Matukio Daima

Tembelea kila siku kwa habari na matukio mbali mbali..

Matukio Daima

Kwa Habari za Kitaifa.

Matukio Daima

Kwa Habari za Kimataifa.

Matukio Daima

Kwa Habari za Uchumi na Biashara.

Matukio Daima

Kwa Habari za Michezo na Burudani.

January 31, 2011

MANISPAA YA IRINGA YAKOSA LITA 10 ZA MAFUTA KUSOMBA TAKA MJINI

Hapa ni soko kuu la manispaa ya Iringa

Hapa ni mtaa wa Kwamwagongo ambako ni miaka zaidi ya mitano taka hazijaondolewa

UONGOZI wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa mkoani Iringa umesema kuwa umeshindwa kusomba takataka zilizorundikana mitaani kwa zaidi ya miezi miwili sasa kutokana na kukosa fedha za kununulia mafuta lita 10 kwa kila tripu moja ya gari hilo kuzunguka mitaani kuondoa taka hizo.

Kutokana na uongozi wa Manispaa ya Iringa kushindwa kuzoa takataka hizo katika vituo vya taka baadhi ya maeneo yakiwemo ya Isoka , Mtaa wa kwa Mwagongo na maeneo mbali mbali ya mji wa Iringa kwa sasa yamezungukwa na uchafu mwingi pamoja na harufu kali iliyosababishwa na takataka hizo jambo lililopelekea wananchi kutishia kuandamana hadi kwa mkuu wa mkoa wa Iringa kulalamikia hali hiyo.

Wakizungumza na mtandao huu wa
www.francisgodwin.blogspot.com wananchi wa eneo la Isoka na mtaa wa kwa Mwagongo mjini hapa walisema kuwa takataka hizo zimekuwa kero kubwa na kuwa ni zaidi ya miaka mitano katika mtaa wa kwa Mwagongo takataka hizo hazipasombwa na kufanya eneo hilo kuzongwa na taka hizo huku makaburi yaliyopo eneo hilo kufukiwa na taka hizo.

Alisema John Sanga mkazi wa eneo hilo kuwa wakati wa kampeni CCM ilifanya mkakati wa kupeleka dampo la kuhifadhia takataka katika eneo hilo ila baada ya mgombea wao Monica Mbega kuangushwa na mchungaji Peter Msigwa (chadema) dampo hilo liliondolewa usiku.


Huku wakazi wa Isoka wakidai kuwa takataka katika eneo hilo zimeendelea kuwa kero kubwa pamoja na uongozi wa Manispaa ya Iringa kutumia gharama kubwa kujenga vizimba maalum kwa ajili ya kuweka taka hizo ila toka kujengwa kwa vizimba hivyo takataka zimekuwa hazitolewe na kufanya mae neo hayo kuwa na uchafu mwingi.
Katika mahojiano maalum namtandao huu wa www.francisgodwin.blogspot.com kwa niaba ya mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Teresia Mahongo ,afisa afya wa Manispaa ya Iringa Deodata Rukupwa .

Alisema kuwa kuwa ili gari hilo la kusomba takataka katika Manispaa ya Iringa liweze kuzunguka mitaani kusomba taka linahitaji kujaza mafuta lita 10 kwa kila tripu moja kutoka eneo husika kwenda kumwaga eneo la Kihesa kilolo nje kigodo na mji wa Iringa.


Hata hivyo mkurungenzi mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa alipofuatwa na mwandishi wa habari hizi ili kuthibitisha madai hayo ya Manispaa ya Iringa kukosa fedha za kununulia mafuta lita 10 kwa ajili ya gari hilo aligoma kukutana na mwandishi wa habari hizi kwa madai kuwa msemaji ni afisa habari wa Manispaa ya Iringa ambaye pia hakuwa na majibu.

MWISHO

January 30, 2011

BREAKINGNEWs AJALI MBAYA IRINGA USIKU HUU ,NI BAISKALI NA PIKIPIKI YAUA

Mwendesha piki piki mmoja mkazi wa Izazi Mtera katika wilaya ya Iringa vijijini aliyefahamika kwa jina moja la Ilomo amekufa papo hapo baada ya kugongana uso kwa uso na mwendesha baiskeli aliyetambuliwa kwa jina la Yusuph Moyo ambaye amejeruhiwa vibaya kwa kuvunjika miguu yake na mkono.

Ajali hii imetokea usiku huu majira ya saa 3 katika eneo la uwanja wa ndege Nduli wakati mwendesha pikipiki huyo akitokea Mtera kuja Iringa mjini na mwendesha baiskeli huyo akitokea Mjini .

TIMU YA RADIO OVERCOMERS FC YAWAADHIBU MADEREVA TAXI 3-2

Mshambuliaji wa Overcomers Fc (mwenye njano) akikabana na mchezaji wa timu ya madereva Taxi ambayo hata hivyo ilichapwa 3-2
Mshambuliaji wa timu ya Overcomers Fc Gerald Malekela (mbele) akiufukuza mpira

Kikosi cha Overcomers Fc wakiwa na baadhi ya mashabiki (mwenye kofia ni mmiliki wa mtandao huu Bw.Francis Godwin pia mchezaji wa Overcomers FC)
Ilikuwa kazi ngumu kwa madereva hapa kipa wao akiutazama mpiraMCHEZO wa kirafiki kwa ajili ya kuhamasisha michezo ndani ya mkoa wa Iringa kati ya timu ya watangazaji wa kituo cha radio Overcomers FC na madereva Taxi eneo la soko kuu umemalizika kwa timu ya madereva kupokea kichapo cha mabao 3-2.

Mchezo huo wa kihistoria katika mkoa wa Iringa kati ya wanataaluma hao na madereva Taxi ulichezwa katika uwanja wa Samora mjini Iringa na kuvunja rekodi ya kupata na mashabiki wengi zaidi kuliko hata michezo ya Lipuli na Polisi iliyopata kuchezwa katika uwanja huo.

Katika mchezo huo ulipigwa majira ya saa 8 za mchana jana timu ya Redio Overcomrs FC ilianza kujipatia bao la kwanza mnamo dakika ya 24 kipindi cha kwanza kupitia mchezaji wake nguli kutoka nchini Uganda Emanuel Nyeho ambaye aliweza kuunganisha shuti kali katika lango la madereva Taxi na kumshinda mlinda malango wao.

Hata hivyo timu ya madereva Taxi iliendelea kupata wakati mgumu katika mchezo huo kwa kipindi chote cha kwanza kutokana na kasi kubwa ya ushambuliaji ambayo ilitumiwa na wachezaji wa timu ya Overcomers FC .

Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika timu ya Overcomers Fm ilikuwa mbele kwa goli 1-0 dhidi ya madereva taxi .

Kipindi cha pili timu zote ziliingia uwanjani hapo kwa kukamiana kupita kiasi na kupelekea timu ya Radio Overcomers Fc kujipatia goli la pili dakika ya 65 ,huku dakika ya 70 madereva taxi waliweza kujipatia goli la kwanza kabla ya kuongezwa goli la tatu dakika ya 79 na radio Overcomers Fc .

Kama haitoshi maredeva taxi walionyesha jitihada zaidi dakika za mwisho wa mchezo na kubahatika kupata goli la pili ambalo lilidumu hadi mwisho wa mchezo huo ambao ulimalizika kwa overcomers Fc 3 dhidi ya goli 2 za Madereva taxi.

BREAKINGNES ...MAPIGANO MAKALI IRINGA YAUA MMOJA


MAPIGANO makali ya kugombea eneo la kunyweshea mifugo yaibuka katika kijiji cha Pawaga wilaya ya Iringa vijijini kati ya wafugaji jamii ya kimasai na wasukuma na kusababisha kifo cha mtu mmoja aliyeuwawa kwa kukatwa katwa mapanga huku kijana aliyetambuliwa kwa jina Merick Vanihi kujeruhiwa vibaya kwa mshale katika mkono wake wa kulia.

Wakielezea juu ya tukio hilo mashuhuda walimweleza mwandishi wa habari hizi kuwa chanzo cha mauwaji ya ni wafugaji jamii ya wasukuma ambao wamekuwa na kawaida ya kulazimisha wakulima kukubali mashamba yao yatumike kama sehemu ya malisho ya mifugo yao.

Imeelezwa kuwa eneo hilo yalipotokea mapingano hayo kuna dimbwi la maji ambalo limetokana na mvua zinazoendelea kunyesha na jirani wamekuwa wakiishi wafugaji jamii ya kimasai ambao pia wamekuwa wakiendesha kilimo katika eneo hilo .

Hivyo siku ya tukio wafugaji jamii ya kisukuma walifika katika eneo hilo na kulazimisha kunywesha maji mifugo yao pamoja na kulisha mifugo mazao ya wenyeji wa eneo hilo jamii ya kimsai kwa kutumia nguvu zaidi hali ambayo iliibua ugomvi mkubwa kati ya pande hizo mbili.

Kutokana na nguvu zaidi zilizotumiwa na jamii ya wafugaji wa kisukuma ,wafugaji jamii ya kimasai pia walilazimika kuingilia kati ili kusaidia wenzao na kupelekea ugomvi huo kuwa mkubwa na kuwafanya wasukua kutumia silaha kali kujinusuri zaidi.

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Iringa Evarist Mangalla amethibitisha kutokea mauwaji hayo kuwa yametokea juzi majira ya saa 7 mchana na kumtaja mfugaji jamii ya kimasai aliyeuwawa katika mapigano hayo kuwa ni kijana Iyani Kalihi (24).

Kamanda Mangalla alisema kuwa kijana huyo aliuwawa kwa kuchomwa katika sehemu mbali mbali za mwili wake na kitu chenye ncha kali .

Aliwataja watu wanaoshikiliwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za kuhusika na mauwaji hayo Machia Bachilo (54) Msukuma ,Kimbemba Bachilo (56),Sandu Magosi(28),Tewe Bundara(30),Zachalia Sanga (34)

Hata hivyo alisema kuwa majeruhi huyo amelazwa katika hospitali ya mkoa wa Iringa akiendelea kupatiwa matibabu zaidi kutokana na mapigano hayo..

January 28, 2011

UV CCM IRINGA MJINI YAPONGEZA WANAFUNZI WALIOFANYA VEMA

Mwenyekiti wa UVCCM wilaya ya Iringa mjini Ibrahim Ngwada akizungumza na wanafunzi wa shule ya msingi Ipogolo baada ya kutembelea shule hiyo leo kukabidhi vifaa vya shule kwa wanafunzi waliofanya vizuri mwaka jana,UVCCM ipo katika maandalizi ya sherehe ya miaka 34 ya kuzaliwa kwa CCM itakayofanyika Feb.5 mwaka huu
Mwenyekiti wa chipukizi wilaya ya Iringa mjini Ashura Mpogole akimkabidhi zawadi mwanafunzi wa shule ya msingi Mtwivila


Viongozi wa UV CCM wakisalimia wanafunzi wa shule ya msingi Mtwivila mjini Iringa
Diwani wa kata ya Ruaha Alphonce Mlagala (kushoto) na mwenyekiti wa UVCCM wilaya ya Iringa mjini Ngwada wakikabidhi zawadi kwa mwanafunzi wa shule ya msingi Ipogolo leo

January 27, 2011

ASKOFU DKT MDEGELLA ASEMA BARAZA LA MAWAZIRI BADO HAJALIONA...


ASKOFU wa kanisa la kiinjili la Kilutheri Tanzania (K.K.K.T) Dayosisi ya Iringa Dkt Owdenburg Mdegella (pichani)amedai kuwa utendaji mbovu wa baraza la mawaziri la serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Jakaya Kikwete umekuwa unatokana na mawaziri na viongozi kufanya kazi kwa kutegeana .

Pamoja na hali hiyo bado amesema kuwa ipo hatari ya maendeleo ya Taifa kuyumba zaidi iwapo chama cha mapinduzi (CCM) kitaendelea kuwepo madarakani na watendaji wa chini kuendelea kumdanganya Rais kwa ajili ya kuonekana wema.

Dkt Mdegella amesema kuwa ili nchi kurudi katika heshima yake ni vema azimio la Arusha kurudishwa ambalo litasaidia kumaliza ufisadi nchini na kuondoa tofauti ya serikali na mawaziri wake.

Dkt Mdegella aliyasema hayo wakati wa mahojiano maalum na gazeti hili kuhusiana na mwenendo wa serikali iliyopo madarakani na sakata la malipo ya dowansi ambayo kwa upande wake amesema kuwa malipo hayo ya dowansi na danganya toto na kuwa serikali italaumiwa zaidi iwapo itakubali kulipa malipo hayo hewa.

Pia Dkt Mdegella alisema kuwa kasi ndogo ya utendaji kazi kwa baraza la mawaziri umeanza kuwakatisha tamaa wananchi na kuwa ni vema baraza hilo la mawaziri kuongeza kasi zaidi ya utendaji ili kuharakisha kasi ya maendeleo kwa wananchi badala ya mawaziri kuendelea kufanya kazi za chama tawala pekee na kukitetea kwa uovu unaofanyika.

Hata hivyo alikitaka chama tawala kukaa chini na kukinusuru chama hicho kwa kuwapata wabunge wasema kweli daima ambao watafikisha ukweli wa mambo kwa mwenyekiti wa chama hicho na Rais Kikwete badala ya ilivyosasa kila kiongozi anataka kuonekana mwema kwa Rais na kueleza mazuri pekee na kuacha kufikisha ukweli kwa maana ya hali halisi ya nchi inavyokwenda.

DKt Mdegella alisema kwa upande wake haweze kutabili kama baraza la mawaziri la sasa litavunjwa ama lah na japo anachokiona sasa ni kushindwa kazi kwa baraza hilo la mawaziri hasa waziri wa nishati ambapo gharama za umeme zimezidi kupaa bila wizara husika kuonyesha uhai wake wa kushusha bei hizo.

"Mawaziri wengi wa Rais Kikwete wamekuwa wakifanya kazi ya kujipendekeza kwa Rais ....sasa hofu yangu mimi Taifa linaendelea kuyumba ....ila napenda kusema mimi si mtabiri kama Shekh Yahaya ambaye amekuwa akitabili ila naeleza kutokana na uhalisia wa mambo yanavyokwenda sasa

Alisema kuwa sehemu kubwa ya mawaziri wamekuwa wakionyesha kuogelea katika nafasi zao na kuwa iwapo mambo yataendelea kuwa hivyo nchi inazidi kuyumba zaidi .

Pia alisema kuwa matamko mbali mbali yanayoendelea kutolewa na CCM kupitia jumuiya zake ni kielelezo tosha kuwa chama hicho kinazidi kufilisika sera na maadili ya CCM ambayo wengi waliyazoea yameonyesha kuyumba zaidi .

Katika hatua nyingine askofu huyo aliionya serikali kuacha mara moja kuzuia wananchi kufanya maandamano ya kuipongeza ama kuipinga serikali yao kwani kufanya hivyo ni kuzidisha jazba kwa wananchi na kusababisha makubwa zaidi kama ilivyotokea Arusha.
MWISHO

WANANCHI KIGONZILE WATUMIA MAJI YA VYOONI (MAJI TAKA) KUNYWA

Hii ni foleni ya maji Kigonzile katika korongo la mto mchambawima mto unaomwaga maji ya vyooni

Mto mchambawima unaotumika kupata huduma ya maji Kigonzile

Hata kunywa tunakunywa haya haya

Habari kamili inakuja

January 26, 2011

T.F.A IRINGA NI MKOMBOZI WA KWELI WA MKULIMAKazi yetu ni kukuwezesha mkulima na mfugaji Iringa kupata bidhaa zilizo bora zaidi
Kazi yetu ni kuhakikisha wakulima wa Tanzania wanafanikiwa kwa kupata huduma zilizo bora zaidi
Huna sababu ya kupata tabu kujua duka bora la pembejeo za kilimo sogea sasa T .F.A ni jibu lako
Hapa nipo tayari kwa kuingia shamba

Karibu T.F.A kwa mbegu bora za kilimo na madawa ya kilimo pamoja na dhana za kisasa za kilimo pamoja na mifugo tupo jirani na RETCO mjini Iringa ama waweza kuwasiliana nasi kwa Phone .0262702298/2702049
Fax o262700957
Mobile ;+255 754 528151 au +255 786528151

Website.tfatz.com
AMA INGIA HAPA

January 25, 2011

BREAKINGNES ..WANAFUNZI CHUO CHA RUCO IRINGA WAGOMA

Gari ya matangazo ya kituo cha radio Overcomers Fm (98.6) Iringa likiingia katika lango kuu la chuo cha Ruco Iringa kwa ajili ya kurusha Breakingnews baada ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza katika chuo hicho kugoma leo

Rais wa serikali ya wanafunzi wa chuo cha Ruco Iringa akihojiwa na Radio Overcomers Fm 98.6 Iringa leo
Wanafunzi wa chuo cha Ruco wakiwa katika mgomo leo wakishinikiza bodi ya mikopo kuwaingiza fedha zao za kujikimu kiasi cha shilingi 300,000 kama ilivyokuwa katika chuo cha Mkwawa na UDOM hivi karibuni ,mgomo huo umeanza majira ya asubuhi chuoni hapo

January 24, 2011

WABUNGE WA CCM WAPIKWA LEO


Waziri Mkuu Mh. Mizengo Pinda na Waziri Mkuu Mstafu na mbunge wa Monduli Mh. Edward Lowassa wakiwa katika mazungumzo wakati wa mapumziko katika semina ya wabunge wa CCM bofya hapa

January 21, 2011

MTOTO WA MIAKA 12 AELEZA ALIVYOKUWA AKIPAA KAMA NDEGE

Mtoto wa miaka 12 mkazi wa Mlandege katika Manispaa ya Iringa pichani akiwa katika kituo cha Overcomers Power Center akifanyiwa maombi baada ya kusumbuliwa kwa zaidi ya miaka miwili akidai kushiriki vikao vya kishrikina na wenzake ,mtoto huyo amesalimisha dawa ambazo alikuwa akitumia kufanya kila akipendacho na kueleza jinsi alivyopata kuishi majini ,habari zaidi sikiliza Radio wapo Fm kwa wakazi wa jijini Dar es Salaam na Iringa sikilizeni Overcomers Fm 98.6 MHz

Hapa dawa hizo zikiteketezwa kwa moto ,tukio hilo limefanyika usiku huu mjini Iringa kumbuka habari zaidi ya tukio hilo utazipata katika gazeti la Jibu la Maisha wiki ijayo

BREAKINGNES CHADEMA IRINGA YATANGAZA KUMSIMAMISHA UANACHAMA MWANACHAMA WAKE KISA KUMSHUSHA KTK GARI MBUNGE

CHAMA cha demokrasia na maendeleo (Chadema) wilaya ya Iringa mjini kimetangaza kumemsimamisha uanachama na kumfukuza ndani ya chama hicho aliyekuwa mgombea udiwani wa kata ya Kwakilosa jimbo la Iringa mchini Abumeleck Changawa kutokana na utovu wa nidhamu dhidi ya mbunge wa jimbo hilo mchungaji Peter Msigwa.

Changawa anadaiwa pamoja na kukikosea heshima chama hicho na wananchi wa jimbo la Iringa mjini ambao walimchagua mchungaji Msigwa kama mbunge wao bado alimdhalilisha mbunge huyo kwa kumtoa katika gari yake na kumtupa nje ya gari walilokuwa wakisafiria pamoja na mbunge huyo.

Akitoa tamko la chama mbele ya waandishi wa habari leo ofisini kwake katibu wa Chadema wilaya ya Iringa mjini Suzana Mgonokulima (pichani kulia)alisema kuwa chama kimelazimika kuchukua hatua kutokana na kutoafiki tabia ya mwanachama huyo mwenye kadi namba 0234984 ambaye kwa makusudi amekuwa akiendelea kukichafua chama na mbunge Msigwa.

Katibu huyo alisema kuwa Changawa ameendelea kutoa lugha chafu dhidi ya mbunge huyo ikiwa ni pamoja na kutoa vitisho jambo ambalo baraza la wazee wa chadema ,na kamati ya utendaji ya chama kuamua kukutana na kutoa tamko dhidi ya mwanachama huyo.

Hata hivyo alisema kuwa Changawa katika taarifa zake za kumchafua mbunge Msigwa ambaye pia ni mwenyekiti wa wilaya wa Chadema alimtaka mchungaji Msigwa kama mwenyekiti wa Chadema wilaya kujiuzulu nafasi hiyo kwa madai kuwa ni msimamo wa waliokuwa wagombea udiwani wa Chadema jimbo hilo jambo ambalo ni uzushi wake binafsi na sio msimamo wa wenzake.

Katibu huyo alisema kuwa tayari kamati ya utendaji ,madiwani kivuli wamepata kukutana na kutoa mapendekezo yao yanayokiagiza chama kuchukua hatua ya kinidhamu ya kumwajibisha mwanachama huyo.

Akitoa uamuzi wa chama hicho wilaya katibu huyo Mgonokulima alisema kuwa kuanzia leo chama kimemsimamisha uanachama ndani ya chadema mwanachama huyo Changawa .

Mgonokulima alisema kuwa katika kikao kilichoketi Januari 16 mwaka huu baada ya chama kujiridhisha na mtiririko wa makosa ya makusudi ya utovu wa nidhamu kwa chama chenyewe na kwa kiongozi huyo wa chama na mbunge wa jimbo la Iringa mjini ,kimelazimika kumsimamisha uanachama Changawa kwa kusema ovyo dhidi ya chama kinyume na katiba ya chama hicho.

Hata hivyo chama kimetoa muda wa siku 7-14 kwa Changawa kujibu kwa maandishi sababu za kukosa nidhamu na iwapo atashindwa kufanya hivyo atakuwa amejivua uanachama ndani ya chama hicho na chama kitampokonya kadi ya uanachama .

Kwa upande wake Changawa alisema kuwa hadi sasa bado hajapokea barua yoyote toka chama inayomtaka kujieleza na kuthibitisha kuzungumza na vyombo vya habari juu ya mawazo yake ya kumtaka mbunge huyo kuachia nafasi ya ue nyekiti ili kubaki na nafasi moja ya ubunge kama sehemu ya kuachia majukumu kwa wengine wenye sifa.

Kuhusu kutakiwa kurejesha kadi ya chama hicho iwapo siku 14 zitapita bila kujieleza juu ya suala hilo ,Changawa alisema kuwa hadi sasa yeye hana kadi ya Chadema na kuwa kadi ipo kwa mbunge huyo na kuwa hata fomu yake ya kugombea udiwani ilijazwa na mbunge Msigwa na kuwa namba ya kadi yake haitambui na kuwa yupo tayari kuondoka ndani ya chama kama viongozi wataendelea kutetea uovu.

January 19, 2011

WALIMU IRINGA WAIPUUZA WIZARA YA ELIMU KUHUSU MICHANGO,WAZAZI WAOMBA ADA IRUDISHWE SHULE ZA MSINGI

Waziri wa elimu Dk Shukuru Kawambwa
WALIMU wa shule za msingi katika manispaa ya Iringa wameonyesha kukiuka maagizo ya wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi kuhusu agizo la wizara hiyo la kupiga marufuku michango kwa watoto wanaosoma elimu ya msingi baada ya walimu hao kudai kuwa wizara hiyo ilitoa agizo hilo kisiasa bila kujua sababu ya michango hiyo.


Wakizungumza kwa nyakati tofauti walimu hao ambao walipata kuhojiwa na mtandao huu wa http://www.francisgodwin.blogspot.com/ walidai kuwa michango hiyo ilikuwepo hata kabla ya baraza jipya la mawaziri wa serikali ya awamu ya tano kuundwa hivyo kupinga michango hiyo ni sawa na kuzuia jambo ambalo wizara hiyo halilijui.

Alisema baadhi ya walimu wa shule za msingi mjini hapa ambao hata hivyo hawakupenda kutaja majina yao kwa madai kuwa wao si wasemaji wa ofisi ya elimu wilaya ya Iringa na kuwa wizara hiyo imekuwa ikitoa maagizo ya mdomo yasiyo na waraka wowote na kuwa wao hawawezi kusitisha michango hiyo hadi watakapopewa mwongozo wa kuendesha shule hiyo.

Kuhusu utitili wa michango isiyo na risiti katika shule mbali mbali za manispaa ya Iringa na mkoa wa Iringa walimu hao walisema kuwa michango hiyo inatambuliwa hata na ofisi ya afisa elimu mkoa na ndio sababu ya wao kuendelea kuwafukuza wanafunzi wasio na michango hiyo .

Walitaja michango hiyo kuwa ni pamoja na michango ya mitihani ,karatasi ,walinzi ,maji ,umeme ,posho kwa walimu na michango mingine ambayo ni fedha za ukarabati wa majengo ya shule na ununuzi wa madawati katika shule hizo.

Michango hiyo imeendelea kuwa kero kubwa kwa wazazi mjini Iringa ambao baadhi yao wamedai kuwa sehemu ya michago hiyo kama shule ya msingi Ipogolo wamekuwa wakimsaidia mkuu wa shule hiyo kutengeneza gari lake la kusambaza nyama mjini Iringa .
Hivyo wamemwomba mbunge wa jimbo la Iringa mjini Mchungaji Peter Msigwa (Chadema) kusaidia kutatua kero hiyo ya michango kwa wazazi wanaosomesha watoto wao katika shule za msingi na kuiomba serikali kurudisha ada kuliko michango hiyo holela.

Mbunge Msigwa amesema kuwa kwa upande wake haungi mkono uwepo wa michango hiyo na kuwa ni vema wanananchi wakakutana na kamati za shule na kuhoji juu ya michango hiyo na kuwataka wazazi kuvuta subira juu ya kero hiyo na kuwa lazima ahakikishe ameishughulikia.

Huku mbunge wa viti maalum mkoa wa Iringa Ritta Kabati (CCM) akipiga marufuku wazazi kuendelea kuchangia michango hiyo isiyo na risiti na kuwa kinachofanywa na walimu hao ni wizi mtupu .

BREAKINGNES ....WANANCHI MBOZI WACHOMA MOTO BASI LILILOGONGA MTU


IGP MWEMA
Wananchi wanao daiwa kuwa na hasira kali wakazi wa wilaya ya Mbozi mkoani Mbeya wameteketeza basi kwa moto baada ya basi hilo kumgonga mtembea kwa miguu.


Kamanda wa polisi wa mkoa wa Mbeya Advotece Nyombi ameuambia mtandao huu hivi punde kwa njia ya simu kuwa pamoja na wananchi hao kuchoma moto basi hilo bado wameweza kufunga barabara na kupelekea msongamano mkubwa wa magari katika eneo hilo la tukio.


Alisema kuwa tukio hilo limetokea leo majira ya jioni na kuwa hadi sasa jeshi la polisi linaendelea na jitihada za kuwasihi wananchi hao kutuliza jazba ili kufungua barabara hiyo.


Kamanda huyo alisema mbali ya mtu mmoja huyo aliyegongwa na basi hilo hakuna mtu mwingine ambaye amepata kufa wala kujeruhiwa katika tukio hilo.


Taarifa zaidi endelea kutembelea mtandao huu.

January 18, 2011

MWENYEKITI WA WAZAZI KILOLO LAZARO MNYAMWOGA AMEFARIKI

Marehemu Lazaro Mnyamwonga aliyekuwa mwenyekiti wa wazazi wa CCM Wilaya ya Kilolo ,Iringa amefariki dunia akiwa mkoani Dodoma
Mbunge wa Kilolo akipokea mbuzi zawadi huku Marehemu Mnyamwoga ( wa watu kulia mwenye suti nyeusi akishuhudia)

Mbunge wa jimbo la Kilolo Prof .Peter Msolla akiwahutubia wanamichezo huku marehemu Lazaro Mnyamwoga ( wa tatu waliokaa mwenye suti nyeupe akishuhudia )
Taarifa za uhakika kutoka katika familia ya marehemu zinadai kuwa Mnyamwonga amefariki dunia jana akiwa mjini Dodoma na mwili wake umezikwa leo wilayani Kilolo,katika maisha yake amepata kutumikia nafasi mbali mbali ndani ya chama ikiwemo ya udiwani na uenyekiti wa jumuiya ya wazazi wilaya ya Kilolo nafasi ambayo alikuwa akiiongoza hadi mauti yanamkutaBEREAKINGNEWS.....UWANJA WA AMANI MAKAMBAKO WAKOSA AMANI SHABIKI AUWAWA KINYAMA


Rais wa TFF Leodgar Tenga akiwa naaliyekuwa katibu wa TFF Frederick Mwakalebela

MASHINDANO ya ligi daraja la tatu ngazi ya wilaya wilayani Njombe yameingia dosari baada ya uwanja wa Amani Makambako kukosa amani na shabiki mmoja kuuwawa kwa kuchomwa kisu uwanjani wakati wa mchezo kati ya Njombe mjini na Mbeya Road .

Tukio hilo lilitokea jana jioni katika uwanja wa Amani Makambako wilaya ya Njombe Shabiki huyo aliyetajwa kwa jina la Geofrey Mwalongo alikuwa ni shabiki wa wa timu ya Njombe mjini .

Kwa mjibu wa mashuhuda wa tukio hilo walidai kuwa shabiki wa Mbeya Road alimvamia shabiki huyo wa Njombe mji ambaye kwa muda wote alikuwa ametulia katika jukwaa la timu yake akiendelea kushangilia kwa nguvu zote hali iliyoonyesha kumkwaza shabiki huyo wa Mbeya Road ambaye hakupenda timu ya wageni Njombe mji kushangiliwa zaidi ya timu mwenyeji Mbeya Road.

Hata hivyo shabiki huyo aliyefanya mauwaji anadaiwa kuvamia jukwaa la Njombe mji huku akiwa amehifadhi kisu katika koti lake refu mvano wa ninja na kumvamia shabiki huyo ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha nne katikashule ya sekondari Mpechi Njombe na kumvuta pembeni ya uwanja na kumchoma kisu tumboni na kumwacha utumbo ukiwa nje kasha kutoka nje ya uwanja huo kabla ya kukamatwa na mashabiki hao wa soka na kufikishwa polisi.

“Baada ya kukamatwa mashabiki walimvamia na kuanza kumwadhibu kwa kichapo kwa kutaka kumuua kama alivyofanya mauwaji dhidi ya mwenzake huyo hali iliyopelekea askari polisi kuingilia kati kumwokoa..” alisema mmoja kati ya mashuhuda wa tukio hilo Mwanahabari Hamisi Kasapa.

Alisema kuwa baada ya tukio hilo lashabiki huyo kuchomwa kisu jitihada mbali mbali zilifanyika katika kuokoa maisha yake ikiwa ni pamoja na kumkimbiza katika Hospitali ya mji wa Makambako ,Njombe na baadaye kukimbizwa hospitali ya Rufaa ya Mbeya ambako leo asubuhi alifariki dunia.

Hata hivyo alidai kuwa sanjari na vurugu hizo zilizopelekea mauwaji ya shabiki huyo bado uwanja huo umekuwa ukiongoza kwa kuwa na vurugu mbali mbali ambapo mchezo wa kwanza kati ya timu hizo mashabiki walitolewa uwanjani kwa mabomu na mchezo wa pili walikimbizwa na virungu na polisi baada ya fujo kubwa kuibuka katika michezo hiyo..

Mbali ya matukio hayo pia moja kati ya viongozi wa soko mkoa wa Iringa (I.R.F.A) alipata kuzichapa ngumi na kiongozi wa soko wilaya ya Njombe wakati wakibishana juu ya kupinga uwanja huo wa Amani kuendelea kukosa amani wakati wa michezo mbali mbali

Vingozi wa timu hiyo ya Njombe mji wamethibitisha kutokea kwa mauwaji hayo na kuwa tayari walipata kukiomba chama cha soka mkoa wa Iringa kubadili uwanja huo ila walipinga maombi hayo .

Hata hivyo kamanda wa polisi wa mkoa wa Iringa Evarist Mangalla hakuweza kupatikana kuelezea hatua zilizochukuliwa na jeshi la polisi juu ya tukio hilo japo katibu msaidizi wa chama cha soka mkoa wa Iringa Ramadhan Mahano alithibitisha kutokea kwa mauwaji hayo japo alitaka msemaji mkuu awe katibu wake Eliud Mvella ambaye hata hivyo hakuwepo mkoani Iringa baada ya kuwepo jijini Dar es Salaam kwa zaidi ya siku mbili sasa .

“… Ni kweli tukio hilo la kuuwawa kwa shabiki lipo na nimepata kulisikia ila siwezi zungumza chochote labda mtafute katibu wangu Eliud Mvella atakuelezea zaidi “ alisema na kukata simu.


January 17, 2011

KOCHA WA STARS APEWA SHAVU

KOCHA wa zamani wa Yanga, Sredojevic Milutin 'Micho', amesema ni vyema Watanzania wakampa muda Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Jan Poulsen ili aijenge timu, kwani namna alivyoiona kuna kazi kubwa inahitajika ili ilete matunda mazuri.

Amesema ni vigumu kuamini namna Taifa Stars inavyocheza kama ilikuwa na kocha mmoja kwa miaka minne, badala yake inaonekana ni timu mpya na yenye kocha anayeanza moja kufundisha, hivyo matunda yake yatachelewa kuonekana.

Alitoa kauli hiyo juzi mjini hapa, baada ya kumalizika mchezo wa kuwania nafasi ya tano kati ya timu ya Taifa Stars na Sudani katika michuano ya soka Nchi za Bonde la Mto Nile Uwanja wa Al Salam na Stars kulala mabao 2-0 yote yakifungwa kipindi cha pili.

Micho ambaye kwa sasa ni Kocha Mkuu wa El Hilal ya Sudan, hakumtaja kwa jina lakini kocha aliyekuwa kabla ya Poulsen ni Mbrazil Marcio Maximo aliyefika Tanzania Julai 2006 na kuondoka Julai 2010 na Poulsen raia wa Denmark alirithi mikoba Agosti mwaka jana na amesaini mkataba wa miaka miwili.

Desemba mwaka jana Poulsen aliiongoza timu ya Taifa ya Tanzania Bara 'Kilimanjaro Stars' kutwaa Kombe la Chalenji kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati, wakati Maximo Januari mwaka juzi aliiongoza Taifa Stars kucheza fainali za Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) zilizofanyika Ivory Coast na kuishia hatua ya makundi.

Alisema Stars sasa ndiyo inaanza kujengwa upya, inaonekana si timu ya ushindani na haioneshi kama kweli ilikuwa na kocha mmoja kwa miaka minne mfululizo, badala yake kinachoonekana ni timu mpya na kocha mpya anaanza kuijenga.

Micho yupo mjini Cairo na El Hilal iliyoweka kambi kujiandaa na michuano ya kimataifa na alisisitiza hasemi kocha aliyekuwepo Stars kabla ya Poulsen ni mbaya, lakini Stars haionekani kama ilikuwa ikinolewa na kocha mmoja kwa miaka minne.

Michuano ya soka Nchi za Bonde za Bonde la Mto Nile ilitarajiwa kumalizika jana usiku kwa mchezo wa fainali kati ya wenyeji Misri na Uganda, ambapo Kenya na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) zenyewe zilicheza kuwania mshindi wa tatu. Burundi imeshika nafasi ya saba kati ya timu saba.

Wakati huo huo, Poulsen akizungumza juzi baada ya vijana wake kufungwa mabao 2-0 alisema kuna makosa waliyafanya sehemu ya ulinzi na ndiyo yaliiangusha timu yake na kuruhusu mabao kipindi cha pili.

Hata hivyo alisema soka ndivyo lilivyo, lakini hakuwa tayari kuzungumzia kwa ujumla kufanya vibaya kwa timu katika michuano

hiyo au kitu gani ilichopata kiufundi na kusema atafanya hivyo akishafika Dar es Salaam na kujipanga vizuri.

Timu itaondoka Cairo leo saa tano usiku na inatarajiwa kufika Dar es Salaam saa 11 ikiwa imeshika nafasi ya sita kati ya tmu saba zilizoshiriki michuano hiyo, ambayo bingwa amejinyakulia zaidi ya sh. milioni 200 za Tanzania, wa pili zaidi ya sh. milioni 170 za Tanzania na wa tatu zaidi ya sh.milioni 130 za Tanzania.

BREAKINGNEWS............WANAFUNZI CHUO CHA MKWAWA NAO WAGOMA

Wanafunzi wa chuo cha MKwawa Iringa wakiwa katika mgomo wao leo

Mkuu wa chuo Prof Philimon Mushi akizungunza na wanahabari

SAKATA la migomo ya wanafunzi wa vyuo vikuu nchini linaendelea kutikisa nchi baada ya jana wanafunzi wa mwaka wa kwanza katika Chuo Kikuu kishiriki Cha Ualimu cha Mkwawa (MUCE) mkoani Iringa kufanya mgomo wa kuingia madarasani wakiwashinikiza viongozi wa DARUSO kujiuzulu huku wakiituhumu bodi y a Mikopo kwa kuchelewa kuwapa mikopo yao kwa ajili ya chakula na malazi.


Hata hivyo mgomo huo umepelekea kukamatwa na kuwekwa kizuizini kwa muda mwandishi wa habari wa mtandao huu ambaye pia anawakilisha gazeti la Tanzania Daima na redio ya Over comers Fm mkoani Iringa kwa madai ya kufika chuoni hapo kuzungumza na wanafunzi bila kuitwa na viongozi wa chuo hicho.

Wakizungumza mbele ya waandishi wa habari waanafunzi hao hao walidai kuwa sababu ya wao kugoma kuendelea na vipindi ni kutokana na fedha hizo za mikopo ambazo ni shilingi 00,000 kwa kila mmoja fedha ambazo zilitakiwa kutolewa januari 14, mwaka huu kuendelea kucheleweshwa hadi sasa na kupelekea baadhi yao kulala bila kula chochote kwa zaidi ya siku moja huku baadhi yao wakishindia maji na vyakula vya kuomba omba mitaani kwa wenyeji.


Pamoja na mgomo huo ambao wao wanafunzi walidai utamalizaka pele tu bodi ya mikopo itakapotimiza wajibu wake bado wanafunzi hao walieleza kulilalamikia jeshi la polisi mkoa wa Iringa kwa askari wake kutumia risasi za moto juzi usiku wakati wa kuwatawanya wanafunzi hao na mmoja kati ya wanafunzi kunusurika kuuwawa kwa risasi .

Wanafunzi hao walisema kuwa kutokana na kukosa fedha hizo tokea Januari 14 wamekuwa wakiishi kwa shida kwasababu ya kukosa pesa ya kununulia chakula na mahitaji yao mengine huku wakiponda kiasi cha Sh 5,000 wanachopewa kila siku kwamba hakikidhi mahitaji yao, kimepitwa na wakati na kinatakiwa kurekebishwa mara moja na serikali na kuongeza kuwa serikali inauweza mkubwa wa kutumia fedha za dowansi na zile wanazolipwa mafisadi wengine kuboresha maisha ya wanavyuo nchini .

Waliyataja madai mengine dhidi ya uongozi wa chuo na serikali kwamba ni kucheleweshewa vitambulisho vya bima ya afya ambayo kila mwanafunzi uilipia Sh 50,000, kitabu cha muongozo wa masomo na mgao wa umeme.

Mkuu wa Chuo hicho cha Mkwawa Iringa Profesa Phillemon Mushi alikanusha madai hayo japo alidai kuwa ni kweli wanafunzi wanne walikamatwa na kwa mahojiano kuhusiano na mgomo huo na hatimaye kuachiwa japo hakukuwa na vurugu zozote za za kuita polisi kutumia nguvu hata kutumia risasi za moto.


Aidha mkuu wa Chuo hicho, Profesa Mushi alisema uongozi wa chuo umefanya mawasiliano na Bodi ya Mikopo, ambayo imethibitisha kwamba fedha za wanafunzi hao zilianza kuwekwa kwenye akaunti zao tangu Ijumaa.

Alisema wana uhakika mpaka kesho Jumanne(leo) taratibu za kibenki zitakuwa zimekamilika na wanafunzi hao watakuwa wamepata fedha zao.

Kuhusu kitabu cha muongozo wa masomo na umeme, Profesa Mushi alisema kinaandaliwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kitakapokuwa tayari kitagawanywa kwa wanafunzi hao

Kuhusu tatizo la umeme chuoni hapo alisema kuwa imekuwa ikisababishwa na mgao wa umeme ambao unaendeshwa nchini nzima na kuwa pale mgao wa umeme unapokuwepo eneo hilo umeme wa jenereta umekuwa ukitumika kusambaza umeme katika vyumba vyote vya kusomea, bwalo la chakula na maktaba ili kuwawezesha wanafunzi kusoma vizuri .


Kuhusu mwandishi aliyekamatwa na kuzuiwa kuendelea kutimiza wajibu wake wa kuchukua habari kwa wanafunzi hao mkuu huyo Prof.Mushi alimwomba radhi mwandishi huyo na waandishi wengine kwa kunyanyashwa na watu wa usalama chuoni hapo na kuwa wanahabari wanawajibu wa kuwasikiliza wanafunzi hao kama sehemu ya kazi yao .

Mwandishi huyu aliwekwa kizuizini katika ofisi za usalama chuoni hapo kwa zaidi ya dakika 15 akihojiwa na kutakiwa kueleza mamlaka ya kufika chuoni hapo ameyapata wapi bila wao kumruhusu kuongea na wanafunzi hao.

Kutokana na tukio hilo waandishi wa habari mkoa wa Iringa kupitia klabu yao ya waandishi wa habari mkoa wa Iringa (IPC) wameeleza kusikitishwa na uamuzi wa wanausalama hao wa chuo kumzuia mwandishi na kumweka kumhoji sababu za kuwasikiliza wanafunzi hao na kuwa kufanya hivyo ni kuzuia uhuru wa vyombo vya habari kutoa habari na uhuru wa wananchi kupata habari za uhakika zaidi.

Katibu wa IPC Frannk Leonard alisema kuwa pamoja na uongozi wa chuo kuomba radhi kwa kitendo hicho ila bado jamii inapaswa kutambua kuwa vyombo vya habari zinawajibu wa kuhabarisha na kwenda moja kwa moja katika maeneo ya matukio na kupata habari kamili kwa kuzungumza na pande zote badala ya kukaa ofisini kupata habari za upande mmoja.

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Iringa Evarist Mangalla amethibitisha kuwepo kwa mgomo huo wa wanafunzi chuo cha Mkwawa japo amekanusha madai ya wanafunzi juu ya polisi kutumia risasi za moto kuwatawanya na kuwa hakuna askari polisi aliyekwenda katika mgomo huo Mkwawa na kuwa jeshi la polisi si walinzi wa chuo hicho .
Hadi sasa bado wanafunzi hao wanaendelea na mgomo japo jitihada za mazungumzo zinafanywa na viongozi wa chuo hicho.