwa kukabidhi ng’ombe baada ya uongozi wa kijiji hicho kufanya uchakachuaji wa ng’ombe hiyo kwa kununua ng’ombe mdogo zaidi ukilinganisha na ng’ombe ambao kata nyingine zilipata kununua na kutolewa zawadi.

“Ndugu zangu naomba kuuvunja utaratibu wa kutoa ng’ombe katika kata hii kwani nimebaini harufu za ufisadi hapa …..kata zote ng’ombe ambaye nimekuwa nikimtoa wa shilingi 300,000 na ni ng’ombe mkubwa kweli sasa hapa huyu ng’ombe aliyenunuliwa ni ndama mdogo sana na yawezekana huyu ng'ombe akawa anauzwa kati ya shilingi 150,000 ama shilingi 200,000 sasa nasema sikubali kumtoa zawadi ng’ombe mdogo hivyo nabadilisha badala ya kutoa ng’ombe natoa fedha tasilimu ili mshindi akaamua kwenda kununua ng’ombe mwenyewe ama kutumia fedha “

Katika mashindano hayo ya kuhamasisha michezo kwa vijana katika wilaya ya Ludewa mkoani Iringa yaliyoanzishwa na mbunge wa jimbo la Ludewa Deo Filikunjombe (CCM) yameendelea kutimua vumbi katika kata mbali mbali za jimbo hilo huku katika kata ya Madilu timu ya Manga ikifanikiwa kutwaa ubingwa wa kombe la Dhahabu na Ng’ombe .

Timu hiyo ya Manga Fc ilifanikiwa kutwaa ubingwa huo katika mchezo wa fainali uliopigwa katika uwanja wa Mfalasi na kufanikiwa kuigagadua (kuifunga) timu ya Ilininda Fc kwa jumla ya goli 1-0.

Katika mchezo huo uliovunja rekodi kwa kushuhudiwa na mashabiki wengi zaidi ulionyesha kuwa ni mchezo mgumu kwa timu ya Ilininda Fc pamoja na timu hiyo kuonyesha kujiamini kupita kiasa kabla ya mchezo huo na dakika 45 za mwanzo wa mchezo huo.

Hata hivyo hadi mwamuzi wa mchezo huo anazipumzisha timu hizo kwa kipindi cha kwanza hakuna timu ambayo ilipata kuzifungua nyavu za mwenzake .

Katika dakika ya 20 kipindi cha pili timu ya Manga ilipata kuzichana nyavu za Ilininda Fc kwa mkwaju mzito uliomshinda mlinda mlango wa Ilininda Fc na kupelekea timu hiyo ya Manga Fc kujihakikishia kutwaa ubingwa huo.

Pamoja na kikosi cha Ilininda Fc kujaribu kuonyesha cheche zake kwa lengo la kurudisha bao hilo bado walijikuta katika wakati mgumu zaidi na kufananishwa na sikio la kufa baada ya Manga Fc kuzidisha mashambulizi zaidi na kuifanya Ilininda Fc kufanya jitihada zaidi za kufikiri ili kuzuia kuongezwa mabao zaidi .

Hadi mwamuzi wa mchezo huo anapuliza filimbi ya mwisho dakika 90 za mchezo timu ya Ilininda Fc ilikuwa haijabahatika kusogelea nyavu za Manga Fc timu ambayo ilikuwa iliongoza kwa kuwa na mashabi ambao ni wazee wengi zaidi kuliko vijana na timu iliyosafiri zaidi ya kilometa 10 kwa mguu kutoka kijijini kwao huku Ilininda Fc wao wakitumia usafiri wa gari kufika katika uwanja huo wa ugenini kwa timu zote

Timu zilizopata kushiriki mashindano hayo na kuzawadiwa vifaa vya michezo mbali ya kutolewa ni mfalasi,Madilu ,Ilininda na Manga ambao walitwaa ubingwa .

EID MUBARAKA WADAU WOTE WA MTANDAO HUU

Kwa heshima na unyenyekevu mwingi napenda kuchukua nafasi hii kutoa baraka za Eid kwa wadau wote wa mtandao huu na kubwa zaidi tunaposherekea sikukuu hii kubwa tukumbuke kuwatazama wenye shida mbali mbali wakiwemo yatima

imetolewa na Francis Godwin mkurugenzi wa kampuni ya free Community Medias kwa niaba ya timu nzima ya watenda kazi katika mtandao huu na mingine yote inayomilikiwa na kampuni hii ya kihabari

August 30, 2011

HOT NEWS ...LUDEWA WAANDAMANA KWA MBUNGE KUILALAMIKIA BENKI YA NMB

Wananchi wa jimbo la Ludewa ambao ni wateja wa benki ya NMB tawi la Ludewa wametinga nyumba kwa mbunge wa jimbo hilo Deo Filikunjombe wakitaka awasaidie kuishtaki benki hiyo kwa madai ya upotevu wa fedha zao katika mazingira tata.

Agnesi Mapunda ni mtumishi wa Halmashauri ya Ludewa idara ya ardhi ambaye ni mteja wa benki hiyo mwenye akanti namba 6012400590 NMB tawi la Ludewa ambaye alidai kuwa akaunti yake ilikuwa na fedha zaidi ya shilingi milioni 1 ila mwezi wa sita alikuta akaunti hiyo ikiwa na salio la shilingi 144,000 pekee na baada ya kuuliza aliambiwa fedha zake zimetolewa kwa huduma ya pesa fasta na NMB Mobel huduma ambayo kwa upande wake hajawahi kuitumia toka awe mteja wa benki hiyo.

Hata hivyo alisema baada ya kuhoji sana ndipo benki hiyo ilipoamua kuchunguza suala hilo na kubaini majina ya watu waliohamisha fedha hizo na kuwa hadi sasa suala hilo lipo polisi linafanyiwa kazi.

Huku baadhi ya wateja wakienda benki hapo na polisi kutaka kufunga akanti zao na kuhama uteja na benki hiyo .

Walidai kuwa kuna uwezekano wa wafanyakazi wa benki hiyo kukopeshana fedha zao kinyume na utaratibu na baada ya muda kuzirejesha.

Kwani walisema kuwa wakati mwingine baada ya kufika na kulalamika katika benki hiyo na kuambiwa wafiki baada ya siku mbili ama tano wmekuwa wakikuta akaunti zao zinapesa kama walivyoziacha .

Mbunge wa jimbo hilo Filikunjombe amekili kupokea malalamiko hayo na kuwa tayari amewasiliana na meneja wa kanda na meneja wa benki hiyo ili kutolea ufafanuzi suala hilo.

Hata hivyo alisema kuwa majibu ambayo ameelezwa na viongozi hao wa kuwa yawezekana fedha hizo zinachnukuliwa na jamaa wa wateja hao ambao wamekuwa wakiwapa namba zao za siri bila kujua ama kwa kujua ama ni kampuni ya simu ambayo inashughulika na huduma hiyo .

Pia alisema kuwa ameshangazwa na ushirikiano mdogo wa wafanyakazi wa Benki hiyo tawi la Ludewa kwa kushindwa kutoa ushirikiano kwa wateja wao wenye matatizo hayo kwa kuwataka waende polisi kufikisha malalamiko yao huku wakijua wazi kuwa wateja hao wameingia mkataba na benki ya sio polisi .

Hata hivyo meneja wa NMB tawi la Ludewa alipotafutwa kwa simu alisema kuwa hana mamlaka ya kulizungumzia suala hilo na kuwa uongozi wa juu wa benki hiyo ndio unaweza kuzungumzia suala hilo .MTOTO WA RAIS MSTAAFU SMZ AANZISHA KUNDI LA MUZIKI WA TAARAB

MTOTO wa Rais Mstaafu wa Zanzibar, Amin Salmin ‘Mourinho’, amenzisha kundi jipya la muziki wa Taarab(pichani) linalojulikana kwa jina la T Moto Morden Taarab ‘Real Madrid’ linaloundwa na wasanii mahiri waliopata kutamba katika makundi ya Jahazi Morden Taarab, Five Star na mengineyo.

Akizungumza na mwandishi wetu Sufian Mafoto ,Amin alisema kuwa ameamua kuleta mabadiliko na ushindani katika muziki wa taarab kutokana na muziki huo kutokuwa na makundi yenye ushindani wa kisanii zaidi ya majungu na kufanya baadhi ya makundi yakivunjika kwa kushindwa kutoa upinzani na kubuni vitu vipya vinavyoweza kusaidia kulibakiza kundi katika jukwaa la muziki huo.

Aidha alisema kuwa ni siku nyingi alikuwa na ndoto ya kumiliki kundi la muziki wa Taarab, kutokana na kuvutiwa zaidi na muziki huo, lakini amekuwa akisikitishwa na baadhi ya wanamuziki wa taarab wanaopotea na vipaji vyao ama kushindwa kuwa na maisha mazuri hali ya kuwa wanakuwa wamefanya kazi kubwa ambayo hutokea kupendwa na mashabiki na kuuzika.

Amini anayejiita Mourihno kutokana na ‘kusajili’ wanamuziki nyota kutoka katika makundi makubwa ya muziki huo amesema kuwa wanamuziki aliowapata kuunda kundi hilo, anatarajia kuwa kundi hilo litafanya mambo mazuri na makubwa yatakayowashitua mashabiki wa muziki huo kwa kipindi kifupi kutokana na umahiri wa wanamuziki hao wenye hari zaidi na morari ya kufanya kazi kwa mageuzi na maslahi.

“Kutokana na kuuelea vyema muziki huu, kundi letu tumeamua kutumia aina ya kipee kati ya makundi yote yanayopiga muziki huu kwa kutumia jumla ya magitaa matatu ili kuweza kuleta radha na vionjo tofauti vya muziki huu, tofauti na makundi mengine ya taarab ambayo hutumia magitaa mawili tu” alisema Amini.

Aliwataja wanamuziki wanaounda kundi hilo jipya kwa upande wa waimbaji kuwa wanaongozwa na mwanamuziki mkongwe, Mwanahawa Ali, Mosi Suleiman aliyetoka kundi la Dar Morden Taarab, Joha Kassim, kutoka kundi la Five Star, Hasina Kassim, kutoka kundi la New Zanzibar Morden Taarab, Hassan Ali kutoka kundi la Five Star na Mrisho Rajab mshiriki wa BSS 2011.

Kwa upande wa wapiga vyombo wanaongozwa na mpiga Solo, Jumanne Ulaya ‘Mkono wa Biashara’ aliyetoka kundi la Jahazi Morden Taarab, Wapiga kinanda ni pamoja na Amour Saleh Zungu, aliyewahi kupita katika bendi za Twanga Pepeta, TOT na nyinginezo, Moshi Mtambo, kutoka kundi la New Zanzibar Morden Taarb na Omary Kisila kutoka, wengine ni pamoja na mpiga gitaa la rythim, Fadhili Ali Mnara, aliyekuwa katika muziki wa dansi katika baadhi ya Hoteli na mpiga Gitaa la Besi, Rajab Kondo kutoka kundi la New Zanzibar na Mussa Mipango, nayefanya kazi kwa mkataba kutoka kundi la TOT.

Aidha Amini alisema kuwa Kundi hilo hivi sasa bado linaendelea kujifua kuandaa vitu vipya ikiwa ni pamoja na nyimbo sita ambapo nne kati ya hizo zitaitambulisha albam yao ya kwanza itakayokwenda kwa jina la Aliyeniumba Hajanikosea, uliotunga na kuimbwa na Bi Mwanahawa Ali.

Nyimbo nyingine ni, Mtoto wa Bongo, inayoimbwa na Hassan Ali, Unavyojizani Mbona Hufanani, inayoimbwa na Joha Kassim, Mchimba Kaburi Sasa Zamu yake Imefika, inayoimbwa na Mrisho wa BSS, Mwenye Kustili Mungu na kumbe Wewe ni Shoti zote zikiimbwa na Mosi Suleiman, ambapo moja kati ya hizo itakuwa katia albam ya.

Kundi hilo limeingia Studio leo Agosti 29 kwa ajili ya kuanza kurekodi nyimba zake mpya ambazo kwa pamoja zitaanza kusikika hivi karibuni.

Naye kiongozi wa kundi hilo, Jumanne Ulaya ‘Mkono wa Biashara’, aliwataka wapenzi wa miondoko hiyo ya Taarab, kukaa mkao wa kula wakisubiri vitu vipya kutoka kwa kundi hilo vyenye utofauti mkubwa na ambavyo vitakuwa na radha ya kutochosha kusikiliza.

“Nawaahidi tu wapenzi wa muziki wa Taarab wakae mkao wa kula wasubiri kusikia kilichotuingiza kambini na nyimbo ambazo kwa kweli hazichoshi kusikiliza, kwani tumetua kundi hili kikazi zaidi na majungu” alisema Jumanne

HALMASHAURI YA MERU YAHAMISHA SOKO

Na Julieth Peter,Arumeru

HALMASHAURI ya Wilaya ya Meru Mkoani Arusha,imeamua kuhamisha soko la Kijiji cha Mbuguni kwenda kijiji cha Shambarai Burka hivyo kubadili eneo hilo la soko kuwa kituo cha magari ya kubebea abiria.

Wakizungumza kwenye kikao maalumu cha maendeleo cha kata hiyo kilichofanyika Wenyeviti wa vijiji vya kata ya Mbuguni wakiongozwa na Diwani wa kata hiyo Thomas Mollel,walidai kuwa mahali soko la awali lilipokuwa ni eneo dogo hivyo patageuzwa kuwa kituo cha mabasi.

Walisema eneo hilo ni mali ya Halmashauri ya Meru na ndiyo wenye idhini ya kubadilisha mradi huo,kisha wakaagiza utekelezaji na wao wameamua kutekeleza kwa faida ya halmashauri na uchumi wa wafanyabiashara mmoja mmoja hususan wanawake.

Mollel alisema kuanzia Agosti 24 mwaka huu,soko hilo litahamishwa kutoka kijiji cha Mbuguni hadi kijiji cha Shambarai Burka na hivi sasa soko hilo litakuwepo mara mbili kwa wiki kwa siku za Jumatano na Jumamosi,huku kituo cha magari kikitumika kwa kila siku.

Naye Mwenyekiti wa kijiji cha Mikungani Mussa Senzighe,alisema eneo la soko la awali la Mbuguni ni dogo hivyo baada ya kugeuzwa kituo cha mabasi na soko kuhamishwa kutakuwa ni faida kubwa kwa vijiji vya Mbuguni,Shambarai Burka Mikungani,Kikuletwa na Msitu wa Mbogo.

Senzighe alisema kwenye kituo hicho cha magari ya abiria,biashara nyingine zilizokuwa zinaendelea katika soko la awali za uuzaji wa maduka ya rejareja,hoteli,chipsi,Grocery,mbogamboga na mitumba zitaendelea kila siku.

Hata hivyo,Mwenyekiti wa kijiji cha Mbuguni Wilbert Melanyi alidai kuwa baadhi ya wakazi wa kata hiyo wanaeneza fikra potofu kwamba Diwani wa kata hiyo,anawaburuza wenyeviti wa vijiji kwa kutoa maamuzi peke yake.

“Mheshimiwa Diwani anaendesha vikao vyake kihalali kwa kufuata taratibu na maamuzi na pia sisi hatuwezi kupinga kila kitu lakini hatuwezi kuburuzwa na kukubali jambo ambalo halina maslahi kwa wananchi,” alisema Melanyi.

Alisema kuwa baadhi ya vijana wachache wanapinga kuhamishwa kwa soko hilo huku wafanyabiashara wengi hususan wanawake wakiunga mkono kitengo cha kuhamisha soko hilo na kugeuza eneo hilo kuwa kituo cha magari ya abiria.

Alisema kituo cha mabasi cha Mbuguni kinatarajia kuingiza zaidi ya sh200,000 kwa wiki,badala ya soko hilo lililokuwa linaingiza chini ya sh30,000 kwa wiki hivyo kuongeza kipato kwa halmashauri yao na pia kusogeza huduma kwa jamii.