Matukio Daima

Tembelea kila siku kwa habari na matukio mbali mbali..

Matukio Daima

Kwa Habari za Kitaifa.

Matukio Daima

Kwa Habari za Kimataifa.

Matukio Daima

Kwa Habari za Uchumi na Biashara.

Matukio Daima

Kwa Habari za Michezo na Burudani.

DOWNLOAD MATUKIO DAIMA APP HAPA

https://play.google.com/store/apps/details?id=com.matukiodaima
https://drive.google.com/open?id=0B7pDgIUPsc8Db3NOT1ZQcUozdVk

September 22, 2017

TACAIDS IMETAJA IDADI YA WATANZANIA WANAOGUA UKIMWI 2017


PIX 1
Kaimu Mkrugenzi Mkuu wa TACAIDS Bw.Jumanne Issango akieleza jambo kwa waandishi wa habari(hawapo pichani) wakati wa mkutano kuhusu changamoto na mafanikio katika kupambana na ukimwi nchini uliofanyika katika ukumbi wa ofisi za TACAIDS leo Jijini Dar es Salaam.
PIX2
Kaimu Mkrugenzi Mkuu wa TACAIDS Bw.Jumanne Issango akieleza jambo kwa waandishi wa habari(hawapo pichani) wakati wa mkutano kuhusu changamoto na mafanikio katika kupambana na virusi vya ukimwi nchini kulia ni Kaimu Mkurugenzi Muitiko wa kitaifa wa TACAIDS Bi.Audrey Njelekela mkutano uliofanyika katika ukumbi wa ofisi za TACAIDS leo Jijini Dar es Salaam.
Picha na Paschal Dotto-MAELEZO
………………..
Na Fatma Salum – MAELEZO
21/09/2017
Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) imeendelea kuiasa jamii kuhusu kubadili tabia ili kuepuka maambukizi ya virusi vya UKIMWI kwani ugonjwa huo bado ni janga kwenye nchi yetu.
Hayo yamesemwa leo na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa tume hiyo Bw.Jumanne Issango alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu mafanikio na changamoto za tume tangu ilipoanza kutekeleza majukumu yake.
“UKIMWI bado ni changamoto katika maendeleo ya Taifa letu na umeendelea kuathiri kila sekta, kila imani, matajiri na masikini nchini kote hivyo ni wajibu wa kila mmoja kujitathmini mwenendo wake na kuacha tabia hatarishi ambazo zinachangia kuongeza maambukizi ikiwemo uasherati, ngono zembe, ulevi na kadhalika,” alisema Issango.
Alieleza kuwa kwa miaka ya karibuni hali ya maambukizi ya UKIMWI imeendelea kupungua ingawa kuna tofauti kwenye mikoa, wilaya na makundi ya kijamii.
Issango alibainisha kuwa kiwango cha maambukizi Tanzania Bara ni asilimia 5.3 na takwimu hizo ni kutokana na Utafiti wa Viashiria vya UKIMWI mwaka 2012.
Kwa mujibu wa utafiti huo wanawake walioambukizwa ni asilimia 6.2 na wanaume ni asilimia 3.8 ambapo idadi ya Watanzania wanaokadiriwa kuishi na VVU ni zaidi ya milioni 1.5.
“Mikoa inayoongoza kuwa na maambukizi makubwa ni Njombe asilimia 14.8, Mbeya asilimia 9 na mikoa yenye maambukizi ya chini zaidi ni Manyara asilimia 1.5, Tanga asilimia 2.4 na Dodoma asilimia 2.9,” alifafanua Issango.
Aidha alisema kuwa licha ya maambukizi mapya kupungua kwenye jamii bado kiwango cha maambukizi kwenye makundi maalum kimeendelea kuongezeka.
Akitaja makundi hayo Issango alisema kuwa ni pamoja na madereva wa magari ya masafa marefu, wachimba madini, wavuvi, wafungwa na wale wanaofanya biashara ya ngono.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Idara ya Muitikio wa Kitaifa kutoka Tume hiyo Bi. Audrey Njelekela alisema Serikali kupitia TACAIDS inaendelea kufanya jitihada mbalimbali za kukabiliana na janga hilo ikiwemo kuandaa na kutekeleza mikakati madhubuti itakayosaidia kupunguza maambukizi kwa kiasi kikubwa.
“Mkakati wa Tatu wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI 2013/14 – 2017/18 unalenga ifikapo 2018 kiwango cha maambukizi kishuke kufikia asilimia 0.16 ikilinganishwa na mwaka 2012 ambapo utafiti unaonesha maambukizi ni asilimia 0.32,” alisema Njelekela.
Alitaja hatua nyingine zinazochukuliwa na tume hiyo ni pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa umma hasa kwa vijana, wanawake wajawazito na makundi maalum ikiwemo kujenga Vituo vya Maarifa vinavyotoa huduma za VVU/UKIMWI kwa madereva wa magari ya masafa marefu.
Aliongeza kuwa juhudu za Serikali kutoa dawa za kufubaza makali ya Virusi vya UKIMWI (ARVs) zimesaidia kupunguza vifo vitokanavyo na ugonjwa huo ambapo kwa sasa wanaotumia dawa hizo ni zaidi ya watu laki 8.
Pia Serikali imeanzisha Mfuko wa Udhamini wa Shughuli za Kudhibiti UKIMWI kwa ajili ya kusaidia kununua dawa, kutoa elimu ya UKIMWI, kupima, kufanya tafiti na kutoa elimu ya uzazi kwa vijana.
TACAIDS ilianzishwa kwa Sheria ya Bunge Na. 22 ya mwaka 2001 kwa lengo la kutoa uongozi wa kimkakati, uratibu na kuimarisha juhudi za wadau wote wanaojishughulisha na kudhibiti UKIMWI nchini.

ZITTO ASHUSHA MAMBO 10, SERIKALI YAYAPANGUA


 Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe jana amesisitiza msimamo wake kwa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kuwa Bunge limekosa meno na limeingiliwa na mhimili wa Serikali, huku pia akiihusisha Serikali na shambulio la risasi kwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.
Hata hivyo, Msemaji wa Serikali Hassan Abbas amekanusha madai ya Zitto akimtaka kufuata kanuni za Bunge na kuheshimu sheria za nchi.
Zitto aliyekamatwa juzi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) akitokea Kigoma, alikiri kutoa maoni kwenye mitandao ya kijamii akimkosoa Spika wa Bunge, Job Ndugai na Serikali na kusisitiza kuwa anatumia uhuru wake wa kikatiba kutoa maoni.
Awali, Zitto alimkosoa Spika baada ya ripoti ya kamati aliyoiunda kuchunguza biashara ya madini ya almasi na Tanzanite kwenda kusomewa Ikulu, Septemba 7, jambo lililosababisha aitwe kwenye kamati hiyo. Hata hivyo, kabla hajaenda kwenye kamati hiyo, Zitto aliandika tena kwenye mtandao wa Twitter akimshutumu Spika Ndugai. Katika maelezo yake kwa kamati hiyo ya Bunge ambayo gazeti hili limeyaona, Zitto alikiri kuandika maoni yake katika mtandao wa Twitter yenye kichwa cha habari ‘Bunge siku hizi ni Idara ya Tawi la Utawala’ akisema Bunge la 11 limekuwa likifanya kazi kwa kuingiliwa na Serikali chini ya Rais John Magufuli. “Maneno na vitendo vya Rais yanaashiria kuwa Bunge halina uhuru wake na mimi kama mbunge nina wajibu wa kuonyesha kutopendezwa kwangu,” alisema. Mbunge huyo alitaja mambo 10 ambayo alisema yanathibitisha maelezo yake kuwa ni pamoja na kuzuiwa kuonyeshwa kwa vipindi vya Bunge moja kwa moja kupitia televisheni akisema ilikuwa ni kwa kisingizio cha kupunguza gharama za uendeshaji wa mhimili wa Bunge.
“Ni dalili ya wazi ya kufifisha sauti ya Bunge na kupandisha sauti ya Serikali. Hata vituo binafsi ambavyo vilipanga kurusha Bunge Live bila malipo vilizuiwa, lakini vinarusha live mikutano ya Rais,” alisema.
Pia, aliseka kitendo cha uongozi wa Bunge kurudisha serikalini Sh6 bilioni bila ridhaa ya wabunge kwa kisingizio kwamba zimebaki kutokana na kubana matumizi ni dalili ya “kujipendekeza” kwa Serikali na kuongeza kuwa; “Wakati Uongozi wa Bunge ukirejesha kiwango hicho cha fedha, kuna taarifa kwamba kamati nyingi za Bunge zinashindwa kutekeleza wajibu wake kwa sababu ya ukata.”.
Alitaja sababu ya tatu kuwa ni maelekezo ya Serikali kwa Bunge kupitia maagizo ya Rais Magufuli kwa Spika Ndugai aliyoitoa wakati akipokea Ripoti ya Profesa Osoro kuhusu mikataba ya madini Juni 12, 2017 aliposema awashughulikie wabunge aliowaita waropokaji.
Alisema kauli hiyo inaonyesha picha dhahiri kuwa Bunge linapokea maelekezo kutoka serikalini ya kuwadhibiti wabunge hasa wanaoiwajibisha Serikali.
Pia, alisema kitendo cha Bunge kuhariri hotuba za kambi ya upinzani kwa kushinikiza kuondolewa kwa vipengele vinavyoikosoa Serikali ni sababu mojawapo ya Bunge kukosa nguvu, huku akitoa mfano wa hotuba ya Msemaji wa Kambi ya Upinzani wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Godbless Lema iliyoamriwa kuondolewa maneno yanayohusu kashfa ya mkataba wa Lugumi, kumhusisha Rais na kuuzwa kwa nyumba za Serikali, mauaji ya wanasiasa pamoja na Bunge kulinda wahalifu.
“Kauli ya Rais Magufuli ya Novemba 4, 2016 akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari kuwa mzizi wa mhimili wa Serikali ni mrefu zaidi kuliko mihimili mingine, baada ya kuulizwa juu ya matumizi ya Serikali nje ya bajeti inaonyesha dhahiri fikra ya Rais na Serikali yake juu ya ukuu wa mhimili wa Serikali dhidi ya Bunge,” alisema Zitto.
Alitaja pia kitendo cha ripoti ya kamati za Tanzanite na Almasi kusomwa nje ya Bunge na kuwasilishwa kwa Waziri Mkuu na Rais bila kuwasilishwa na kujadiliwa bungeni ili kuwekewa azimio la Bunge akisema kinazifanya kamati hizo kuonekana kuwa za Serikali badala ya Bunge. “Kauli ya Rais kuwa Spika alimpigia simu kumuuliza juu wajumbe wa kuwaweka kwenye kamati ya Bunge ya Tanzanite na Almasi inaonyesha dhahiri kuwa Spika anafanya kazi kwa maelekezo ya Rais. Bunge na Spika hawajawahi kuikana kauli hii ya Rais,” alisisitiza.
Vilevile alikitaja kitendo cha Serikali kutowasilisha taarifa za utendaji wa robo mwaka kwenye Kamati ya Bunge ya Bajeti kwa mujibu wa Sheria ya Bajeti ya mwaka 2014 ni dharau kwa mhimili wa Bunge.
“Ni dharau zaidi kwamba Serikali ilileta muswada wa sheria kuondoa kifungu kinacholazimisha Waziri wa Fedha kutoa taarifa hizo na Bunge kupitisha kuwa Sheria, hivyo kuondoa kabisa uwajibikaji wa kibajeti wa Serikali ndani ya Bunge,” alisema.
Alisema licha ya Katiba kuonyesha mihimili mitatu ya dola ambayo ni Serikali, Bunge na Mahakama kufanya kazi bila kuingiliana kikatiba, mbali na wajibu wake wa kutunga sheria, Bunge ni kama kiranja wa Serikali. “Haijapata kutokea katika historia ya Bunge letu, wabunge kukamatwa hovyo mbele ya mageti ya Bunge na kusafirishwa usiku usiku bila hata Spika kujulishwa kama taratibu za mabunge ya Jumuiya ya Madola zinavyotaka. Tukio linalolenga kuliziba mdomo Bunge,” aliongeza.
Shambulio la Lissu
Akiendelea kufafanua mambo hayo 10, Zitto aligusia suala Lissu kushambuliwa kwa risasi wakati mkutano wa Bunge ukiendelea Septemba 7 akisema ni mara ya kwanza kwa historia ya nchi. “Kitendo cha ‘watu wasiojulikana’ kummiminia risasi zaidi ya 30 Mbunge wa Singida Mashariki, Ndugu Tundu Lissu akitokea bungeni tena kwenye makazi yake ambayo kwa mujibu wa sheria ni sehemu ya Bunge ni dharau ya hali ya juu kwa mhimili huu,” alisema.
Katika makala yake aliyoiandika kwa ajili ya kuwasilisha kwenye kamati hiyo ya Bunge yenye kichwa cha habari ‘Asiyehusisha jaribio la mauaji ya Lissu hana moyo; asiyeamini kwamba vyombo vya dola vinahusika hana kichwa’, Zitto amejenga dhana ya shambulio hilo akilihusisha na Serikali
Msemaji wa Serikali
Akizungumza kwa njia ya simu, Msemaji wa Serikali, Dk Hassan Abbas alikanusha madai ya mhimili wa Serikali kuingilia Bunge akimtaka Zitto kuchukua hatua kama sheria zimevunjwa. “Serikali ina majukumu yake, inatoa bajeti kwa Bunge, huko ndiyo kuingilia Bunge? Bunge linatunga sheria ndiyo tuseme linaingilia mahakama? Mahakama inapotafsiri sheria inaingilia Bunge? Hii mihimili haiwezi kufanya kazi in isolation (kwa kutengana).”
Kuhusu Serikali kuhusika na shambulio la Lissu, Dk Abbas alimtaka Zitto kusubiri uchunguzi wa Serikali badala ya kujadili hisia.

September 21, 2017

UTAMBUZI WA MAGONJWA KUONGEZA TIJA YA UZALISHAJI WA MAZAO YA MIFUGO.


Na Ismail Ngayonga,
MAELEZO

DAR ES SALAAM
21.9.2017

SEKTA ya Mifugo ina mkubwa katika kujenga uchumi imara wa Taifa, kuongeza kipato kwa Watanzania wanaotegemea mifugo, na kutoa fursa za ajira sanjari na kuhifadhi rasilimali za Taifa.

Kulingana na takwimu na Ofisi ya Taifa ya Takwimu mwaka 2013, sekta ya mifugo ilikua kwa asilimia 3.8 ikilinganishwa na asilimia 3.1 mwaka 2012 na kuchangia asilimia 4.4 katika pato la Taifa ikilinganishwa na asilimia 4.6 mwaka 2012.
Mkutano wa wadau wa tasnia ya mifugo uliofanyika Arusha mwaka 2001, ulibainisha matatizo makuu sita yanayoathiri ufanisi wa Sekta ya Mifugo kuwa ni pamoja na kuenea kwa magonjwa ya mifugo nchini ikiwemo magonjwa ya mlipuko, magonjwa yanayoenezwa na wadudu na magonjwa ya mifugo yanayoambukiza binadamu.
Magonjwa ya milipuko na yasiyokuwa na mipaka ambayo hutokea zaidi nchini ni pamoja na ugonjwa wa miguu na midomo, homa ya mapafu ya ng’ombe, sotoka ya mbuzi na kondoo, homa ya bonde la ufa, mapele ya ngozi na homa ya nguruwe.
Taarifa ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ya mwaka 2013 inaelezwa kuwa wa  ugonjwa wa  mlipuko wa homa ya bonde la ufa uliotokea mwaka 2007 ulisababisha hasara ya Tsh. Bilioni 12 na kupoteza maisha ya watu 144 na kabla ya kudhibitiwa na Serikali kwa kuagiza chanjo dozi Milioni 5.5 na kuchanja ng’ombe, mbuzi na kondoo.
Licha ya magonjwa hayo kuleta hasara za kiuchumi na kijamii, pia magonjwa hayo yalisababisha maambukizi kwa binadamu, vifo na vizuizi vya biashara ya mifugo na mazao yake ndani na nje ya nchi.
Akiwasilisha Hotuba ya makadirio ya bajeti ya mapato na matumizi kwa mwaka 2017/18, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Dkt. Charles Tizeba anasema mwaka katika mwaka  2016/2017 Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) iliendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya utafiti katika kanda za ki-ikolojia nchini.
Anasema upitia miradi hiyo, Serikali ilitekeleza miradi ya Kipaumbele inayohusu utafiti na maendeleo ya uzalishaji wa ng’ombe wa maziwa, uboreshaji na uzalishaji wa malisho, mbuzi, kondoo na kuku katika kupitia vituo vyake saba vilivyopo Mpwapwa (Dodoma), Mabuki (Mwanza), Kongwa (Dodoma), Tanga, Naliendele (Mtwara), Uyole (Mbeya), na West Kilimanjaro.
“Katika mwaka 2016/17 Wizara kupitia Wakala wa Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) imefanya uchunguzi na utambuzi wa magonjwa ya mifugo nchini katika sampuli 4,908 zilizopokelewa” anasema Tizeba.
Anayataja magonjwa yaliyotambuliwa ni pamoja na ndigana kali, ndigana baridi, kimeta, kichaa cha mbwa, Mdondo, gumboro, sotoka ya mbuzi, homa ya nguruwe, minyoo, ugonjwa wa kutupa mimba na blue tongue.
Aidha Dkt. Tizeba anasema jumla ya sampuli 1,111 za vyakula vya mifugo zilifanyiwa uhakiki wa ubora na usalama wake ambapo asilimia 18 ya sampuli hizo zilibainika kuwa na   upungufu wa protini na nishati.
Aidha Waziri Tizeba anasema TVLA kupitia Taasisi yake ya utafiti na uzalishaji wa chanjo iliyopo Kibaha imezalisha na kusambaza chanjo dozi  30,055,100 za ugonjwa wa mdondo, dozi  680,900 za  ugonjwa wa Kimeta, dozi 121,550 za  ugonjwa wa Chambavu na dozi 10,000 za chanjo ya ugonjwa wa Kutupa Mimba.
Waziri Tizeba anasema TVLA ipo katika mpango wa kuzalisha chanjo za homa ya mapafu ya ng’ombe (CBPP) na chanjo ya sotoka ya mbuzi na kondoo (PPR) ili kutimiza lengo mafunzo yametolewa kwa mtalaam mmoja huko PANVAC nchini Ethiopia na pia imeshapokea mbegu ya chanjo hizo kama mchakato wa awali wa uzalishaji wa chanjo hizo.
Kwa mujibu wa Dkt Tizeba anasema TVLA kupitia vituo vyake vya utafiti wa teknolojia za kuangamiza mbun’go waenezao ugonjwa wa Nagana na Malale vya Tanga na Kigoma imeendelea kufanya utafiti wa njia nzuri za kupunguza au kumaliza mbung’o katika maeneo mbalimbali nchini.
“Utafiti huo pia umejikita katika kuangalia mwenedo wa mbung’o na ndorobo kati ya wanyama pori na wafugwao na uwezo wao wa kuambukiza wanyama na binadamu, ambapo hata hivyo ndorobo wote waliopatikana ni wale wasioambukiza binadamu. Ili kuendeleza tafiti za kudhibiti mbung’o, maabara imeendelea kuzalisha na kuhifadhi mbung’o wazima 506 na mabuu 556” anasema Waziri Tizeba.
Anasema Serikali itaendelea na tafiti za kudhibiti magonjwa mengine ya mifugo na kujenga uwezo wa kuyatambua na na kufuatilia mwenendo wa ugonjwa wa Sotoka ya Mbuzi katika wilaya za Handeni, Mbarali, Masasi, Ruangwa, Kiteto, Simanjiro na Ngorongoro ambapo uwepo wa ugonjwa wa Blue Tongue uligunduliwa.
Aidha Tizeba anasema katika mwaka 2017/18 TVLA itaendelea na uzalishaji na usambazaji wa chanjo dozi milioni 100 za Mdondo, 500,000 za Kimeta, 500,000 za Chambavu na 500,000 za ugonjwa wa Kutupa Mimba.
Serikali ya Awamu ya Tano inaingia katika mwaka wa pili wa utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa miaka mitano wa mwaka 2016-21 unaojitika katika uchumi wa viwanda wenye lengo la kuifikisha Tanzania katika uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Ili kufikia malengo hayo ni wajibu wa sekta binafsi kuunga mkono Serikali katika kuinua sekta mbalimbali za kiuchumi ikiwemo bidhaa za mazao ya mifugo ikiwemo nyama, ngozi na maziwa. 
MWISHO  

SERIKALI YAFUNGUKA KUHUSU TUNDU LISU

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO

Serikali imesema ipo tayari kugharamia matibabu ya Mbunge wa Jimbo  la Singida Mashariki  Tundu Antiphas Lissu  ambaye kwa sasa hivi yupo Jijini Nairobi kwa matibabu kufuatiwa shambulio alilolipata Septemba 7,mwaka huu Mkoani Dodoma.
Hayo yamesemwa Jijini Tanga na Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Ummy Mwalimu wakati akiongea na waandishi wa habari kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo.

Waziri Ummy Mwalimu alisisitiza  Serikali inasubiri kupata maombi kutoka kwa familia ya mgonjwa ikiambatana na taarifa rasmi kutoka kwa  madaktari kuhusu mahitaji ya matibabu zaidi  ya mgonjwa”Serikali ipo tayari  kugharamia matibabu  zaidi ya Mhe.Lissu popote Duniani”. 
Akiwa kama Mtanzania na Mbunge,Serikali inayo wajibu wa kugharamia matibabu yake hadi apone ili aweze kuendelea na kazi ya kuwahudumia Watanzania na wana Singida Mashariki.

Serikali  inapenda kusisitiza kwamba iko tayari kuendelea kushughulikia matibabu endapo maombi ya kufanya hivyo yatawasilishwa rasmi Serikalini,ikiwemo kupata taarifa ya maendeleo ya afya yake kutoka kwa Madaktari wanaomhudumia hapo Nairobi ambayo itatakiwa kupatikana kupitia ridhaa itakayotolewa na Mhe.Lissu au Mwanafamilia wa karibu kama taratibu za Kidaktari zinavyoelekeza.

Aidha, Serikali imeshangazwa na dhana ya kuchangishana kwa ajili ya matibabu ya Mhe. Lissu, kwani kwa kufanya hivyo kunaweza kutokea matapeli watakaochangisha Watanzania fedha kwa madai kwamba Mbunge huyo amekosa hela za matibabu.

Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia na Watoto anawashukuru Madaktari wa watoa huduma wote wa Hospitali ya Rufaa Dodoma kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya katika kuokoa masiha ya Mhe.Lissu
Imetolewa na;
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Afya
21/9/2017

HAYA NI MAELEZO YA MBUNGE ZITTO KABWE LEO ALIPOHOJIWA

TAARIFA KWA UMMA
_______
Kwa siku za hivi karibuni imeibuka tabia kwa baaadhi ya Wanasiasa na Wananchi 
kulishambulia Bunge na Viongozi wake kwa kutoa maelezo potofu kwamba Bunge la 
Kumi na Moja halina meno, halitekelezi wajibu wake ipasavyo na kwamba Bunge 
limetekwa na Serikali hivyo linaendeshwa kwa kufuata maelekezo kutoka Serikalini. 
Aidha, kwa kutumia lugha za kejeli, matusi na uchochezi watu hao wamekuwa 
wakilikebehi Bunge na Viongozi wake, mathalan kwamba Mhe. Spika anatumia ubabe, 
ameshindwa kusimamia uhuru na hadhi ya Bunge, hafuati Kanuni na hatendi haki kwa 
baadhi ya Wabunge. 
Gazeti la kila wiki la MwanaHALISI Toleo Namba 409 la Jumatatu, Septemba 18 -24, 
2017 nalo limefuata mkondo huo wa kulishambulia Bunge kupitia makala zenye vichwa 
vya habari kama vile “Risasi yakwama kwenye waleti” (Saed Kubenea), “ Ndugai 
anatamani aendeshe Bunge Kiimla” (Chris Alan,) “Ndugai Atumia Polisi Kuita Kubenea, 
Zitto” (Mwandishi Wetu), “Ubabe wa Ndugai si Ujasiri” (Gululi Kashinde) na “Kwa 
Mwenendo huu Ndugai hatamkaribia Sitta” (Mwananchi, Buguruni Malapa). Makala zote
hizo zimejaa upotoshaji kuhusu uendeshaji wa shughuli za Bunge. Makala zote hizi zina
maelezo yanayopotosha mwenendo wa shughuli za Bunge na mamlaka aliyonayo Mhe. 
Spika katika kusimamia shughuli za Bunge.
Ni wazi kuwa upotoshaji huo, kashfa na matusi vinalenga kumshambulia na
kumdhalilisha Mhe. Spika na Bunge kwa ujumla pamoja na kumchonganisha Mhe. Spika 
na Wananchi. Chanzo cha kashfa hizo ni maelezo ya Mhe. Spika aliyoyatoa kwa nyakati 
tofauti kufafanua utaratibu wa matibabu kwa Wabunge, kauli na vitendo vya baadhi ya 
Wabunge vinavyovunja Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge na utekelezaji wa shughuli 
za Bunge.
Bunge linachukua fursa hii kufafanua kwamba, Ibara ya 100 na 101 za Katiba ya 
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 imetoa uhuru kwa Wabunge kujadili hoja 
mbalimbali Bungeni na kufikia uamuzi. Kanuni za Bunge zimeweka utaratibu mahususi 
wa kuwezesha uamuzi wa wengi kuwa ndio uamuzi ya Bunge. Hivyo, Katiba, Sheria na 
Kanuni za Bunge hazitoi nafasi kwa chombo kingine chochote kulielekeza Bunge jambo 
au uamuzi unaopaswa kufikiwa Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge (Sura ya 296) inatoa ufafanuzi wa Haki na 
Kinga za Bunge na Wabunge. Vilevile Sheria hiyo na Kanuni za Kudumu za Bunge 
vinazuia mtu yeyote kuingilia kinga, uhuru, haki na madaraka ya Bunge na kutoa
adhabu kwa wanaokiuka Sheria na Kanuni hizo. Miongoni mwa makatazo hayo ni 
kusema uongo, kudhalilisha Bunge na kudharau mamlaka ya Mhe. Spika. 
Mbunge au Mwananchi anayekiuka misingi ya kinga, uhuru haki na madaraka ya Bunge 
hufikishwa kwenye Kamati ya Bunge inayosimamia masuala ya maadili ambako 
mlalamikiwa hutakiwa kupewa Hati ya Wito (Summons). Endapo mlalamikiwa atakataa 
wito huo, Sheria imeweka utaratibu wa kulitumia Jeshi la Polisi kuhakikisha anafika 
mbele ya Kamati.
Kumekuwa na upotoshaji kuhusu utaratibu uliotumika katika kuunda Kamati Maalum za 
Bunge. Mhe. Spika ana mamlaka kuunda Kamati mbalimbali kwa ajili ya kurahisisha 
utekelezaji wa shughuli za Bunge. Kanuni zilizopo zinajitosheleza hivyo hakuna 
uwezekano wowote wa Mhe. Spika kushinikizwa kupanga Wajumbe wa Kamati. Vilevile
Kanuni ya 5 imempa Mhe. Spika mamlaka ya kuamua jambo lolote ambalo 
halijawekewa utaratibu na Kanuni za Bunge. Moja ya mambo hayo ni uundwaji wa 
Kamati Maalum za Bunge. Utaratibu huu ndio uliotumiwa na Mhe. Spika kuunda Kamati 
zilizofanya uchunguzi kuhusu Mfumo wa uchimbaji wa Madini ya Tanzanite na Almasi
nchini. Aidha kwa kutumia mamlaka yake chini ya Kanuni ya 5 Mhe. Spika alizielekeza 
Kamati hizo kuwasilisha kwake Taarifa za uchunguzi huo. Kwa muktadha huo taarifa 
hizo huwa haziingii Bungeni. Utaratibu huo sio mpya kwani Kamati iliyofanya uchunguzi 
kuhusu bomba la gesi, kushauri kuhusu vyanzo vipya vya mapato (Chenge 1 & 2) 
zilitumia utaratibu huo.
Madai kwamba Bunge linaendeshwa kibabe na kwa misingi ya kibaguzi kwa itikadi za 
vyama pia si sahihi. Kanuni ya 5(4) inatoa fursa kwa Mbunge yeyote asiyeridhishwa na 
namna Mhe. Spika anavyoendesha Bunge au uamuzi anaoutoa kuwasilisha sababu za 
kutoridhishwa kwake kwa Katibu wa Bunge ambaye atafanyia kazi kwa mujibu wa 
Kanuni.
Aidha Kanuni ya 71 inatoa haki kwa raia yeyote ambaye atajisikia kwamba amepata 
athari hasi kutokana na kauli, maneno au shutuma kutokana na mjadala Bungeni 
kuwasilisha maelezo yake kwa Mhe. Spika. Kanuni hiyo imetoa haki ya raia huyo 
kujisafisha dhidi ya kauli hizo.
Aidha, katika kusimamia utaratibu wa majadiliano Bungeni Kanuni za 59 – 68 hutumika. 
Kanuni hizo zinazuia Wabunge kutoa kauli za uongo, zisizoruhusiwa na zenye kuudhi. 
Katika kusimamia utekelezaji wa Kanuni hizi walalamikaji hudhania kuwa Mhe. Spika 
anatumia ubabe.
Kanuni za 74, 75 na 76 zimeweka utaratibu mahsusi kwa ajili ya kudhibiti fujo Bungeni 
ambapo Kanuni hizo zimempa Mhe. Spika mamlaka ya kuhakikisha kwamba amani na 
utulivu unakuwepo Bungeni wakati wote wa Vikao vya Bunge. Kwa kutumia mamlaka 
yake huweza kuwatoa nje Wabunge wanaokiuka Kanuni hizo na vilevile anayo mamlaka 
ya kumtaka Mpambe wa Bunge kuingia ndani ya Ukumbi wa Bunge na kudhibiti fujo 
zinapotokea ikiwemo kuwatoa nje ya ukumbi Wabunge wanaosababisha vurugu.
Ikumbukwe kwamba, hakuna adhabu yoyote iliyowahi kutolewa kwa Mbunge kinyume 
cha Sheria na Kanuni. 
Kuhusu madai ya kutelekezwa kwa Mhe. Tundu A. Lissu, Bunge linapenda 
kuukumbusha umma kwamba, Mhe. Spika zaidi ya mara moja alitoa ufafanuzi 
kuhusiana na jitihada zilizofanywa na Viongozi wa Bunge katika kuhakikisha Mhe.
Tundu A. Lissu anapata matibabu. Aidha alielezea kuhusu uamuzi uliofikiwa na 
Viongozi wa CHADEMA na familia ya Mhe. Tundu A. Lissu kwamba waliona ni busara 
kumsafirisha Mheshimiwa Lisu kwenda Nairobi nchini Kenya kupata matibabu kwa 
utaratibu binafsi badala ya utaratibu wa kawaida wa matibabu kwa Wabunge kwa njia 
ya Bima ya Afya. 
Tunapenda kuukumbusha Umma kwamba Bunge ni chombo cha uwakilishi wa 
wananchi kinachoendeshwa na Sheria, Kanuni, taratibu zilizowekwa na kuzingatia mila 
na Katiba, desturi za Mabunge mengine yenye utaratibu wa kibunge unaofanana na 
utaratibu wa Bunge la Tanzania. Toka kuanzishwa kwake chombo hiki kimekuwa rafiki 
kwa wananchi kwa kusikiliza na kutatua matatizo mbalimbali yanayowakabili, hivyo 
wananchi wasikubali kupotoshwa kwa maneno ya baadhi ya watu wenye chuki na nia 
mbaya dhidi ya Bunge na Viongozi wake. Aidha, ikumbukwe kwamba maneno na 
vitendo vya dharau, kushusha heshima na kulidhalilisha Bunge ni mambo yasiyokubalika 
na yanapaswa kupigwa vita na watu wote wanaoitakia mema nchi yetu. 
Imetolewa na:
Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano,
Ofisi ya Bunge,
DODOMA.
20 Septemba, 2017

ZITTO KABWE ATOLEWA POLISI DODOMA KWENDA KUHOJIWA MCHANA HUU


ZITTO APELEKWA KAMATI YA BUNGE YA HAKI, MAADILI NA MADARAKA YA BUNGE
Ndugu Zitto Kabwe ametolewa Ofisi ya Polisi Mkoa wa Dodoma alikoshikiliwa tangu saa tatu asubuhi na sasa anapelekwa Ofisi za Bunge kuhojiwa na Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge inayoongozwa na Mbunge wa Newala Ndugu George Mkuchika.
Tutaendelea kuwajuza kinachojili.
Wenu,
Ado Shaibu, Katibu Mwenezi Taifa
ACT Wazalendo
Tarehe 21 Septemba 2017

MERKEL "TUNATOFAUTIANA NA TRUMP KUHUSU KOREA KASKAZINI

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amefanya mahojiano maalumu na DW, na kuelezea mtazamo wake kuhusu masuala kadhaa muhimu kimataifa, ukiwemo mzozo wa nyuklia wa Korea Kaskazini, na pia uchaguzi ujao nchini Ujerumani.
Merkel: Tunatofautiana wazi wazi na Trump kuhusu Korea ya Kaskazini
Katika mahojiano na DW, Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amesisitiza kuwa lazima mzozo wa Korea Kaskazini usuluhishwe kwa njia za kidiplomasia. Na amesema Ujerumani inaweza kuwa msuluhishi katika mzozo huo.
Katika mahojiano hayo, Kansela Merkel ameikosoa hotuba iliyotolewa na Rais Donald Trump wa Marekani mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Rais Trump alitishia katika hotuba hiyo, kwamba Marekani inaweza kuiangamiza kabisa Korea Kaskazini.
Kansela Merkel amesema kwamba anapinga vitisho vyovyote. ''Napinga vitisho vya aina zote. Lazima niseme maoni yangu binafsi na ya serikali, ni kwamba suluhisho la kijeshi halifai, tunapendelea juhudi za kidiplomasia. Hili lazima litekelezwe kwa dhati. Kwa maoni yangu, vikwazo na kutekeleza vikwazo hivyo ni jibu sahihi. Kitu kingine zaidi kuhusu Korea Kaskazini nadhani ni makosa. Na ni kwa sababu hiyo tunatofautiana kabisa na rais wa Marekani.'' Amesema Kansela Merkel.
Ujerumani tayari kuwa msuluhishi
Deutschland wählt DW Interview mit Angela Merkel (DW) Kansela Angela Merkel akizungumza na waandishi wa DW, Ines Pohl na Jafaar Abdul Karim
Ujerumani ni miongoni mwa nchi chache ambazo bado zina ubalozi katika mji mkuu wa Korea Kaskazini, Pyongyang, na pia ubalozi wa nchi hiyo mjini Berlin, huku pia ikiwa na mahusiano mema na China, Japan, Korea Kusini na Marekani.
Wakati huo huo, Kansela Merkel amesisitiza utayarifu wa Ujerumani kutoa mchango wake katika kuutafutia suluhisho mzozo wa Korea Kaskazini.
''Ingawa mzozo huo uko mbali nasi kijiografia, bado unaweza kuwa na athari kwetu'', amesema Kansela Angela Merkel katika mahojiano hayo maalumu na DW.
Kansela Merkel amekumbushia mazungumzo ya kuhusu mzozo wa nyuklia ya Iran, ambamo Ujerumani ilishiriki. ''Tunataka majibu ya kidiplomasia, kama tunavyofanya kuhusiana na mgogoro wan Ukraine''. Amesema Merkel, na kuongeza kuwa alimweleza hayo Rais Trump kwa njia ya simu, kabla ya hotuba ya rais huyo katika Umoja wa Mataifa mjini New York.
Uwezekano wa kuwasiliana na Kim Jong-un?
Alipoulizwa kama binafsi anaweza kuwasiliana na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un, Kansela Merkel amesema, ''Hilo haliko kwenye agenda kwa sasa, sizungumzii uamuzi ambao haujachukuliwa.
Kansela Angela Merkel amezungumzia pia mvutano uliopo baina ya Uturuki na Ujerumani, akisema, ''Hatutaki kuhamishia matatizo ya Uturuki nchini Ujerumani''.
Na kuhusu chama cha Mbadala kwa Ujerumani, AfD ambacho kinapigiwa upatu kupata kura nyingi katika uchaguzi wa Septemba 24, Bi Merkel amesema ''kamwe siwezi kufanya kazi na chama hicho''.
Ujerumani haitaki mgogoro na Uturuki
Hivi karibuni, mzozo kati ya Ujerumani na Uturuki umekuwa ukishika kasi, lakini katika mahojiano haya, Kansela Merkel amesema Ujerumani haitaki uhasama na Uturuki. Kinachompa wasiwasi, amesema Kansela Merkel, ni uwezekano kuwa makundi ya Waturuki waishio nchini Ujerumani, yanaweza kuwa yakichunguzana. Amesema Ujerumani haiyataki hayo; ''Tutahakikisha kwamba makundi hayo yote yanaishi kwa amani hapa, bila kudhurika''. Amesema Merkel.

HOT NEWS : SERIKALI KUMTIBU TUNDU LISU POPOTE DUNIANI....


SERIKALI imesema ipo tayari kumpeleka katika matibabu nchi yoyote duniani mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lisu iwapo familia yake itaomba serikali kusaidia kufanya hivyo

Kauli hiyo njema imetolewa leo na waziri wa afya Ummy Mwalimu

Aidha Serikali imeshangazwa na taarifa za upotoshaji na dhana ya kuchangishana kwa ajili ya matibabu ya Mhe. Lissu, akiwa Mtanzania na Mbunge, Serikali inayo wajibu wa kugharamia matibabu yake hadi apone ili aweze kuendelea na kazi ya kuwatumikia watanzania na wana Singida Mashariki

RAIS MAGUFULI KUMALIZA CHANGAMOTO ZA WATANZANIA


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imedhamiria kumaliza tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama pamoja na huduma ya umeme katika maeneo mbalimbali nchini zikiwemo wilaya za Chemba na Kondoa mkoani Dodoma.
Amesema serikali kupitia kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya kumtua mama ndoo, itahakikisha wananchi katika maeneo yote nchini watapata huduma ya maji safi na salama katika umbali usiozidi mita 400 kutoka kwenye makazi yao.
Waziri Mkuu ameyasema hayo wakati  akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa wilaya ya Chemba na Kondoa waliomsimamisha katika maeneo ya Chemba, Kalema, Bicha na Bereko akiwa njiani kuelekea mkoani Arusha kwa shughuli za kikazi.
Alisema kwa sasa Serikali imeendelea na uchimbaji wa visima virefu, vifupi pamoja na kuweka mtandao wa mabomba ya kusamba maji katika maeneo mbalimbali nchini yakiwemo na ya wilaya hizo ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo karibu na makazi yao
Kufuatia hali hiyo Waziri Mkuu aliwaagiza watendaji wawachukulie hatua watu wote watakaokutwa wakiendesha shughuli mbalimbali kama za kilimo, ujenzi wa makazi na uchungaji wa mifugo ndani ya vyanzo vya maji kwa kuwa zinasababisha ukame.
Aidha Mh. Majaliwa ameagiza wakandarasi wamalize maeneo yaliyosalia katika REA awamu ya pili ndipo waendelee na awamu ya tatu. Alisema Serikali imetenga sh. trilioni moja kwa ajili ya kusambaza umeme katika vijiji 8,000 ambavyo bado havijaunganishiwa nishati hiyo.
"Rais wetu Dkt. John Magufuli anajali sana wananchi wake, hivyo ametenga fedha nyingi zitakazotosheleza kusambaza umeme katika vijiji vyote vikiwemo na vya wilaya za Chemba na Kondoa. Gharama za kuunganishiwa umeme huo ni sh. 27,000 tu" amesema.

ASHA ROSE MIGIRO AREJESHWA UMOJA WA MATAIFA

Image result for asha migiro


Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres ameteua jopo la wataalamu 18 watakaokuwa na kazi ya kuhakikisha wanatumia uzoefu wao kukabiliana na migogoro duniani kwa njia ya kidiplomasia, huku mwanadiplomasia wa Tanzania, Dk Asha- Rose Migiro akiwa miongoni mwa wateule hao.
Hatua ya kuteuliwa Dk Migiro aliyewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa UN kwenye jopo hilo imeelezwa na wataalamu wa masuala ya diplomasia kuwa ni uthibitisho mwingine wa namna Tanzania ilivyo mshiriki muhimu katika kusaka amani ya dunia.
Jopo hilo ambalo linafahamika kama ‘Bodi ya Ngazi ya Juu ya Ushauri kuhusu Usuluhishi’ limeundwa kwa kuzingatia usawa wa kijinsia na uwakilishi wa kikanda, pia likizingatia historia ya wahusika katika masuala ya diplomasia na utatuaji wa migogoro.
Pamoja na Dk Migiro ambaye kwa sasa ni Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, wengine walioteuliwa ni aliyekuwa mke wa rais wa Msumbiji na baadaye akaolewa na Rais Nelson Mandela wa Afrika Kusini, Graca Machel, Rais mstaafu wa Nigeria, Olesegun Obasanjo, Rais wa zamani wa Chile, Michelle Bachallete na Rais mstaafu wa Finland, Tarja Halonen.
Pia, wamo wanadiplomasia, mawaziri wa zamani, watu waliowahi kuongoza taasisi za kimataifa na watu wengine mashuhuri. Jopo hilo pamoja na kazi nyingine litakuwa na jukumu la kumshauri Katibu Mkuu wa UN kuhusu njia zinazopaswa kuzuia migogoro na kushiriki kutatua mizozo katika maeneo yanayokumbwa na hali hiyo.
Baadhi ya wataalamu wa masuala ya diplomasia wamesema kuteuliwa kwa watu kama Dk Migiro na Graca Machel kwenye jopo hilo kunaonyesha jinsi walivyoiva kidiplomasia na watatoa mchango mkubwa katika kuhakikisha amani inapatikana duniani.
“Mtu kama Dk Migiro ana uzoefu mkubwa wa mambo haya na kuteuliwa kwake kunadhihirisha namna Tanzania ilivyo mstari wa mbele katika kusaidia kupatikana kwa amani duniani,” amesema Innocent Shoo, Mhadhiri wa Chuo cha Uhusiano wa Kimataifa na Diplomasia (CFR).
Amesema Tanzania imekuwa ikishiriki katika utatuzi wa migogoro katika maeneo mbalimbali duniani, hivyo kuteuliwa kwake hakushangazi kwa vile kunaendelea kudhihirisha diplomasia ya Tanzania kwenye eneo hilo.
“Hivi sasa tunaweza kuona jinsi Rais wetu mstaafu Benjamin Mkapa anavyoendelea na upatanishi katika mzozo wa Burundi, wakati Rais Jakaya Kikwete akipatanisha nchini Libya na hata Dk Migiro amewahi kushiriki kikamilifu katika kusaka amani katika eneo la Nchi za Maziwa Makuu wakati alipokuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania na hata alipokua UN kama Naibu Katibu Mkuu,” amesema.
Kuhusu Graca Machel amesema amekuwa mstari wa mbele katika kupigania usawa ambao mara nyingi unapokosekana huwa chanzo cha kuzuka kwa migogoro mingi duniani.
 “Lakini pia alishiriki katika kusaka amani nchini Kenya wakati wa machafuko baada ya uchaguzi wa mwaka 2007,” amesema.

HOT NEWS JITIHADA ZA KUMSAFIRISHA TUNDU LISU KWENDA MAREKANI ZAKWAMA


Huku awali alijitolea kumsaidia Tundu Lisu kwenda nchini Marekani kwa matibabu zaidi, Mbunge wa Singida Kaskazini Lazaro Nyalandu amesema jitihada za kumpeleka Lissu Marekani kutibiwa kwa sasa zimegonga mwamba.

Lazaro Nyalandu ametoa taarifa hiyo kwenye ukurasa wake wa facebook ambapo amendika ujumbe kuhusu kauli ya madaktari wanaomtibia Tundu Lissu jijini Nairobi Kenya, na kueleza kwamba madaktari hao wamesema hawawezi kuruhusu Tundu Lissu asafirishwe kupelekwa Marekani kutokana na hali yake jinsi ilivyo.
“Kwa sasa mipango ya kumsafirisha Mheshimiwa Tundu Lissu nje itasimama kutokana na ushauri wa madaktari wa hospitali ya Nairobi, ili kuruhusu kukamilishiwa huduma za tiba ambazo tayari ameanzishiwa hadi hapo itakavyoshauriwa au vinginevyo, ama endapo kutatokea umuhimu wa kufanya hivyo katika siku zijazo”, ameandika Lazaro Nyalandu.
Hapo jana Lazaro Nyalandu alitoa taarifa kwamba wanafanya jitihada za kumpeleka Tundu Lissu Marekani kwa ajili ya matibabu zaidi, huku wakisubiria ripoti ya madaktari wa hospitali ya Nairobi ambako mbunge huyo anatibiwa, na ndipo ilipokuja taarifa hiyo kwamba haitowezekana kumsafirisha kwa sasa.
Ikumbukwe kuwa Mbunge Tundu Lissu alipigwa risasi na watu wasiojulikana Septemba 7, 2017 mjini Dodoma majira ya mchana, na usiku wa siku hiyo hiyo alikimbizwa jijini Nairobi kwa ajili ya matibabu zaidi, kutokana na hali yake kutokuwanzuri.
WWW.TUMAINIJIPYA MEDICAL TRAINING COLLAGE FORM.COM