WATU 13 wamekufa papo hapo na wengine 12 kujeruhiwa vibaya baada ya basi la Kampuni ya Summry kupinduka kutokana na kupasuka tairi la mbele.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Advocate Nyombi, alisema tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo (Mei 28) majira ya saa 4:00 usiku wakati basi hilo lenye namba za usajiri T 949 BCT aina ya Nissan Diesel likitoka Mkoani Arusha kuja Mbeya.

Alisema ajali hiyo imetokea eneo la Igawa wilayani Mbarali mkoani Mbeya mpakani mwa mkoa wa Iringa na Mbeya.

Alisema kati ya watu 13 waliokufa, wanaume ni wanane na wanawake ni watano ambao hata hivyo majina yao bado hayajapatikana na maiti zimehifadhiwa katika Hospitali ya Wazazi Meta Mbeya.

Aliwataja waliokufa kuwa ni dereva wa basi hilo, Makame Juma, Frolence Kitaule Mwalimu wa shule ya Msingi Ubaruku wilayani Mbarali,Thomas Mchalo Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe.

Wengine Bupe Mwaijumba, Magret Komba ambaye ni Muuguzi katika hospitali ya wazazi Mbeya pamoja na mumewe aitwaye Kandi Komba.

Alisema watu saba waliokufa katika ajari hiyo bado hawajatambuliwa na miili yao imehifadhiwa katika Hospitali ya Wazazi Meta ambapo ndugu na jamaa hadi kufika saaa 6;30 mchana walikuwa wakiendelea kumiminika katika hospitali hiyo kutambua waliokufa.

Kamanda Nyombi alisema majeruhi 11 wa ajari hiyo wamelazwa katika hospitali ya Wilaya ya Rujewa-Mbarali na mmoja katika hospitali ya Ilembula na hali zao zinaendelea vizuri.

Aliwataja majeruhi hao kuwa ni Twarib Fakiri, Lupi Mwaipalo, Martine Costantine (25) mkazi wa Moshi, Thadeus Logate (43) Mkazi wa Soweto, Andrew Adolf (6), Ezekiel Adolf ambaye ni mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Meta iliyopo Jijini Mbeya.

Majeruhi wengine ni Riziki Chuwa (25) mkazi wa Mbeya, Erasto Kiwaga (25), mkazi Mbeya, Hassan Mohamed mkazi wa Iringa,Bakari Zayumba mkazi wa Dar es Salaam na Halima Abdallah.

Kwamujibu wa Kamanda Nyombi chanzo cha ajali hiyo kilitokana na kupasuka tairi la mbele upande wa kushoto.

Alisema baada ya tairi kupasuka basi hilo liliserereka na kuacha njia hatimaye kupinduka upande wa kushoto na hivyo kusababisha vifo na majeruhi hao.

Ametoa wito kwa wananchi kujitokeza katika Hospitali ya Rufaa Mbeya kutambua ndugu zao waliokufa katika ajali hiyo.

Habari hii imeandikwa na timu ya Blogu hii JOachim Nyambo,Thobias Mwanakatwe na Francis Godwin